Zitto ashauri Serikali kuweka mazingira bora na rafiki kwa sekta binafsi ili kusaidia ukuaji wa uchumi

kirerenya

JF-Expert Member
Joined
Aug 27, 2013
Messages
1,692
Points
2,000

kirerenya

JF-Expert Member
Joined Aug 27, 2013
1,692 2,000
Mwanza. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe ameishauri Serikali iweke mazingira rafiki na bora kwa sekta binafsi ambayo ndiyo injini ya uchumi wa Taifa.

Ametoa ushauri huo jijini Mwanza leo Jumatano Januari 24,2018 wakati wa kipindi cha Tujadiliane kinachoandaliwa na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari nchini (UTPC).

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo amesema, “Tuongeze uzalishaji na kuuza nje kuliko tunavyoagiza na tuwekeze kwenye miradi yenye kugusa maisha na uchumi wa mwananchi moja kwa moja.”

Amesema ujenzi na uboreshaji miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa anga ni muhimu, lakini uendane na shughuli zinazozimua na kusisimua uchumi kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa za sekta ya kilimo ili kuvihakikishia malighafi viwanda vya ndani.

“Kabla ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli, tungewekeza kwenye uzalishaji wa chuma kule Liganga na Mchuchuma. Hii si tu ingetumika kama malighafi kwenye mradi wa ujenzi wa reli nchini, bali pia katika nchi jirani za Kenya na Rwanda ambazo pia zinawekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya reli,” amesema.

Akizungumzia utekelezaji wa sera ya Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025, Zitto amesema suala hilo linapaswa kufungamanishwa na uzalishaji wa mazao ya kilimo kama vile pamba, korosho, michikichi na mengine yatakayotumika kama malighafi.

Ameshauri uwekezaji wa fedha, teknolojia na maarifa katika sekta ya kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania kwa kutoa ruzuku kwa wakulima ili pamoja na kuongeza uzalishaji, pia iwahakikishie fidia bei inaposhuka katika soko la dunia na mafao ya uzeeni wanapokosa uwezo wa kuendelea kulima.

“Wafanyakazi wanalipwa mafao wanapostaafu. Je, mkulima anapozeeka na kukosa uwezo wa kulima anapata wapi mafao?” amehoji Zitto.

Akijibu swali kuhusu maisha yake baada ya siasa, amesema anakusudia kuwa mhadhiri katika taasisi za elimu ya juu na kuandika vitabu vya kiuchumi, kitaaluma na harakati za kisiasa.

Chanzo: Mwananchi
 

Forum statistics

Threads 1,392,176
Members 528,565
Posts 34,100,975
Top