Zipo kiasi gani kulipia wawekezaji wazembe?

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
127
Na Mwandishi Maalum
SERIKALI imepandikiza chuki. Wiki iliyopita, ilitangaza kulipia mishahara ya wafanyakazi wa Kampuni ya Reli (TRL), ambao walishindwa kulipwa na muwekezaji aliyekodishwa shirika hilo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ndiye aliyetangaza kwamba serikali italipa mishahara ya wafanyakazi kuanzia Machi mwaka huu hadi Agosti, ili kuipa uwezo muwekezaji wa kujiendesha.

Kiasi cha Sh. 3.6 bilioni zitatumika kwa kazi hiyo.

Kama inadhani inasaidia muwekezaji, basi imekosea. Kwa vile haijui itendalo bali kuamini inasaidia uwekezaji, inatangazia wananchi kuwa ina fedha za kutosha kulipia mishahara iliyopaswa kulipwa na wawekezaji.

Hatua hii inakuja chini ya mwezi mmoja tangu menejimenti ya TRL, inayoongozwa na Vinal Agarway, anayewakilisha kampuni kubwa ya Rites iliyopewa zabuni ya kuendesha lililokuwa Shirika la Reli nchini (TRC), kuahidi kulipa wafanyakazi wake.

Leo inasema haina uwezo wa kulipa fedha hizo ambazo wafanyakazi wanatarajia kuongezewa kima cha mshahara hadi Sh. 160,000 kwa mwezi. Kwanini waliahidi wasichoweza kukitimiza?

Tunahoji haya baada ya kuona viongozi wakisema na kurudia kila siku kuwa serikali haina uwezo wa kutosha kukidhi bajeti yake na hivyo kulazimika kuendelea kutegemea wafadhili.

Inaokoa wawekezaji ambao waliposaini mkataba Septemba, mwaka jana, wa kuendesha TRC, waliahidi kuingia na mkopo wa dola 43 milioni kutoka Benki ya Dunia na dola 26 milioni nyingine zitakazotokana na biashara.

Nani aliwaahidi wawekezaji injini 92 za kuanzia kazi ya kusafirisha abiria na mizigo wakati walizokabidhiwa ni injini 55 tu. Injini 37 ziko wapi?

Kinachoonekana hapa ni ulaghai uleule unaotokana na tabia za kifisadi ya wenzetu waliopewa jukumu la kuandaa mkataba.

Tuseme kwamba wawekezaji walipotoshwa kuhusu hali halisi ya shirika na hivyo kupata shauku zaidi ya kuingia wakiamini kazi ya kujenga mazingira mazuri ya kibiashara itakuwa nyepesi?

Haya yanatukumbusha yaliyotokea wakati wa kuandaa ripoti ya hali halisi ya kampuni ya gesi ya oksijeni nchini (TOL) iliposemekana kuwa wataalamu wasio waaminifu walipika takwimu kwa nia ya kuvutia wawekezaji.

Matokeo yake nini? Imechukua miaka mingi, tangu 1998, kampuni hiyo ikiendelea kukosa uwekezaji wa maana na hivyo kusababisha wana hisa kutolipwa gawio kwa muda mrefu.

Hadi sasa TOL ingali ikiendeshwa kimazonge kwa kuwa haijapata wawekezaji wa kuaminika, zaidi ya mipango ya menejimenti ya kujaribu kuiendeleza ili tu isife. Ndio maana inakabiliwa na ushindani mkubwa kutokana na ushiriki wa watu wengi katika kuendeleza sekta hiyo.

Ni mambo ya kusikitisha na kuudhi wananchi waliotumia nguvu kubwa kujenga mashirika ya namna hii. Kwa hakika mambo yanayofanywa nchini, yanaibua hisia nzito za chuki kutoka kwa wananchi.

Wana kila sababu ya kuwa hivyo. Haiwezekani watu wachache kwa jina la wataalamu wazalendo, wanaachiwa fursa ya kuhodhi madaraka ya kutengeneza mikataba yenye matumaini, kumbe hatimaye ni kuitia nchi katika fedheha.

Nini malipo ya watu hawa? Hayapo wala Waziri Mkuu, Pinda, hakueleza wafanyakazi wa TRL wataalamu waliodanganya wawekezaji watafanywa nini. Yaleyale, maji ya futi na nyayo.

Serikali inawapa wataalamu kazi lakini inapokea ripoti za mielekeo ya kifisadi na haichukui hatua yoyote dhidi ya wahusika. Nini cha kukitegemea katika hali kama hiyo ya waovu kuachiwa watambe?

Tunakosea nini tukisema kwamba hata wawekezaji wenyewe ni wababaishaji? Utachukua vipi shirika ambalo hukufanya utafiti kuthibitisha yaliyoandikwa kwenye ripoti?

Hivi hawakujua kwamba wanakuja Tanzania, nchi inayotajika sasa kwa ubabaishaji katika kufanya mambo yake?

Sasa serikali inachota fedha kulipia wafanyakazi wa TRL. Je inafanya nini kujenga maslahi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wanaolia njaa wakati mabilioni ya fedha yanalipwa waovu?

Itafanya nini kwa wafanyakazi wa Shirika la Bima (NIC) wanaozidi kulia njaa kwa sababu viongozi wao hawataki mabadiliko wakati wao wanapata maslahi yao?

Maswali kama haya yanaweza kuwa mengi, maana mashirika mengi yaliyokuwa imara, wamefisidiwa na sasa hayana kitu.

Lazima tufike mahali tuamue hasa kwamba mali na raslimali za taifa zinalindwa ipasavyo kwa ajili ya maendelea ya wenyewe, Watanzania ambao wengi wao wanaishi katika ufukara.

Source: MwanaHalisi
 
Sasa Nyie Waswahili Ndio Wahusika Wakubwa Katika Kuuwa Na Kudidimiza Mashirika Haya Pamoja Na Mali Zake , Hao Ni Baba Zenu Wajomba Zenu Na Majirani Zenu Wengine Ni Wazee Wenu Wa Makanisa Ndio Wanaofanya Kufuru Hizo Aibu Sana
 
Jamani usemi wa Kiswahili usemao 'wajinga ndiyo waliwao' mnaukumbuka? Msamiati 'uwekezaji' unaeleweka? kama kashindwa kuwekeza anaitwaje mwekezaji? Sheria ya mikataba iko wazi kwa nini serikali isisitishe mkataba? Sisi wananchi kwa vijisenti vyetu kwa kutumia vitu kama vipande vya umoja ua NIKOL tunaweza tena serikali yetu isituaibishe.
 
Jamani usemi wa Kiswahili usemao 'wajinga ndiyo waliwao' mnaukumbuka? Msamiati 'uwekezaji' unaeleweka? kama kashindwa kuwekeza anaitwaje mwekezaji? Sheria ya mikataba iko wazi kwa nini serikali isisitishe mkataba? Sisi wananchi kwa vijisenti vyetu kwa kutumia vitu kama vipande vya umoja ua NIKOL tunaweza tena serikali yetu isituaibishe.

Mhe Kipesile,

Unaposema vijisenti ni matumaini yangu huamanishi 1 million dollar maana wengine tunashindia mapande ya mihogo kisha mnatukejeli kuita mijihela yote hiyo vijisenti
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom