Zipo sababu za msingi za kupiga marufuku bodaboda katikati ya jiji la Dar es Salaam

Shoctopus

JF-Expert Member
Dec 29, 2015
3,434
1,985
Asalam-alaikhoom Wana-JF!
Kwanza niwapongeze sana Rais SSH na Mkuu wa Mkoa Amos Makala kwa kusimamia zoezi la 'kuwapanga upya' wamachinga jijini, na kwa kusimamisha marufuku ya bodaboda na bajaji mjini; ili kufanya mashauriano na timu ya wataalamu wao na wadau wengine kabla ya utekelezaji.

Kwahiyo naenda kwenye mada moja kwa moja.

1. Jiji letu la Dar es Salaam hasa eneo la katikati (CBD area) ramani yake ni mbaya sana. Kawasababu ni finyu sana. Barabara ni nyembamba mno majumba yamebanana hadi hakuna open spaces za kusaidia mzunguko wa hewa safi.

Matokeo yake mjini kuna kelele na msongamano mkubwa wa watu, magari, bajaji, bodaboda, daladala, wamachinga nk.

Magorofa marefu yamejengwa bila nafasi za maegesho na mandhari za kuvutia bila msongamano. Njia za miguu (pedestrian walkways) ni nyembamba mno hamuwezi kutembea na kupishana kwa raha.

Kwa ujumla jiji letu halivutii; sio rafiki kwa wenye magari, waenda kwa miguu, bodaboda, watoto, wazee, walemavu, wagonjwa na hata watalii! Na ni hao wote ambao mahitaji yao lazima yazingatiwe katika kulifanya jiji kuwa mahali pazuri kwa wakazi, wasafri, wageni, wafanyakazi, wafanyabiashara na kila binadamu na viumbe hai waliopo. Ambao wanahitaji maji na hewa safi, nafasi bora za kuishi na kuendesha shughuli za maisha yao; ikiwa ni pamoja na starehe, ibada, mazoezi, mapumnziko nk.

Mahali penye msongamano mkubwa wa watu hupelekea kuharibika kwa mazingira na kuleta vurugu na kelele, uchafu, maambukizi ya magonjwa, hewa chafu na hata kuvunjika kwa amani. Hakuna Binadamu anaependa kuishi katika mazingira kama hayo, maana ya MAENDELEO ni kuepusha kadhia kama hizo katika jamii.

Lakini ni ukweli pia kwamba msongamano huzaa msongamano zaidi, vivyohivyo uchafu huzaa uchafu zaidi, kelele pia, nk. Bila kuwa na hatua madhubuti za kuweka hali sawa (social engineering) hakutakuwa na MAENDELEO na mwisho jamii huweza kuangamia.

2. Pili, kuhusu baadhi ya watu kudai kwamba zuio la bodaboda CBD area linakinzana na katiba napenda kujibu kama ifuatavyo:

* Marufuku ya bodaboda na bajaji inahusu biashara ya vyombo vya usafiri katika jamii nzima ya wakazi, wasafri, wageni, wafanyakazi nk, katika eneo la katikati ya jiji; sio mtu kwa maana ya dereva au abiria, au kikundi fulani cha watu!
Bodaboda pia ni biashara, kama ilivyo kwa biashara ya machinga. Sio dereva tu au abiria, mteja au chombo pekee.
Mipangomiji ni pamoja na kuratibu masuala ya biashara za aina mbali mbali katika mazingira ya jiji. Na ni halali kikatiba kwa Serikali kufanya kazi hiyo.

Lazima tujue kwamba Katiba inazungumzia uhuru wa kwenda au kuishi popote (bila kukiuka sheria) ni kwa Binadamu, na si kwa shughuli zake, kama kujenga, kulima, kufuga mbuzi na kufanya biashara nk.

* Katiba inampa Rais na Serikali mamlaka ya kupanga, kugawa na kusimamia matumizi ya ardhi (land use planning, and zoning regulations) mijini na vijijini kwa lengo la kuleta MAENDELEO, na kwa faida ya JAMII NZIMA ya Watanzania. Na hii ni kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo.

* Kwa sababu kuu hizi mbili hapa juu, na kama ilivykuwa muhimu kuwapanga upya wamachinga jijini Dar; ni muhimu pia kwa bodaboda na bajaji kupangwa upya. Kwasababu mambo hayo mawili yanachangia kuzorota kwa mazingira ya jiji kama nilivyoeleza hapa juu.

Lakini kazi ya kupanga kugawa na kusimamia matumizi ya ardhi mijini na vijijini ni kazi ya kudumu.

* Amri kama hizi za viongozi wa Serikali naamini hutolewa kutokana na ushauri wa wataalamu na wadau husika. Na ikitokea bahati mbaya isifanyike hivyo, ni haki lawama apewe kiongozi husika.

Kwahiyo hatuna budi kurudi nyuma ili tuone wapi kuna mapungufu.

Q1. Sheria ya Master plan ya jiji ipo au haipo? Na:

Q2. Kama ipo ina mapungufu gani ya kimuundo na kiutekelezaji?

Q3. Sheria ya Baraza la mazingira, NEMC ipo au haipo? Na:

Q4. Kama ipo ina mapungufu gani ya kimuundo na kiutekelezaji?

Maswali yapo mengi na hata iweje sitaweza kuyajibu yote humu jukwaani. Kwahiyo najaribu kujibu hayo machache kwa kifupi:


Q1. Sheria ya Master plan ya jiji, kiuhalisia ni kama ipo ipo tu. Kama ipo, ni kwenye makaratasi tu, haifuatwi au kuheshimiwa. Haina MENO. Labda inatumika kuombea mikopo, misaada na porojo za kisiasa. Kama hivyo ndivyo, kuna mapungufu makubwa sana katika muundo wa kisheria ambao unafanya sheria na master plan kupuuzwa.

Q2. Kuhusu muundo na utekelezaji wa Sheria ya Master plan hauko sahihi kama wadau na wananchi hawakushirikishwa kikamilifu kabla ya kujadiliwa kikamilifu, na kupitishwa na Bunge.
Q3. Sheria ya NEMC nayo si shirikishi na haikupewa MENO kimuundo na kiutekelezaji. Kwasababu kama nilizotoa kuhusu Sheria ya Master plan.

Nisiwachoshe.
Nihitimishe mada yangu kwa kusema kwamba MAENDELEO ni lazima kwanza yatokane na utambuzi wa vikwazo (changamoto) halisi za jamii na pili kubuni mipango na mikakati ya kutatua vikwazo na changamoto mbalimbali.

Katika mchakato mzima ni lazima wananchi wawe CHANZO cha utambuzi wa vikwazo na changamoto na kubuni sheria mbalimbali, mipango na mikakati ya utekelezaji, na usimamizi wa yote hayo. Sheria yoyote haiwezi kamwe kuwa na MENO kimuundo na kiutekelezaji bila WADAU, WANANCHI na Serikali kupitia wataalamu wake. kushirikishwa.

Mwisho: Kazi ya kupanga na kugawa ardhi mijini na vijijini ni kazi ya kudumu kama tunataka MAENDELEO.

WATU wanaongezeka kila siku lakini ardhi ni ileile. Changamoto za tabia na mahitaji ya watu huongezeka na/au hubadilika kutokana na mazingira ya leo na kesho. Wananchi wakielewa na kushirikishwa katika malengo na mikakati ya Serikali; utekelezaji wa sheria na mipango ya MAENDELEO utakuwa rahisi.
 
Back
Top Bottom