ZITAMBUE CHANGAMOTO SITA KWA KILA UCHUMBA/NDOA

Joseverest

JF-Expert Member
Sep 25, 2013
51,937
69,218
Ukweli ni kuwa watu wawili wanapoamua kwa dhati kuwa katika mahusiano ni kwamba wanakuwa tayari katika akili zao wamejenga matarajio au matumaini ya kunufaika na uhusiano husika, hata kama hawawezi ambiana moja kwa moja kuwa “ aisee, mie kuwa na wewe nataraji moja , mbili, tatu….”.

Kunapokuwepo na upendo, basi pia kunaleta majukumu, ambapo bila ya kutimizwa kwa majukumu yanayotarajiwa kutimizwa, maana halisi ya mahusiano bora inapotea.

Hii si tuu kwa mahusiano ya kimapenzi, bali hata dini zinatufundisha kuwa Mungu anatupenda, na katika hilo, tunajukumu la kutii amri zake, na kwamba tusipotii amri zake, tunakuwa tumeharibu maana nzima ya upendo wake, kwani tutajikuta tumeingia motoni/jehanamu (Kinyume cha upendo).

Hata katika familia, tumesikia mzazi pamoja na upendo alioonyesha kwa mtoto wake toka yupo tumboni mpaka mtoto ameweza kujitegemea, endapo mtoto husika akashindwa kumjali ( hili ndio jukumu linalokuja na upendo wa mzazi), basi unaweza sikia mzazi huyo akitoa ‘laana’ au ‘akamwachia radhi’ mtoto wake mwenyewe wa kumzaa.

Ni wazi kuwa mara nyingi majukumu yanayoletwa na upendo huwa hayaelezwi wazi wazi, hata hivyo katika mahusiano, mambo yafuatayo yanaweza kuwa sehemu ya matarajio ambayo wapenzi wanaweza kuwa makini ili waweze kuwapendeza wenzao. Kwa maana nyingine ni kuwa yafuatayo, ndio maeneo ambayo mtu aliye kwenye mahusiano ni muhimu ‘acheze’ vema ili kulinda mahusiano/penzi:-


1. Fedha:

Katika swala la fedha, jambo kubwa linalojitokeza ni namna ya kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya fedha. Ni muhimu kuweka mikakati ya pamoja kwa mambo ya msingi kimaisha , na kila mmoja kutilia maanani mipango hiyo, kabla ya kuamua kutumia kipato chake kwa mambo ambayo pengine hayapo nje ya mipango ya kifedha ya wawili nyie kama wapenzi. Bila shaka, kuendana na aina yenu ya kipato, aina yenu ya maisha, kama wapenzi mtakuwa na kiwango fulani cha fedha ambacho si busara mmoja wenu kuamua kutumia bila kumtaarifu mwenzake , hata kama matumizi husika ni muhimu sana, na haijalishi nani kazitafuta fedha husika.


2. Imani:

Katika swala la imani, ni muhimu kufahamiana vema mwenendo wa kiimani wa mwenza wako, na kuheshimu kuwa swala hili ni nyeti, na mabadiliko ya kweli hayawezi kulazimishwa. Imani inaweza athiri namna mnavyoweza kuwasiliana kama wapenzi – kwani mwingine mwenye msimamo mkali wa kidini, anaweza kukataa jambo fulani hapo baadae, jambo ambalo pengine mwenza wake anaona ni jambo la kawaida tuu. Imani inaathiri malezi ya watoto, na inaweza athiri shughuli za kiuchumi za wawili nyie, mfano pale mmoja wenu anapoamua kujikita katika ‘huduma’ zaidi, kuliko familia na shughuli za kuingiza kipato.


3. Mahali pa kuishi:

Mtaa gani , wilaya gani, mkoani gani, nchi gani au bara gani kila mmoja wenu anatazamia muishi ni jambo la msingi kuliweka wazi kati yenu. Jambo hili linaweza kuendana na mambo mengine mengi ambayo yanachochea mabadiliko ya muda mfupi na hata muda mrefu katika maisha yenu, kama vile , aina ya kazi mnazotarajia kila mmoja wenu kufanya, na aina ya kazi unazotamani au kufikiri ni vema mwenza wako afanye.


4. Watoto:

Hili ni jambo zito haswa katika vipengele vya lini watoto wapatikane (ujauzito), idadi ya watoto, aina ya malezi kwa watoto watakaopatikana, na zaidi sana majukumu ya kifedha katika malezi ya watoto (mfano, nani atalipa ada ya shule, n.k). Pamoja na kutafakari hayo, watu wawili mlio katika mahusiano, ni muhimu mkatengeneza picha ya maisha ya watoto wenu endapo mmoja wenu atatangulia mbele za haki (atafariki), na hata ikiwezekana mwaweza fikiria na kupanga aina ya maisha mnayotaka watoto wenu waishi pale nyote wawili hamtokuwepo duniani. Inapotokea mambo kama hayo yaliyotajwa hapo juu hayajawekwa wazi mbele yenu, ni rahisi mmoja wenu kufanya mambo yasiyompendeza mwengine –mfano wakati mwingine anafikiria akiba ya baadae ya watoto ili wakasome international school, mwingine anafikiria namna ya kutanua ili ‘kuuza sura’.


5. Falsafa ya maisha:

Swala hili linahusu wa kipekee na tafakari huru ya kila mmoja wenu kuhusu mambo kadhaa ya kimaisha kama vile mtazamo wa kila mmoja wenu kuhusu biashara (mwingine biashara ni kitu cha kuweka heshima kwa jamii, wakati mwingine biashara ni kielelezo cha huduma kwa jamii na hivyo kinahitaji muendelezo).

Falsafa pia inahusu namna kila mmoja wenu anavyochukulia mambo kama vile kusaidia watu wengine, kuwa na mahusiano na watu wa jinsia tofauti (wapo wasiotaka hata classmet ampigie simu mpenzi wake). Falsafa pia inahusika na namna kila mmoja anavyotafsiri mafanikio katika maisha, na alivyo tayari kufanya yanayopaswa kufanywa kufikia mafanikio (Mfano, wengine mafanikio ni mali na umaarufu, wakati kwa wengine mafanikio ni namna anavyoweza kuwa na furaha na uhuru , pamoja na kusaidia wengine).

Katika juhudi za kufikia mafanikio unawea kukuta wapenzi mnatofautiana kwani mmoja anaweza amini rushwa ndio suluhisho pekee la kufikia anakotaka, wakati mwingine anaamini tofauti na hivyo.


6. Hisia za kimapenzi:

Ni jambo la msingi kutokupuuzia hisia za kimapenzi za kila mmoja wenu. Tambua vile mwenzako angependa akuone unamvutia na vile ambavyo unamjali hisia zake. Ni kweli kuwa katika mahusiano, hisia za kimapenzi zinaweza zisichukue nafasi kubwa kati yenu kwani kuna mambo mengi ya kufanya pamoja kama wapenzi, hata hivyo pamoja na udogo wake wa muda, jambo hili nyeti lisipopewa kipaumbele, linaweza sababisha mengine yote kuharibika. Zaidi sana, kumbuka wewe na mpenzi wako, ni watu wa jinsia mbili tofauti, kinachowafanya muungane kiasili ni hizo hisia za mapenzi kati yenu.


Hitimisho:

Sio lazima kama watu wawili mlio katika mahusiano muwe na mtazamo sawa katika hayo yote yaliyoelezwa hapo juu, hata hivyo, ni muhimu sana kwenu nyote kuwa na picha kichwani ya mtazamo wa mwenza wako kuhusu mambo hayo niliyotaja hapo juu.

Pale mnapokubaliana kutofautiana katika mambo yaliyotajwa hapo juu (mf.mambo ya fedha, na imani), hakikisheni mnakubaliana bila kutofautiana kuhusu athari za kutofautiana kwenu, na jukumu la kukubali athari hizo kwa mahusiano yenu.



C,E &P..
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom