Barua ya wazi kwa Tundu Lissu

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
Mhe Tundu Antipas Lissu,

HABARI za siku nyingi? Pole na hongera kwa mapambano! Hakika unastahili sifa ya kuitwa mpambanaji. Katika kuzungumzia mustakabali wa kisiasa nchini, wewe ni mtu muhimu sana na nimeona nijaribu ikiwezekana kusikia zaidi kutoka kwako kwa mtindo wa ‘dialogue’ kutokana na masuala ya msingi yanayotukabili kama taifa.

Nimejitahidi kwa kiasi changu kufuatilia historia yako na sina budi nianze na tukio moja nililosoma katika maktaba kuu zamani kidogo. Tukio hilo lilihusiana na umuhimu wa kuwa na mfumo wa vyama vingi ambako ulijitahidi kupaza sauti yako baada tu ya kumaliza masomo ya sekondari katika mazingira ambayo hayakuwa rahisi. Nafahamu pia ulijiunga mapema sana na chama cha NCCR ila sijasoma popote kama ulipata kuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho.

Ukiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) uliendeleza harakati za mageuzi hadi kugombea ubunge bila mafanikio. Hukukata tamaa na ulijikita kwa muda kwenye harakati kupitia masuala ya kisheria. Sijui ni lini hasa ulijiunga na Chadema lakini nafahamu Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ndiye aliyekushawishi na hatimaye mwaka 2004 ukawa mwanasheria mkuu wa chama hicho hadi sasa.

Mwaka 2010 ulishinda ubunge na kazi yako ni dhahiri kwa wengi.

Ni vyema nikukumbushe kwamba miezi michache baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, nilihudhuria mdahalo kati ya Chadema na CUF uliofanyika katika hoteli ya Royal Palm wakati huo, sasa Serena, ambako washiriki walikuwa ni Mbowe na wewe kwa upande wa Chadema na kwa upande wa CUF walikuwepo Hamad Rashid na Shaweji Mketo.

Ulikuwa ni mdahalo safi na kwa bahati mbaya baadhi ya wanachama wa CUF walizusha vurugu za ajabu kiasi cha kusababisha mdahalo usiishe kwa mpangilio uliotakiwa.

Ni vyema niongeze kwamba kati ya mwaka 2013 na 2014, nilikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria hafla ya kuichangia Chadema katika hoteli ya Serena. Wakati huo chama chenu kulikuwa na kitu kijulikanacho kama Movement for Change (M4C). Mbunge mmoja mashuhuri wa chama chenu aliniomba si tu nishiriki bali niwahamasishe watu wengine wajitokeze. Nilifanikwa kuongozana na watu wanne na kutoa mchango kwa niaba ya wote kwa kila sahani. Tukio hilo lilirushwa moja kwa moja na Star Tv.

Nikiri tukio hilo la uchangiaji lilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria na kushuhudia kwa uwazi jinsi gani Chadema kinavyosimamia mambo yake. Kwa kweli kulikuwa na maneno ya kuhamasisha kama ile nukuu murua ya Mahatma Gandhi inayosema: “Be the change you wish to see in the World”.

Juhudi kubwa iliendelea kufanyika ya kuwachangisha watu fedha zaidi ya ile tuliyopanga. Ikafikia mahali, maneno yakazungumzwa kufananisha mapambano hayo na ya yale ya kupata uhuru wa nchi ambapo watu walitoa hata “thumni”.

Sina budi kusema baada ya siku ile, vijana wa Chadema waliendelea kutuhimiza sana kutoa michango bila kuchoka. Kwa namna fulani nilijikuta hapo najiuliza maswali kadha wa kadha kwa msingi wa wasiwasi kidogo juu ya mustakabali wa Chadema.

Kuna usemi wa kizungu kwamba vitu vidogo vinakupa picha ya yale makubwa. Sababu ya kusema hivyo ni kwamba kwa uzoefu wangu wa nyanja mbalimbali, masuala ya michango ni nyeti sana. Kwanza, si jambo la kiafya kuhimiza michango kila kukicha kwa watu vinginevyo kuna hatari ya pesa kutumika vibaya.

Mambo makubwa yanaweza kufanyika kwa uchache na kuleta matokeo mazuri sana. Kwa mfano, utakuwa umepata kuisikia Bank M Dar Rotary Marathon. Rotary Marathon imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa na hufanyika kila Oktoba 14, siku ya kukumbuka kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Ni shughuli kubwa kabisa na mara nyingi mgeni rasmi amekuwa ni Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Nakumbuka kuna kipindi kiongozi mmoja wa Rotary Club aliniomba kusaidia kutoa mchango kila mwaka kadri ya uwezo wangu. Nilikubali na aliendelea kunieleza kwamba nikiweza kutoa kiasi kadhaa, basi jina langu litaonekana hadi kwenye tovuti yao na kadhalika. Yote ni ishara ya kumchukulia mchangiaji kama mdau muhimu. Bahati mbaya sikuwa na uwezo wa kuchangia kiasi kikubwa ila nikajikuta nalinganisha mazingira ya Rotary Marathon na Chadema.

Kufuatia shughuli ya M4C, nilitarajia angalau wachangiaji wenu maalum kuandikiwa barua kama ishara ya shukrani na kutambuliwa kwao. Huu ni utaratibu wa kawaida kwenye taasisi nyingi makini. Wasiwasi wangu ulikuwa kwamba kama hata barua ya shukrani ni ngumu, maana yake ni kwamba chama hicho pengine si shirikishi inavyopaswa. Kwenye masuala makubwa kabisa ya chama maana yake kutakuwa na usiri wa hali ya juu kama tulivyokuja kuona kwenye uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho ambaye alisimama kwa niaba ya UKAWA. Kwenye hili nadhani nafanana na mzee Mustafa Sabodo aliyejitolea bila woga kuisaidia Chadema ila leo ameikatia tamaa Chadema.

Mheshimiwa Lissu, nadhani utakumbuka mwaka 2015, wakati suala la mgombea urais wa muungano wa vyama vyenu vinne likipamba moto, tulikutana kwa muda mfupi katika hoteli ya Colosseum na nilijaribu kukufikishia kwa kadri ya uwezo wangu jambo la kutafakari kabla ya uamuzi kufanyika. Siku ile ulionyesha imani asilimia 100 kwa Dk. Wilbrod Slaa. Ipo siku naamini ukiachana na siasa na pengine kuamua kuandika kitabu juu ya maisha yako ya mapambano, utaeleza jinsi gani ulipigwa na butwaa na uteuzi wa Edward Lowassa kiasi cha kutoamini, hivyo kujificha kwa muda pengine ukitafakari.

Naamini uteuzi huo wa Lowassa lilikuwa mtihani mgumu mno kwako na baadhi ya wenzako. Nimejiuliza mara nyingi sana, hivi Katiba ya nchi ingekuwa inaruhusu mgombea huru, tungekuwa na hali gani tofauti ya kisiasa nchini? Pengine jambo zito kama hilo la kumteua Lowassa lingesababisha baadhi ya watu ndani ya chama chako kujitoa kutokana na kuminywa nafasi ya kuzungumza?

Sina budi niseme kutoruhusiwa kwa mgombea binafsi ni miongoni mwa mambo ya hovyo kufanyika nchini na chama tawala cha CCM. Lakini pamoja na CCM kuipinga hoja ya mgombea binafsi miaka yote na kujidai kuiweka kiujanja kwenye Katiba Pendekezwa, nilitarajia Lissu kwa kumbukumbu yako ya upambanaji, ungekuwa umelivalia njuga kweli kweli! Haitoshi tu kusema kwamba mliipendekeza pamoja na mambo kadhaa kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwenye mazungumzo yenu Dodoma. Hili ni jambo la msingi kwa binadamu, hasa ikizingatiwa hali ya umungu mtu unaofahamika ndani ya vyama vingi vya siasa.

Twende sasa kwenye tukio la hivi karibuni ambapo ulimshutumu Rais John Magufuli kwa jinsi anavyoendesha nchi kwa mtindo wa kidikteta. Katika kulitazama hili kuna haja ya kupanua wigo. La kwanza, ningependa kumrejea Mwalimu Nyerere, japo naamini kutokana na matamko fulani uliyoyatoa bungeni juu ya Nyerere, wewe ni miongoni mwa watu ambao pengine walimchukulia Nyerere kama dikteta.

Hiyo ni haki ya mtu kufikiri hivyo na kwa kweli kuna mengi sana kuhusu Mwalimu ambayo kama nchi hatujayafanyia tathmini kwa mtindo wa kujisahihisha kama alivyotuasa tufanye. Nakumbuka mwanahabari nguli, Jeneral Ulimwengu, aliwahi kuandika kwamba watawala wetu wana mambo ya kutosha ya kuelezea utawala wa Nyerere ulivyofanya vibaya kwenye maeneo kadhaa lakini hawathubutu kutokana na kushindwa kuyaelezea pia yale mazuri ya Nyerere.

Na kuna wakati nilimwuliza Ulimwengu kwamba hivi Nyerere alipouita mfumo wetu wa chama kimoja kuwa “Demokrasia ya Chama Kimoja”, ilikuwa sahihi au ilipaswa kujulikana kama ilivyokuwa Kenya kipindi fulani kuwa ni “Udikteta wa Chama Kimoja”? Akanijibu tu kwamba jibu hilo litategemea mtazamo wa mtu binafsi.

Lissu, natamani Watanzania wafurahie mjadala kuhusu historia ya kisiasa ya nchi yao kutokana na kwamba Nyerere alikuwa mtu ambaye ameandika sana kuhusu mfumo unaotufaa kama nchi na vile hata mwaka 1965 kufuatia mabadiliko ya Katiba, aliweka wazi kwamba Katiba inampa madaraka makubwa kiasi cha yeye kuweza kuwa dikteta.

Sasa kama kweli Nyerere alikuwa dikteta haikuchukua muda wa miaka miwili kama ukilinganisha na kipindi alichokaa Magufuli Ikulu mpaka sasa. Kuna masuala mengi hadi kufikia mtu kuwa dikteta.

Sehemu niliyotaka sasa kumnukuu Nyerere ni hotuba ya mwezi Agosti mwaka 1990, akiwa anastaafu uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi: “Lakini ni vizuri nikasema pia kwamba kwa maoni yangu hatuwezi tukaamua kuacha mfumo wa demokrasia ya chama kimoja, tukajaribu mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kwa matumaini ya kwamba tukikuta kuwa mfumo huo hautufai, basi tutarudia tena demokrasia ya chama kimoja.

“Tutajidanganya, haiwezekani na ni vigumu kabisa. Ukimwacha mkeo ukaoa mwingine, na ukagundua kuwa huyu wa pili ni balaa, ni vigumu kumrudia mkeo wa kwanza. Demokrasia ya vyama vingi ikitushinda, mfumo ambao ni rahisi kufuatia utakuwa ni udikteta wa mtu mmoja au utawala wa kijeshi. Hiyo ni sababu nyingine muhimu ya kutofanya uamuzi kwa pupa. Inafaa tukajipa muda wa kutosha kuelewa athari zinazoweza kutokea kutokana na uamuzi wowote tutakaoufanya. Si vema kuruka bila kuwa na hakika utaangukia wapi!

Imani yangu hapo ni kwamba Mwalimu alipotoka kidogo. Hatua ya mtu kuwa dikteta si mzaha. Mara nyingi wanakuwa na mizizi kweli kwenye siasa. Alipaswa kujikita zaidi si kwenye “udikteta wa mtu mmoja bali ubabe wa mtu mmoja”. Kuna tofauti hapo. Wababe ni wengi hata kama wanajifanya wastaarabu. Mkiwagusa kidogo kwenye maslahi yao ya kisiasa wanabadilika kabisa.

Kilicho kweli kabisa ni kwamba demokrasia ya vyama vingi ni kama imetushinda kutokana kwanza na kutokuwepo na demokrasia ndani ya vyama vyenyewe. Hapo sasa ni ubabe mtindo moja, na hasa ukizingatia hulka ya Magufuli ambaye alishawahi kuwatia ndani bila sababu ya maana waandishi wa gazeti fulani akiwa waziri.

Kwa maoni yangu, Magufuli si dikteta. Na njia ya kumkabili Magufuli ni rahisi sana kutokana na kwamba mara nyingi historia huonyesha wababe kuwa waoga pia. Wala hukuhitaji kugombea uongozi wa ckhama cha Wanasheria Tanganyika au TLS ili upate nguvu zaidi ya kumkabili.

Tena ninachokijua kuhusu chama kama hicho katika mataifa mbalimbali ni kwamba, ni vizuri zaidi mtu akiwa Rais wa chama hicho ndio aanze maandalizi ya kuwa mwanasiasa akitaka na si mtu umeshafikia hatua ya kuwa mbunge na unashuka chini. Mfano mzuri sana ni mwanasheria na mwanasiasa mashuhuri wa Kenya, Paul Muite.

Katika kupigania mabadiliko ya msingi ya kisiasa, silaha kubwa ni kutambua bila shaka wala woga udhaifu na nguvu ya viongozi wa upinzani. Kama alivyosema Jenerali wakati mmoja, tuwe kama Wakurya na tutasonga mbele. Na vilevile tuache kutoa mifano ya nchi fulani bila kuijua barabara. Mfano katika kampeni ya uchaguzi mkuu, Lissu ulifikia hatua na baadhi ya wenzako kutoa mfano wa nchi moja au zaidi ya moja zilizofanikiwa kuondoa vyama vikongwe madarakani. Nilishangazwa na wepesi wa maelezo.

Mathlan, tuitazame nchi ya Kenya. Hatua ya kufikia kumpata mgombea mmoja haikuwa rahisi hata kidogo. Katika kitabu kilichoandikwa hivi karibuni na Makamu wa Rais wa zamani, Moody Awori, ambaye alikuwa pia Mwenyekiti wa kikao cha juu cha uamuzi wa muungano wa NARC, anaeleza jinsi gani wagombea urais walikuwa wengi na wenye sifa na wote walishirikishwa kwenye kikao hicho. Kazi ya kumpata Kibaki ilizingatia mambo mengi sana.

Nitafafanua kidogo. Ukiangalia kwa haraka, Mzee Kibaki ni mtu ambaye historia yake ni ya kutukuka tangu anasoma Chuo Kikuu cha Makerere. Yaani ni mtu ambaye alionekana kama asingeingia kwenye siasa ambayo ilikuwa wito wakati huo, basi kwenye taaluma yake ya uchumi angefika mbali sana, mfano kuwa hata Rais wa Benki ya Dunia.

Maneno haya si yangu bali yalipata kutamkwa na mtu aliyewahi kuwa Rais wa Benki ya Dunia huko nyuma, Robert McNamara, aliyetamka takribani miaka arobaini iliyopita kwamba “Kibaki alikuwa miongoni mwa watu wachache sana wenye upeo wa juu sana kuhusu masuala ya uchumi barani Afrika”.

Jarida maarufu duniani la Time, lilimtaja zamani sana kuwa miongoni mwa watu 100 duniani ambao wangefika mbali kwenye uongozi. Vilevile huyu ni mtu ambaye alitumikia nchi yake kama Makamu wa Rais vizuri na bila doa. Na alifikia mahali alijitoa KANU na kuanzisha chama chake cha DP. Na kutokana na ushindani mkali nchini Kenya, ilimchukua mara tatu tu hadi anafanikiwa kuwa Rais. Wakati wote huo hakuyumba na alizidi kujijenga miongoni mwa makundi mbalimbali ya kuheshimika. Niseme tu pamoja na sifa zote za Kibaki, alipata chini ya 65%. Angekuwa mtu legelege ingekuaje hapo?

Haya tukienda nchini Zambia, Frederick Chiluba katika miaka yake 17 ya uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Zambia (ZCTU), alikuwa mtetezi mkubwa wa wafanyakazi kiasi cha kuwekwa kizuizini na Kaunda mwaka 1981, akituhumiwa kuchochea madai ya hali bora ya wafanyakazi. Si chini ya mara mbili serikali ya Kaunda ilijaribu sana kumpatia nafasi serikalini bila mafanikio. Kwa kweli alijitahidi mno kuonyesha msimamo thabiti kwenye masuala ya msingi.

Haishangazi basi kwamba Waziri maarufu wa zamani, Vernon Mwaanga, anamwelezea vizuri sana Chiluba kwenye kitabu chake walipokutana kwa mara ya kwanza mwaka 1974, mjini New York, kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Anaeleza jinsi alivyovutiwa mno na uelewa wake wa masuala ya msingi. Anasema vilevile kwamba alikuwa mtu aliyesimamia nidhamu, kanuni na utekelezaji wa ratiba juu ya mambo ya umma.

Niongeze kwamba kufuatia kuruhusiwa kwa vyama vyingi mwishoni mwa 1990, chama cha MMD kilichagua Halmashauri Kuu ya Kwanza, kikiongozwa na Chiluba kama Rais na hayati Levy Mwanawasa, Makamu wa Rais. Mwenyekiti wa Taifa alikuwa Elias Chipimo na Katibu Mkuu alikuwa Brigedia Jenerali Godfrey Miyanda, kutaja tu majina machache maarufu. Ni vizuri kusema kwamba kwenye nafasi ya Makamu wa Rais, Mwanawasa aliwashinda washindani wake wawili, Luteni Jenerali Christon Tembo na Baldwin Nkumbula.

Zaidi ya hilo, lilipofika suala la mgombea urais, wanachama wazito walichuana kama Arthur Wina, aliyekuwa Waziri wa kwanza wa Fedha wa taifa hilo na Humphrey Mulemba ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais na Chiluba mwenyewe ambaye aliibuka mshindi. Kwa kweli jinsi walivyochuana ilikuwa hatua ya kupongeza. Kilichofuata kilikuwa ushindi wa kishindo kwa MMD dhidi ya chama tawala cha UNIP.

Lissu, ushindani ni jambo muhimu sana ili kuwajenga watu. Hapa nyumbani tuliambiwa kwamba Lowassa aliingia Chadema na masharti mengi ikiwa ni pamoja na kutoshindanishwa na mtu yeyote. Hili lilikuwa jambo la kurudisha nyuma sana maendeleo ya Chadema na demokrasia kwa ujumla wake – chama ambacho kinajitambulisha kwanza kama chama cha kidemokrasia.

Nakumbuka mwaka 2005, chini ya Mwenyekiti mpya Freeman Mbowe, chama hicho angalau kilionyesha dalili ya kutoa changamoto ya aina yake kwa CCM. Kwenye kitabu cha Mzee Edwin Mtei, anaeleza kwamba CHADEMA kiliamua kuwa na uwazi wa hali ya juu wa kidemokrasia katika kumpata mgombea urais kwa mara ya kwanza. Iliamuliwa kwamba mwanachama yeyote ataweza kugombea urais na walifika sita. Utaratibu ulikuwa kwamba wagombea hao wote waliokuwa wamejitokeza kugombea urais watembelee kanda sita na kuhutubia mikutano mikuu ambako watajieleza namna gani watatekeleza ilani ya chama endapo watachaguliwa. Kati ya hao sita, walikuwemo pia wanawake wawili.

Wagombea watatu wanaume walijitoa kabla ya mkutano wa mwisho na kuachia wanawake wawili, Anna Komu na Chiku Abwao, pamoja na Mbowe ambaye alipata zaidi ya 80% ya kura. Mgombea mwenza naye alipatikana siku hiyo. Haya twende 2010. Upatikanaji wa Dk Slaa ulikuwa kwa mtindo wa kushtukiza kukaribia uchaguzi. Alikuwa amejiandaa kurejea bungeni. Mwaka 2015 hali ya usiri ilitanda zaidi na zaidi.

Chama chochote pia ambacho hakiko tayari kuchunga hata kauli za viongozi wake kana kwamba wananchi watasahau tu ni tatizo. Mfano mlipiga kelele sana kuhusu kuwachukua makapi wa CCM. Ukiacha hiyo kuna maneno makali yaliyotamkwa na Mbowe juu ya Lowassa kuelekea mchakato wa kumchagua mgombea urais wa CCM. “Lowassa ni dhaifu sana, amekaa serikalini zaidi ya miaka 30 na hakuna maendeleo yanayoonekana ndani ya serikali zaidi ya kila siku wizi na ubadhirifu kuongezeka. Hao wanaomtaka Lowassa ni wale wanaojua watanufaika binafsi akipita kwenye urais, lakini kimsingi huyu jamaa ni dhaifu sana na hafai kuongoza Tanzania ya sasa yenye changamoto lukuki. Wapambe wake wanasema Lowassa si msemaji bali mtendaji, hivi nani atakubali porojo hizo wakati tunajua akiwa Waziri Mkuu hakufanya lolote kukemea wizi, ubadhirifu na ufisadi? Richmond ilikuja akiwa wapi?

“Sina ugomvi wala simchukii Lowassa binafsi, lakini ni vema hawa wanaosema ni mtu wa maamuzi magumu wakaueleza umma wakati watendaji wa serikali wakitafuna mabilioni ya fedha, CCM wakipitisha Katiba Inayopendekezwa ya hovyo pale Dodoma, yeye alisema au kufanya nini?”

Nchi hii inalilia sana mabadiliko makubwa. Jibu lako na la wenzako kuhusiana na uchaguzi mkuu uliopita ni kwamba Lowassa alifanikiwa kupata kura takriban milioni sita kabla ya suala la wizi. Hii haitoshi. Mbona basi hata Mrema alizoa kura nyingi na pengine isingekuwa Nyerere kuzunguka mikoani matokeo yangeweza kuwa tofauti?

Nihitimitishe kwa kusema kwamba suala la kufanikisha ukombozi wa pili ni suala rahisi ila kuna haja ya kujipanga upya kabisa! Kuna viongozi walitamka kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwamba UKAWA isiposhinda basi itachukua muda mrefu sana hadi upinzani ufanikiwe. Leo hii hakuna kuachia ngazi. Wengi hawazungumzi tena suala la Katiba Mpya na ufisadi wa CCM humo.

Nimeshtuka sana juzi kumsikia Lowassa akizungumzia miaka miwili yake nje ya CCM huku akisema: “Yapo mambo mazuri anayofanya Rais Magufuli, aungwe mkono. Na kwa kiasi kikubwa anafanya mazuri, lakini hayajatoka mbinguni, bali ni wajibu wake.”

Ndugu yangu Tundu Lissu, si ulitaka nchi inyimwe msaada kutokana na ukandamizwaji wa Magufuli? Sasa inakuaje tena kiongozi mwingine anaongea lugha ya kumsifia mkuu wa nchi? Matokeo yake unakuta wananchi wengine wanaona kinachoendelea tu ni uCCM A na B.

Chanzo
Raia Mwema
 
Nimependa bandiko hili kwani lina uchambuzi wa kina. Mimi ni mshabiki wa kutupwa wa cdm na huwa sisiti kukiri na kusema kama kuna mahali cdm tulifanya kosa la karne ni kumchukua Lowassa na kisha kumpa nafasi nyeti na kubwa sana ya kugombea urais. Nakumbuka cdm mwanzo tulipata fundisho kutoka kwa Shibuda kuhusu kuwachukua wanaccm tena dakika za mwishomwisho na kisha kuwapa nafasi ya kugombea uongozi. Nikadhani tutakuwa tumejirekebisha, kumbe kama ni kosa sasa ndio tukaamua kulifanya kubwa zaidi kwa Lowassa.

Leo hii cdm inaonekana kupoteza haiba yake kwa sababu ya Lowassa, hatuna ajenda ya uhakika wangalau ya kufuta kosa la kumpokea Lowassa. Kibaya kabisa mitazamo ya Lowassa isiyo na mashiko ndio inayogeuzwa kuwa pia mitazamo ya chama japo sio rasmi. Kingine kinachonitisha zaidi wapenzi na wanachama wa cdm hatukemei hali hii huku tukiangalia chama kikinajisiwa kwa mitazamo binafsi. Mimi kwa hili la Lowasa kuwa chamani sintokaa kimya kwani ndio kikwazo kwa cdm kwa sasa. Sina chuki binafsi na Lowassa lakini sio mtu sahihi kwenye uongozi wa cdm yetu.

Cc: Tindu Lissu, John Mnyika, Ephata Nanyaro,
 
Hamna hoja hapo! kauli za kisiasa kwenye chama hasa zile zinazotolewa na watu binafsi. Kama ungekuwa makini sana kwenye kauli ungeogopa zile kauli zinazotolewa na viongozi wa serikali kwani ndio zina athari kubwa katika uendeshaji nchi.
Kinana na Polepole au Lissu na Lowassa wakitofautiana kauli madhara yake yako ndani ya vikao vya chama na wanachama wake lakini sio nchi.
Ila kauli kama za Makamu wa Rais kuwa Watoto wa kike wakipata mimba wanapaswa kufikiriwa kupta elimu tena baada ya kujifungua, huku Rais akisema "katika utawala wangu ukipata mimba hakuna kusoma tena, sifundishi wazazi mie"
Hizo ndio kauli zenye utata kabisa na kasoro kubwa kwenye kuendesha nchi.
Mleta mada angejikita huko kwanza.
 
Mhe Tundu Antipas Lissu,


Nimeshtuka sana juzi kumsikia Lowassa akizungumzia miaka miwili yake nje ya CCM huku akisema: “Yapo mambo mazuri anayofanya Rais Magufuli, aungwe mkono. Na kwa kiasi kikubwa anafanya mazuri, lakini hayajatoka mbinguni, bali ni wajibu wake.”

Ndugu yangu Tundu Lissu, si ulitaka nchi inyimwe msaada kutokana na ukandamizwaji wa Magufuli? Sasa inakuaje tena kiongozi mwingine anaongea lugha ya kumsifia mkuu wa nchi? Matokeo yake unakuta wananchi wengine wanaona kinachoendelea tu ni uCCM A na B.

Chanzo
Raia Mwema

Mkuu hata mimi nilikuwa na swali kama lako,Lakini nikagundua Lowasa bado anahitaji sifa/kuugwa mkono na C.C.M... Hivyo hahitaji kuwa mpinzani wa kusema mambaya ya kiongozi ila anahihitaji kutambua utendaji kazi wake Lakini kwa kuonesha yeye unaweza Fanya mazuri zaidi yake na kwa njia rahisi sana

mwanza kwetu
 
Maada ngumu sana hii, ila weng CDM huwa wanafuata mkumbo na wshindwa kuwaelewa watu wao

Lissu ni mkubwa sana mno zaidi kuliko TLS, kugombea TLS kulikuwa na maana ya yeye kutojitambua thamani yake na potential zake

CDM kwa sasa inapaswa iwe chini ya Lissu na hili nililiata kusema hapa

Lissu awe Mwenyekiti CHADEMA na Lema awe Katibu

Mengine yote ya kuwa kigeugeu , kuwa roporopo na kuwa confused ni kwa sababu hana platform nzuri na chama chake anakijua yeye!!

tunasubiri 2021 wakija na maneno ya kuwa tutaingia ikulua 2025!!! ha ha

mpaka akili ziwaingie
 
Tindu lisu leo humu kazi anayo uzi wa 3 huu leo unaamshiwa

Sent using Jamii Forums mobile app
Ujue hiyo ndiyo agenda ya leo waliyopewa Lumumba. Wao kusikia Bill Gates katoa msaada wa Bilion777 wanaona kama pigo kwa Lissu wakati huo ni msaada wa kibinadamu ambao umetoka kwenye taasisi binafsi na unaenda moja kwa moja kwa walengwa bila serikali kuingiza mikono yake michafu humo
 
Ujue hiyo ndiyo agenda ya leo waliyopewa Lumumba. Wao kusikia Bill Gates katoa msaada wa Bilion777 wanaona kama pigo kwa Lissu wakati huo ni msaada wa kibinadamu ambao umetoka kwenye taasisi binafsi na unaenda moja kwa moja kwa walengwa bila serikali kuingiza mikono yake michafu humo
Kweli mkuu mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali akae tu macho

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom