ATCL yadaiwa bil 60 ya kukodisha ndege mbovu

dosama

JF-Expert Member
Dec 25, 2010
912
957
Kampuni ya Wallis Trading Inc ya Lebanon, iliyoikodisha Kampuni ya Ndege ya Taifa (ATCL) ndege ya A320, imeanza tena kuibana Serikali kuishinikiza kulipa deni la Dola milioni 40 (Sh bilioni 60).
Deni hilo linajumuisha mkopo na riba fedha zinazotokana na ATCL kukodi ndege ya kampuni hiyo mwaka 2007 ambayo hata hivyo haikufanya kazi.
Ndege hiyo A320-214 muda mfupi baada ya kukodi iligundulika kuwa na matatizo makubwa ya kiufundi hivyo kubaki kwenye matengenezo baada ya kushindwa kuruka.
Wallis inataka kulipwa mara moja bila kupewa visingizio kuwa Serikali haina fedha ama Hazina inahitaji idhini ya Baraza la Mawaziri.
Katika waraka wa kampuni hiyo ulioandikwa Mei 16, mwaka 2012 kwa Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ATCL, Wallis inaikumbusha serikali kuwa mwanzoni mwa mwaka huu ilipanga jedwali la jinsi ya kuanza kulipa mkopo huo kwa utaratibu wa awali unaoanzia na malipo ya Dola milioni 10.67.
Barua hiyo inaibana serikali kuwa ililiandaa jedwali la malipo kwa awamu nne kuwa Januari italipa Dola 3,000,000 na riba ya Dola 90,000 hivyo kuweka kwenye akaunti ya Wallis Dola 3,090,000.
Malipo mengine yangefuata Februari kwa kulipa Dola nyingine 1,590,000 wakati pia Machi ingelipa kiwango hicho hicho na kumalizia na Dola 3,090,000 mwezi Aprili.
“Hadi kufikia Aprili 26, 2012 hakuna pesa iliyolipwa huku deni na riba vyote vikifikia Dola 10,672,895.57. Kwa kuzingatia ushahidi huu wa kutosha wa makubaliano dhidi ya deni la Dola milioni 39 tunarudia tena ombi letu kuwa tafadhali utulipe mara moja deni letu kwa mkupuo,” ilisema sehemu ya barua hiyo, ambayo nakala yake imetumwa Wizara ya Ujenzi, Hazina, ATCL na Shirika Hodhi la Serikali (CHC).
“Tunataka kulipwa bila visingizio kuwa serikali haina fedha na maelezo mengine yanayotolewa kuwa utahitaji idhini ya Baraza la Mawaziri kwani serikali ndiyo mdhamini wa ATCL anayewajibika kulipa Dola milioni 39 na riba inayotozwa katika mkopo huu,” ilisema barua hiyo ya kurasa mbili.
Kampuni hiyo ililalamika kuwa kuchelewesha malipo kunaisababishia Wallis gharama zaidi za ushauri wa sheria na usafiri ambazo ATCL italazimika kuzilipa.
Baadhi ya wajumbe wanaotajwa na waraka huo kuwa walishiriki kuandaa jedwali la malipo mwanzoni mwa mwaka huu ni pamoja na Katibu Mkuu wa Hazina, Ramadhani Khija, Geoffrey Mkilla ofisi ya Msajili wa Hazina, Ezamo Mapunda kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Esmail Kassimu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Hata hivyo, NIPASHE ilipowasiliana na wahusika kuhusu deni hilo ilijibiwa na kiongozi mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake kuwa kama serikali imeahidi kuwalipa, itawalipa hakuna haja ya kulalamika.
Aliitaka kampuni hiyo kuwa na imani kwani si wao peke yao wanaoidai serikali.
 
Back
Top Bottom