Askofu Boniface Kwangu atimuliwa kazi kwa Ufisadi wa mamilioni ya Kanisa

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,582
6,627
KANISA la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Viktoria Nyanza (DVN) lililopo jijini Mwanza, limemtimua rasmi Askofu wa kanisa hilo, Boniface Kwangu kufuatia na ubadhirifu wa zaidi ya Sh. Milioni 600.

Askofu Kwangu aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minane, katika uongozi wake alishawahi kutuhumiwa na waumini wake kuwa anajihusisha na dini ya "Freemasons" huku wengine walikuwa wakimtuhumu kwamba anatumia nguvu za giza(uchawi).

Askofu Kwangu na wenzake wanne wanatuhumiwa na kanisa hilo kwa ubadhirifu wa zaidi ya Sh. Milioni 600 pamoja na kuendesha Kanisa bila kufuata kanuni na taratibu za Kanisa hilo kitendo ambacho kimesababisha kutimuliwa kwake.

Askofu Kwangu, anatuhumiwa na upotevu wa Sh. Milioni 500 za shule ya kimataifa ya Isamilo, kuuza gari la dayosisi hiyo, kufukuza wafanyakazi wa Kanisa hilo na kusababisha wadaiwe Sh. Milioni 60, kujipatia kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 15 toka kwa Mhasibu wa Kanisa, Sam Wisa bila kibali.

Akisoma tamko la kumfukuza kazi, Mwenyekiti wa Nyumba ya Wahudumu kutoka DVN, Andrew Kashilimu, amesema Askofu huyo amelisababishia hasara kanisa hilo zaidi ya Sh. Milioni 600 kutokana na kufanya kazi bila kufuata kanuni na taratibu.

Amesema, askofu Kwangu amekiuka viapo vya uaskofu, katiba ya jimbo, katiba ya DVN na amekiuka maadili na kanuni, kuendekeza matabaka ndani ya wahudumu na waumini na kutoa ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za kanisa.

Amedai katika kikao kilichoketi Septemba 1 mwaka jana, kilithibitisha mambo hayo na kukubaliana kwamba Askofu huyo ajiuzulu kwa afya ya Kanisa la Mungu lakini alikaidi maagizo hayo hadi kutolewa kwa tamko hilo.

“Askofu (Kwangu) ametumia vibaya madaraka yake na alikuwa anatumia vibaya mali na fedha za kanisa, kwa hali hiyo tusingeweza kuwa na kiongozi wa namna hiyo,” amesema Kashilimu.

Mmoja wa waumini ambaye alikumbwa na fagio la Askofu Kwangu, Edwar Kibiti, amesema kwamba kutimuliwa kwa kiongozi huyo wa kiroho katika kanisa hilo kutasaidia kurudisha matumaini kwa waumini walio wengi.

Kibiti ambaye pia ni Mchungaji amesema kuwa walipokuwa wakijaribu kuhoji sababu za Askofu Kwangu kuuza mali za kanisa likiwamo gari alilochangiwa na waumini alikuwa akiwafukuza watu waliotaka kufahamu suala hilo.

“Tulipokuwa tunahoji matumizi ya mali za Kanisa tulichokuwa tukiambulia ni kwenda Polisi na wengine kufukuzwa. Huyu (Askofu Kwangu) alikuwa anafanya kazi kwa majungu, mpaka anaondoka alishafukuza wachungaji 19,” amesema Kibiti.

Amesema kuwa baada ya Askofu huyo kuona wachungaji wazawa wanaanza kumfuatilia alianza kutafuta wachungaji wengine kutoka nchi mbalimbali hususani ni kutoka Rwanda, ili kuficha maovu yake anayoyafanya.

Mmoja wa Waumini, Joycelyn Juma, amesema kilichomgharimu Askofu huyo ni upungufu wa mambo ya kiuongozi ambayo yamechangia kusababisha kuwepo kwa mwanya wa wizi wa mali na fedha za Kanisa hilo.

“Kiufupi nimefurahi sana kwa sababu mambo ya ufisadi ama wizi wa fedha haviendani na mambo ya Mungu na nimefurahi kuona suala hili limefikia mwisho na sasa tutakuwa na amani,” amesema Juma.

Sanjali na kufukuzwa kazi ya Uaskofu DVN, pia uongozi wa Kanisa hilo limemfungulia kesi Askofu Kwangu na wenzake wanne, Katibu wa Bodi, James Mtaritinya, Mhasibu wa Shule ya Isamilo, Sam Wisa, Samson Maganga na John Magawa.

Kesi iliyofunguli ni ya Januari 10 mwaka huu, Mw/Rb/265/2016 ambalo ni jalada la uchunguzi kwa watuhumiwa.
 
Last edited:
DVN migogoro haiishi, Askofu Changai aliyekuwepo kabla ya huyu naye alikumbwa na kashfa zinazofanana sana na hizi hadi akatolewa kinguvu.
 
Last edited:
Kama hizo tuhuma ni za kweli basi hafai kuitwa ASKOFU bali fisadi kama mafisadi wengine.
 
Freemason ni dini gani? ni kitu ambacho ni imaginary na inaonekana waamini wa kanisa hilo wanaomtuhumu wana imani za hovyohovyo za kishirikina. Tatizo kubwa hapa ni kuwapata viongozi kwa kupigiana kura kama ilivyo viongozi wa kisiasa. makundi huwa hayaishi na hayo ni matokeo ya fitna za makundi. Dini zooote zinazochaguana kwa kampeni na kura lazima hayo hayataisha waige mfano wa kanisa katoliki katika kusimika viongozi wake." ROMA LUCUTA CAUSA FINITO"
 
Kama cheo chenyewe kinapatikana kwa kupigiana kura basi hapo kuna tatizo..tatizo ni uaskofu!!!
 
Labda ameona pesa zimekosa kazi na yeye ni mjasilia mali.Naomba nimtetee kwa hilo.
 
Back
Top Bottom