Alichokisema Dkt. Lwaitama na Prof. Shiviji ni hiki hapa

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
[h=1][/h]Posted on August 11, 2012 by zanzibaryetu
Professa Issa Shivji akiwa katika moja ya mikutano iliyotayarishwa na kigoda cha Mwalimu Nyerere katika chuo kikuu cha Dar es Salaam

Sikuwahi kusikia mahali popote ambapo Prof Sheriff alitamka kuwa eti “anataka” Muungano uvunjwe, yeye kama yeye. Sasa huyu mwandishi Datus Boniface halipata wapi ujasiri wakumlisha mwanataaluma ya historia huyu wa Kitanzania, hata kama ni Mzanzibari pia? Uandishi wa habari wa aina hii ya Datus Boniface ni wa kusikitisha sana.
Tamko la DKt. Lwaitama kuhusu habari ya “Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe”
11/08/2012
JUU YA MUUNGANO: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimesikitishwa na aina ya uandishi wa habari uliojiweka wazi katika taarifa iliyonukuliwa kuandikwa na mwandishi wa gazeti moja la kila siku (Tanzania Daima la tarehe7 Agosti 2012), Datus Boniface. Huyu mwandishi, pamoja na wahariri wake walioruhusu habari hiyo kuchapwa walithubutu kusema uongo kuwa eti “Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na Prof Shivji waliushambulia Muungano..” Tena, mwandishi huyu na wahariri walioruhusu habari hiyo ichapishwe wakaenda mbali zaidi na kutumia kichwa cha habari kilichosema eti ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’.
Nafahamu Prof Shivji tayari ameisha toa tamko juu ya upotoshwaji wa hali ya juu uliobebwa na kichwa cha habri hiki na makala nzima ya mwandishi huyu mwenye aina yake ya ujuzi wa kuandika habari, Datus Boniface. Mimi katika tamko langu sitojisemea mimi tu kama alivyosema Prof. Shivji katika tamko lake. Nitajaribu kueleza kile ambacho nilidhani kilizungumzwa na kila aliyechangia katika Mazungunzo ya yale ya Kifungua Kinywa ( Breakfast Talk), Jumatatu tarehe 6 Agosti 2012, yaliyofadhiliwa na Baraza la Habari Tanzania( MCT).
Wakwanza kuzungumza alikuwa Prof Abdul Sheriff na aliainisha kile alichotaka kibainike kama historia a sababu za kuwepo Muungano katika ya Tanganyika na Zanzibar. Alieleza kile alichotaka kieleweke kama mapungufu ya kisheria katika mchakacho wa kuwepo Muungano. Pia alieleza kile alichotaka kieleweke kama Muungano kukosa kuwa na uhalali wa kisiasa ( political legitimacy) kutokana na ushirikishwaji hafifu wa viongozi wa Serikari ya mapinduzi wa wakati huo na wananchi kwa ujumla. Akahitisha maelezo yake kwa kusema Wazanzibari walio wengi sasa hivi wamefikishwa mahali ambapo wanatamani kutumia mchakato wa kuandika katiba mpya uliozinduliwa hivi karibuni unaoongozwa na Jaji SJoseph Sinde Warioba kujadili Muungano kwa kina na kuingia kwenye maridhiano mapya juu ya kama Muungano uendeleee kuwepo na kama ndiyo kwa mfumo wa serikali ngapi. Ilikuwa wazi kuwa Prof Sheriff alikuwa haamini kuwa walikuwepo Wazanzibari wengi waliokuwa tayari kuendelea na Muungano wa serikali mbili kama wa sasa. Sikuwahi kusikia mahali popote ambapo Prof Sheriff alitamka kuwa eti “anataka” Muungano uvunjwe, yeye kama yeye. Sasa huyu mwandishi Datus Boniface halipata wapi ujasiri wakumlisha mwanataaluma ya historia huyu wa Kitanzania, hata kama ni Mzanzibari pia? Uandishi wa habari wa aina hii ya Datus Boniface ni wa kusikitisha sana.
Aliyezungumza wa pili alikuwa mimi, Dkt Azaveli Lwaitama. Mimi kazi yangu ilikuwa kujibu hoja (Discussant) za mzungumzaji mkuu ambaye kwa kweli alikuwa Prof. Abdul Sheriff peke yake. Kwanza nilimkosoa ndugu yangu, Mtanzania mwenzangu, Prof Abdul Sheriff, kwa kuomba wote tukubali kuwa viongozi wetu waliotuunganisha na kusimamia kuzaliwa taifa letu la Tanzania walikuwa watu walioongozwa na dhamira safi iliyochimbuka katika kuwa waumini thabiti wa itikadi ya Umajumui wa Kiafrika ( Pan Africanism) ya kutaka kuwaunganisha watu wa dola zetu hizi za watu waliokuwa wamekusanywa pamoja na wakoloni na kupachikwa majina kama Tanganyika na Zanzibar bila ridhaa ya wakazi walikuwa ndio wengi wa sehemu hii ya Bara la Afrika. Nikaeleze jinsi mbavyo mwelekeo wa viongozi hawa haukuwa wa kufungwa sana na matakwa ya kisheria bali na kile walichokiamini kingesadia kufanikisha lengo la kuwaunganisha Waafrika wote bila kujali kabila ( tribe) au uzawa ( race). Nikatolea mfano wa jinsi Mwalimu Nyerere alivyoshirki katika kuimiza kuungana kwa Shiraz Association na African Association kuzaa Afro Shiraz Party ( ASP) tarehe 5 Februari 1959, siku na mwezi ambavyo mwaka 1967 vilikuja kuwa siku na mwezi wa kuzaliwa Azimio la Arusha , na mwaka 1977 vilikuja kuwa ni siku na mwezi kilizaliwa Chama cha Mapinduzi kutokana na kuunganisha Tanganyika African National Union ( TANU) na Afro Shiraz Party ( ASP).
Nilisisitiza kuwa leo tunaweza kuyaona wazi mapungufu makubwa katika taratibu za kisheria zilizogubika mchakato wa kuunda Muungano lakini si vizuri kusema eti tuukatae Muungano kutokana tu na mapungufu haya ya kisheria. Si vizuri na si busara kusahau kuwa Muungano uliundwa kwa sababu za dhamira ya kuunganisha Washiraz, Waafrika, Waarabu, Wahindi na Wazungu na kuwaweka pamoja kama Waafrika waumini wa Umajumui wa Kiafrika (Pan Africanism), wawe wa dola lilosimikwa na wakoloni la Zanzibar au dola lililo simikwa na wakoloni la Tanganyika. Mwalimu Nyerere na Mzee Abedi Karume walisukumwa na kutaka kuunda taifa ya Kiumajui wa Kiafrika jipya la TANZANIA, baada ya kuona Mzee Jomo Kenyata wa Kenya na Ndugu |Milton Obote wa Uganda hawakuwa tayari kwa wakati huo, mwaka 1964, kuunda dola jipya ambalo lingeongozwa na itikadi ya vuguvugu la utaifa wa Umajumui wa Kiafrika ( Pan Africanist nationalist movement) la Shirikisho la Afrika Mashariki.
Kwa waasisi hawa wa Muungano taratibu za kisheria hazikupewa kipaumbele bali dhamira safi ya kutenda liloonekana kuwa la manufaa kwa wananchi walio wengi wa sehemu hii ya Afrika. Tukumbuke kuwa Mzee Karume na Mwalimu Nyerere walikuwa wanafanya kazi katika mazingira ya kivuli cha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964 mwezi mmoja baada ya Uhuru wa Zanzibar tarehe 9 Desemaba 1963 uliopatikana kwa kufuata taratibu za kisheria lakini matokeo yake yakapinduliwa kijeshi tarehe 12 Januari 1964 kwa vile taratibu hizo za kisheria zilitumika kukwepa kupatikana kwa ridhaa ya kisiasa ya walio wengi katika kupatika Uhuru ule wa Zanzibar wa Desemba 1963!!
Nilitumia muda kuelezea jinsi ambavyo tabaka la mabepari uchwara Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar lilivyokuwa na ushawishi mkubwa juu ya uongozi wa serikali ya Muungano na serikali ya Zanzibar. Nilianisha kuwa hii ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya kukosekana kwa wanasiasa madhubutu wenye ushwaishi ndani ya CCM ya miaka kuanzia 2006 wenye utashi wa kutetea dhamira ya waasisi wa Muungano waliokuwa waumini wa itikadi ya Ujamaa na Umajumui wa Kiafrika. Nikabainisha kuwa utetezi wa mfumo wa serikali unatolewa kikasuku na viongozi wa juu wa CCM ya wanamtandao ya kuanzia mwaka 2006 ni utetezi wa kinafiki kwani juhudi za makusudi za kuutetea Muungano kwa vitendo hazikuwa dhairi. Niliorodhesha nyanja kama uteuzi wa wakuu wa vyombo vya dola kama polisi na jeshi la wananchi au Benki Kuu ambao ungekuwa umefanywa kwa lengo la kulinda Muungano hata kero za Muungano zinazotajwa na wanasiasa wa Zanzibar zingekuwa pungufu.
Nilisahau hata kutaja jinsi wana-CCM wa kundi la Mtandao walivyozima kwa njia za hila na hiyana kupatikana kwa Rais wa awamu ya Nne Mzanzibari, yaani Dk. Salim Ahamed Salim mwaka 2005. Nilibainisha kuwa hii ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya watetezi wa dhati wa Muungano wa Serikali Mbili wenye kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere kama mimi, wanaosukumwa na kuwa waumini wa itikadi ya Umajumui wa Kiafrika, kukikri kuwa kwa sasa ukitaka kulinda Muungano katika mazingira ya sera za uchumi na siasa za uliberali mambo leo lazima kukuballi kuwepo kwa Muungano wa serikali Tatu.
Nilitumia muda mrefu zaidi nikieleza kufurahishwa kwangu na msimamo wa mwanasiasa kijana wa chama cha Chadema, Mheshimiwa Zito Kabwe, kuelezea, katika gazeti la kila wiki la Fahamu hivi karibuni, kuwa mwalimu wake wa nje ya darasa Dk Lwaitama sasa alikuwa anaunga mkono dhana ya kutafuta kuulinda Muungano kwa kuridhia kuwepo kwa Muungano wa serikali Tatu. Nilielezea jinsi Mheshimiwa Zito alivyofafanua kuwa dhana hii ya kuulinda Muungano kwa kukubali sera ya serikali Tatu amekuwa nayo kwa muda sasa na ingelenga kuwepo kwa Serikali na Bunge la Muungano. Serikali hii ya Muungano ingekuwa ndogo, yenye kushughulikia mambo ya Muungano machache. Mimi mwenye nilielezea kuwa niliishapendekeza mahali pengine kuwa labda Serikali ya Muungano ingekuwa na wizara kuu zisizozidi nne au tano zenye uteuzi wa mawaziri wa sawa kwa sawa, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, huku Urais wake ukiwa kwa zamu.
Wizara kuu zingelihusu mambo ya ndani ( yaani uhamiaji, uraia, polisi), mambo ya nje ( yaani ulinzi wa nje na mahusiano ya kimataifa), uratibu wa mambo ya fedha na mipango ya uchumi ( yaani sarafu, sera ya uwekezaji, mambo wa ushuru, na kodi), na miundo mbinu inayoitaji uwekezji mkubwa( teknohama, uzalishaji na usambazaji umeme, usafiri wa bahari na maziwa, reli, na anga). Hata haya mambo ya muungano mengi yake baadaye yangelishugulikiwa na Jumuya ya Afrika Mashariki kadili itakavyo kuwa inaimarika kuelekea kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki.
Nilielezea pia jinsi Mheshimiwa Zito alivyokuwa amependekeza kuwa kungelikuwepo serikali mbili za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar zilizo sawa kila moja ikiongozwa na Waziri Mkuu na kila moja ikisimamiwa na Baraza la Wawakilishi. Nikaeleza jinsi Mheshimiwa Zito alivyopendekeza katika uchanguzi mkuu kungewepo uchanguzi wa Rais na Makamu wa Rais Mwenza wa Serikali ya Muungano na Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano pamoja na Uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Tanzania Bara na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Tanzania Zanzibar . Muda mwingi niliutumia katika kuunga mkono mawazo haya ya awali ya mwanasiasa huyu kijana na mzalendo , Zito Kabwe nikionesha furaha yangu kuwa mwanasiasa kijana wa chama cha upinzani cha Chadema kama huyu ameweza kuona mbali kiasi hiki kuliko viongozi wa sasa wenye ushawishi ndani ya chama kilichouasisi Muungano cha CCM.
Nakumbuka katika mjadala uliofuata mchango wangu mwanahabari mwanandamizi amabaye ni Mhariri Kiongozi wa gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile, alionyeshwa kuvutiwa mapendekezo haya ya jinsi ya kunusuru Muungano nay eye kupendekeza kuwa ingekuwa vizuri ikiwa Tanzania Zanzibar itaitwa Tanzania Visiwani!. Lengo la wachangiaji wote siku hiyo lilionekana kutafuta njia za kuzidi kuimiza kuukubali utambulisho wa kujiita Watanzania, iwe mtu ni anatokea kuwa mkazi wa Tanzania Bara au mkazi wa Tanzania Zanzibar na polpole kufifisha mawazo ya kubanguana kwa misingi ya Utanganyika na Uazanzibari. Mimi nilisisitiza kuwa utambulisho wa kwa misingi ya Utanganyika na Uazanzibari, majina tuliyopachikwa na wakoloni, ulikuwa ni utambulisho uliokinzana na kuwa waumini wa itikadi ya Umajumui wa Kiafrika, ambayo ndiyo ilituunganisha katika kupigania uhuru wa bendera miaka ya 1940 na 1950.
Kwa lengo hili hili la kuufanya utambulisho wa Utanzania ushamili zaidi na zaidi, na kufifisha mwelekeo wa kubanguana kwa misingi ya Utanganyika na Uazanzibari, pendekezo langu liloonekana kuridhiwa katika andiko la Mheshimiwa Zito lilikuwa kuwa Mawaziri Wakuu wa Seriakali za Tanzania Bara an Tanzania Zanzibar wangeteuliwa na vyama vya siasa vilivyoandikishwa ki- Muungano kama sasa kutegemea ni chama kipi au muungano wa vyama vipi ungekuwa umepata viti vingi au kura nyingi katika changuzi za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi husika.
Pendekezo langu lilikuwa kuwa kutokuwepo kwa uchanguzi wa wakuu wa serikali ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kungesaidia katika kupunguza, polepole, ushabiki na hamasa za kisiasa zinazojikita kwenye utanmbulisho wa Utanganyika au Uzanzibari. Haya yote lengo lake lingekuwa kutafuta njia za sasa za kuendelea kuwaenzi waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, ambao dhamira yao ilikuwa nzuri ya kuunganisha Waafrika wote bila kuwabagua kwa misingi ya kabila, rangi, dini, uzawa au upande wa bahari ya Hindi mtu alikokuwa anaishi kwa sasa au hapo nyuma.
Nilisisitiza umuhimu wa itikadi ya Umajumui wa Kiafrika kwa kusema hata kama itatokea ushawishi wa tabaka lenye kutaka kuvunja Muungano wakawashauwishi Wazanzibari kwa sasa kuridhia kuuvunjika kwa Muungano basi Watanzania Bara waendelee kujiita Tanzania Bara na Wazinabari waendeleee kujiita Tanzania Zanzibar, kama Wasudani Kusini walivyoridhia kujiita Sudani Kusini licha yakupata uhuru. Mapendekezo yote haya yangesaidia kuimiza kuendeleza juhudi za kusimika utambulisho wa Kiumajumui wa Kiafrika wa U-Tanaznia ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere na Mzee Karume. Hii nngekuwa kama ilivyo kwa kama kuendelea kuwepo utambulisho wa Sudani kwenye utambulisho wa Wasudani wote, Kusini na Kazikazini!!!! Sielewi uandishi wa Datus Bonaface ni wa aina gani uliomruhusu kusuka maneno kutoka kwenye mchango wangu hapo juu wakusema eti ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’ au eti “ Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na Prof Shivji waliushambulia Muungano..” Inasikitisha sana kuwepo waandishi wa aina hii na wahariri wanaoruhusu uchapishwaji wa uongo wa kiwango hiki!!!
Wachangiaji kadhaa walifuata mchango wangu kabla ya Prof Shiji kutoa mchango wake ambao ameulezea vizuri sana katika tamko lake kuhusu upotoshwaji wa hali ya juu ulifanywa na mwandishi Datus Bonaface pamoja na wahariri walioruhusu habari hii ya uongo kuchapishwa. Laiti kama wahariri wale wangeomba ushaidi wa kanda ya kilichozungumza wangegundua mara moja kuwa mwandishi Datus Bonaface ni mwandishi wa ajabu kweli kweli. Naliambatisha Tamko la Prof. Shivji kama alivyolitoa, na nalo bila shaka yeyote ninaonesha wazi kuwa Prof. Shivji kamwe hakutamka mahali pale kitu chakumfanya mwandishi aseme eti ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’ au eti “ Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na Prof Shivji waliushambulia Muungano..” Inasikitisha sana kuwepo waandishi wa aina hii na wahariri wanaoruhusu uchapishwaji wa uongo wa kiwango hiki!!!
Mwl. Azaveli Feza Lwaitama
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jukwaa la Dira Afrika Mashariki
&
Mhadhiri Mwandamizi Mstaafu,
Kitengo cha Falsafa,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kerezesia_mukalugaisa@hotmail.com
+255784432696/ +255782807728
Agosti 11, 2012
Tamko la Prof. Shivji kuhusu habari ya “Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe”
09/08/2012
JUU YA MUUNGANO: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimeshitushwa na gazeti moja la kila siku (Tanzania Daima la tarehe7 Agosti 2012) lilonipandikizia maneno katika kichwa chake cha habari kwamba ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’. Siwezi nikamsemea Dr. Lwaitama lakini kwa upande wangu sijasema wala kumaanisha kwamba ‘Muungano uvunjwe’.
Source: Tamko la Prof. Shivji kuhusu habari ya "Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe" - wavuti
Mosi, kwamba wasomi, wakiwemo wanahabari, wana jukumu zito la kutokupinda ukweli wa kihistoria kwa lengo la kuhalalisha mtazamo na msimamo wao kuhusu Muungano. Nikatoa mfano wa jinsi Merehemu Sheikh Karume anavyodekezwa katika msimamo wake juu ya Muungano. Wasemaji hapa bara wanamsifu kwa kuwa muasisi mwaminifu na mshabiki mkubwa wa Muungano tangu mwanzo. Huko Zanzibar, wasemaji hawachoki kumnukuu Mzee Karume kuwa tangu mwanzo yeye hakutaka Muungano isipokuwa alikuwa anafikiria Shirikisho.
Wanaendelea kusema kwamba aliposaini Mkataba wa Muungano, Mzee Karume alifikiri kwamba anasaini Shirikisho la Serikali tatu, lakini kutokana na kiwango cha elimu yake hakuelewa vizuri mantiki na maana ya alichokuwa anasaini.
Nikaendelea kueleza kwamba maelezo haya yote mawili hayaungwi mkono na ushahidi wa kihistoria. Ukweli ni kwamba, Mzee Karume aliingia katika Muungano kutokana na hesabu zake mwenyewe za kisiasa. Muungano kwake ulikuwa njia ya kuondoa upinzani, au upinzani tarajiwa, wa utawala wake. Yaani ilikuwa ni tendo la mwanasiasa yeyote yule kudumisha utawala wake (political survival).
Na kwa watawala wote wa Zanzibar waliomfuata, wakiwemo wa upinzani, ndivyo ilivyokuwa. Wamekuwa wakitumia mwavuli wa muungano wakati utawala wao uko hatarini na kushawishi wananchi wao dhidi ya muungano wakitafuta umaarufu wa kisiasa.
Nikitoa mfano nikasema kwamba kuna taarifa kwamba chama kimoja huko Zanzibar kinapandikiza pendekezo la ‘muungano wa mkataba, sio wa katiba’ bila ya kueleza waziwazi maana yake. Ukweli ni kwamba huwezi ukawa na muungano wa mkataba bila kwanza kuuvunja muungano. Kwa hivyo, wanachoshawishi moja kwa moja ni kuuvunja muungano. Basi waseme hivyo badala ya kujificha nyuma ya pazia la ‘muungano wa mkataba’.
Jambo la pili nililorudia ni kwamba tuliangalie suala zima la muungano kwa mtazamo na maslahi na matakwa ya Umma wa Zanzibar na Umma wa Tanzania bara, hususan matabaka ya hali ya chini. Katika hali yao kimaisha – kiuchumi na kisiasa – hakuna tofauti kati ya wananchi wa Zanzibar na wananchi wa Tanzania bara. Uduni wa hali yao ni uleule; ukosefu wa ajira ni uleule; kutokuwa na mfumo wa dhati wa demokrasia unaojali walalahoi ni kulekule.
Kwa hivyo, umuhimu kwao ni mshikamano wao kuboresha mifumo ya uchumi na siasa. Wasiburuzwe na wanasiasa na vyama vyao kwa maslahi yao binafsi ya muda mfupi ya kudumisha, au kuingia kwenye, utawala.
Jambo la mwisho nililogusia ni kwamba kiini cha suala la muungano si idadi ya serikali (mbili au tatu) bali ni mgawanyo wa madaraka (distribution of power) kati ya dola la Zanzibar na dola la Muungano. Na katika hili kila muungano duniani ni wa kipekee kutokana na hali halisi yao ya kihistoria na uwiano wa kisiasa. Sisi pia tukiwashirikisha wananchi kikamilifu na tukaelewa vizuri matakwa yao tunaweza kubuni muundo wetu wa muungao ambao ni wa kipekee bila kujali idadi ya serikali.
Nimeona niweke wazi mtazamo wangu kwa sababu ya baadhi ya vyombo vya habari kuwa na hulka ya kupotosha mambo kutokana na ushabiki wao bila kujali madhara yanayoweza kutokea.
Mwishoni ningependa kusema kwa dhati kwamba uvunjaji wa muungano hauwezi kuwa kwa manufaa ya walio wengi. Ukweli ni kwamba unaweza ukasambaratisha nchi na jamii zetu pande zote mbili za muungano. Tukianza kubaguana kati ya Watanganyika na Wazanzibari, tutaendelea kubaguana kwa msingi wa Uislamu na Ukristo, na Usukuma na Uchaga, Uarabu na Uafrika, weusi na weupe bila kikomo.
Kama alivyosema Mwalimu, ukishaonja nyama ya mtu basi utaendelea kumtafuna.
Issa Shivji
Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Agosti 8, 2012
Source: Tamko la Prof. Shivji kuhusu habari ya "Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe" - wavuti
 
Back
Top Bottom