Zitto na ACT, wabariki uuzwaji wa kiwanja cha Hospitali ya Wilaya kilichotengewa tsh mil 400

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,490
54,884
ZITTO NA ACT WABARIKI UUZWAJI WA KIWANJA CHA HOSPITALI YA WILAYA KILICHOTENGEWA TSH MIL 400 ZA UJENZI KATIKA BAJETI HII 2017/2018

Katika habari ambazo Mbunge wa Kigoma mjini kupitia tiketi ya chama cha ACT –WAZALENDO ZITTO ZUBERI KABWE amekuwa muoga kuizungumzia ni kuhusiana na kiwanja cha umma namba PB2 BUZEBAZEBA, na hata alipobanwa kwenye mkutano wa wananchi uwanja wa Mwanga Community Centre, hakufurahishwa kabisa na swali hilo na akalazimika kulijibu kimafumbo huku akibariki uporwaji huo kwa kusema kuwa ‘’ hospitali ya wilaya itajengwa’’ watu wakauliza wapi ? akasema kuwa ‘’ pale pale tutaamua kama tutajenga chini ama juu’’.

Kwa kuwa Zitto amekuwa muoga kuliongelea swala hili huku chama kikitoa onyo kali kwa madiwani na viongozi watakaothubutu kuendeleza mjadala wa mgogoro huo, sambamba na madiwani wakitishiwa kunyang’anywa kadi za chama na kuzima baraza la madiwani la dharura lililoitishwa 09/11/2017 ndani ya Manispaa ya Kigoma/ujiji.
Fuatilia Makala hii ya kina ili kuelewa Zaidi mgogoro huu, kisha naomba popote ukimuona Zitto nisaidie kumuuliza swali hili hili mpaka pale atakapokuja na majibu sahihi ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ukizingatia serikali imekwisha pitisha tsh milioni 400 za ujenzi hivyo tunapaswa kuanza kujadili utekelezaji sambamba na kumkumbusha Mh. Mbunge aache kuingilia maamuzi rasmi ya vikao vya baraza la madiwani.

Makala hii na mwandishi wetu
Wakati viongozi wa chama cha ACT –WAZALENDO kwa makusudi kabisa na maslahi mapana ya matumbo yao wakiazimia kuuzika mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda wa miezi mitatu mfululizo, mgogoro baina ya wananchi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kiwanja Na. 2PB Buzebazeba kilichotengewa tsh mil 400 za ujenzi wa hospitali ya wilaya katika bajeti ya 2017/2018 , dhidi ya taasisi ya kidini ya madhehbu ya Shia ikifahamika kama AHLULBAYT ISLAMIC CENTRE chini ya mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ndg Mohsin Mohamedtaki Abdullah Laljimaaraufu kama SHENI.

Nikiwa kama mtafiti mwandamizi wa jarida la THE FRONT-PAGE nimezama chimbo na kuibuka na madudu ya ajabu na nyaraka kibao zenye viasharia vya 100% ya rushwa dhidi ya madiwani wa ACT-Wazalendo, Rushwa dhidi ya viongozi wakuu wa chama ACT-Wazalendo, pamoja na ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Ungana nami kusoma Makala ya uchambuzi wa kina niliyokuandalia juu ya mgogoro huo kumbuka kwamba Manispaa ya Kigoma/Ujijini mwanachama wa OGP (Open Government Partnership) hivyo niko katika utekelezaji wa OGP katika ngazi ya chini kabisa kwa wananchi.

DIBAJI (INTRO)
Mgogoro huu ni wa muda mrefu ambapo mabaraza ya madiwani yalioyotangulia yalimkatalia katukatu kujenga katika eneo hilo bw.Mohsin Mohamedtaki Abdullah Lalji(SHENI) chini ya taasisi yake ya AHLULBAYT ISLAMIC CENTREkwa madai kwamba ni eneo la zahanati na uongozi wa manispaa umekusudia kujenga hospitali ya wilaya. Bwana sheni kwa kipindi chote alikuwa akijaribu kuzirubuni tawala zilizopita bila mafanikio.

KUIBUKA KWA MGOGORO HUO
Mnamo tarehe 03/10/2017 majira ya asubuhi bwana Sheni alionekana akianza ujenzi katika eneo hilo swala ambalo lilimlazimu mwenyekiti wa Mtaa wa TAIFA bw. Bakari Songoro kumzuia kwa madai kwamba eneo hilo ni la umma (public) liko chini ya zahanati ya buzebazeba ndipo BW. SHENI akaonyesha kibali cha ruhusa ya ujenzi (BUILDING PERMIT) cha tarehe 23 april 2015 kilichosainiwa na Engineer wa Manispaa Bw. Boniface William chenye kumb. Na. KUMC/WK/AHLULBAYT/01

Licha ya kuonyesha kibali hicho m/kiti huyo wa mtaa alimkatalia kwa madai kwamba kibali hicho hakitumiki kwani nichamuda mrefu. Bw. Sheni akafanya magumashi siku hiyohiyo akaja na kibali kingine kimesainiwa naEngineer wa Manispaa ambaye hakuandika jina lake lakini kinachotia fora Zaidi kibali hicho kimeandikwa 2017/2018 lakini sehemu ya tarehe ya kutolewa kibali haikujazwa kwa maana haijulikani kimetoka lini hivyo akaendelea na ujenzi.

Taarifa za ujenzi katika kiwanja hicho ziliwashtua wakazi wengi wakiwamo waheshimiwa madiwani ukizingatia katika kikao cha kupitisha bajeti ya mwaka 2017/2018 walitenga fungu la ujenzi wa hospitali ya wilaya katika eneo hilo na kwa bahati nzuri serikali ya rais Dk. John Pombe Magufuli ikapitisha tsh milioni 400 badala ya mil 70 zilizoombwa kwenye rasimu ya bajeti. Siku iliyofuata tarehe 04/10/2017 Jumla ya madiwani 6 wakiongozwa na Revocatus Chimpando (Baba levo) walimuashia moto mkurugenzi na kumtaka aziwie ujenzi mara moja. Nae mkurugenzi akatekeleza kwa kuandika STOP ORDER(hati ya zuio la ujenzi) mnamo tar 05/10/2017.

Taarifa ya STOP ORDERilimshtua bw. Sheni siku hiyo hiyo ya tar 05/10/2017 akaenda kulalamika kwenye chemba ya sheria (Kigoma Advocates Law Chamber) nao wakandika barua ya malalamiko kwa mkurugenzi wa manispaa iliyojaa vitisho na ujuaji, huku wakijikanganya katika maelezo yao.

Barua hiyo inasomeka kwamba “TAARIFA YA MADAI NA KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI PINDI UTAKAPOTEKELEZA AMRI YA KUSIMAMISHA UJENZI (STOP ORDER)” huku katika hoja yao ya kwanza wameandika kwamba ‘’mteja wetu ni mmiliki halali wa kiwanja na. 2PB buzebazeba tangia tar 01/04/2017 baada ya kulipia ada zote stahiki na kupewa kiwanja hicho’’. Wanashindwa kuelewa kwamba awali Bw. Sheni alikuja na kibali cha ujenzi cha tar 23 april 2015. Barua zote zipo na zinafahamika na mwenye kutaka anaweza kuzipata muda wowote akizihitaji.

Barua hiyo ilipokelewa masijala ya manispaa na kupigwa muhuri tar 06/10/2017 lakini cha kusikisha kaimu mkurugenzi Dr. John S. Tlatla akaandika barua akiwajibu Chemba Ya Sheria siku hiyo hiyo ya tar 06/10/2017 ya kuruhusu kuendelea na ujenzi huo kwa maelezo kwamba“ napenda kukufahamisha kwamba uongozi wa manispaa ulijadiliana na mteja wako jana tar 05/10/2017 …. Hivyo unajulishwa kuwa mteja wako AHLULBAYT ISLAMIC CENTRE ameruhusiwa kuendelea na ujenzi”.


BREAK- TUTAFAKARI KIDOGO KWA KUJIULIZA MASWALI YAFUATAYO;
tar 05/10/2017 - STOP ORDERtoka kwa Kaimu Mkurugenzikwenda kwa sheni hatujui ilikuwa saa ngapi?
Tar 05/10/2017 - SHENI kwenda Law Chamberna kulalamikia STOP ORDER hatujui ilikuwa saa ngapi?
Tar 05/10/2017 - LAW CHAMBER wakaandika barua ambayo iliyopokelewa tar 06/10/2017 masijala
Tar 05/10/2017 - UONGOZI WA HALMASHAURI ulijadiliana na viongozi wa AHLULBAYT ISLAMIC CENTRE na kuruhusu ujenzi uendelee.hatujui ilikuwa saa ngapi?
Je michakato hiyo yote inawezekana ndani ya siku moja?

Inawezekanaje kukaa kikao cha kujadili malalamiko siku moja kabla ya barua ya malalamiko kufika ofisini yaani kikao cha kujadili malalamiko tar 05/10/2017 na tar 06/10/2017 masijala kupokea barua ya malalamiko.

Kwa nini michakato yote ifanywe na kaimu mkurugenzi hasa pale mkurugenzi anapokuwa amesafiri.
Vilevile Kwenye kabrasha la orodha ya vibali vya ujenzi vilivyotolewa mwaka 2015 ambapo jumla ya vibali 197 vilivyotolewa hakuna kibali kilichotolewa kwa taasisi ya AHLULBAYT ISLAMIC CENTRE.
hivyo kibali chenye kumb. Na. KUMC/WK/AHLULBAYT/01 kilichosainiwa na eng. Boniface William bado ni kiashiria cha uwepo wa rushwa kwenye mchakato huo.

Kama ulibahatika kuona taarifa ya habari iliyorushwa na AZAM TV kuhusu mgogoro huu hasa baada ya Mwanachama wa ACT Bw. Wiston Mogha kufanya Press Conference(kikao na waandishi wa habari) akimtaka m/kiti wa kamati ya mipango miji bw. Butije ambaye pia ni diwani wa kata yenye mgogoro ya Rusimbi kuacha kutumika kibiashara na arudi kusimamia maslahi ya wananchi, katika story hiyo ambayo niliirekodi pia (ninayo) mkurugenzi mtendaji analalamika kwamba “…… mnamo tar05/10/2017 tulimuandikia mwekezaji huyo STOP ORDER ila tunashangaa mpaka sasa hajarespond” (yaani hajatii amri ya kuzui kuendelea na ujenzi).

Hivi mkurugenzi anaposema kuwa jamaa mpaka leo hajatii amri ya kuzuia ujenzi inamaana haitambui barua ya tarehe 06/10/2017 yenye kumb. Na. L20/2/Vol V/216 iliyotoa ruhusa ya kuendelea na ujenzi yenye maneno yafuatayo “napenda kukufahamisha kwamba uongozi wa manispaa ulijadiliana na mteja wako jana tar 05/10/2017 …. Hivyo unajulishwa kuwa mteja wako AHLULBAYT ISLAMIC CENTRE ameruhusiwa kuendelea na ujenzi”.

TUNAENDELEA BAADA YA BREAK
Baada ya ofisi ya mkurugenzi kutoa kibali cha ujenzi, baadhi ya madiwani waliona kuwa mkurugenzi anataka kuwaingiza kwenye mgogoro na anawaletea dharau hivyo tarehe 25/10/2017 kamati ya mipango miji ikakutana kwa dharura kujadili kadhia hii na kuhudhuriwa na wajumbe 8 kati ya tisa, kamati ilikwenda mbali Zaidi kwa kumwalika aliyekuwa m/kiti kamati ya mipango miji wa baraza lililopita 2010 – 2015 (Mwl Adamu), katika mazungumzo na mwenyekiti huyo alieleza kuwa hata muhula wao wa utawala bw. Sheni alikuwa akijaribu kurubuni baadhi ya wadiwani ila hakuweza kujenga katika eneo hilo kwa sababu ‘’tulikuwa na msimamo na kumkatalia ukizingatia sheni hakuwa na nyaraka yoyote iliyotokana na kikao halali cha baraza la madiwa kilichomridhia aweze kupea eneo hilo’’.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa sheni alidiriki kwenda hadi kwa Rais Kikwete ila Rais alimrudisha na kumtaka arudi kwa wananchi kwa kuwa eneo hilo ni la umma (Public Building) hivyo ridhaa ipo kwa wananchi wenyewe.
Sheni alirudi Manispaa ya Kigoma/Ujiji kisha akaomba kikao na wajumbe wote wa kamati ya mipango miji, kikao alichokigharamia mwenyewe bw. Sheni. Licha ya mazungumzo ya muda mrefu katika kikao hicho lakini wajumbe kwa mara nyingine tena walimkatalia na kumpa alternative (njia nyingine au mbadala), mwalimu adamu anaelezea kuwa,kwa kuwa dhamira ya sheni ni kujenga chuo cha walimu na kwa kuwa Manispaa kipindi kile ilikuwa inaendelea na upimaji wa viwanja vipya katika maeneo ya KASIMBU, BURONGE na MWASENGA hivyo sheni alishauriwa kuchagua katika maeneo hayo ambayo upimaji unaendelea ili wampatie kiwanja lakini Bw. Sheni alikataa. Hayo aliyasema mwalimu adamu katika kikao cha kamati ya mipango miji cha tar 25/10/2017.

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu kikao kikaenda kwenye agenda ya maazimio na wajumbe kwa pamoja wakaazimia ya kwamba;
Ujenzi usimame na lipelekwe zuwio la pili (stop order) nyingine kuzuwia ujenzi katika kiwanja hicho
Mkurugenzi alete ramani ya michoro (master plan) ya zamani
Mkurugenzi alete muhtasari wa kikao kati ya kamati ya mipango miji na bw. Sheni kilichoketi utawala uliopita (2010 -2015)
Kamati iitishe mkutano wa baraza la madiwani la dharura kuhusu mgogoro wa kiwanja PB 2 kilichotengewa milioni 400 za ujenzi wa hospitali ya Wilaya ili kumaliza utata huu unaoendelea.

Siku iliyofuata Revocatus Chimpando (baba levo) alianza kukusanya saini za madiwani ili kupata akidi ya kuitisha kikao cha baraza la madiwani la dharura na baadae akafanikiwa kupata saini 14 kati ya 28 ambayo ni idadi ya madiwani wote (14//28) hivyo kutimiza akidi na kaim meya (HUSSEIN KALYANGO) akaridhia kikao cha baraza maalumu la madiwani kifanyike tarehe 9/11/2017. Siku moja kabla ya kikao magumashi yakaanza madiwani wakatumiwa sms kwamba kikao hakitokuwepo, ndipo baadhi ya madiwani wakahamaki na kuanza kumshambulia Meya kwa simu baadae meya akawa mpole na kutengua maamuzi yake na kusema kwamba basi kikao kitakuwepo.
Asubuhi saa moja siku ya kikao tar 9/11/2017, Madiwani wote wa chama cha ACT Wazalendo wakaitwa kwenye kikao cha CHAMA. Huko zikaibuka pande mbili, madiwani na wanachama wacheche walikuwa upande wa wananchi na wengine walisalia kwa bepari (sheni), pande hizi zilivutana bila mafanikiohuku wananchi tuliotaka kuhudhuria kikao hicho tukipigwa doro hadi saa 5 madiwani wa ACT walikuwa hawajafika kwenye ukumbi wa manispaa. Mara pap!!! Manidwani wakiongozwa na meya wakaingia ukumbini kabla hata ya jambo lolote kutendeka meya akasimama akanukuu kanuni ya nne ya uendeshwaji wa baraza la madiwani na hapo hapo akakifunga kikao kabla ya kikao hakijafunguliwa. Watu wakatoka kimakundi makundi wakizozomoka ( minong’ono ya kutokuridhishwa na jambo).

Basi kuanzia hapo harakati za kudai kikao cha baraza maalum zikawa zikiendelea kwa kasi ikawa gumzo kutoka kila kona ya mji swala ambalo lilipelekea kukipasua chama mara mbili sambamba na kulipasua baraza la madiwani. Baadhi ya madiwani waliitwa kwenye kikao cha maadili na kupewa onyo kali la kutishiwa kunyang’anywa kadi za chama.
RIPOTI YA UCHUNGUZI YA CHAMA CHA ACT KUHUSU SAKATA LA KIWANJA PB2
Kamati ya sekretarieti ya mkoa ilikutana tarehe 22/10/2017 katika ukumbi wa AWIMO kwa kile ilichoeleza kwenye ripoti hiyo kuwa ni kutokana mgogoro huu kusambaa katika mikutano ya kijamii na kuwa gumzo. Kamati iliwahoji viongozi wa jimbo waliowakilishwa na KATIBU (Azizi Ally, Mwaiposa, Hanzuruni Kibera), Katibu wa madiwani (Hamisi Rashidi) Kaimu Meya (Hussein Kalyango), ofisi ya mbunge iliwakilishwa na Katibu wa mbunge (Deo Nzigama) pamoja na diwani Revocatus Chipato.

Baada ya majibu ya waliohojiwa kujikanganya, 23/10/2017 kamati ya serketariete ya mkoailikutana ukumbi wa Malonya -Kibirizi na iliamua kuunda KAMATI NDOGO YA UCHUNGUZI WA KINA kuhusiana na sakata hili na kwa maslahi mapana ya chama. Kamati iliwateuwa Ayubu Akida, Juma Ramadhani na Salim Shaban.

Katika utekelezaji wa majukumu yao KAMATI YA UCHUNGUZI WA KINA iliwaita baadhi ya madiwa akiwemo Meya na Naibu meya, mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji,Katibu wa Jimbo na Katibu wa madiwani bw. Hamisi rashidi. Kamati iliwataka watoe maelezo yao kwa maandishi ndani ya masaa 48 na baadae iliwahoji mmoja mmoja kwa nyakati tofauti isipokuwa katibu wa madiwani ambaye aligoma kujibu wala hakuitikia wito.

Kamati ya uchunguzi ilikuja na ripoti ya kamili na majibu ya uchunguzi wa utafiti wao yalikuwa kama ifuatavyo;
ALHULBAYT ISLAMIC CENTREsio mmiliki wa kiwanja PB2 kwa kuwa hakuna kikao chochote cha baraza la madiwani kuanzia mwaka 2007 kilichoketi na kupitisha/kumilikisha kiwanja hicho.

Kamati ya uchunguzi imegundua kuwa Alhulbayt Islamic Centre walitumia njia ya mkato kujipatia umiliki wa kiwanja hicho.
Ripoti ya kamati imegusia mambo mengi yakiwemo ya vibali feki vya ujenzi bila kuzingatia utaratibu wa sheria kama vile kibali alichopatiwa sheni mwezi wa 10/2017 kisichokuwa na tarehe na wala hata aliyesaini hakuandika jina lake. Ripoti inaeleza kuwa mgogoro huo umechochewa kwa kiasi kikubwa na utaratibu wa magumashi (njia ya mkato) katika kujipatia kiwanja hicho.

Na mwisho kamati iligundua kuwa kuna udhaifu mkubwa kwa baadhi ya viongozi wa chama na madiwani, hivyo kamati kupitia ripoti hiyo imetoa mapendekezo ya adhabu zinazopaswa kuchulikwa na sekretarieti ya ACT – MKOA dhidi ya wafuatao;

MEYA; meya kushindwa kutumia mamlaka yake kikamilifu na kupelekea mgogoro huu kuendelea na kutopatiwa ufumbuzi mpaka sasa ikiwa ni pamoja na kuachia ujenzi kuendelea katika kiwanja hicho, Kushindwa kumchukulia hatua za kinidhamu makamu meya kwa kuondoa zuwio la ujenzi(STOP ORDER) bila kuwasiliana naye. Mwenyekiti wa mipango miji kutoitisha kikao cha kamati ya mipango miji kutatua mgogoro huu na kupata ukweli wa utolewaji wa kibali cha kuendeleza ujenzi.

MAAZIMIO YA KAMATI YA UCHUNGUZI
Viongozi wa jimbo wapewe onyo kali kwa viongozi wafuatao
Selemani Simba – M/Kiti Wa Jimbo
Azizi Ally – Katibu Wajimbo,
Anzuruni Kibera – Katibu Mwenezi Wa Jimbo
Meya apewe onyo kali na kumuelekeza ahakikishe mgogoro huo unapata ufumbuzi na kiwanja hicho kinarudishwa kwenye mikono ya serikali.

NAIBU MEYA apewe onyo kali
MWENYEKITI WA MIPANGO MIJI; aondolewe kwenye kamati ya mipango miji kufuatia kamati hiyo kukumbwa na migogoro mbalimbali isiyoisha inayopelekea kuwagawa baadhi ya madiwani kwa kutuhumiwa kwa rushwa.

KATIBU WA MADIWANI (Hamisi Rashidi) kuvuliwa ukatibu wa madiwani.

Binafsi ninapenda kuwapongeza chama cha ACT kupitia Sekretarieti ya Mkoa na KAMATI HALALI YA UCHUNGUZI WA KINA kwa juhudi na ukomavu wa kizalendo walionyesha mpaka kufikia maamuzi haya. Lakini jambo la kusikitisha na kuchefua Zaidi ni pale maamuzi haya kwa mukusudi kabisa na maslahi mapana ya matumbo ya viongozi wa wakuu ACT (TAIFA) walipoamua kuja kuyazima maamuzi halali yaliyotokana na ripoti ya utafiti ya KAMATI HALALI YA UCHUNGUZI iliyoundwa (Ayubu Akida, Juma Ramadhan (katibu mwenezi ACT-Mkoa) na Salim Shaban) kupitia kikao rasmi.

Ushiriki wa mh. Mbunge zitto katika sakata hili ni wazi kuwa yeye ndiye aliyezuwia ripoti ya kamati ya uchunguzi isisomwe kwenye kikao maalum kilichoketi ofisi ya mkoa ya chama na badala yake chama cha ACT MKOA kilikuja na maazimio ya kibabe. Azimio la kwanza lilisomwa na makamu mwenyekiti ACT bara BW. SHABANI MAMBO ambaye alitoa msimamo wa chama ya kwamba , kiwanja chenye mgogoro ni mali ya SHENI na chama kimeamua SHENI ajenge hivyo chama kimeufunga (kuuzika) mjadala wa mgogoro wa kiwanja namba 2PB. Mwenyekiti huyo alikwenda mbali zaidi kwa kuwapiga marufuku madiwani na viongozi wa chama kulizungumzia swala hili hadharani na endapo diwani wa kata akibainika kazungumza tunamnyang’anya kadi na kumfukuza uanachama.

Azimio la pili lilisomwa na mwenyekiti wa mkoa ambaye ataunda timu ya watu wachache kwa kuwashirikisha wenyeviti wa kamati ili waende kumuona bw. SHENI na kitakachopatikana ninaamini tutafurahi wote. Na hapo ndipo ikawa mwisho wa mjadala juu ya kiwanja … na hata maazimio yale ya kamati ya mipango miji ya kumng’oa mwenyekiti wa kamati ya mipango miji kushiriki ubadhirifu wa kupoteza kiwanja cha umma yakafia hapo.
Siku hiyo hiyo ya kikao ripoti ya kamati ya uchunguzi ilisambazwa kwa kasi ya ajabu kwenye mitandao ya kijamii, swala ambalo liliwashtua viongozi wa chama pamoja na wajumbe wa kamati ndipo wakaanza kumsaka aliyesambaza. Baada ya siku tatu RAPHAEL LUKINDO akafikishwa kituo cha polisi kigoma kati (CENTRAL POLICE) kwa madai ya kusambaza ripoti hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook lakini mpaka sasa hawajawahi kuikana ripoti bali wanamshinikiza kueleza alipoitoa ripoti hiyo.

Kwa ufupi ni kwamba kigugumizi cha mh. Mbunge, na namna anavyokacha kujibainisha yuko upande gani, ni dhahiri kwa mh. Mbunge anahusika kwa 100% hasa ukizingatia mkutano wake wa mwisho na wananchi haikuwa sehemu ya agenda yake na hata alipoulizwa hakufurahishwa na swali hila na kulijibu kwa mafumbo kuwa hospitali itajengwa katika eneo lililobaki kama halitotosha watapandisha ghorofa.
Kauli hii ni dhahiri kuwa mbunge anahusika ila hataki wananchi wamwelewe kama yuko upande wa BEPARI.

MWISHO WA MAKALA HII NDIO MWANZO WA MAKALA NYINGINE
 
Mkuu hii tabia ya kuleta habari ya upande mmoja huwa haina mashiko siku hizi.... Ni kwanni usingeleta na maamuzi aliyoyasoma Mr mambo na hoja alizotoa zaidi unaweka tu hoja za upande mmoja bila kuweka na za upande wa uongozi wa ACT ili sisi wenyewe tupime nani yuko sawa nani kakosea

Bila kufanya hivyo ingawa bandiko lako lina mashiko ila litaonekana kama kuchafuana maana siamini mtu makini kma zitto anaweza kufanya ufisadi kitoto hivi na akakosa majibu ni vizuri ungeweka na hoja zake au za Mr Mambo ili tuamue wenyewe sio kulalia upande mmoja unakuwa hutoi fair judgement

Ni hayo tu
 
Zitto na siasa za ujanja ujanja, Zitto aliutangazia UMMA WA TANZANIA kuwa kupitia Manispaa yake inayoongozwa na ACT, watawasomesha watoto wote wanao jiunga kidato cha Tano, sasa cha kushangaa wamewatupa watoto, watoto wanajilipia wenyewe tu..

Nimefanya utafiti zaidi ya shule kumi mkoa wa kigoma, watoto walilipiwa elfu 30 za muhula wa kwanza baada ya hapo, wanajilipia wenyewe
 
Mkuu hii tabia ya kuleta habari ya upande mmoja huwa haina mashiko siku hizi.... Ni kwanni usingeleta na maamuzi aliyoyasoma Mr mambo na hoja alizotoa zaidi unaweka tu hoja za upande mmoja bila kuweka na za upande wa uongozi wa ACT ili sisi wenyewe tupime nani yuko sawa nani kakosea



Ni hayo tu
weka wewe
 
weka wewe
Kwani mie ndio mtoa taarifa..... Yeye ndio amesema eti ZITTO KAJIBU ILA HAJARIDHISHA sasa kwanini anaconclude bila kutuwekea hapa hicho alichosema zitto ili wananchi waujiji tujue nani mkweli kuliko kusema tu HAJARIDHISHA naoma anakuwa hamtendei haki

Pili anasema Mhe Mambo alitoa msimamo wa chama cha ACT ila hapa hajauweka zaidi ana conclude kuwa msimamo huo ni wa KIMABAVU kwanni asingeupaste hapa

Hizi tabia za kuweka hoja za upande mmoja ni kuchafuana tu bora uweke na majibu ili tujue mbivu na mbichi ssa nyie hapa mtaanza kushabikia tu mafisadi oooh Mwizi wakati bila kuskiliza upande wake naye anasemaje

Ni hayo tu
 
tuweke na upande wa pili walichosema ili habari ibalance japo hao mashia nawachukia vibaya mno maana kwa kuhonga hawana mfano duniani
 
Back
Top Bottom