CAG: Bilioni 190 za mikopo ya halmashauri zaliwa na wanufaika hewa

ChoiceVariable

JF-Expert Member
May 23, 2017
43,161
49,915
CAG anasema Kwa miaka 5 iliyopita zaidi ya Bilioni 190 zimeliwa na Wajanja Kupitia mikopo ya pesa za ndani za Asilimia 10 kutoka Halmashauri.

Pesa hizo hazijulikani zilikoenda na pia hazijarejeshwa.

=====

Kichaka kipya ufisadi nchini
Kwanini? Katika miaka mitano sita ya fedha iliyopita (2016/17-2021/22), jumla ya Sh. bilioni 192 hazijarejeshwa na wanufaika wa mikopo hiyo huku Rais Samia Suluhu Hassan akikiri kuwa fedha hizo hazikusanyiki tena kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwamo kukopeshwa kwa 'watu hewa'.

Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21 iliyowasilishwa bungeni Aprili 12, mwaka jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alibaini mabilioni ya shilingi yako hatarini kupotea kutokana na kutokuwa na udhibiti mzuri wa usimamizi wa mikopo inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalum.

CAG Charles Kichere alibainisha kuwa kwa mwaka huo wa ukaguzi, halmashauri 155 hazikukusanya Sh. bilioni 47.01 za marejesho ya mikopo iliyotolewa kwa makundi hayo.

Kwa mujibu wa CAG, hali iliyobainika katika ukaguzi wake wa mwaka 2020/21 ni mwendelezo wa kile alichokibaini katika miaka mitano iliyopita kuhusu mikopo hiyo.

Mwaka Hal. Kisichorejeshwa Asilimia

2020/21 155 Bil 47/- 70

2019/20 130 Bil 27.79/- 65

2018/19 111 Bil. 13.79/- 59

2017/18 90 Bil 10.04/- 59

2016/17 84 Bil 5.81/- 63

Jedwali la mikopo isiyorejeshwa inayotolewa na serikali kwa makundi maalum kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri nchini. CHANZO: RIPOTI YA CAG 2020/21.

Katika mukhtasari wa ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22 aliyoiwasilisha kwa Rais Samia Jumatano ya wiki iliyopita, CAG Kichere alibainisha kuwa Sh. bilioni 88 zilizokopeshwa na halmashauri kwa makundi maalum kwa mwaka huo wa fedha, hazijakusanywa.

Hii ina maana kwamba kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi mwaka uliopita wa fedha, jumla ya Sh. bilioni 192 hazijakusanywa kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo.

UCHUNGUZI WA CAG
Katika ripoti yake ya 2020/21, anabainisha kuwa katika kufuatilia uzingatiaji wa matakwa ya sheria iliyopo, alibaini wanufaika wa vikundi katika mamlaka 155 za serikali za mitaa hawakurejesha Sh. bilioni 47.01 kama marejesho ya mkopo waliopewa.

CAG pia anasema alibaini mamlaka 83 za serikali za mitaa hazikuchangia Sh. bilioni 6.68 katika mfuko kama inavyotakiwa kisheria, jambo ambalo linazuia azma ya serikali ya kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kupunguza umaskini.

"Pia nilibaini mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 178.61 ilitolewa kwa vikundi visivyokuwa na sifa na Sh. bilioni 1.24 hazikuhamishwa kutoka akaunti za amana za mamlaka 11 za serikali za mitaa (halmashauri) kwenda akaunti maalum ya mfuko, kinyume cha Kanuni ya 22(1) na (2) ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu," CAG anabainisha.

Anazitaja halmashauri ambazo hazikuhamishia Sh. bilioni 1.24 katika akaunti maalum za mikopo ni: Ushetu (Sh. 308,528,550); Bahi (Sh. 54,222,488); Iringa (Sh. 236,486,588); Busega (Sh. 49,090,000); Nanyumbu (Sh. 179,268,173); Momba (Sh. 41,795,000); Kilolo (Sh. 122,596,622); Gairo (Sh. 38,679,672); Rungwe (Sh. 115,777,111); Ileje (Sh. 32,043,700); na Sengerema (Sh. 59,511,900).

SHIDA ILIPO

CAG anabainisha kuwa kutorejeshwa kwa mikopo hiyo kunatokana na kutokuwa na udhibiti mzuri wa usimamizi wa mikopo, akifafanua kuwa mamlaka za serikali za mitaa husika zilitoa mikopo kabla ya kufanya uchambuzi wa kina wa historia ya ulipaji wa kikundi na kupitia mapendekezo ya mradi husika ili kuhakikisha kikundi kina uwezo wa kurejesha mkopo kwa wakati.

Vilevile, CAG anasema amebaini hakuna ufuatiliaji wa karibu wa kukusanya marejesho ya mikopo ambayo bado haijalipwa kutoka kwenye vikundi.

Ili kufikia lengo na uendelevu wa mfuko, CAG anasisitiza mamlaka za serikali za mitaa kufanya tathmini kabla ya kutoa mikopo na kuweka juhudi zaidi katika kukusanya madeni ambayo hayajalipwa.

Pia anaishauri Ofisi ya Rais - TAMISEMI ianzishe hatua madhubuti za kurejesha mikopo kwa kuhusisha wataalamu wa usimamizi wa mikopo ambao watahimiza uzingatiaji wa urejeshaji wa mikopo kwa hiari ili kufikia ukuaji endelevu wa mfuko.

CAG pia anabainisha kuwa tathmini aliyoifanya katika akaunti za benki za biashara ambako mamlaka za serikali za mitaa hutunza fedha za mfuko, ilibainisha Sh. milioni 156.23 za mfuko zililimbikizwa katika akaunti kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kukopeshwa kwa wanufaika pasipokuwa na sababu za msingi.

Halmashauri zilizokuwa na bakaa ya muda mrefu katika benki za biashara ni za wilaya za Mpwapwa (Sh. 108,703,450) na Nyasa (Sh. 47,530,700).

Anataja dosari nyingine katika mikopo hiyo ni kutoshirikishwa kwa wataalamu wa usimamizi wa mikopo katika mchakato wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo.

"Nilibaini kuwa uhakiki wa vikundi vilivyoomba mikopo ulikuwa haufanyiki kabisa kabla ya mikopo kutolewa. Hii ni kutokana na ukosefu wa utaalamu wa kufanya uhakiki unaostahili katika mikopo.

Anasisitiza mamlaka za serikali za mitaa kufanya tathmini kabla ya kutoa mikopo na kuweka juhudi zaidi katika kukusanya madeni ambayo bado hayajalipwa.

Aidha, TAMISEMI ianzishe hatua madhubuti za kurejesha mikopo kwa kuhusisha wataalamu wa usimamizi wa mikopo ambao watahimiza uzingatiaji wa urejeshaji wa mikopo kwa hiari ili kufikia ukuaji endelevu wa mfuko.

"Ninapendekeza kuwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI itumie benki za serikali au wataalamu wa usimamizi wa dhamana na uwekezaji kama vile Benki ya Maendeleo na Benki ya Biashara Tanzania katika kuongeza ufanisi kwenye kutoa, kufuatilia na kusimamia urejeshwaji wa mikopo na kwa kuzingatia gharama nafuu ya uendeshaji.

USULI NA HISTORIA

Inaporejewa historia ya mikopo hiyo, inaonyesha kwamba, mwaka 1993 serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilianzisha Mfuko wa Fedha wa Maendeleo kwa Wanawake na Vijana ili kuwainua kiuchumi ambao wengi wao hawakidhi vigezo vya mikopo inayotolewa na taasisi za fedha kutokana na ukosefu wa dhamana.

Kwa wakati huo, mikopo hiyo ya uwezeshaji ilitolewa asilimia tano kwa wanawake na asilimia tano kwa vijana.

Mwaka 2019, serikali kupitia Bunge, ilirekebisha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290 (iliyorejewa 2019) kwa kuongeza kifungu cha 37A mahususi kwa ajili ya kuwezesha mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Vilevile, Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, 2019 (Tangazo la Serikali Na. 286 la 5/04/2019) zinataka mamlaka zote za serikali za mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani ili kutoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Madhumuni ya mfuko huo ni kuongeza uwezeshaji kiuchumi kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kufanya shughuli za kiuchumi ili kuboresha kiwango chao cha maisha.

SAMIA ASHTUKA
Baada ya kupokea ripoti mpya ya CAG Jumatano ikionyesha kwa mwaka 2021/22 Sh. bilioni 88 zilizotolewa na halmashauri kama mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu hazikurejeshwa, alisema kadhia hiyo inasababishwa na utaratibu mbovu wa utoaji mikopo hiyo na ufuatiliaji hafifu.

Marekebisho yanayotajwa na Rais Samia yanahusu kubadili mfumo wa utoaji mikopo hiyo kutoka halmashauri ili kazi hiyo ifanywe na benki ambayo itakuwa imeteuliwa na serikali kusimamia jambo hilo, ushauri ambao ulitolewa na CAG katika ripoti ya mwaka 2020/21.

Chanzo: Nipashe
 
Huo upotevu, CAG wa nyakati Ile alishindwa kuuanika??.


Kwan Ex CAG Assad yeye mpaka anaondolewa uCAG 2019, anasemaje ?.
 
wanaitwa STUPID tu na mambo yanaisha. Kibaya zaidi juzi nikaona Mwenyekiti wa mafisiemu Samia Hangaya Hassan akimuagiza Rais na Sirikali yake Samia suluhu hassaan awashughulikie wabadhirifu , nilicheka sana ila tuna kazi ngumu sana mbele huko.
 
Pia anaishauri Ofisi ya Rais - TAMISEMI ianzishe hatua madhubuti za kurejesha mikopo kwa kuhusisha wataalamu wa usimamizi wa mikopo ambao watahimiza uzingatiaji wa urejeshaji wa mikopo kwa hiari ili kufikia ukuaji endelevu wa mfuko.

Yaaani urejeshaji uwe wa HIARI,hivi huo ni USHAURI kweli,asiporejesha je huyo mkopaji si ndio yaleyale?
Kwa nini mkopaji asilazimishwe kurejesha???
 
Screenshot_2024-03-28-15-56-53-1.png
 
Back
Top Bottom