Cheyo atishia `kuilipua` Serikali

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,320
33,125
Cheyo%288%29.jpg

Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo



Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), ametishia ‘kuilipua’ serikali bungeni akiituhumu kwamba, imefikia makubaliano mengi na wafadhili katika kuipatia Tanzania misaada, ambapo baadhi yake hayakubaliki kama yangewasilishwa bungeni.
Cheyo, ambaye alikuwa akichangia hoja katika mjadala kuhusu Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2010/2011, alisema kama angepata muda wa kutosha, angeweza kuyaanika mambo hayo bungeni juzi.
Katika mchango wake, Cheyo alitaja changamoto kadhaa, ambazo ni kikwazo kikubwa cha ukuaji wa uchumi nchini.
Miongoni mwa changamoto hizo, alisema ni pamoja na tabia ya serikali ya utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili, huku nchi ikiwa imesheheni rasilimali nyingi, kama vile madini ya uranium, zinazoweza kuiingizia kipato na kuondokana na umaskini.
Alisema utegemezi huo umechukua sura tofauti na ilivyokuwa zamani, ambapo misaada ilikuwa kama neno lenyewe (misaada) lilivyo, lakini sasa misaada, ambayo Tanzania inapatiwa kutoka kwa wafadhili inaitwa ‘control’ au utawala, ikiwa ina masharti mengi, ambayo hayakubaliki.
“Wanataka kukuambia utengeneze sheria gani, wanataka kukuambia ufike hapa wapi,...na kama ningelikuwa na wakati mkubwa, ningeweza kukuonyesha hapa katika bajeti hii general budget support. Kuna mambo lukuki, ambayo serikali imekubaliana na wafadhili, ambapo mambo mengine hayakubaliki kabisa kama yangewekwa mbele ya Bunge lako Tukufu hapa,” alisema Cheyo.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni namna ya kuwasaidia wakulima na kusema bado serikali haijapata namna iliyo sawa ya kuwasaidia.
Cheyo alisema hotuba ya bajeti imetaja idadi ya watu wanaotegemea kilimo, lakini bado hakuna uhuru kwa mkulima, badala yake bado mkulima anashikiliwa na serikali, ambayo inaamua auze wapi mazao yake au asiuze kabisa.
Alisema changamoto nyingine ambayo bado serikali haijaweza kuitatua, inahusu pembejeo, ambazo ugawaji wake alisema umetawaliwa na “wizi mtupu”.
“Juzi hapa sisi kule Kanda ya Ziwa tumepewa vocha ya mbegu. Watu wameiba, wameandika majina Maduhu Masanja na anaweka mtu mmoja na hakuna serikali iliyo na uwezo wa kukamata mtu yeyote. Mimi naona baadhi ya watumishi wa serikali ni washiriki kabisa katika mchezo huo. Kwa hiyo, serikali inatoa fedha upande huu wengine wanazichukua wanaweka mfukoni mwao.”
Alipendekeza kuwekwa utaratibu mzuri utakaowezesha pembejeo kuwafikia wakulima, ikiwa ni pamoja na kuweka bei inayoeleweka.
Cheyo alisema changamoto nyingine inahusu tabia ya nchi, ambapo alisema zamani ilikuwa ikijulikana wakati wa kulima, lini mvua itanyesha, lakini hivi sasa mambo hayo hayajulikani.
Kutokana na hali hiyo, alipendekeza kuwa uwekezaji katika kilimo, uhusishe kilimo cha umwagiliaji na kuitaka serikali kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuimarisha miundombinu.
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Kojani, Salim Yussuf Mohamed (CUF), alisema bajeti zilizotengewa mikoa ni kubwa kulinganisha na ile iliyotengewa Wizara ya Katiba na Sheria.
Alisema wakati mkoa kama vile Mwanza ukiwa umetengewa sh. bilioni 205.5, wizara hiyo imetengewa sh. bilioni 117.97.
Mikoa mingine na bajeti ilizotengewa kwenye mabano, aliitaja kuwa ni Kagera (sh. bilioni 135.1), Dar es Salaam (sh. bilioni 146.3), Dodoma (sh. bilioni 127.2), Arusha (sh. bilioni 125.2), Iringa (sh. bilioni 142.6), Kilimanjaro (sh. bilioni 141.6), Mbeya (sh. bilioni 167.7), Morogoro (sh. 145.5),Tanga (sh. bilioni 148.2) na Shinyanga (sh. bilioni 166.3).
Alisema uamuzi huo unatishia kuathiri utendaji wa wizara hiyo na idara zilizo chini yake, ikiwamo kuchelewesha kesi katika mahakama.
Mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi (CCM), akichangia bajeti hiyo, alisema amevutiwa na Sera ya Matumizi kwamba serikali itaendelea kuongeza ufanisi katika kusimamia fedha za umma ikilenga katika maeneo, ambayo yanalenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato.
Hata hivyo, alisema wananchi wa Muleba Kusini, wanakabiliwa na hatari kutokana na kushambuliwa na ugonjwa mpya, unaoitwa kitaalamu ‘Mnyauko’, unaotokana na kirusi kinachokula migomba na kusababisha kuoza na kunuka.
Alisema wataalamu kutoka nchini Uganda na Kenya wakishirikiana na wa Maruku, mkoani humo, wamezunguka kwenye maeneo hayo kuangalia tatizo hilo na kuahidi kwamba kuna chanjo ya kuzuia ugonjwa huo.
“Na sisi Muleba Kusini tunategemea migomba kwa ajili ya chakula. Tuna kula ndizi na tunategemea ndizi hizo hizo kama zao la biashara. Tunauza ndizi Shinyanga na Mwanza. Watu wanaoishi Kahama huko, wanajua ndizi zetu ni tamu sana na utamu wake hauna mfano,” alisema Masilingi.
Kutokana na hali hiyo, alisema ameshaongea na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, ambaye ameahidi kuwa atakwenda.
“Ninamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu amuwezeshe Waziri wa Kilimo aende haraka sana kwa sababu hajaondoka tangu Bunge hili limeanza namuona humu humu ndani. Mimi nimesema kule ndizi zinakwisha na huyu ni mtani wangu Mheshimiwa Wasira, anadhani ni mzaha.
Tutakufa kwa sababu serikali haiwezi kulisha watu wa Muleba Kusini migomba ikioza yote, Mheshimiwa Wasira ninakuomba uondoke na ukichelewa nitamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu akuagize uondoke haraka sana kwa sababu hili ni jambo la kutisha anaweza akadhani ninatania Mheshimiwa Waziri Mkuu.”



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Back
Top Bottom