Zombe utavuna ulichopanda/atoa chozi 3hrs | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Zombe utavuna ulichopanda/atoa chozi 3hrs

Discussion in 'Celebrities Forum' started by Pdidy, Feb 11, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Feb 11, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,613
  Likes Received: 5,782
  Trophy Points: 280
  mod tunaomba ikae kwa muda,,huyu mhuni ameuwa ndugu zetu wacha mungu amwadhibu,kwema lakini??

  Zombe ajitetea kwa muda wa saa tatu huku akimwaga machozi
  Na James Magai

  MSHTAKIWA wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka mjini Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam, Abdallah Zombe jana alijitetea kwa zaidi ya saa tatu huku akimwaga machozi wakati akiwasilisha utetezi wake.

  Zombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) ambaye alikuwa mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dar es Salaam, alijikuta akimwaga machozi mara kadhaa wakati akijitetea mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Masatti kuhusu tuhuma hizo dhidi yake pamoja na askari wenzake tisa.

  Hatua ya kupanda kizimbani jana na kuanza kujitetea ilikuja baada ya mahakama hiyo kuridhika kuwa Zombe, ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa akikaimu nafasi ya kamanda wa kanda ya Dar es salaam, pamoja na wenzake wana kesi ya kujibu kuhusu mauaji ya watu hao kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

  Zombe, ambaye jana alisimama pia kama shahidi wa kwanza upande wa utetezi dhidi yake (Dw1), alibubujikwa na machozi wakati akitoa ushahidi wake na kujifuta kwa kitambaa mara kadhaa huku akigeukia pembeni.

  Kutokana na kilio hicho cha kimya kimya, mara nyingine alijikuta akikabwa na kigugumizi cha uchungu kiasi cha kushindwa hata kuzungumza.

  Akiongozwa na wakili wake, Jerome Memwa katika utetezi wake uliochukua saa 3:38, Zombe alikanusha ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo kuwa si wa kweli na kwamba ulipangwa tu kwa lengo la kummaliza kwa sababu ambazo hata hivyo hakuweza kuzieleza.

  Katika hali hiyo Zombe alimtupia lawama Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwa ni miongoni mwa watu waliohusika katika kupanga ushahidi kwa lengo la kummaliza katika hali ya kutapatapa baada ya kuona kuwa hawana ushahidi wa kumhusisha na tukio hilo.

  Huku wakati mwingine akibishana na wakili wake katika namna ya kujitetea, Zombe alidai yeye hakuhusika na mauaji hayo kwa kuwa hakuwahi kuwafahamu marehemu hao kabla, wakati na hata baada ya vifo vyao.

  Wakili Msemwa alikuwa akijaribu kumzuia kwa ishara wakati fulani, lakini Zombe alionekana kumbishia kwa ishara na wakati fulani kulazimika kuomba ruhusa kwa jaji ili aendelee kutoa maelezo yake.

  Zombe alianza kwa kuileza mahakama jinsi alivyokamatwa na kufikishwa mahakamani.

  “Mimi nilikamatwa Juni 6 mwaka 2006 nikiwa makao makuu ya Jeshi la Polisi. Siku hiyo niliitwa kwa mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali (IGP), Saidi Mwema na nilimkuta akiwa na makamishna wawili. Alikuwepo Kamishna Mtweve na Kamishna wa Mafunzo jina ambaye nimemsahau," alidai Zombe.

  IGP alinieleza kuwa leo ninaunganishwa katika kesi ya mauaji ya watu wanne, akaniambia kuwa mkurugenzi wa mashtaka ameleta barua kuwa niunganishwe katika kesi hiyo, kisha akanikabidhi barua hiyo,” alidai Zombe na kuitaja barua hiyo kuwa ni ya Juni 6 mwaka 2006.

  Alisema barua hiyo, ambayo ilikuwa ikijibu barua ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ya Mei 31 mwaka 2006, ilieleza kuwa baada ya kukamilisha mambo kadhaa ya kiupelelezi na kwa ushahidi ulioko katika jalada tumefikia maamuzi kuwa Zombe aunganishwe katika kesi hiyo.

  “Sikubaliani na maelezo ya barua hiyo kwa kuwa ni ya kupangwa,” alidai Zombe akiongozwa na wakili wake.

  “Barua hiyo ni ya tarehe 6/6/2006, DPP huyo huyo siku tatu kabla, yaani tarehe 3/6/2006, alikuwa amepokea barua kutoka kwa askari waliokuwa mahabusu katika gereza la Ukonga ambao ni mshtakiwa wa tatu, mshtakiwa wa tano, mshtakiwa wa saba mshtakiwa wa tisa na wa 10.”

  Zombe alisema barua hizo, ambazo alizitoa mahakamani hapo kama kielelezo, zilikuwa zikienda kwa DPP na kwamba washtakiwa hao waliziandika kwa maelekezo ya DPP.

  Zombe alidai kiutaratibu barua hizo zilipaswa zipitie kwa Mkuu wa Gereza na kwamba ingawa zilionekana kuwa zimepitia kwa mkuu wa gereza, lakini ukweli ni kwamba zilikuwa zimepitia katika mlango wa panya.

  “Naomba hii ya mshtakiwa wa tano niizungumzie kidogo na ninaomba busara za mahakama na za wazee wa baraza zitumike. Barua hii imeandikwa tofauti na nyingine zote sababu kwa sababu mshtakiwa huyu anakaa Segerea (mahabusu). Bila shaka maelekezo ya DPP hakuyapata au aliyemfundisha hakumuelewa vema,” alidai.

  Alidai baada ya barua hiyo ya DPP ndipo alipokamatwa ofisini kwa IGP mnamo saa 2.00 asubuhi na kwamba kufikia saa 2.15 alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 9 mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Ady Lyamuya.

  Zombe alisema siku ya mauaji hayo alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) na pia alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi akiwa na wasaidizi wapatao sita, katika nafasi ya kaimu RPC, wakati katika katika ofisi ya RCO alikuwa na wasaidizi watano.

  Miongoni mwa wasaidizi hao wa RCO aliwataja kuwa ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Charles Mkumbo ambaye aliyekuwa mkuu wa kitengo cha ujambazi na uhalifu mbalimbali Dar es Salaam.

  Kuhusu kuhusika katika tukio hilo, Zombe alidai siku hiyo alikuwa na shughuli maalumu ya kuongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa na ziara za kutembelea wizara mbalimbali na kutoa maelekezo ya utendaji na kwamba majukumu yake aliyakabidhi kwa SSP Mafie.

  Aliongeza kuwa kwa nafasi ya RCO, jukumu hilo alilikabidhi kwa SSP Mkumbo na kwamba alikuwa ingawa wasaidizi hao walikuwa wakimuelezea yaliyokuwa yakitokea jijini, lakini wakati mwingine alikuwa akichelewa kurudi na hivyo alikuwa akienda nyumbani moja kwa moja.

  Akielezea muundo wa jeshi la Polisi Zombe alisema kuna ngazi na madaraja mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakuu wa polisi wa wilaya (OCDs) ambao ndio huwajibika kwa RPC na kwamba hakuna sheria yoyote kwa RPC kwenda katika kituo chochote cha polisi kwa kuwa vyote viko chini ya RPC.

  “Shahidi katika ushahidi uliotolewa hapa ni kwamba wewe ulikwenda katika kituo cha Polisi Urafiki, hebu iambie mahakama ni lini ulikwenda kwama RPC na kwa nini?” aliuliza Wakili Msemwa.

  “Kama Mtukufu Jaji alivyosema, hii ni moja ya sababu ya kunibakisha mimi katika kesi hii ili nisaidie kutoa ushahidi. Wasaidizi wa RPC ni OCD. Katika utaratibu wetu kama kuna tatizo kuna mawili ama kumwita aenda mwenyewe au kumwita ofisini,” alijibu Zombe.

  Hata hivyo, Zombe aliieleza mahakama kuwa siku hiyo alikwenda kituoni hapo baada ya kuitwa na OCD wa Magomeni, SSP Matage kuwa kuna tatizo ambalo alikuwa akihitaji msaada wake.

  “Siku hiyo nilikuwa nimekwenda kumchukua mke wangu Hospitali ya TMJ katikati ya jiji. Dereva wangu aliyekuwa amebaki katika gari alikuja ndani akanitaarifu kuwa OCD Matage alikuwa akiniita," alidai Zombe.

  Nilikwenda tukaingia na mke wangu kwenye gari nikamuuliza OCD Matage mahali alikokuwa akaniambai alikuwa Kituo cha Urafiki. Nilimuuliza alikuwa na jambo gani na kama kulikuwa na umuhimu wa mimi kwenda, akasema ilikuwa ni muhimu.”

  Alisema walipofika ofisini walimkuta mkuu wa kituo hicho, SP Juma Ndaki, OCD Matage, SP Mkumbo, mshtakiwa wa pili, SP Christopher Bageni na mshtakiwa wa tatu, ASP Ahmed Makelle.

  “Matage aliniambia kuwa hawa ofisa wa polisi (Bageni na Makelle) wanatoka kwenye tukio la uporaji wa pesa za Bidco ambako zimeokolewa Sh5,750,000, lakini Sh.1mil haipo.. hapa kuna Sh4 milioni na bastola. Hawa ni maofisa wakubwa sasa nisaidie tufanyeje," alidai Zombe akimkariri Matage.

  OCD alithibitisha Bidco wenyewe waliziona. Nilishangaa OCD kuniita kwa swala hilo ndipo nilimuuliza OCD kuwa kama ameshindwa kazi anithibitishie sababu haiwezekani kielelezo kikapotea na ndipo nilipokasirika na si vinginevyo nikatoa maelekezo kuwa nataka pesa hizo hizo zionekane kesho yake. Nikaondoka kwenda nyumbani kwangu.”

  Alidai kwa kesho yake asubuhi mshtakiwa wa pili, Bageni alizipeleka na kumweleza kuwa zilipatikana kwenye gari. Asubuhi hiyo hiyo akawaita OCD wa wilaya zote lakini na askari wa chuo kikuu tu ambapo walizungumza hali ya uhalifu maana kwa kuwa wakati huo kulikuwa na ujambazi sana watu walikuwa wakiuawa bila sababu.

  Alidai walizumgumzia tukio la Bidco na kuwapongeza askari waliohusika kwa kuwatoa kimasomaso na kwamba pesa hizo zilifikishwa na kwamba ndipo baadaye aliwaita waandishi wa habari ili kuwaeleza tukio hilo na kuwaonyesha fedha hizo na bastola hiyo.

  “Tena nakumbuka gazeti la Mwananchi lilinionyesha nikiwa nimeshika hizo fedha na nikiwa nimeshika ile bastola. Fedha hizo pia zilifikishwa katika Tume ya Rais Kikwete.” alidai na kuongeza kuwa OCD wa eneo husika pia aliandika taarifa ya tukio hilo.

  Alidai taarifa za matukio yote huandaliwa tangu ngazi ya chini na kutumwa kwa viongozi wa juu hatua kwa hatua hadi kwa IGP kupitia katika mitambo maalumu na kwamba hata Ikulu kuna mtambo huo ambao ni mkubwa unaopokea matukio hayo yote.

  “Hata zinapofika kwa RPC huzinakili kama zilivyo bila kuongeza ili kama likitokea jambo kama hili lililotuweka hapa, tunarudi kwenye taarifa hiyo,” alisisitiza.

  Zombe alikanusha ushahidi wote hasa kuwa aliwavamia baadhi ya ndugu wa marehemu Muhimbili na kuwatishia na kwamba hata maelezo yao yanatofautiana jambo ambalo alisema linaashiria ushahidi wao si kwa kweli.

  Zombe alidai ripoti ya tume ya polisi iliyoundwa kuchunguza tukio hilo ilikamilika tofauti na ilivyoelezwa na upande wa mashtaka na kwamba ilisainiwa na kupelekwa kwa IGP.

  Alidai kuwa taarifa hiyo haikumhusisha na tukio hilo, lakini kuna watu ambao hawakuifurahia. Alisema aliweza kuipata taarifa hiyo kwa kutumia mbinu zake kwa kuwa yeye ni mchunguzi na alikanusha madai kuwa alikataa kuandika maelezo na kutoa nakala ya maelezo yake aliyoyaandika Mei 29, 2006.
   
 2. Next Level

  Next Level JF-Expert Member

  #2
  Feb 11, 2009
  Joined: Nov 17, 2008
  Messages: 3,159
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Nini kinafuta baada ya utetezi wake? Hukumu au vipi?
   
 3. B

  Boney E.M. JF-Expert Member

  #3
  Feb 11, 2009
  Joined: Jan 22, 2007
  Messages: 425
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  Kwa wasiomjua Zombe tangu anasoma napenda niwaambie kuwa hakika alikuwa katili tangu O level alipokuwa anasoma Mwenge Secondary. Iwe ni kwenye michezo au katika mazungumzo ya kawaida utaona ni mtu hatari sana. Kikundi chake kilikuwa kinapenda kuonea na kuwa na tabia za ajabu ajabu tu. Labda zake zimefika- sheria ichukue mkondo wake.
   
 4. Bill

  Bill JF-Expert Member

  #4
  Feb 11, 2009
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 4,172
  Likes Received: 1,256
  Trophy Points: 280
  Ndio amejieleza, ni lazima ajitete karibu na ukweli. Lakini acha na wengine wanaoujua ukweli watueleze. Na hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
   
 5. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #5
  Feb 11, 2009
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,635
  Trophy Points: 280
  Mkuu Boney M heshima mbele.

  Kutokana na maelezo yako kuna uwezekano mkubwa kwa jeshi letu la polisi kuajiri watu wasiokuwa na sifa nzuri.Nina mfano mzuri sana wa jinsi chombo muhimu kama jeshi la polisi lisivyokuwa makini wakati wa ajira kuna jamaa mmoja mkorofi sana tulimaliza wote A level nilikuja shangaa amekuwa mkuu wa polisi Arumeru na sasa ni RCO Morogoro.
  Nilipoulizia kwa askari polisi wengine inakuwaje askari wa aina hii anapanda cheo kwa haraka nikajibiwa baba yake alikuwa RPC msahafu.
   
 6. M

  Mfumwa JF-Expert Member

  #6
  Feb 11, 2009
  Joined: Aug 29, 2008
  Messages: 1,456
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Unamzungumzia Msangi ama?. Kwa jeshi na polisi hayo ni mambo ya kawaida, watoto wao wengi ndio huchukua kazi zao ambayo tunaweza sema ni aina ya ufisadi walionao.

  Tunatakiwa tusubiri mahakama itasema nini, si haki kumhukumu mtuhumiwa kabla haijathibitishwa makosa yake. Hivyo wote sasa hivi ni watuhumiwa.
   
 7. C

  CottonEyeJoe JF-Expert Member

  #7
  Feb 11, 2009
  Joined: Jan 8, 2008
  Messages: 330
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35
  Zombe bwana.... I see he tried to pull a "Pinda Stunt 101" to see if he can get some sympathy like the PM..lol!!!!
   
 8. Next Level

  Next Level JF-Expert Member

  #8
  Feb 11, 2009
  Joined: Nov 17, 2008
  Messages: 3,159
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  I think he forgot that, this technique doesn't work every where......!
   
 9. Jeremiah

  Jeremiah JF-Expert Member

  #9
  Feb 17, 2009
  Joined: Feb 17, 2009
  Messages: 642
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35
  Asante sana kwa kwa kuniunganisha na jambo forum. maana yake nilikuwa nitafuta namna ya kutoa hata maoni yangu nashindwa .lakini sasa hapa ni mahali pake . asanteni tena .
  Kuhusu Zombe mimi nasema asubiri mkono wa sheria ili aipate haki anayostahili . malipo yake yapo hapapa duniani. Zombe atapata adhabu zote mbili .Duniani na mbinguni .kwa hali isiyotegemewa na wengi Rais kikwete anaweza akasaini hati ya kumnyonga hadi kufa bwana zombe . na ndiyo itakuwa haki yake kisheria. nashukuru kwa maoni ya wasomaji wa forum hii.
   
 10. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #10
  Feb 19, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,613
  Likes Received: 5,782
  Trophy Points: 280
  Habari zaidi!
  Mshitakiwa adai Zombe amemponza
  Maulid Ahmed
  Daily News; Wednesday,February 18, 2009 @19:27


  Mshitakiwa wa tisa katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa Mahenge, Morogoro, Michael Chonza, amedai mahakamani kuwa kukubali kwake kupewa mkono wa pongezi na Zombe, kumemponza.

  Mshitakiwa huyo wakati akitoa utetezi wake alipokuwa akihojiwa na Mzee wa Baraza, Magreth Mosi mbele ya Jaji Salum Massati jana, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, alidai kuwa mkono wa Zombe umemponza na kufanya ajumuishwe kwenye kesi ya mauaji ambayo hahusiki nayo.

  Alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo, kama aliona ni kawaida kupongezwa kwa kazi ambayo hakuifanya, Chonza alisema: “Nilijua tunapewa pongezi za jumla za kituo changu cha kazi Chuo Kikuu”.

  Yeye ni mmoja wa washitakiwa wanaokabiliwa na tuhuma za kuwaua wafanyabiashara Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi ‘Jongo’, Mathias Lung’ombe na dereva teksi Juma Ndugu. Tukio hilo lilitokea Januari 14, 2006 katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, Dar es Salaam.

  Siku moja baada ya tukio la kuuawa kwa wafanyabiashara hao, Zombe aliwaita askari wote wa kituo cha Chuo Kikuu waliokuwa doria siku ya tukio na kuwapongeza kwa kuwapa mkono na kuwaamuru maofisa Polisi waliokuwapo ofisini kwake, kuwapa mikono kwa madai wamefanya kazi nzuri ya kukamata majambazi.

  Katika utetezi wake, mshitakiwa wa 10, Abeneth Saro alidai mahakamani hapo kuwa alishangazwa kuingizwa katika orodha ya askari waliopaswa kushitakiwa wakati jina lake halikuwa kwenye orodha hiyo.

  Aliieleza Mahakama Kuu ya Tanzania inayosikiliza kesi hiyo, kuwa yeye na askari wengine waliitwa ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye alisoma majina ya askari wanaopaswa kushitakiwa na yeye jina lake halikuwamo.

  “Aliita majina na jina langu halikuwamo, hivyo akaniruhusu niondoke, nilipanda gari kurudi kituoni, nikiwa eneo la Jangwani, RPC alimpigia simu ofisa wa zamu ambaye alikuwa akiendesha gari kuwa anirudishe ofisini kwake, sikutoroka nilirudishwa na huko alinijumuisha na askari wanaopaswa kushitakiwa,” alidai mahakamani hapo.

  Sehemu ya mahojiano kati ya Abeneth na wakili wa utetezi, Majura Magafu yalikuwa kama ifuatavyo: Wakili: Tarehe 14/1/2006 kati ya saa 9 na 10 jioni ulikuwa sehemu gani? Saro: Polisi Magomeni. Wakili: Ulikwenda kwenye shughuli gani? Saro: Kawaida Ijumaa na Jumamosi OCD Mantage (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) mwenyewe anatupangia kazi.

  Wakili: Zoezi la kupewa maelezo na kupangiwa kazi liliisha muda gani? Saro: Kama saa 12 jioni. Wakili: Ulipangiwa wapi? Saro: Ubungo, Mabibo hadi Kibangu(Ubungo), nilikuwa na Konstebo Jane, Edson, Selemani, Emmanuel na Florian. Wakili: Kati yao wangapi walitokea idara ya CID? Saro: Ni wote. Wakili: Mlitumia usafiri gani? Saro: Kwanza OCD aliniongezea askari wawili wa official.

  Tulitumia daladala. Wakili: Katika kundi la askari, wote mlikuwa na silaha? Saro: Mimi nilikuwa na bastola aina ya Chinese wengine hawakuwa nazo, lakini wawili walikuwa wakachukue silaha kituo cha Urafiki. Wakili: Mlipanda pamoja daladala? Saro: Niliwaamuru kila mtu apande kivyake, mimi na Jane tukapanda Hiace moja.

  Wakili: Mlipanga kukutana wapi? Saro: Ubungo ila askari wawili na mimi na Jane tulipanga kupita Urafiki kuchukua redio. Wakili: Mliposhuka kulitokea nini? Saro: Tulipokuwa tunataka kuingia Urafiki, tulimkuta Mkuu wa CID Urafiki (Ahmed Makelle, mshtakiwa wa tatu) akitoka na askari wawili waliovaa sare.

  Wakili: Aliwapa maelezo yoyote? Saro: Aliniita haraka na Jane tukaingia katika gari akatwambia kuna dharura. Wakili: Bosi wenu aliwaambia mnaelekea wapi? Saro: Kwanza hakusema, wakati tunakata barabara ya Shekilango, alisema kuna ujambazi umetokea Sam Nujoma na kututaka tuwe makini.

  Wakili: Mlipofika mbele ya shule ya Mugabe mlikuta nini? Saro: Watu wamejikusanya, tulisogea na gari kabla ya kufika mbele, askari mwenye sare akasimamisha gari. Wakili: Aliwaambia nini? Saro: Makelle akanipa redio nisikilize, yeye akamfuata askari.

  Wakili: Jane alikuwa wapi? Saro: Nyuma ya gari, akafungua mlango akamfuata afande Makelle, mimi sikuwafuata kwa sababu niliambiwa na afande niangalie redio na gari kwani kulikuwa na watu wengi. Wakili: Ilichukua muda gani afande wako akarejea? Saro: Kama dakika tano. Wakili: Walirudi na kitu chochote? Saro: Hakuna.

  Wakili: Kuna jambo bosi wako alifanya? Saro: Alichukua redio na kusema majambazi wamekamatwa wakiwa na Sh milioni tano na bastola na yeye aliamuru wapelekwe Chuo Kikuu kuhojiwa. Wakili: Control room walisemaje? Saro: Walimuuliza kama ana majina, aliwajibu hana na walishaondoka na polisi wa Chuo Kikuu na call sign yao haijui.

  Wakili: Mlielekea wapi? Saro: Ubungo stendi ya mabasi yaendayo mikoani, tulipoahidiana kukutana na wenzangu. Wakili: Bosi wenu alifanya nini? Saro: Alitupa maelekezo ya kazi akaondoka. Wakili: Ulijua lini na wewe unahusika na mauaji haya? Saro: Februari tulipokwenda Tume ya Jaji Kipenka Musa kuhojiwa.

  Wakili: Taarifa ya kuitwa tume uliipataje? Saro: Kuna mtu alikuja ofisini na hati ya kuitwa kwenye tume. Tulikwenda na Jane kwa siku tofauti, nilitoa maelezo yangu waliandika na kurekodi. Wakili: Ulifika tume ya IGP iliyokuwa chini ya Mgawe? Saro: Sikuwahi kuitwa. Wakili: Kwingine kuhojiwa? Saro: Central Police, nilitoa maelezo yanayofanana na haya ya mahakamani.

  Wakili: Unaieleza nini Mahakama? Saro: Kwenye suala hili sihusiki kwa namna yoyote, sikukamata wala sijaua mtu yeyote, natumaini mahakama yako itatenda haki. Awali kesi hiyo ilikuwa inawakabili watuhumiwa 13, lakini washtakiwa watatu ambao ni Konstebo Noel Leonard, Koplo Nyangelera Morris na Koplo Felix Cedrick waliachiwa na mahakama hiyo baada ya kubainika hawakuwa na kesi ya kujibu.

  Washitakiwa waliobaki ni pamoja na Zombe, Christopher Bageni, Makelle, Jane, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Saro, Rashid Lema, Rajabu Bakari na Destus Gwabishabi. Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo baada ya wakili Denis Msafiri anayemtetea mshitakiwa wa 11, Lema, kuomba kuahirishwa ili aweze kwenda kuonana na mshitakiwa huyo kujua afya yake, kama anaweza kufika mahakamani leo kutoa utetezi wake. Kwa wiki nzima Lema hakuhudhuria mahakamani kutokana na kuugua.
   
 11. k

  kidumeso Member

  #11
  Feb 20, 2009
  Joined: Mar 23, 2007
  Messages: 49
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Huyo mkuu wa polisi aliyetajwa kuwa ni mtoto wa mkubwa aliye staafu(Marehemu), hata kuzungumza kingereza ni shida kubwa,kuna kipindi wakati akiwa muendesha mashitaka RMS Court arusha alikuwa anakimbia kesi zenye kuelekea watu kusema kizungu, bomu kabisa, nasijui nina alimpandisha cheo, hivi yule muhaya aliyekuwa PP RMS Court arusha alipotelea wapi?alikuwa kiwembe!!!!!!!!!!!
   
 12. Washawasha

  Washawasha JF-Expert Member

  #12
  Feb 20, 2009
  Joined: Aug 7, 2006
  Messages: 8,701
  Likes Received: 428
  Trophy Points: 180
  Tukifanya masihara zombe tutakuwa naye tena uswazi,si unajua serikali yenyewe hii zuga?
   
 13. Nemesis

  Nemesis JF-Expert Member

  #13
  Feb 20, 2009
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 3,844
  Likes Received: 1,110
  Trophy Points: 280
  Mkuu Zombe kisha cheza dili, mpaka sasa Serikali 1 : 3 Zombe mechi bado inaendelea. Mabao ya Zombe
  1. kutopatikana fedha wala madini na hata vilikopotelea.
  2. Kutofika katika eneo lolote la tukio, kufika polisi Urafiki na kufoka na kupotea bila kusalimia wala kutaka maelezo.
  3. kumtia kipapai Afande Lema (shahidi muhimu, aliyesema ukweli, aliyewapeleka wapelelezi msituni pande mahali yalipofanyika mauaji.

  Inasemekana kwamba Zombe ameshirikiana na rafiki zake, ambao ni askari magereza wamemnyesha sumu huyo shahidi ili ashindwe kutoa maelezo. Na mawakili wanacheza defence kali kuzuia magoli kwa kukataa kuendelea na kesi mpaka afande Lema apone.

  Hii mechi inaweza kuisha kwa 1 : 5 yaani ushindi mnono kwa Zombe.
   
 14. Balantanda

  Balantanda JF-Expert Member

  #14
  Feb 20, 2009
  Joined: Jul 13, 2008
  Messages: 12,322
  Likes Received: 1,039
  Trophy Points: 280
  Karibu sana Jeremiah.....Kiusahihi ni Jamii Forums na si Jambo Forums....Ubarikiwe sana mkuu na karibu sana JF,where we dare to talk openly
   
 15. u

  uporoto01 JF-Expert Member

  #15
  Feb 21, 2009
  Joined: May 23, 2008
  Messages: 4,741
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  Hivi mahakama inashindwa nini kahamia kwa muda jela kumsikiliza shahidi muhimu Lema ambaye yuko hoi na wafungwa wanadai hatamaliza wiki salama au ni mbinu ya huyu muuaji mzoefu Zombe kurudi uraiani?
   
Loading...