Zungu- Kampuni za simu zinaiibia Serikali

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,144
MBUNGE wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), ameitaka Serikali kutokubali kuendelea kuangalia wizi unaofanywa na kampuni za simu za mkononi nchini kwa kukwepa kodi na kupeleka fedha zao nje ya nchi.

Ili kukabiliana na ukwepaji wa kodi kwa kampuni hizo, ameitaka Serikali kuamka na kufunga mtambo wa kurekodi simu zinazopigwa ndani na nje ya nchi ili ifahamu mapato ya kampuni hizo na ipate kodi kutokana na upigaji huo wa simu.

Akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia iliyowasilishwa na Waziri Profesa Makame Mbarawa jana bungeni, Zungu alisema, Serikali iwe na mkakati wa 'Kodi kwanza' kama ilivyofanya kwenye 'kilimo kwanza'.

"Nchi kama Uganda na Ethiopia zimefunga mtambo huo, nasi tusiyaogope makampuni haya, Serikali ituambie itafunga lini mtambo huo. Mfano kwa wote waliosajiliwa milioni 22 kila mmoja akitozwa Sh 200 tu kwa mwaka, kutapatikana trilioni 1.5, lakini sasa hakujulikani kipato chao.

“Shilingi yetu inashuka kwa sababu wanapeleka dola zote nje na hawawekezi kitu zaidi ya minara hata majengo hawana wanakodi, tusipobana upotevu wa kodi wataendelea kutufanya shamba la bibi,” alisema Zungu.

Kwa upande wa Msemaji wa Upinzani katika wizara hiyo, Profesa Kulikoyela Kahigi alisema, kampuni za simu za mkononi zinakwepa kodi pale zinapouzwa na Serikali kutoshirikishwa.

Alitolea mfano Celtel ilipouzwa kwa Zain nao kuuza kwa Airtel na kufafanua:

"Zain ilipouzwa kwenda Airtel, Serikali ingeweza kukusanya dola za kimarekani milioni 312...hata Vodacom ilipouzwa kwa Vodafone ya Uingereza haijaweka wazi kama Serikali ilipata chochote, zinafanya biashara humu nchini na kuuziana bila Serikali kuingilia kati na kukusanya mapato”.

Upinzani waliishauri Serikali kufanya mabadiliko ya sheria mapema ili iwe inatoza kodi kampuni hizo zinapouzwa.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara hiyo, Mjumbe wa kamati hiyo, Ritha Mlaki aliitaka Serikali izishawishi kampuni za simu kuondoa gharama za kupiga simu kati ya mtandao mmoja na mwingine ili kuwapunguzia wananchi gharama za kupiga simu na kutembea na simu zaidi ya moja.
 
Back
Top Bottom