BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,020
Kama CCM safi, inaogopa nini?
Lula wa Ndali-Mwananzela Januari 21, 2009
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Lula wa Ndali-Mwananzela Januari 21, 2009
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
HIVI ukimuona mtu kwa mbali amevaa suti nzuri yenye rangi ya kupendeza, amevaa viatu vya bei mbaya huku ameshikilia mkongojo kwa fahari na akinukia manukato mazuri utaamini kuwa ni msafi?
Ukimsogelea kwa karibu na kugundua kuwa amechana nywele zake vizuri, kucha zimekatwa vizuri, amejipaka mafuta inavyopaswa na meno yake yamepigwa mswaki kama wale watu wa kwenye matangazo ya Colgate si utakubali kuwa mtu huyo ni msafi?
Wakati unamuangalia mtu huyo unaangalia aliposimamia na unagundua kuwa amesimama kwenye shimo la takataka lenye kunuka kila aina ya uvundo na akisema kuwa yeye ni msafi utamkubalia?
Ukichukulia kwa maana ya mtu msafi hivi usafi ni usafi wa mtu tu na si mazingira aliyopo pia?
Kwa muda mrefu sasa nimekaa pembeni nikiangalia kichekesho cha malumbano kati ya CCM na wapinzani wake ambapo wapinzani (wakiongozwa na kina Dk. Wilbroad Slaa na Zitto Kabwe) wakidai kuwa CCM si safi huku wao CCM wakiongozwa na watetezi wake kama Mzee wetu John Malecela na Amos Makalla wanadai kuwa CCM ni safi!
Baada ya kuangalia kituko hicho kwa muda mrefu na mimi naombe niongeze munyu kwenye mjadala huu kwa kutangaza kuwa CCM ni chama kinachodai kuwa ni kisafi huku kikiwa kimesimama juu ya lundo la uchafu, kikauzoea, kikapoteza hata uwezo wake wa kunusa harufu mbaya inayozunguka.
Ukiona mtu anakukawiza kawiza kuingia sebuleni basi ujue kuna kitu; na kama umeenda kumtembelea rafiki yako wa mwenye kibanda cha chumba kimoja naye akawa anakuambia subiri kidogo basi usiharakishe kwenda ndani! Kuna wakati ambapo mgeni akikaribishwa anaonyeshwa maeneo fulani fulani tu lakini yale mengine nyeti anafichwa kwani hadi mazingira yaboreshwe.
Inapokuja kwenye vyama vya kisiasa, ukiona chama cha kisiasa hakiko tayari kufungua mahesabu yake mbele ya umma basi usiwe na shaka ndani kuna matatizo. Hakuna chama kilichopokea fedha nyingi za umma za walipa kodi wa Tanzania kama Chama cha Mapinduzi, lakini pia ndicho chama ambacho hakijathubutu kuweka wazi mapato yake yote na matumizi yake kwani si vyote viko sawasawa.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka jana inaonyesha kuwa vyama vya kisiasa vyote havikuwasilisha taarifa zao za mwaka za fedha na kutolea mahesabu kiasi cha shilingi bilioni 13. Kwa vile CCM ndicho chama tawala na ndicho ambacho kinadai kusimamia utawala bora na sheria inashangaza sana ni kwanini hakikutoa ripoti hiyo wakati wa ukaguzi.
Lakini zaidi kinachoshtua ni kutokukaguliwa kwa vitabu vyake na taasisi huru na matokeo yake kuacha chama hicho kikongwe zaidi cha kisiasa nchini kugubikwa na wingu la tuhuma za kuhusika na ufisadi.
Mwaka 1995 CCM inadaiwa ilipata msaada wa kiasi kikubwa cha fedha kutoka Zimbabwe ili kuweza kufanikisha kampeni yake ya uchaguzi mkuu. Mwaka 2000 kuna habari kuwa CCM ilitumia Benki Kuu kujichotea mabilioni ya shilingi ili kufanikisha kampeni zake. Kuelekea uchaguzi wa 2005 tuhuma za fedha nyingine ziliibuka.
Mwezi wa Aprili 2005, gazeti mashuhuri la Uingereza la Africa Confidential liliandika habari kuwa fedha karibu shilingi bilioni mbili zilikuwa zimeingia katika mchakato wa uchaguzi kutoka Oman. Baadaye zilikuja habari nyingine kwamba kulikuwa na fedha zimetoka Iran.
Kinachoshangaza kuhusu habari hizo ni kwamba kampuni moja, Kagoda ilikwisha kupata mikataba na makampuni ya kigeni ya Nishizawa ya Ujapani (JPY 956,110.986- Tarehe 10 Septemba, 2005) na kampuni ya Textima (dola 9,057,463.90 12 Septemba, 2005), tatizo ni kuwa kampuni ya Kagoda haikuwa imesajiliwa hadi tarehe 29 Septemba, 2005.
Je, yawezekana hakukuwa na taarifa sahihi za fedha hizo kwa kudhaniwa kuwa ni za Iran kumbe zikiwa ni za Kagoda?
Sasa naweza kusema mengi ambayo tayari yamesemwa na wengine. Leo hii CCM inatumia karibu shilingi bilioni moja (na sehemu nyingine bilioni mbili) katika chaguzi ndogo za kuziba viti vya ubunge. Tukichukulia kwa haraka tu kuwa gharama ya jimbo moja kwa CCM ni shilingi bilioni moja tunajiuliza mwaka 2005 CCM ilikuwa na wagombea katika majimbo yote ya uchaguzi nchini. Je ni kiasi gani cha fedha kilitumika?
Pamoja na gharama ya uchaguzi mkuu tunakumbuka kuwa katika kila jimbo CCM ilikuwa na kura zake za maoni ambazo iligharimia, je, ni kwa kiasi gani? Kwa hesabu za haraka haraka CCM ilihitaji si chini ya shilingi bilioni 100 (ukizingatia gharama ya jimbo moja ni bilioni moja lakini ukiwa na majimbo mengi kwa wakati mmoja gharama inapungua) kufanya kampeni za madiwani, wabunge na Rais. Fedha hizo zote zilitoka wapi?
Lakini cha kushtua zaidi ni kuwa hadi hivi sasa kuna kila dalili kuwa kampuni ya Kagoda haitawekwa wazi isipokuwa watu wawili watatu wanaweza kufikishwa mahakamani kwa udanganyifu, kughushi nyaraka n.k. Nawahakikishia kama CCM inataka Kagoda ifahamike ingeshafahamika mwaka juzi!
Wapo wale ambao wanataka tuamini kuwa kufikishana mahakamani kunakoendelea sasa hivi kunaonyesha jinsi gani Serikali iko makini katika kusimamia sheria. Mawazo hayo yameanza kurudiwa na viongozi mbalimbali wa CCM ambao wanataka wananchi waamini kuwa Serikali iko makini kupambana na ufisadi!
Kwa haraka haraka mtu anaweza kuamini hivyo. Hata hivyo, tunajiuliza hivi haya yote yanayowafikisha watu mahakamani yametokea chini ya utawala wa chama gani? Tunawauliza hivi baadhi (kama siyo wote) wa watuhumiwa ni wanachama wa chama gani cha kisiasa? Je, wale waliokuwa mawaziri ambao wamefikishwa mahakamani kwa makosa wanayodaiwa kuyafanya hivi waliyafanya wakiwa ni mawaziri wa Serikali iliyoundwa na chama gani?
Mkataba wa IPTL uliingiwa na Serikali ya chama gani? CCM.
Mkataba wa Richmond uliingiwa na viongozi wa Serikali ya chama gani?- CCM. Mkataba wa Buzwagi uliingiwa na Waziri wa Serikali ya chama gani? CCM.
Mkataba wa ununuzi wa rada iliingiwa na Serikali ya chama gani? CCM.
Mkataba wa ununuzi wa dege la Rais uliingiwa na Serikali ya chama gani? CCM. Kuleta ubia wa uendeshaji wa ATCL na SAA ulifanywa na serikali gani? CCM.
Kuleta waendeshaji wa Tanesco kulifanywa na Serikali ya chama gani? CCM.
NI serikali gani iliingia mkataba na kampuni ya RITES Consortium kuendesha shirika letu la Reli hadi leo wamewakumbushwa kuwa mataaluma ya reli kumbe yetu? CCM.
Wizi wa mabilioni ya EPA umefanyika wakati Serikali gani ikiwa imelala kwenye usukani? CCM.
Ufujaji mkubwa wa matumizi ya fedha za walipa kodi ulioonyeshwa katika ripoti ya CAG ulifanyika ndani ya Serikali ya chama gani? CCM.
Rais anayedaiwa kufanya biashara akiwa Ikulu na kujitajirisha kinyume na maadili ya uongozi alitoka chama gani? CCM!
Hiyo ni mifano michache ya kitaifa tu, wakitaka turudi kwenye halmashauri na miji mbalimbali nchini, na ufisadi kwenye idara na vitengo mbalimbali tunaweza!
Leo wanapokamatana wenyewe kwa wenyewe ndiyo wanataka tuanze kuwashangilia kuwa wao ni safi? Hivi kama hayo hapo juu ni usafi basi uchafu umepoteza maana yake!
Hivi, wanaposimama majukwaani na kudai kwa kiburi cha chama kuwa CCM ni safi wanatufikiriaje sisi, majuha?
Mpaka pale chama nikipendacho, chama nilichokulia, chama cha Baba wa Taifa kitakapokubali kuwa kinanuka kitakapokubali kuwa ni kichafu kitakapokubali kuwa si tu mtu mmoja mmoja ni mchafu bali mfumo mzima wa chama na utamaduni wa chama ni mchafu ndipo hapo tu kitakapoanza kweli kujisafisha na kusafishika.
Na ndugu zangu CCM washukuru Mungu kuwa huko kwenye Upinzani usafi wenyewe nao wa kutafuta! Vinginevyo kikija chama kilicho kisafi kweli, CCM uchafu wake utakuwa ni dhahiri kuliko gari la taka!
Nilichotaka kusema kwa kifupi ni kuwa CCM isiringie uzuri wa suti zake, na utamu wa sauti za wapambe wake; isiringie uzuri wa makada wake au ukuu wa vyombo vyake vya kijeshi. CCM isichanganye wananchi kukubali wachafu kidogo waongoze kuwa ni kuwa wananchi wanaamini kuwa CCM ni safi kweli. Siku moja watakaposhikiwa sabuni na kutupwa mtoni kuogeshwa ndipo watakapogundua uchafu wao ulivyo.
Kuna njia moja ya uhakika na isiyo na shaka itakayoisafisha CCM mbele ya umma. Njia hiyo haiwahusishi kina Yusuf Makamba wala Malecela kujipigia debe. Njia hiyo ni ya kisayansi na ambayo inaweza kuzima mjadala wote wa CCM chafu. Njia hiyo ni kwa CCM kualika kampuni ya kimataifa ya mahesabu, ifanye ukaguzi wa maheshabu yake kuanzia angalau 2005, na kutoa taarifa hiyo hadharani.
Endapo taarifa hiyo itasema kuwa mahesabu yote ya CCM ni mazuri na hayana shaka na ya kuwa vyanzo vyote vya fedha vinaeleweka, na ya kuwa fedha zote zinajulikana zilikotoka na zilivyotumika, na vyanzo hivyo vyote vikawekwa hadharani kwa mwananchi yeyote kuvitambua, basi ni hapo tu nitakaposimama na mimi kwa fahari kusema CCM ni safi. Sasa hivi tunazugana kwa maneno ya mapambo, na kwa kauli za ulimbo!
Wito wangu ni kuwa CCM ianze kujisafisha sasa na kutoka kwenye shimo la taka ambako imesimama huku ikitangazwa kwa kipaza sauti mimi msafi. Usafi si mavazi tu, na si kuonekana tu, usafi ni pamoja na mazingira uliyopo. Kwa sasa mazingira ya CCM ni machafu, na hivyo yanaifanya CCM kutokuwa safi. Mwenye kubisha abishe, habari ndiyo hiyo!
Barua-pepe: lulawanzela@yahoo.co.uk