Siku ya Jana ilikuwa ni siku ya kumuaga aliyepata kuwa spika wa bunge la tisa, Samwel Sitta kwa mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma. Sitta aliagwa bungeni Dodoma sehemu aliyoitumikia muda mrefu kama mbunge na hatimae spika wa bunge almaarufu kama bunge la tisa lenye kasi na viwango na kuwa mtu wa kwanza kuagwa ndani ya ukumbi wa bunge kwa heshma kubwa aliyojijengea wakati akiongoza bunge hilo. Miongoni mwa waliopata nafasi ya kutoa salam za pole ni mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe.
Zitto katika salam zake fupi alisema Sitta anakumbukwa kama spika pamoja na vyeo vingi alivyoshika kwa sababu ya 'Legacy' yake aliyoiacha kwenye bunge ikiwemo kuandikwa sheria mpya ya bunge na uanzishwaji wa mfuko wa bunge.
Pia Zitto alimsema Sitta kama mtu aliewabana mawaziri wajibu kwa ufasaha na kutoa fursa kwa wabunge wote ikiwemo wa vyama vya upinzani. Kuomba radhi popote alipokosea na Zitto amesema unafaa kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi.
Zitto aliongeza kwa kusema njia pekee ya kumuenzi Samwel Sitta ni kuimarisha uhuru na heshma ya bunge. Zitto alimaliza kwa kusema Sitta Ameishi katika uzalendo, ndoto ya Tanzania imara na yenye heshima na vijana wengi aliowafunda.
Aidha Tundu Lissu katika salam zake alisema Sitta alama ya Sitta katika miaka yake mingi ya utumishi, ni miaka mitano ya uspika wake katika bunge, alitaka bunge lenye meno na kuisimamia na kuidhibiti serikali. Alihitaji bunge kama mhimili wa dola na sio msindikizaji wa mihimili mingine ya dola. Aliongeza hakuwa kibaraka wa mtu yeyote na alionyesha kuwa mtu mwenye msimamo huru.
Mwili wa Samwel Sitta unatarajia kuzikwa leo Urambo mkoani Tabora, ameacha mjane na watoto watano.