Zitto awasilisha mapendekezo kuhusu namna bora ya kukabiliana na virusi vya Corona

ACT Wazalendo

ACT Wazalendo

Verified Member
381
1,000
UJUMBE WA KIONGOZI WA CHAMA CHA ACT WAZALENDO, NDUGU ZITTO ZUBERI KABWE KWA WATANZANIA KUHUSIANA NA NAMNA BORA YA KUKABILIANA NA VIRUSI VYA KORONA – JUMAPILI, TAREHE 29 MACHI, 2020

Watanzania wenzangu,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muumba Mbingu na Ardhi, kwa kuendelea kutupa neema yake ya uhai na uzima na leo hii tukaweza kuwasiliana kupitia njia hii ya mitandao ya kijamii.

Nakushukuruni pia na nyinyi Watanzania wenzangu mlioacha shughuli zenu na mkaamua kuutumia muda huu kunisikiliza. Ahsanteni sana kwa upendo wenu.

Juzi tarehe 27 Machi, 2020 nimemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuhusiana na mapendekezo yangu na ya Chama cha ACT Wazalendo kuhusiana na namna bora ya kudhibiti na kukabiliana na virusi vya KORONA hapa nchini. Barua hiyo ilifikishwa jana.

Kutokana na uzito wa suala hili nimeona kuna haja ya kukushirikisheni Watanzania katika suala hili ili mjue tulichoshauri na kupendekeza ili na nyinyi pia muweze kutupa maoni yenu na kwa pamoja tushirikiane na Mheshimiwa Rais na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuona vipi tutaisaidia nchi yetu isiingie katika athari kubwa ambazo nchi za wenzetu zimefikia.

Watanzania wenzangu,
Kwa sasa, hapana asiyefahamu kwamba Dunia imekumbwa na taharuki inayotokana na mlipuko wa virusi vya Korona ambavyo vimeenea kwa kasi duniani kote na kusababisha vifo vya watu 30,627 (sawa na 5% ya walioambukizwa) mpaka jana saa 6 usiku kutokana na maambukizi ya watu zaidi ya 659,435 duniani kote.

Mifumo ya afya ya nchi mbali mbali imeemewa kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa, na uchumi wa Dunia umelazimika kuingia kwenye mdororo (recession) kutokana na shughuli za uzalishaji kudorora au kusimama kabisa.

Viongozi mbali mbali duniani na hususan Wakuu wa Nchi katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamechukua hatua za haraka kuzuia kasi ya maambukizi ya virusi hivi.

Mheshimiwa Rais na Serikali anayoiongoza nao wametangaza hatua mbali mbali za kupunguza kasi ya maambukizo ikiwemo wananchi kujizuia na mikusanyiko isiyo ya lazima, Wananchi kunawa mikono yao kwa maji yanayotiririka kwa kutumia sabuni mara kwa mara na kuundwa kwa Kamati 3 za Baraza la Mawaziri kuratibu mkakati mzima wa kukabiliana na Virusi vya Korona. Hatua hizi za awali ni hatua muhimu na za kupongezwa.

Watanzania wenzangu,
Pamoja na hatua hizo zilizotangazwa na Rais na Serikali, nikiwa Kiongozi wa Chama cha Siasa chenye Wanachama zaidi ya Milioni Moja Tanzania Bara na Zanzibar, nikiwa Mbunge na nikiwa Mtanzania mwenzenu, nimeona nina wajibu wa kumuandikia barua Mheshimiwa Rais ili Mosi, kuweka MSHIKAMANO wa pamoja kama viongozi katika kushughulikia mlipuko huu hatari katika historia ya Dunia, na Pili kushauri baadhi ya hatua ambazo tunalazimika kuzichukua ili kulinda uhai wa Watanzania wengi na kuhami uchumi wa Taifa letu.

Watanzania wenzangu,
Yapo mambo kadhaa ambayo ni muhimu kuyafahamu:

1. Ugonjwa huu kama tunavyofahamu ni mpya na hivyo taarifa nyingi juu yake bado hazijulikani. Wanasayansi duniani wanakadiria kuwa kinachojulikana mpaka sasa kuhusu virusi vya ugonjwa huu ni 15% - 20% tu.

Tafiti bado zinaendelea kufanywa na kila wakati tunapata taarifa mpya. Kwa mfano, (a) Muda wa mgonjwa kuanza kuonyesha dalili za ugonjwa (incubation period): ilikadiriwa kuwa ni siku 1 - 14. Tafiti mpya zinazoendelea zinaonyesha kuwa kipindi hiki chaweza kuwa hata siku 24.

(b) Kuenea na kuambukizwa kwa ugonjwa (transmission): Mpaka sasa njia kuu ya kuenea kwa ugonjwa huu iliyothibitishwa ni kuingiwa na majimaji yatokayo kwenye njia ya hewa wakati mtu aliyeambukizwa apigapo chafya ama kukohoa au kwenye makamasi yake (droplet infection).

Hata hivyo tafiti zinazoendelea zimeonyesha kuwepo kwa uwezekano wa ugonjwa huu kuweza kuambukiza kwa njia nyingine kama vile kwa kuvuta hewa yenye virusi (airborne) na kwa njia ya kinyesi (fecal-oral). Watafiti wanaendelea kutafiti kila siku na hivyo hatupaswi kupuuza kabisa njia mbalimbali za maambukizi. Tafiti pia zinaonyesha kuwa watu wasiokuwa na dalili za ugonjwa lakini wameambukizwa wanaweza pia kueneza ugonjwa huu.

Ni jambo la dhahiri kuwa uwezo wetu wa kukabiliana na virusi vya Korona ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchumi duni, uwekezaji mdogo kwenye sekta ya afya hasa kwenye vifaa tiba na wataalamu, na kiukweli tamaduni zetu za ‘KUSADIKI KWA TOMA NI KUONA’. Maeneo machache yafuatayo ni changamoto kubwa kwa nchi yetu;
Uchache wa Vyumba vya Wagonjwa Mahututi (ICU spaces):

Takwimu rasmi za Serikali zinaonyesha kuwa nchi yetu ina ICU chache sana na muda mwingi zinakuwa zimejaa. Uzoefu wa Duniani unaonyesha kuwa angalau 5% ya watakaombukizwa Korona watahitaji huduma ya ICU.

Uchache wa Vifaa Tiba vya kutibu wagonjwa wa Korona kama vile mashine za kusaidia kupumua - Ventilators, PPE, kwa ajili ya watoa huduma za afya na kadhalika.

Uchache wa Wataalamu wa Afya ambapo tuna nakisi ya wataalamu wa ngazi zote wanaozidi 150,000. Wataalamu wa kuendesha Ventilators ni wachache mno. Pamoja na uhaba wa wataalamu wa afya, waliopo wanahitaji kujengewa uwezo ili waweze kuwahudumia wagonjwa wa Korona haswa wale wanaohitaji huduma ya ICU.

Wazee na Idadi kubwa ya watu wenye maradhi hatarishi wakipata Korona: Tanzania ina jumla ya watu 1.6 milioni wenye kuishi na virusi vya UKIMWI sawa na 4.6% ya watu wazima (umri 15-49). Vile vile Tanzania ina Wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 wapatao 1.8 milioni sawa na 3% ya Watanzania wote wanaokaribia kufika 60 milioni.

Zaidi ya hapo kuna Watanzania wengi wenye magonjwa mbalimbali kama vile sukari, shinikizo la damu nk. Hawa watu wote wapo katika kundi hatarishi la kuambukizwa haraka na kupoteza maisha kutokana na virusi vya Korona. Hawa wanahitaji kulindwa zaidi na jamii.

Kutokana na uwezo mdogo tulionao Sisi Watanzania tuna njia moja madhubuti ya kuepukana na madhara makubwa ya mlipuko wa Korona nayo ni KINGA. Wahenga walisema KINGA NI BORA KULIKO TIBA. Kama Taifa hatuwezi kuongeza wataalamu kwani unahitaji miaka 5 kusomesha daktari mmoja na miaka 3 kupata nesi aliyefuzu, hatuna uwezo wa kununua vifaa tiba kwa haraka kwa sababu dunia nzima sasa inapigania vifaa hivyo na nchi kama Marekani zinatumia sheria za wakati wa vita kulazimisha makampuni binafsi kuzalisha vifaa kama ventilators, na wala hatuwezi kuongeza kwa kasi vyumba vya wagonjwa mahututi kwa sababu hata kwa kutumia JKT na kuondoa fedha kwenye ujenzi wa reli na Bwawa la Rufiji kuzielekeza kwenye afya bado tutahitaji zaidi ya miezi 6 kujenga ICU za kutosha.

Kwa sababu hizo basi, KINGA – kwa maana ya KUZUIA MAAMBUKIZI na MAAMBUKIZI MAPYA ndio njia bora zaidi kwa nchi fukara kama yetu. Ingawa hatujui KWA UHAKIKA maambukizi yalivyosambaa nchini kwa sababu ya kukosa uwezo wa kupima, bado tuna muda wa kuzuia maambukizi mapya. HATUJACHELEWA.

Watanzania wenzangu,
Kutokana na hali hii niliyoieleza na kutokana na uzito wa masuala haya; na kwa kuzingatia msingi wa UZALENDO unaokiongoza Chama chetu cha ACT Wazalendo na mapenzi yetu kwa Watanzania, katika barua yangu kwa Mheshimiwa Rais nimependekeza kwake kwa heshima na taadhima, mambo yafuatayo;.

Jambo la Kwanza linahusu Umoja wa KITAIFA: Hakuna wakati nchi yetu inahitaji umoja kama wakati huu. Mheshimiwa Rais akiwa ndiye Mkuu wa Nchi ana wajibu mkubwa wa kutuweka Watanzania pamoja kwa vitendo.

Tukiwa wamoja tutaweza kupambana na virusi vya Korona na kushinda pamoja na ikibidi kushindwa tushindwe pamoja. Korona haitambui itikadi zetu za vyama, dini zetu wala makabila yetu. Korona inaua Mashekhe na Makasisi, Wanasiasa na Wananchi wa kawaida, wanadiplomasia na wanamichezo na mbaya zaidi inaua hata wataalamu wa afya kama madaktari na manesi. Nimemsihi sana Rais aunganishe nchi yetu sasa bila kuchelewa.

Nimemshauri azungumze na Viongozi wote wa Vyama vya Siasa, Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia na Makundi mengine na kukubaliana kwa pamoja njia za kujikinga na mlipuko huu na kuzuia maambukizi kusambaa kwa Wananchi. Mimi binafsi, pamoja na Viongozi wa ACT Wazalendo, tupo tayari kushirikiana na Serikali kuandaa mikakati ya kukabiliana na madhara kwenye uchumi wetu kwa kutoa mawazo yenye ushahidi wa kisayansi.

Jambo la Pili linahusu Wataalamu: Licha ya Imani zetu mbalimbali ama za dini au nadharia tu za maisha, TUSIDHARAU SAYANSI. Damu ya kila Mwanadamu inaweza kupata maambukizi ya virusi vya Korona. Ni muhimu sana Sisi viongozi kuepuka kutoa maneno ya jumla jumla ambayo yanawapa wananchi wetu matumaini hewa na hivyo kusababisha hatari zaidi.

Tutoe nafasi kwa Wataalamu wa Afya kutuongoza katika mapambano haya ya kudhibiti ugonjwa wa Korona. Ni lazima sasa, maneno tunayoyasema kwa Umma na Maamuzi tunayoyachukua katika kudhibiti mlipuko huu yazingatie ushauri wa wataalamu badala ya imani zetu au fikra zetu. Tusipokuwa makini tutapoteza maisha ya watu wetu. Tusifanye kosa la kuchanganya imani na sayansi.

Jambo la Tatu na muhimu sana ni KUPIMA: Uzoefu wa Nchi kama Ujerumani umeonyesha kuwa licha ya maambukizi kuwa makubwa wamefanikiwa kuzuia vifo kwa sababu ya kampeni kubwa ya kupima watu. Wastani wa vifo kwa walioambukizwa nchini Ujerumani ni 0.6% tu wakati wastani wa Dunia ni takribani 5% sasa.

Nimemshauri Rais katika barua yangu kuwa Serikali iweke nguvu kubwa kwenye kupima watu wetu ili kuwatambua wenye maambukizi, kuwatenga wasiambukize wengine, kuwatibu na kuwafutilia maendeleo yao. Kasi yetu ya kupima hapa Tanzania ni ndogo mno na inategemea msaada wa Mashirika ya Kimataifa kama Center for Disease Control and Prevention (CDC) na Tajiri wa China Jack Ma, mmiliki wa Alibaba.

Takwimu zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhusu idadi ya Watu waliopimwa ni 10% tu ya vipimo ambavyo Serikali ilipewa na CDC. Ni kwanini 90% ya vipimo havijatumika? Au kama vimetumika matokeo ya vipimo hivyo ni nini?

Nimemuomba Mheshimiwa Rais atuongoze Taifa zima katika zoezi la kupima na iwe kampeni ya kitaifa. Tutumie vipimo hivi tulivyopewa na CDC, Jack Ma na tutumie Fedha za Dharura ambazo Bunge lilizipitisha kwenye Bajeti ya mwaka 2019/2020 kununua vipimo vingi zaidi ili tupime watu wetu. KUPIMA watu ni hatua muhimu kwa nchi yetu kudhibiti maambukizi ya Ugonjwa huu. Kama kuna jambo nalisisitiza kwa uzito wake basi ni KUPIMA, KUPIMA, KUPIMA!

Jambo la Nne ni UWAZI: Uwazi wa takwimu za maambukizi, maambukizi mapya, wagonjwa mahututi na vifo ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa huu wa Korona. Uwazi umesaidia sana nchi kama Korea ya Kusini, na USIRI umeathiri kwa kiwango chake nchi kama China. Nimemnasihi Mheshimiwa Rais kwamba tusione aibu hata kidogo kuweka wazi Idadi ya Wagonjwa wa Korona kwani kuna faida zaidi kuliko kuficha.

Jambo la Tano ni KUEPUKA MAELEKEZO YANAYOPINGANA: Serikali ilichukua hatua muafaka kufunga shule na vyuo kote nchini ili kuzuia maambukizi. Hata hivyo, tunatuma ujumbe gani kwa wananchi, na hasa watoto wetu wanapoona wao wamefunga shule lakini Viongozi wanahutubia makumi ya watu hadharani? Wanapata ujumbe gani wanapoona Bunge linaendelea na vikao? Wanapata picha gani wanapomuona Rais wao anaendelea na mikutano yenye mikusanyiko? Nimemuomba kwa heshima zote Mheshimiwa Rais, hatua zichukuliwe kusimamisha vikao vyote vya Kiserikali ikiwemo Bunge, Mahakama n.k.

Bunge linaweza kukutana mwezi Mei na likaendelea na vikao tukiwa salama na tumedhibiti maambukizi. Mahakama zinaweza kukutana mwezi Mei na Mikutano mingine ya kiserikali inaweza kufanyika kwa njia ya mtandao kama Video Conference, kama alivyofanya Waziri Mkuu juzi akiwa na Wakuu wa Mikoa.

Jambo la Sita ni kuhusu MAHABUSU na WAFUNGWA: Nimemshauri Mheshimiwa Rais kwamba Mwendesha Mashtaka wa Serikali aondoe zuio la dhamana kwa kesi zote ambazo kazuia dhamana na zile ambazo hazina dhamana kisheria lakini upelelezi bado unaendelea watuhumiwa wasubiri upepelezi wakiwa majumbani mwao ili kupunguza msongamano magerezani.

Watuhumiwa au Wafungwa wenye umri zaidi ya miaka 65 na wagonjwa wenye magonjwa hatarishi kwa Korona (underlying conditions) waachiliwe warudi majumbani mwao ama kumalizia vifungo au kusubiri upelelezi wa kesi zao.

Nyakati kama hizi zinahitaji maamuzi yanayoponya Taifa, na nimemsihi sana Rais apokee ushauri huu kusaidia kuzuia maambukizi na vifo kwa Raia wa Tanzania.

Jambo la Saba ni kuhusiana na Shughuli za kila siku: Kwa vyovyote vile Nchi yetu haiwezi kuendelea na uendeshaji wa mambo kama tulivyozoea yaani ‘business as usual’ wakati huu. Ninafahamu madhara makubwa ya kiuchumi na kwa maisha binafsi ya watu wetu iwapo tukizuia shughuli za kila siku kama ilivyofanyika nchi nyengine kama vile Afrika ya Kusini na India. Hata hivyo tunaweza kuwa na njia mbadala ya kuzuia maambukizi bila kuathiri sana shughuli za kila siku za watu wetu.

Kwa mfano, kwa hali ya sasa ni lazima KUFUNGA MIPAKA YA NCHI YETU kwa muda ili kudhibiti maambukizi. Ni lazima kuzuia msongamano wa watu kwenye huduma za usafiri wa umma kwa kuagiza vyombo vya usafiri vya Jeshi la Wananchi, Polisi na hata Watu binafsi kutoa huduma ya usafiri wa Umma kwa uangalifu mkubwa. Hii ni mifano michache tu lakini nimemwambia Rais kwamba tukiwa wamoja kama Taifa tutapata mbinu nyingi za kufanya ili kuokoa watu wengi kupata maambukizi.

Jambo la Nane ni KUHAMI UCHUMI WETU: Bila shaka yoyote, hatua tutakazochukua kuzuia mashambulizi ya Korona lazima zitaathiri Uchumi wetu. Hata bila kuchukua hatua hizo, tayari baadhi ya Sekta za Uchumi zimeshaanza kuathirika kutokana na mlipuko wa Korona Duniani. Sekta ya Utalii nchini tayari imesagwasagwa na inahitaji msaada wa angalau KUIHAMI ili iweze kuinuka Korona ikiisha. Nimemshauri Mheshimiwa Rais aunde Timu ya Wachumi waliobobea waliopo Serikalini na walio nje ya Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa hali yetu na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.

Baadhi ya Watendaji walioko Serikalini ni Wataalamu wa Hesabu za Uchumi haswa Modeli za mahusiano ya sekta za Uchumi. Mfano ni Prof. Adolf Mkenda, anaweza kuwa wa msaada mkubwa sana kwa nchi yetu hivi sasa katika kutazama namna gani Korona imeathiri au itaathiri uchumi na hatua pendekezwa zitakuwa na maana gani kwa sekta mbalimbali za Uchumi.

Nimemsihi sana Rais kuwa Timu ya Wataalamu wa Uchumi Nchini iundwe na kuanza kazi mara moja. Bahati mbaya sana tulivunja Tume ya Mipango kwani ingekuwepo ingefanya kazi hii na kulishauri Taifa mara moja hatua zinazofaa kuchukua. Hata hivyo bado Mheshimiwa Rais anaweza kuunda Timu ya Muda kukidhi haja za sasa.


Watanzania wenzangu,
Haya ndiyo mambo manane ambayo mimi na Chama cha ACT Wazalendo nimemuandikia Mheshimiwa Rais kumshauri na kwa heshima zote kupendekeza kwake yazingatiwe katika kipindi hiki kigumu tunachopitia.

Nimalizie ujumbe wangu huu, kama nilivyofanya kwenye barua yangu, kumuombea kheri Mheshimiwa Rais katika kuongoza nchi yetu kutoka kwenye changamoto hii kubwa.

Mimi binafsi pamoja na Chama ninachokiongoza tutakuwa tayari kutoa ushirikiano wa dhati kwa Watanzania wote bila kujali itikadi zao ili kuihami nchi yetu na kuokoa maisha ya Watanzania.

Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!

Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb.
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo.
29 Machi 2020.


Sent using Jamii Forums mobile app
 
S

swagy

Member
92
150
Vyote ulivyoandika ni vizuri ila pale ulipoandika UWAZI UWAZI UWAZI, Nimepapenda zaidi, taarifa za corona lazima ziwekwe wazi serikali iache kuficha, na ikiwezekana wahusika watajwe na maeneo au mikoa wanapotoka ili kuweza kuchukua tahadhari zaidi

Lakini jpm na uongozi wake ni sikio la kufa,ila kama data za wagonjwa zitaweka wazi hakika tutaishinda hii covid 19

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ramark

Ramark

JF-Expert Member
1,603
2,000
Mimi yote naweza kupinga ila moja tu
Rais akubali watu wapimwe na iwe kampeni ya wote.
 
Bams

Bams

JF-Expert Member
8,253
2,000
Nakubaliana sana na Zito - KUPIMA KUOIMA KUPIMA.
 
N

ngusillo

JF-Expert Member
1,068
2,000
Good... lakini Zitto kwa kushauri hadharani umesababisha serikali kuacha kabisa kutekeleza ushauri wako. Serikali haiwezi kufanya kitu chochote kwa kusikiliza ushauri wa mpinzani. Ni bora kisifanyike kabisa hata kama tutapata hasara au kufa kuliko kufuata maelekezo ya mpinzani.
 
kandamatope

kandamatope

JF-Expert Member
434
500
Corona sio ukimwi
Useme unaficha
Unataka watu wapime corona ili iweje
Kwa mtazamo wangu nafsi yako inasema kimoyo moyo serikali inaficha takwimu za corona ndio maana unang'ang'ania watu kupimwa.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Aisopos

Aisopos

JF-Expert Member
291
250
Mchango mzuri. Hongereni ACT kwa kujishirikisha. Nchi hii ni yetu sote; viongozi wa kisiasa msikubali tofauti zenj na udhaifu wenu binafsi uwe chanzo cha kushindwa kutekeleza wajibu weuu unaotokana na dhamana ya uongozi mliyopewa. Tanzania ni kubwa kuliko ninyi mmoja mmoja na hata serikali.
 
Cannabis

Cannabis

JF-Expert Member
1,404
2,000
Ujumbe mrefu sana, halafu sisi watanzania hatuna utamaduni wa kusoma....
 
Tukundane

Tukundane

JF-Expert Member
10,539
2,000
Nchi jirani zote wakifunga mipaka yao yote tayari na mipaka yetu itakuwa imejifunga yenyewe, suala la kufunga au kutokufunga mipaka yetu siyo la jambo la kuumiza kichwa, Kenya wakifunga mipaka yao moja kwa moja hakuna mtanzania atakayeruhusiwa kuingia Kenya wala mkenya kuja Tanzania.

Hivyohivyo kwenye nchi zingine jirani,pamoja na nchi zingine za karibu, na za mbali wakifunga mipaka yao yote, maana yake ni kwamba mawasiriano ya nchi na nchi ikiwemo Tanzania yatakuwa yamekatika pasipo hata Rais kutoa tamko la kufunga mipaka ya Tanzania.

Cha msingi tuchape kazi huku tukimuomba Mungu tusijetukatiwa jela na corona kwa kigezo cha kujikuta nchi nzima tumewekwa kwenye karantini na corona.
 
N

Nisamehe

JF-Expert Member
479
500
Good... lakini Zitto kwa kushauri hadharani umesababisha serikali kuacha kabisa kutekeleza ushauri wako. Serikali haiwezi kufanya kitu chochote kwa kusikiliza ushauri wa mpinzani. Ni bora kisifanyike kabisa hata kama tutapata hasara au kufa kuliko kufuata maelekezo ya mpinzani.
Nayo kwake hiyo ni kiki ya kisiasa. Raisi akitekeleza baadhi watamsifu zitto. Itikadi za vyama ziwekwe pembeni,Rais wetu aelekeze kinachofaa kwa wakati huu.
 
B

Bukyanagandi

JF-Expert Member
8,035
2,000
Biafsi naona pendekezo la kupima ndilo lipewe kipa umbele zaidi, ametoa mfano wa Ujerumani na ukiangalia watu wanajua mapema hali zao kiafya wengi wanapona, tofauti kabisa na Mataifa yanayo weekea maanani suala la kupima bila kujali kama wana maambukizi au la.
 
B

bagamoyo

JF-Expert Member
8,715
2,000
March 29, 2020

Mh. Zitto Kabwe akihutubia taifa kuhusu ugonjwa wa COVID - 19 unao sababishwa na virusi vya coronavirus na kutoa ushauri ya namna bora Tanzania kama taifa inavyoweza kupambana na gonjwa hili hatari.


Source : Weyani TV
 
B

bagamoyo

JF-Expert Member
8,715
2,000
29 Mar 2020

Mh. Zitto Kabwe akuhutubia Taifa kuhusu corona

Hotuba ya kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, juu ya hali ya mripuko wa kirusi cha #corona nchini Tanzania.


Source : Weyani TV

N.B :
Hotuba murua sana, iliyoshiba data na changamoto inayoweza kuikabilia taifa na mapendekezo ya jinsi ya kwenda mbele kimpango na kimkakati dhidi ya gonjwa hilo hatari si kwa uhai wa watu tu bali na uchumi wa nchi.
 

Forum statistics


Threads
1,424,986

Messages
35,078,036

Members
538,184
Top Bottom