Zoa kimba

Dawa ya Malaria

New Member
Nov 8, 2010
4
0
FIKIRIA uko hapo tuseme Manzese basi. Unapita njia yako unasaka shilingi ambayo inaendelea kuota matairi na mbawa.

Mara ghafla unamwona kijana naye anapita akiwa na mbwa, lakini kamfunga kamba ya shingo ili asing'ate.

Lakini haishii hapo, unajua tena mbwa, haishi kunusanusa, na pia haishi kuacha alama kila anakopita, ili hata akitelekezwa na bwana wake, basi ajue jinsi ya kujirudia nyumbani bila matatizo.

Ndiyo sababu kama wewe ni mfugaji mzuri, ukiona mbwa anakojoa kila anakopita hasa kwenye mti au ukuta, basi ujue tu mwenzio anaweka alama asijepotea wakati anarudi homu baada ya kutelekezwa na bwana wake.

Vivyo hivyo kwa wanyama wengine jamii ya mbwa. Wachunguze duma nao wako hivyo, hawakosi kuacha alama kwenye miti kwa kukojolea. Turudi kwenye stori, mara mbwa anachuchumaa na kuacha bonge la kimba barabarani. Tena barabara ya lami!

Najua hamtashangaa wabongo, kwani ni jambo la kawaida tu hilo kwetu. Na kimba litaachwa hapo lipigwe jua na kisha lijikaukie na pembeni hapo kama hakuna mama n'tilie basi kutakuwa na mkaanga chipsi.

Imani ni kwamba harufu ya kimba la mbwa haiwezi kumzuia mwenye njaa kufakamia, hata kama analishuhudia bado bichi likifuka moshi. Shibe kwanza, mambo ya kuumwa tumbo ni matokeo tu, nani anajali.

Na hilo si kwako tu lakini hata wazee wa Site wanaposhuhudia si tu mbwa hata ng'ombe au mbuzi akivinjari mitaani na kushusha barabarani, wala, hakuna cha hatua wala ndugu yake, wanaona tu yote ni mambo ya kawaida, kwa sababu wengi tumezaliwa vijijini na kukua na wanyama.

Sasa hilo hapa Ughaibuni halipo, fikiria, tuko mtaani na mzee wangu Gabby, tunakula mitaa ya Vienna, Austria, mara jamaa wa Kizungu anakatiza mbele yetu na boonge la jibwa, kalifunga kamba ya shingo kwa sababu ile ile ya mwanzo.

Ghafla anasimama, na lile jibwa linachuchumaa na kuachia boonge la kimba, mbele ya macho yetu. Tunajiuliza, yale yale ya Manzese. Wakati tunajiuliza nini kitafuatia, mara Mzungu naye anachuchumaa na kuokota lile kimba na kulitumbukiza katika pipa la taka.

Kwanza tunashtuka tukidhani kalitoa pekupeku, la hasha, jamaa kumbe anazunguka na mfuko maalumu wa kushikia makimba kama hayo, kwani wanaamini kutokana na menyu ya mbwa wa huku, bila shaka kimba litakuwa likivinjari kila baada za dakika kadhaa hivi.

Akanikumbusha kule kwetu kijijini, ambako akina mama zetu nao wakati fulani kama kitegemezi kikiachia popote, wanakamata kimba na kulirushia porini huko, kuachia kuku koko wetu a.k.a wa kienyeji, wafanye msosi wa siku.

Tunapofuatilia hapa tunaambiwa kama mbwa wako ataonekana anaachia kimba nawe ukaliacha lilipo faini yake utaomba usile mwaka mzima kuifikia. Wenzetu wanaheshimu usafi na wanaupenda na kuuthamini. Sisi tunauchukia na kuudharau.

Ndiyo sababu hatuachi 'kuendesha' kila mwaka. Imekuwa kama msimu hivi, tuliojiwekea kwamba ikifika miezi fulani lazima kila Mbongo aharishe, tunakuwa kama waganga wa jadi, kwamba kila mara mtu anatakiwa aharishe ili kusafisha mwili.

Hivi kama tungekuwa tunajali usafi kama hawa jamaa zetu wa Vienna, huu msamiati wa kipindupindu bila shaka usingekuwa katika orodha ya maneno yetu ya Kiswahili, nzi tungekutana nao maabara tu.

Hebu fikiria nimekaa hapa Ughaibuni kwa haka kawiki kamoja, sijashuhudia nzi, wala mbu wala sisimizi, si kwamba hawapo, ila wamedhibitiwa na pengine kuna maeneo wametengewa ya kuishi na kutembelea hata kujirusha. Bila shaka ningeombwa nipelekwe kwenye zuu yao ningeoneshwa.

Jamaa hapa hawaoni sababu ya binadamu kuchangia makazi na mbu, nzi na wadudu wengine, mpaka hapo wanapokuwa wanahitajika kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi. Nenda baa yoyote Bongo, usipokuta nzi usiingie, inawezekana hapo pakawa pametambikiwa mizimu.

Na ukitaka kujua kuwa huyu ni mwenda baa Bongo au kwa mama n'tilie angalia kiganja chake cha kushoto, kimekaa kama kipepeo fulani hivi, kwa sababu kina kazi kubwa ya kufukuza nzi kwenye glasi na sahani au bakuli la mchuzi.

Mambo mengine tutapeana siku zijazo, lakini lingine la maana ni kwamba hapa jamaa wako katika harakati za uchaguzi wa Meya wa Jiji hili lenye wilaya 23, lakini husikii makelele ya kutukanana wala kuzodoana.

Watu wanafanya mambo yao kwa staha, kimyakimya, hatujasikia oh huyu kalala na fulani, oh huyu sijui kaanguka; wala, wanajibandikia mabango yao, wananchi wanawasikia na kuwaona kwenye luninga na vijimikutano vya kishikaji. Hawana muda wa kupoteza hapa, vinginevyo ile kwao.

Nimegundua kuwa ukiishi sana na nzi na mbu, utakuwa mpayukaji jukwaani, utakuwa na hasira muda wote na mgomvi. Wabongo tunaelekea huko, tukiwakataa nzi na mbu na wadudu wengine wa kisiasa, hatutaona uvivu kuzoa kimba la mbwa anyapo barabarani.

Tunapoonea kinyaa ubovu na uovu, ndipo nasi tunajizika humo na kukosa tofauti ya ubinadamu na mbwa na paka na nzi na mbu na wadudu waumao. Nimejisafishia mimacho angalau najirudia Bongo nikapambane na wadudu wangu nilowamisi kwa kawiki. Alamsiki.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom