Mandown
JF-Expert Member
- Apr 8, 2012
- 1,665
- 503
Wanasheria Msaada hapo jamani
-----
-----
Tumekuwa tukisikia fulani amepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia au fulani ameua bila kukusudia, je unajua nini maana ya kuua bila kukusudia kisheria. Mara ya mwisho neno kuua bila kukusudia limesemwa sana baada ya hukumu katika kesi iliyohusu kifo cha mwanahabari Daudi Mwangosi. Yapo mengi ya kujua kuhusu kuua bila kukusudia.
Kifungu cha 195,sura ya 16, Kanuni za adhabu ndicho huzungumzia kuua bila kukusudia.
1.NINI MAANA YA KUUA BILA KUKUSUDIA.
Katika sheria kuua bila kukusudia (manslaughter) kunatofautishwa na kuua kwa kukusudia(murder). Kuua bila kukusudia ni kuua ambako muuaji anatenda kitendo kinachopelekea kifo lakini hakuwa na nia,dhamira au lengo la kusababisha mtu afe.
Wakati kuua kwa kukusudia ni pale mtu anapotenda tendo ambalo linapelekea mauaji ya mtu lakini amefanya hivyo akiwa amedhamiria kuua. Kwahiyo haraka utaona kuwa tofauti kubwa ya kuua kwa kukusudia na ile ya kuua bila kukusudia ni dhamira, nia au lengo.
Dhamira,nia au lengo likiwa ni kuua, basi huko ndiko kuua kwa kukusudia. Na dhamira,nia au lengo likiwa sio kuua lakini bahati mbaya mtu akafa basi hiyo itakuwa ndio kuua bila kukusudia.
2. UTAJUAJE HUYU ALIUA KWA KUKUSUDIA NA HUYU HAKUKUSUDIA.
Yapo mambo ambayo hutizamwa na mahakama ili kujua iwapo kulikuwa na dhamira ya kuua au haikuwepo. Moja ya jambo kubwa ambalo huangaliwa ni mazingira kabla ya tukio, mazingira wakati wa tukio na baada ya tukio.
Kwa mfano A alimkashifu B kwa matusi mabaya . B akakasirika sana . Baadae B akaenda kwake akaja na panga ambalo alilitumia kumuua A . Hapa B atakuwa ameua kwa kukusudia kwasababu alisafiri kutoka eneo la tukio , akatembea mpaka nyumbani kwake, akatafuta panga, akaanza safari ya kurudi, akamtafuta tena A, akampata ndipo akamuua. Hatua zote hizi za kwenda,kurudi nk. zinathibitisha dhamira, nia au lengo. Hakuna bahati mbaya inayopitia hatua hizi zote.
Lakini ingekuwa palepale baada ya kukashifiwa kwa hasira akampiga na kumuua, ingekuwa kuua bila kukusudia kulikotokana na joto la hasira(heat of passion).
Kwahiyo ushahidi wa mazingira ya tukio kama hayo ndio utaifanya mahakama iamue kama mtuhumiwa ameua kwa kukusudia au hakukusudia.
Upande unaosema aliua bila kukusudia utaleta ushahidi kuonesha mazingira ya tukio na upande unaosema alikusudia nao utaleta ushahidi kuonesha mazingira ya kusudi, nia au dhamira.
3. AINA MBILI ZA KUUA BILA KUKUSUDIA.
Kwanza ni kuua bila kukusudia lakini kwa tendo linalotokana na hiari(voluntary manslaughter). Hii ni pale ambapo ni kweli kuwa fulani alidhamiria kumpiga fulani au alimsukuma lakini hakutaka afe. Kwa mfano mzazi anamchapa mwanae kwa kosa fulani lakini katika kumchapa mtoto anakufa. Au askari anapiga bomu la machozi ili watu wakimbie lakini katika kufanya hivyo bomu linampata raia na kumuua.Hii ni aina ya kwanza ya kuua bila kukusudia.
Aina ya pili ni kuua bila kukusudia kwa tendo ambalo si la hiari( involuntary manslaughter). Kwa mfano breki za gari zinakatika na gari inamuua mtu. Au bunduki imeshikwa vibaya inajifyatua na kuua mtu.
Ni matendo ya uzembe lakini hayakutokana na hiari kama ilivyo hiari kuamua kumchapa mwanao.
Aina hizi zote mbili ni za kuua bila kukusudia.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MWANDISHI WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. ”