JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,308
- 5,458
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza katika mkutano wa hadhara Ktavi, amesema;
"Muswada wa sheria ya usalama wa Taifa una baadhi ya maeneo mazuri sana ambapo kwa asilimia 60 unaboresha idara ya usalama, inarasimisha idara, inaboresha maeneo ambayo ni ya kizamani na sasa yanaenda kuwa ya kisasa.
"Asilimia 40 ya Muswada wa sheria ya usalama wa Taifa ina matatizo,ambapo kuna masuala ya haki za watu yanaenda kukandamizwa na sisi ACT wito wetu ni kutaka mabovu yaboreshwe na hakuna haja ya kuharakisha sheria hii.
"Muswada huu wa sheria ya usalama wa Taifa kama utapita hivi ulivyo, unaenda kutoa kinga ya kijinai kwa Maafisa wa usalama kwamba akifanya makosa ya kijinai kwenye majukumu yake ya kikazi haitowezekana kumshtaki."
"Kipindi ambacho sheria haiwapi kinga wameteka! vipi wakiwa na kinga? Sasa hivi tuna Rais Samia ndiyo ila atamaliza muda wake. Nani kasema CCM haina Magufuli mwingine? Wanao, wanawatoa tu kabatini baada ya kusoma upepo wa kisiasa unavyoenda.
Sheria ya usalama wa taifa ya Marekani imewapa kinga CIA, Uingereza imewapa kinga maafisa wao wa idara za MI5 na MI6.Wenzetu wanachokifanya kwa maafisa wao ni kwamba ukiitumia kinga yako vibaya inaweza kuondolewa na ukafikishwa mahakamani.
"Kwenye muswada wa sheria yetu lazima tuwe na kifungu kitakacholazimisha uwepo wa kamati ya kibunge ya kusimamia idara ya usalama wa Taifa ambayo inaweza kuondoa kinga kwa afisa wa TISS, ili kuruhusu kuchunguzwa pale wanapovunja haki za binadamu kwenye majukumu yao.
"Wakati wa mjadala Bunge likiridhia kuundwa kwa Kamati ya kuisimamia idara ya TISS kwenye muswada huu, kamati itakayoundwa ijumuishe pia wabunge wa upinzani. Bunge kamili linakuja baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,sio bunge hili la sasa.
"Lazima pia mabadiliko haya ya sheria ya usalama wa taifa yaweke udhibiti wa matumizi mabaya ya ofisi kwa maafisa wa usalama wa Taifa (TISS), bila kufanya hivyo na wakafanikiwa kuwa na kinga ya kutoshtakiwa wataua na kutesa sana wananchi."
"Kamati itakayoundwa kuisimamia idara ya usalama wa Taifa (TISS) ifuatilie pia matumizi ya fedha ya idara ya usalama wa Taifa kupitia fungu la 20 ndani ya mafungu ya serikali. Fungu hili huwa halikaguliwi na CAG ilihali JWTZ wenyewe hukaguliwa matumizi yao ya fedha.
"Marekani ukishakuwa mgombea Urais unalindwa na idara ya Secret Service ambayo ni idara inayojitegemea ikiwa tofauti na shirika la Ujasusi (CIA). Kama nasi tunataka Viongozi na Wagombea urais walindwe na usalama wa Taifa basi tuwe na idara maalum itakayokuwa huru.
"Sisi mambo yote ya usalama tumeyaweka ndani ya idara moja kiasi kwamba TISS inatumika sana kisiasa na CCM. TISS wanasahau kushughulika na mambo makubwa ya kiuchumi, ufisadi na uwekezaji wa nje na ndani, wanaanza kuhangaika na wanasiasa - wameenda wapi, wanafanya nini.
"Mapendekezo yetu ACT tuwe na idara inayojitegemea kufuatilia maslahi ya nchi na uwekezaji wa nchi. Iundwe idara maalum ya Tiss kufuatilia mambo ya nje ya nchi na kujua wenzetu wanafanya nini huko vyenye athari kwenye mipango na mikakati yetu ya ndani.
"Tunamuomba sana Mh. Rais Samia Suluhu aondoe hati ya dharura kwenye muswada wa sheria ya usalama wa Taifa, muswada uingie kwa utaratibu wa kawaida ili tupate sheria iliyo bora kwa wananchi na sheria bora kwa maafisa wa usalama wa Taifa."