Zitto: Tukiamua kizalendo uamuzi wa ICSID kuhusu IPTL mshindi anaweza kuwa Tanzania

Kiziwanda chema

JF-Expert Member
Sep 2, 2016
291
477
September 12, 2016 Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji iliwasilisha rasmi maamuzi yake Kwa pande zilizokuwa kwenye mgogoro kuhusu mradi wa kufua umeme Nchini, IPTL. Mahakama hiyo iliamuru kwamba Benki ya Standard Chartered ya Hongo Kong (SCB-HK) ilipwe dola za Kimarekani 148 milioni sawa na Fedha za Kitanzania shilingi 320 bilioni.

Mahakama hiyo Pia imeamuru kuwa kuchotwa Kwa Fedha kutoka akaunti maalumu ya TEGETA Escrow hakukuondoa Haki ya ya Benki ya SCB-HK kwenye kampuni ya IPTL na hivyo kisheria kwamba Benki hiyo Kwa sasa ndio mwenye uhalali wa shughuli zote za IPTL.

Ilinichukua Siku takribani 2 kusoma na kusoma tena tuzo hii (Arbitral Award) ili kuweza kuielewa haswa maana yake Kwa Nchi yetu. Ikumbukwe kwamba niliongoza Kamati ya Bunge iliyoagiza uchunguzi wa sakata la "TEGETA Escrow Account" na kuandaa Taarifa Maalumu ya Kamati ya PAC iliyosomwa na kukubaliwa rasmi na Bunge na kupitisha maazimio 8 yaliyopaswa kutekelezwa na Serikali.

Baada ya kuisoma Kwa kina Tuzo hiyo ya ICSID nilichoona Ni kwamba masuala Yale Yale ambayo PAC iliyafafanua Bungeni Mwezi Novemba, 2014 ndio hayo hayo yaliyopelekea tuzo hiyo. Kwa maana hiyo Ni kwamba iwapo Serikali ingetekeleza Maazimio yote ya Bunge Leo hii tungekuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kulimaliza suala Hilo kabisa na kuachana kabisa na mgogoro huu ambao unanyonya Fedha za Watanzania.

Masuala Makuu:

Kuna masuala Makuu Mawili (2) ambayo yakieleweka suala la kashfa ya IPTL litakuwa limeeleweka na maamuzi yanaweza kufanyika kumalizana nalo:

• Baada ya mbia wa kampuni ya Mechmar kufilisika nchini Malaysia, Ni Nani mwenye Haki na Mali za IPTL?

• Tozo ya malipo ya umeme uliozalishwa na IPTL ilizidishwa?

• Suala la Kwanza

PAC na ICSID zimesema Nini Juu ya Suala la Kwanza?

Kwenye Taarifa ya Kamati ya PAC tulionyesha Kwa vielelezo na ushahidi kwamba kampuni ya PAP haikuwa ina umiliki wa kihalali wa asilimia 70 ya Hisa za IPTL. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alionyesha dhahiri kuwa vyeti vya Hisa (Shares Certificates) za kampuni ya Mechmar kwenye IPTL walikuwa nazo Benki ya SCB-HK Kama dhamana ya mkopo waliowapa IPTL. CAG aliziona hati hizo Kwa macho yake kwenye uchunguzi wake ambao ndio uliotumika na PAC kufikia maazimio 8 ya Bunge.

Vile vile Kamati ya PAC ilionyesha Kwa ushahidi kuwa PAP hawakufuata sheria za Tanzania katika kumiliki IPTL ikiwemo kwamba walikwepa kodi kupitia kampuni iliyoitwa PiperLink ya British Virgin Island. TRA walikiri mbele ya Kamati kuwa wakati Mahakama Kuu inatamka kuwa PAP wapewe masuala (affairs) ya IPTL hawakuwa na uhalali wa kufanya Biashara Tanzania kwani hawakuwa wamepewa kibali na Kamishna Mkuu wa Kodi cha kuthibitisha utwaaji wao wa kampuni ya IPTL.

Hivyo Kamati ililiambia Bunge kuwa PAP ni matapeli wa Kimataifa waliopiga ganzi Mfumo wa Serikali ya Tanzania Kwa kutumia rushwa na hivyo kuhalalishiwa umiliki wa IPTL ili kuchota Fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya TEGETA Escrow Benki Kuu ya Tanzania.

Hata Gavana wa Benki Kuu alipowaomba PAP uhalali wa wao kumiliki IPTL walichotoa ni kitu kinachoitwa Deed of Assignment badala ya shares certificates. Watanzania watakumbuka kuwa Deed of Assignments ndizo zilizotumika kuiba Benki Kuu kwenye wizi wa EPA mwaka 2004-2005.

Jambo la kushangaza Ni kwamba karatasi hiyo ya kugushi ilikubaliwa na hivyo Bwana Harbinder Singh Seth wa PAP akaruhusiwa kuchota mabilioni ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Kwa mujibu wa Mwanasheria wa TANESCO Bwana Richard Rweyongeza TANESCO waliilipa PAP $245m Sawa na shilingi 530 bilioni. Itakumbukwa kuwa wakati PAC inasoma Taarifa yake Fedha hizo zilikuwa tshs 306 bilioni tu.

Katika tuzo yake ICSID imethibitisha kuwa PAP hakuwa mmiliki wa IPTL na hivyo alilipwa Fedha za TEGETA Escrow kimakosa. Hoja hii imethibitisha Hoja ya PAC na Bunge la Tanzania ambayo ilipingwa vikali na Serikali ya wakati huo ambayo iligeuka mtetezi wa PAP. Uamuzi wa ICSID kwamba TANESCO wailipe SCB-HK unathibitisha kuwa PAP alipewa Fedha za TEGETA escrow kitapeli.

• Suala la Pili: Hata Kama PAP wangekuwa Ni Wamiliki halali wa IPTL walilipwa ziada?

PAC tulisema nini?

Itakumbukwa kwamba PAC ililiambia Bunge kuwa mgawo wa Fedha ulipaswa kusubiri kukokotoa kanuni za mgawo ambazo ziliamriwa na Mahakama hiyo ya ICSID. Hoja kubwa ya PAC ilikuwa "Ni Kwanini tulifanya haraka kutoa Fedha kabla ya Uamuzi wa kiwango gani kilipwe?". Hoja hii ndio iliyochagiza kuwa mule ndani ya TEGETA escrow kulikuwa na Fedha za umma.

Uamuzi wa kukokotoa ukatolewa Mwezi Februari mwaka 2014 lakini katika mjadala mzima wa sakata la TEGETA escrow Serikali ilikataa kata kata kutekeleza Uamuzi huu. Hata kwenye Hoja za TANESCO mahakamani huko hawakuwa kabisa na Hoja kulinda Uamuzi ule.

Hata hivyo ICSID imeamua kuwa tulikuwa tunaibiwa Kwa kulipa tozo kubwa zaidi ya kiwango tulichopaswa kulipwa. Hii maana yake Ni kwamba Hata kwenye hizo za wizi tuliilipa PAP zaidi ya tulichopaswa kuwalipa.

ICSID Imeamuaje?

Katika magazeti ya Leo wakili aliyeiwakilisha TANESCO anasema yafuatayo "tulibishania Hoja ya kulipa Kwa viwango vya zamani ikaamuriwa hesabu zifanyike upya, Mahakama iliamuru hesabu zifanyike upya Kwa kutumia mkopo wa wana Hisa". Hii ndio Hoja ambayo PAC iliijenga Kwa muda mrefu na kubezwa na Serikali ndani ya Bunge Kwa mbwembwe zote.

Wakili wa TANESCO anaendelea kusema "kutokana na hesabu hizo gharama ilikuwa chini. IPTL ililipwa zaidi hivyo inatakiwa kurejesha Dola za Marekani zaidi ya milioni 100 Kwa TANESCO".

Hii ndio ilikuwa Hoja ya PAC ambayo ilitokana na maagizo ya CAG kwamba TANESCO wakae chini na SCB-HK kupiga hesabu upya. Hoja hii ilikataliwa na Serikali na TANESCO wenyewe ilipotolewa na PAC lakini Leo mwanasheria wa TANESCO aliyeiwakilisha TANESCO katika Mahakama ya Usuluhishi ya ICSID anakiri tuliwalipa zaidi IPTL.

• Jambo la Kushangaza Baada ya Hukumu Hii:

Jambo la kushangaza Ni kwamba, licha ya ushindi huu mkubwa Kwa Tanzania na TANESCO wanasheria wanataka tukate rufaa. Magazeti ya Serikali ya Dailynews na habari leo ndio yameongoza na habari hiyo. Ikumbukwe kuwa magazeti hayo ndio Siku zote yamekuwa yakiitetea PAP na Bwana Seth.

Ni dhahiri kuwa ama wanasheria wanataka waendelee kulipwa Fedha kwenye kesi au kuna shinikizo kubwa kutoka Kwa wanaofadika na mchezo huu wa kutapeli ili waendelee kufisadi Nchi.

• Tanzania Imeshinda

Uamuzi huu wa ICSID unatuweka kwenye nafasi nzuri sana ya kulimaliza kabisa suala la IPTL kwani umetuonyesha kuwa:

• Kwa miaka yote ya uwepo wa IPTL tumekuwa tunapigwa Kwa kulipa capacity charges Mara mbili ya kiwango tulichopaswa kulipa.

• Tulitapeliwa na Bwana Seth kupitia kampuni ya PAP ambayo Wamiliki wake wengine wenye 50% ya Hisa mpaka sasa hawajulikani Ni kina Nani licha ya kuwajua Kwa jina la Simba Trusts ya Australia.

Wakati wanasheria na baadhi ya maofisa wa Serikali waliofadika na mgawo wa TEGETA escrow wanataka kukata rufaa wanajua kuwa maamuzi ya ICSID hayana rufaa Kwa mujibu wa Ibara ya 53 ya mkataba wa ICSID inayosema "No appeal except those provided for in the ICSID Convention".

Hadhi yake Ni Sawa na maamuzi ya Mahakama ya juu kabisa ya Tanzania Kwa mujibu wa Ibara ya 54 ya mkataba wa ICSID (convention). Hata hivyo maamuzi hayo yanaweza kuombewa kufutwa Kwa kutumia Ibara ya 52(2) Kwa sababu maalumu ambazo ni zifuatazo:

a. Baraza la Usuluhishi halikuundwa kisheria (properly constituted).
• Ijulikane kuwa Baraza hili huteuliwa na washiriki wa kesi. SCB-HK waliteua msuluhishi wao, TANESCO waliteua wao na Kwa pamoja wakateua Rais wa Baraza. Hivyo TANESCO hawana Hoja maana Hata msuluhishi waliomteua wao kakubaliana na maamuzi haya ya tuzo hii.

b. Kwamba Baraza lilienda nje ya mamlaka yake.
• TANESCO walishiriki hatua zote za Mchakato wa Maamuzi haya, na hawakuwa na malalamiko yoyote Juu ya Mahakama kwenda Nje ya Mamlaka yake. Wanawezaje kuwa na malalamiko sasa. Hata msuluhishi wao kakubali maamuzi haya.

c. Kwamba kulikuwa na rushwa kwenye kufikia maamuzi haya.
• Hili litawapasa TANESCO watoe ushahidi kuwa Hata msuluhishi waliyemteua wao (ambaye amekubaliana na hukumu hii) naye alihongwa.

d. Kwamba tuzo haina sababu za kufikia maamuzi haya.
• Kwa walioisoma tuzo hii wanajua kuwa sababu zipo kinagaubaga kabisa.

• Maoni na Ushauri Wangu kwa Serikali

Kwa maoni yangu kutaka kesi iendelee Ni kutaka kulinda maslahi ya wanaofadika na suala zima la IPTL. Suala hili sasa liishe. Nchi imeshaliwa sana. Itoshe.

Ushauri wangu Kwa Serikali Ni Kama ifuatavyo:

• Kutekeleza tuzo hii ya ICSID bila kusita.

• Kuiamrisha kampuni ya PAP kurejesha Fedha zote za ziada ilizolipwa kutoka akaunti ya TEGETA escrow. PAP walilipwa Bilioni 530. Hivyo kwa mujibu wa tuzo hii ya ICSID PAP wanapaswa kurudisha Shilingi Bilioni 202.

• Kuitaka kampuni ya PAP kuilipa Benki ya SCB-HK Shilingi Bilioni 320 Kwa mujibu wa Hukumu hii. Hii kutokana na hati ambayo PAP iliwasilisha Benki Kuu (BOT) "Kwamba madai yeyote yakitokea katika IPTL, PAP ndio watalipa (Kisheria Huitwa "indemnity")."

• Kuishtaki Kampuni ya Kitapeli ya PAP na Bwana Harbinder Singh Seth Kwa utapeli na utakatishaji wa Fedha Kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

• Kuchunguza na kuwashitaki maofisa wote wa Serikali walioshirikiana na Seth kuchota Fedha Benki Kuu.

• Kuilipisha faini Benki ya StanBic Tanzania Kwa kushiriki kwenye vitendo vya kutakatisha Fedha kufuatia miamala ya TEGETA escrow.

• Kufunga kabisa suala la IPTL Kwa kuvunja mkataba na kuitwaa mitambo Kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Zitto Kabwe Ruyagwa
Sept 23, 2016
 
Ushauri unaweza kuchukuliwa lakini pia kuachwa ili swala tukubali tumeshachelewa
 
wanufaika wa mgao ni wengi na wengine ni viongozi wakubwa. ndo maana serikali inapata kigugumizi kuamua.
 
Zitto nakuunga mkono kwa 100%.Wewe kweli ni MZALENDO.Mimi ni mwanasheria, uchambuzi wa Zitto upo kisheria sana. Uwezo wa kukata rufaa haupo kwa mujibu wa mkataba unaounda Tribunal hiyo. Pili, hata kama kungekuwa na fursa ya rufaa, bado hakuna hoja ya msingi ya kukata rufaa. Hiyo kampuni ya mawakili wanataka waendelee kulipwa. Mlipaji wa award/tuzo hilo yupo, PAP. Alijifunga mwenyewe kwa "indemnity clause" iliku justify kupata pesa toka Escrow account. Alisema ikitokea mdai yeyote akajitokeza PAP itawajibika kumlipa. Mdai amejitokeza, PAP wana wajibu wa kumlipa. Siyo serikali ya TZ. Kisheria serikali haina wajibu wa kulipa hata senti tano. Tusubiri tuone what next. Hapa ndo tutajua shareholders wa SIMBA TRUST Co.LtD ni nani. Na je wana uhusiano na serikali?
 
Za umma au sio za umma..... ilikuwaje PAP walipwe kabla ya kukokotoa nyongeza kwenye tozo?
The most worrying thing:
1. Utamwa/ and the Justice system
Inatisha sana kuona hata jaji wa mahakama kuu anapindisha sheria Ki Mafia hivi. Who the hell can invest in this country if the justice system is that corrupt? Pesa iliyotolewa kama loan Na world bank, IPTL wala VIP hawa kuwa Na thamani hata kidogo; how the Utamwa came with that conclusion ?

2. Lowassa ame wahi kuifukiza kampuni ya Uingereza, ile ya Maji. Nothing happened. Why is it a big deal for IPTL to be told to pack and leave? Obvious Kikwete involved and this wil be going on over the years coming!!
 
Hili swala mtego wake ni mdogo sana. Lakini umekaa pabaya sana. Kuutegua inahitajika
 
Angalau Leo Zitto hajamnyooshea kidole Rais. Naona ameanza kuzinduka sasa
 
Ninakubaliana na yote aliyoainisha Zitto. Serikali ifuate ushauri huu mzuri. Baada ya Sing huyo kutekeleza hayo (kulipa alichotutapeli), serikali itaifishe hiyo IPTL na kuwa mali ya TANESCO ambao wataiendesha, wasiikodi wala kuingia ubia na kampuni au mtu mwingine yo yote.

Kwa sasa TANESCO wasimlipe tena capacity charges huyo singasinga. Mheshimiwa rais nadhani anafuatilia ushauŕi unaotolewa kuhusu jambo hili zito. Tuendelee kutoa ushauri wa kujenga.

Suala si ku appeal ila labda kulipeleka kwenye mahakama kuu yetu kukaza utekelezaji wa hukumu hiyo ICSID.
 
Palikuwa na tetesi hapa jukwaani kuhusu wamiliki wa Simba Trust,nadhani wenye ufahamu wa kutosha watujuze hiyo mijizi ni nani
 
Back
Top Bottom