Bado kuna utata mkubwa kuhusu demokrasia ya kweli Barani Afrika, GAZETI LA KULIKONI - JUNI 10, 2011

WISDOM SEEDS

JF-Expert Member
Jun 1, 2011
841
282
Na Bishop J. Hiluka

Dar es Salaam


RIPOTI iliyotolewa na shirika moja linaloheshimiwa sana nchini Afrika Kusini inayoonesha kuwepo
orodha ya wapiga kura hewa milioni 2.6, kwa dhamira ya kuendeleza udanganyifu, katika daftari
la kudumu la wapiga kura nchini Zimbabwe, inatuthibitishia kuwa demokrasia ya kweli barani Afrika
bado ni kitendawili.



Orodha hiyo inaashiria kuwepo zaidi ya watu elfu 41 walio na umri wa zaidi ya miaka 100 - hii ikiwa
ni mara nne zaidi ya idadi ya watu hao nchini Uingereza, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya watu na
muda mrefu wa kuishi ikilinganishwa na Zimbabwe.



Hii imekuja wakati Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, akiitisha uchaguzi ufanyike mwaka huu, huku
mpinzani wake na Waziri Mkuu katika serikali ya mseto, Morgan Tsvangirai, akisema kuwa uchaguzi huo
unapaswa kuandaliwa mwaka 2012 baada ya katiba mpya kuidhinishwa ili kuhakikisha kuwa kuna uhuru
na haki.


Wastani wa umri wa kuishi miongoni mwa raia wa Zimbabwe umeteremka hadi miaka 49, lakini kumeripotiwa
kuwa na wapiga kura 41,100 wanaodaiwa kuwa na zaidi ya umri wa miaka 100.


Serikali za Kiafrika zimekuwa na tabia ya 'kuchakachua' ili ziendelee kutawala, na kuna uwezekano kuwa
nchi nyingi za Afrika pamoja na kujidai kuwa na chaguzi huru huwa zinatawaliwa kwa mabavu na si kwa
ridhaa ya wananchi, kutokana na uchakachuaji kama huu wa kura.



Naamini kwamba kwa mustakabali wa nchi yoyote, vyama vyote vya siasa vina haki sawa mbele ya katiba
ambayo pia inawapa wananchi haki na uwezo wa kuchagua chama chochote kati ya hivyo vilivyopo na
kukiweka madarakani.



Ni kutokana na ukweli huo, sheria na kanuni za uchaguzi zinahitaji kuwepo na mazingira sawa kwa vyama
vyote vinavyoshiriki uchaguzi. Mazingira hayo ni muhimu ili kutoa fursa ya mshindi kupatikana katika misingi
ya kidemokrasia ambayo hustawi katika uchaguzi ulio huru na wa haki.



Kwa msingi huo, Serikali nyingi za Kiafrika zinapaswa kujenga utamaduni wa majadiliano ya kina, kukuza na
kudumisha demokrasia pamoja na kuwashirikisha watu katika mchakato mzima wa kujiletea maendeleo yao,
jambo ambalo litasaidia kwa hakika kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano
kati ya watu.



Lakini hii demokrasia, hasa kwa nchi za Afrika ni neno ambalo kwa miaka mingi sasa limekuwa likipita masikioni
mwa watu wengi hali ya kuwa wengi wao hata hawajui maana na uzito halisi wa neno hilo. Kwa lugha rahisi,
neno hili linatafsiriwa kama aina ya uongozi wa watu kwa ajili ya watu. Uongozi huo hupatikana kwa kufanyika
uchaguzi ambao unatakiwa uwe huru na wa haki.

Uchaguzi huru na wa haki unamaanisha kwamba wananchi wagombee nafasi za uongozi wanazotaka ikiwa
wana sifa zinazostahili, wawe na uhuru wa kuongea na wananchi wenzao kuhusu sera na mipango yao pindi
watakapopewa dhamana ya kuwaongoza ikiwa ni pamoja na kuukosoa uongozi uliotangulia bila uwoga wa
aina yoyote kwa kueleza ukweli waziwazi kuhusu 'madudu' yaliyofanywa na uongozi huo na jinsi gani wao
wataweza kufanya marekebisho na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wenzao pamoja na nchi kwa ujumla.



Pia wawe huru kuwachagua viongozi wanaowataka bila woga wala vitisho, wala kununuliwa hati zao za
kupigia kura kwa kilo mbili za sukari na upande wa khanga kutokana na hali zao kimaisha kuwa duni kiasi
kwamba hawawezi hata kukumbuka ni lini ilikuwa mara ya mwisho kwao kunywa chai yenye sukari!

Katika hili nchi za Afrika zinatakiwa kuacha unafiki wa kujifanya zinafuata demokrasia na utawala bora
wakati sio kweli. Sasa wakati umefika kwa viongozi wa Afrika kuyafanya kwa vitendo wanayohubiri na
kuondokana na mfumo wa utawala jeuri na wa kibabe, kwa ajili ya mafao na maendeleo ya watu wa Afrika,
Bara ambalo kwa miaka mingi linaendelea kukumbana na kinzani, migogoro na hali ngumu ya maisha.

Wakati umefika kwa nchi za Kiafrika kujenga na kuimarisha misingi ya haki jamii, ugawaji bora zaidi wa
rasilimali ya nchi, utengenezaji wa fursa za ajira kwa kuboresha mazingira ya wananchi wanaoishi vijijini ili
waweze kutumia ardhi waliyonayo kwa ajili ya maboresho ya hali ya maisha yao. Serikali hizi zina changamoto
ya kuondokana na ubinafsi, uroho wa mali na madaraka, mambo ambayo yamelitumbukiza Bara la Afrika
katika kinzani, migogoro na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Uongozi ni dhamana nzito ambayo inatakiwa iwe kwa ajili ya watu na nchi husika kwa ujumla na si kwa ajili
ya maslahi binafsi ya wachache kama wafanyavyo wengi katika nchi za Afrika, ambao wengi wao wanaingia
madarakani kiujanjaunjanja au kinyume na misingi ya demokrasia.

Pia kuwepo matumizi ya nguvu na vitisho katika nchi ni dalili ya ung'ang'anizi wa madaraka na hivyo kuondoa
maana halisi ya demokrasia! Ung'ang'anizi huu mara nyingi unaashiria kwamba viongozi wetu hawana sifa ya
kupewa dhamana hiyo.



Vitisho na hasa matumizi ya nguvu kwa wapinzani wa serikali ni dalili ya kufilisika kwa ushawishi, kwani
huambatana na kimbilio la vitisho kama njia ya kujihami! Serikali kutumia vitisho kwa watu binafsi si haki,
kwani mtu unayemzidi uwezo huwezi kumtishia kwa sababu hakutishii au hakusumbui.



Bara la Afrika halina budi kusoma alama za nyakati, kwa kutambua mabadiliko ya uongozi, nafasi na dhamana
ya vijana katika kuleta mabadiliko, bila kusahau athari za matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii,
yanayoiwezesha dunia kuwa kama ulimwengukijiji.

source: gazeti la KULIKONI au BOFYA HAPA
 
Back
Top Bottom