Biteko: Ukuaji wa Sekta ya Madini kwa mwaka 2022 umekuwa asilimia 10.9 ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 9.4 mwaka 2021

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

1698321220280.png

Dkt. Biteko amebainisha hayo leo Oktoba 25, 2023 akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIF) wa Mwaka 2023 jijini Dar es Salaam.

“Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa Sekta hii inachangia asilimia 10 au zaidi katika pato la Taifa ifikapo 2025,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa mchango wa Sekta ya Madini umekuwa ukiongezeka kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.1 mwaka 2022.

Kwamba ukuaji wa Sekta ya Madini kwa mwaka 2022 umekuwa asilimia 10.9 ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 9.4 mwaka 2021.

“Ni matumaini yetu Sote ifikapo mwaka 2025, Sekta ya Madini itafikia lengo la mchango wa asilimia 10 kwenye pato la Taifa,” amesema Dkt. Biteko na kuongeza, “Mchango wa Sekta ya Madini katika fedha za kigeni kwa mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi umeendelea kuimarika kutoka dola za Marekani 1.6 bilioni sawa na asilimia 37 mwaka 2018 hadi dola za Marekani 3.4 bilioni sawa na asimilia 47 mwaka 2022,”.

1698321262031.png


Ameeleza kwamba kwa upande wa mauzo ya bidhaa zisizo asilia (non-traditional), sekta ya Madini ilichangia asilimia 50 mwaka 2018 na asilimia 56 mwaka 2022.

Amesema Takwimu zinaonesha kuwa fursa za ajira zimeongezeka katika sekta ya madini kutoka ajira 7,151 mwaka 2020 hadi ajira 16,462 mwaka 2022 sawa na ongezeko la zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miaka mitatu kwa migodi mikubwa na ya kati pekee.

Kwamba kwa upande wa uchimbaji mdogo wa madini, zaidi ya Watanzania milioni 1.5 wanashiriki katika shughuli za uchimbaji mdogo.

Dkt. Biteko amebainisha kuwa ununuzi wa bidhaa za ndani umeongezeka kutoka manunuzi ya dola za Marekani milioni 715.3 mwaka 2019 hadi dola za Marekani trilioni 1.1 mwaka 2022.

Amebainisha kwamba hiyo inaonesha namna Sekta ya Madini ilivyokuwa muhimu katika uchumi wa nchi.

“Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi. Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali inaboreshwa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji,” amesema Dkt. Biteko.

1698321298635.png

Amesema hadi sasa baadhi ya migodi mikubwa ikiwemo Geita Gold Mines Limited (GGML) na STAMIGOLD Biharamulo Mine ambayo ilikuwa haina umeme kwa muda mrefu sasa imeunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa.

Pia, amesema migodi zaidi ya 350 ya wachimbaji wadogo imeunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji na kurahisisha shughuli mbalimbali za migodi.

Kwamba Serikali inafahamu kuwa bado kuna mahitaji makubwa ya migodi kuunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa.

Napenda kuwahakikishia kuwa, kadri tunavyoimarisha uwezo wetu wa kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme nchini. Hivyo watahakikisha migodi yote mikubwa na midogo inaunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa.

Sambamba na hilo, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa na barabara zinazounganisha maeneo yenye migodi na shughuli mbalimbali za madini ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoingia na kutoka migodini.

“Kwa mfano, kwa sasa Serikali inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa barabara kutoka kijiji cha Paradiso hadi Kitai Mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilomita 22 kwa kiwango cha lami na barabara ya Kabulo-Kiwira yenye urefu wa kilomita 7 mkoani Songwe kwa kiwango cha changarawe,” ameongeza.

Amesema barabara hizo zitakapokamilika zitarahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka migodini kwenda kwa watumiaji wa ndani na nje ya nchi.

1698321320590.png


Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wachimbaji wadogo nchini katika kutoa ajira, kuboresha kipato kwa mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Kwamba kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwezesha shughuli za uchimbaji mdogo kufanyika kwa tija ikiwa ni pamoja na kununua mitambo mitano (5) ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

1698321346420.png


Amesema Mitambo hiyo itawasaidia wachimbaji wadogo kufanya uchorongaji nakupata taarifa za uwepo wa mashapo ya madini kwa gharama nafuu.

1698321377099.png
 
Back
Top Bottom