CHADEMA wamshukia Ngawaiya

superfisadi

JF-Expert Member
May 22, 2009
553
52
CHADEMA yamuonya Ngawaiya asikurupuke

na Grace Masha, Moshi

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro, Thomas Ngawaiya, kuacha kukurupuka kwa kuzungumza mambo ya uongo ili kujitafutia umaarufu.

Mwenyekiti huyo pia amekumbushwa kuwa aliwahi kushiriki katika harakati zilizofanikisha kuwang'oa CCM kwenye majengo ya Halmashauri ya Moshi alipokuwa Mbunge wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), hivyo haeleweki anavyowapinga madiwani wa CHADEMA wanapofanya harakati kama hizo.

Mratibu wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Manispaa ya Moshi, Hawa Mushi, alisema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na waandishi wa habari akijibu madai yaliyotolewa hivi karibuni na Ngawaiya.

Alimtaka kiongozi huyo wa CCM kujijengea utaratibu wa kufanya utafiti kabla ya kuzungumza ili kuepuka kuipotosha jamii huku akimtaka kuweka kumbukumbu ya mambo ili asipinge hata yale aliyowahi kuyafanya au harakati alizoshiriki kuinyang'anya CCM jengo walilokuwa wakilitumia kama ofisi za Wilaya ya Moshi Vijijini.

"Ngawaiya akiwa mbunge wa Moshi Vijijini alishirikiana na madiwani wa TLP wakawatoa CCM kwenye jengo la halmashauri walilokuwa wakilitumia kama ofisi za wilaya… kama jambo hilo si jema ni kwa nini aliyekuwa waziri mkuu wakati huo hakulivinja Baraza la Madiwani? Au kwa kuwa sasa yuko CCM anaona tofauti," alihoji Mushi.

Hivi karibuni Ngawaiya alinukuliwa na vyombo vya habari akipinga hatua ya madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Moshi Mjini kuendesha harakati za kuinyang'anya CCM mali za halmashauri hiyo wanazodai kukalia kimabavu.

Hawa ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalumu wa halmashauri hiyo alisema Baraza la Madiwani halijawahi kuwa na mgogoro na mtu au taasisi yoyote na kuwa vikao vyake huendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni huku akisisitiza kuwa kutofautiana kimtizamo miongoni mwa wajumbe si mgogoro.

"BAWACHA tunaamini uwezo, busara na hekima alizonazo Waziri Mkuu Mizengo Pinda hawezi kufanyia kazi kwa kauli za wanasiasa wanaojitafutia umaarufu wa mambo mepesi hata kama ni ya uzushi ili kulifuta Baraza la Madiwani," alisema Mushi.

Aidha, mratibu huyo alimshangaa Ngawaiya kwa kauli yake aliyodai kuwa CHADEMA walisababisha vikao vya baraza kuvunjika mara mbili kwa kile alichosema kuwa ni uongo, kwani hakuna hata siku moja ambapo kikao kiliwahi kuvunjika hivyo kumtaka kuwa makini na kauli zake.

"Kikao cha Machi 31 mwaka huu kiliahirishwa na mkurugenzi siku moja kabla hakijafanyika na kilifanyika Aprili 20 mwaka huu ambapo mkurugenzi alitoka nje lakini tuliendelea na kikao kama kanuni zinavyotuelekeza na maamuzi tuliyoyafikia tuliyawasilisha kwa mkurugenzi kwa ajili ya utekelezaji, sasa hiyo siku anayosema kuwa tulivunja kikao ni lini?" alihoji Mushi.

Kwa upande wake Ngawaiya akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu alikiri kushiriki harakati kama hizo akiwa mbunge huku akisema kuwa hapingani na uamuzi wao wa kurejesha mali za halmashauri zinazokaliwa na CCM.

Alisema kuwa yeye anapinga madiwani kutumia muda mwingi kujadili suala hilo ambapo aliwashauri ni vema wakatumia mahakama kudai mali hizo ili watumie vikao vya halmashauri kwa ajili ya kujadili masuala mengine ya wananchi.
 
Back
Top Bottom