TUMBIRI
JF-Expert Member
- May 7, 2011
- 1,933
- 1,199
Roma 1,300, CCM 50
Na Ansbert Ngurumo,
MWISHONI mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu, nimekutana na makundi mbalimbali ya watu waliokuwa wanajadili "mwisho wa CCM."
Baadhi yao ni wana CCM wakongwe; wengine ni waasisi wa chama hicho. Wanajadili kifo cha chama chao kwa hoja za kihistoria.
Wanasema kitakachoiangusha CCM ni serikali yake, na kitakachoiangusha serikali ni CCM hii.
Kwao, kwa kuzingatia mfumo wa sasa ulivyo, udhaifu wa serikali iliyopo unatokana na udhaifu wa CCM.
Si hilo tu. Miongoni mwao, wamo waliosema kuwa udhaifu wa CCM unatokana na uwezo mdogo wa serikali kufanya kazi na kutimiza wajibu wake.
Ni wazi, viongozi wa CCM ndio hao hao wanaoongoza serikali. Waliotoa ahadi wakati wa uchaguzi, ndio hao wanaoshindwa kuzitekeleza leo wakiwa serikalini.
Walioahidi umoja na mshikamano wa kitaifa, ndio hao wanaoshindwa kuleta umoja na mshikamano katika chama chao.
Viongozi waliotuahidi maisha bora ndio hao wanaoshindwa kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa na huduma; ndio hao wanaoshindwa kudhibiti au kuondoa pengo linaozidi kuongezeka kati ya maskini wengi na matajiri wachache.
Viongozi hao wanaokusanya kodi kubwa kila mwezi ndio wanaoshindwa kueleza chanzo cha ukata unaoikabili serikali, kiasi cha kutishia uwezo wa serikali kutimiza wajibu wake. Wale wale walioahidi wenzao kwamba wanajivua magamba ili wawe wapya na safi, ndio hao wanavaa magamba mapya na magumu kuliko ya awali.
Historia imetufunza kwamba ukiona ufamle wowote unaishiwa pesa, ujue kuwa ufalme huo unakaribia kuanguka. Tunajua kuwa kupanda kwa gharama za maisha hakuwezi kuongeza mapenzi ya wananchi kwa watawala. Na katika mazingira ambamo huoni watawala wakiwa na mbinu mbadala za kuwakwamua wananchi wao dhidi ya ongezeko la bei kali za bidhaa na huduma, kinachoonekana pale ni dalili za anguko la ufalme huo. Hata maandiko matakatifu yanasema kwamba watawala wanaogawanyika katika makundi hasimu, hawawezi kupanga na kutenda kwa umoja. Hawawezi kumshinda yeyote anayeshindana nao; wataparaganyika na kuanguka.
Serikali inayolipisha wananchi maskini kodi kubwa sana kwa wananchi maskini, huku ikiwaacha matajiri wachache kukwepa kodi na kutajirika kwa kasi, ni serikali inayoelekea kuanguka. Serikali inayovumilia rushwa na uonevu dhidi ya wanyonge, ni serikali inayochochea hasira za wananchi dhidi yake, na inakaribisha anguko lake.
Hata Himaya Kongwe ya Roma, ambayo ilidumu kwa miaka ipatayo 1,300 – ilianguka kwa sababu iliishiwa pesa, kodi zilipanda sana, serikali ilishindwa kutekeleza majukumu yake, ufisadi uliongezeka na kukithiri, ukali wa maisha uliongezeka, matajiri walineemeka na umaskini uliongezeka, na haikuwa na pesa za kutosha kulipa masilahi ya wanajeshi.
Dalili zile zile zinajionyesha kwa watawala wakongwe wa CCM, ambao kwa sababu ya ukata, wamelazimika kukopa mabilioni ya shilingi benki, ili kugharamia sherehe za miaka 50 ya "Uhuru." Tunaambiwa hadi leo serikali inakosa pesa za kufanyia kazi za maendeleo kwa sababu sehemu kubwa ya makusanyo inayopata yanaelekezwa katika kulipa deni hilo! Ndiyo maana serikali inakabiliwa na ukata, inachelewesha mishahara ya watumishi, inapunguza nafasi za ajira mpya, na inakata mafungu ya posho za uendeshaji wa shughuli za wizara na idara zake.
Ndiyo maana wakubwa ndani ya CCM wanaogopa kuingia katika uchaguzi wowote mdogo baada ya Igunga, na sasa wanatafakari jinsi ya kubadili vifungu vya sheria ili kukiepusha chama chao na fedheha ya uchaguzi mdogo. Maana wanajua kuwa bila pesa hawawezi kulangua kura! Kwa kuwa hawako tayari kushindwa kwa kura, wanaona bora wasishindane kabisa. Na kwa wingi wao bungeni, wakiamua kubadilisha sheria yoyote watafanya hivyo, ilimradi inalinda masilahi yao. Serikali inaposhindwa kutekeleza ahadi zilizotolewa na wagombea wa CCM, inakihakikishiaje chama hicho kubaki madarakani kwa muda mrefu ujao?
Serikali inayowanyonya wanyonge, inajihakikishiaje kuwa itakuwa kimbilio la wanaonyonywa na kunyanyaswa? Serikali inayokosa mvuto kwa vijana, ambao kwa takwimu zisizo rasmi ndio asilimia 40 ya Watanzania wa leo, inawekeza katika kizazi kipi kitakachokifanya chama tawala kiendelee kushika madaraka kwa muda mrefu ujao? Kwa msingi huu, wanaojadili mwisho wa CCM hawajakosea. Na wakubwa wenyewe wanajua.
Ndiyo maana tunaona wakihaha na kujitapa kufanya mabadiliko makubwa katika uchaguzi ndani ya CCM mwaka huu, huku wakijitapa kutosana na kukomoana kuelekea 2015. Hizi ndizo dalili za anguko linalozungumzwa na wakongwe hao ninaowazungumzia.
Kama wasemavyo wanahistoria, falme zote huwa zinaporomoka pole pole – hazianguki ghafla. Tumezoea usemi wa Kiingereza kwamba Roma haikujengwa kwa siku moja. Lakini pia haikuanguka kwa siku moja. Iliporomoka pole pole! Ikumbukwe kwamba Himaya ya Roma ‘ilikataa' kuwalipa vizuri wanajeshi wake; huku ikiendelea kuwategemea katika kazi nzito za ulinzi.
Ndio hao ambao hawakuweza kuinusuru serikali hasira za umma zilipoamka; maana umma mzima uligeuka jeshi kubwa dhidi ya dola.
Ukweli huu kuhusu Roma unaihusu CCM pia. Kwa ukali huu wa maisha, ukata na kushindwa kwa serikali, inatengeneza jeshi kubwa dhidi ya watawala. Kilichoitokea Roma katika miaka 1,300 ndicho ninachokiona ndani ya miaka 50 ya CCM. Je, huko tunakoelekea yupo anayeweza kuinusuru?
Source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=32189