Zipi taratibu za kufuata kisheria katika kumiliki kiwanja, shamba na nyumba

Pastory Kimaryo

JF-Expert Member
Jan 16, 2018
810
500
Habari wana JF,

Nahitaji kujua kama kuna mtu ana kiwanja anataka kuniuzia natakiwa nifuate taratibu gani kisheria ili nisije kugubudhiwa baadae, kwa vijijini taratibu zikoje na kwa mijin taratibu zikoje pia nikitaka kununua shamba nifuate taratibu zipi ili hilo shamba liwe mali yangu halali kisheria.

Kama nataka kununua nyumba kutoka kwa mtu au kuachiwa nyumba natakiwa kufuata taratibu gani ili hiyo nyumba iwe mali yangu kihalali?

Natanguliza shukrani! 🙏
 
Feb 26, 2012
55
125
FIKA KWA MWANASHERIA(ADVOCATE). MUELEZEE NA TARATIBU ZOTE ATAKUPA

Kamwe usije nunua eneo kwa kuandikishana kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa au Kijiji au mtendaji. UTATAPELIWA, hawa watu hawana mamlaka katika hilo.
 

Pastory Kimaryo

JF-Expert Member
Jan 16, 2018
810
500
FIKA KWA MWANASHERIA(ADVOCATE) ...MUELEZEE NA TARATIBU ZOTE ATAKUPA


Kamwe usije nunua eneo kwa kuandikishana kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa au Kijiji au mtendaji..UTATAPELIWA...hawa watu hawana mamlaka katika hilo.
Hiv wanasheria si wapo wa sekta mbali mbali ama? Afu mi nipo kijijini sijui namuaccess vip mwanasheria!
 

1kush africa

JF-Expert Member
Dec 13, 2016
8,773
2,000
Yaaan kuna hatua za kufuata.

Nimenunua shamba ila cha ajabu majirani wakilima wanaingia hadi kwangu.

Jana nlikuwa huko kiukweli nimekwazika sana.

Nikamsimulia jamaa yangu ambaye ye alisomea Chuo cha Ardhi
Akasema hapo mchawi kupata Hati ya umiliki tu ili tukanyooshe mipaka yetu.

Amenieleza mambo mengi

Kikubwa kuwaona wahusika

Shamba nlinunua 2018.

Nliweka zile bikon
Upande mmoja hazipo zimeng'olewa .
Kuna changamoto sana.
 

1kush africa

JF-Expert Member
Dec 13, 2016
8,773
2,000
Pole sana braza, sasa hao wahusika unaowazungumzia wewe ni wepi?
Mi naamin ktk washkaj zako ulio soma nao watakuwepo wenye utaalam na hayo mambo wachek.


Mm jamaa yangu anahusika na upimaji ardhi seheme mbalimbali anaju fitna na chochoze zote za halali.. Yeye atanipia bure.
Na ameahidi lazima nipate Hati ya umiliki shamba.

Baada ya hapo ndo nitaanza shughuli zangu.

Ila kwa sasa amesema niturie
 

Pastory Kimaryo

JF-Expert Member
Jan 16, 2018
810
500
Mi naamin ktk washkaj zako ulio soma nao watakuwepo wenye utaalam na hayo mambo wachek.


Mm jamaa yangu anahusika na upimaji ardhi seheme mbalimbali anaju fitna na chochoze zote za halali.. Yeye atanipia bure.
Na ameahidi lazima nipate Hati ya umiliki shamba.

Baada ya hapo ndo nitaanza shughuli zangu.

Ila kwa sasa amesema niturie
Ok poa
 

Pastory Kimaryo

JF-Expert Member
Jan 16, 2018
810
500
SURA YA KWANZA

HISTORIA YA MFUMO WA MILKI YA ARDHI


Chimbuko na misingi ya mfumo wa umiliki na matumizi ya ardhi yaliyopo sasa umepitia katika vipindi vifuatavyo:-

A. MFUMO WA MILKI YA ARDHI KABLA YA UKOLONI

Katika kipindi hiki mfumo wa milki ulikuwa na sifa nne zifuatazo:-

· Ardhi yote ilikuwa ikimilikiwa kimila.

· Ardhi ilikuwa kwa ajili ya matumizi tu. mf-Kilimo,makazi,ufugaji,matambiko nk

· Wananchi walikuwa na sauti ya mwisho katika ardhi yao.

· Viongozi wa mila na jadi walikuwa wasimamizi na wasuluhishaji wa migogoro.

B. MFUMO WA MILKI YA ARDHI WAKATI WA UKOLONI (1890- 1960)

Tanganyika ilitawaliwa na Wajerumani na Waingereza:-

Wajerumani (1890–1919)

- Tamko la Wajerumani la mwaka 1895 liliweka bayana kuwa ardhi yote ni mali ya Mfalme Kaiza wa Ujerumani.

- Walianzisha umiliki kwa njia ya Hati.

Waingereza (1919–1961)

- Walitunga sheria ya Ardhi na 3 ya 1923 kuweka msisitizo katika mfumo ulioanzishwa na Wajerumani na kutamka kuwa ardhi yote ni mali ya umma chini ya Gavana.

- Umiliki wa hati ulikuwa na nguvu kisheria dhidi ya umiliki wa kimila

Katika kipindi cha ukoloni wazawa walipoteza sauti juu ya ardhi yao.

C.
KIPINDI CHA UHURU HADI SASA

Kipindi cha miaka ya 1961- 1990


- Mamlaka ya Gavana juu ya ardhi ilihamishiwa kwa Rais.

- Mwaka 1967 Azimio la Arusha lilitangazwa kuweka misingi ya uzalishaji mali mikononi mwa umma.

- Sheria zilizotungwa katika kipindi hiki ni pamoja na Sheria ya Utwaaji Na. 47 ya 1967 ambayo iliwezesha utwaaji wa ardhi kwa matumizi mbalimbali kama vile uanzishwaji wa Mashamba ya NAFCO na NARCO na Sheria ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa Na. 21 ya 1975 ambayo ilihalalisha uanzishwaji wa Vijiji vya ujamaa.

Kipindi cha kuanzia 1991 hadi sasa

- Licha ya kuwepo kwa Sheria hizo bado vijiji vingi viliendelea kuwa na migogoro kutokana na kuingiliana kwa haki na maslahi kati ya wakazi wa vijiji vipya na vya zamani

- Migogoro hiyo ilipelekwa kuundwa kwa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Masuala ya Ardhi mwaka 1991.

- Mwaka 1992 ilitungwa Sheria ya Milki ya Ardhi Tanzania ambayo ilifuta Vijiji vya asili na kuhalalisha vijiji vya ujamaa.

Tume ilitoa mapendekezo yake mwaka 1992 ambayo ni pamoja na:-

- Ardhi ipewe ulinzi wa Kikatiba

- Kuwepo na Sera na Sheria ardhi za kizalendo

- Kuweka milki ya hatma kwenye vyombo vyenye uwakilishi mpana wa wananchi

- Kuunda mfumo wa usuluhishi na utatuzi wa migogoro ya ardhi kuanzia ngazi ya kijiji

- Ardhi igawanywe katika makundi

Mapendekezo hayo yalipelekea kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sheria za Ardhi Na. 4 na Na. 5 za mwaka 1999.

SURA YA PILI

MASUALA MUHIMU KATIKA SERA NA SHERIA ZA ARDHI NCHINI TANZANIA

SERA YA TAIFA YA ARDHI YA 1995


Sera hii inaweka kanuni za msingi zinazotawala mfumo mzima wa umiliki, usimamizi na matumizi ya ardhi nchini. Kanuni hizo ni pamoja na:-

· Kutambua kuwa ardhi yote ya Tanzania ni mali ya umma na kuwa imewekwa mikononi mwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya raia wote.

· Kulipa fidia kamili, ya haki na kwa wakati kwa mtu yeyote ambaye haki miliki inafutwa matumizi yake.Pia kuwezesha ardhi kugawiwa kwa haki na kupatikana kwa raia wote

· Kuwawezesha raia wote kushiriki katika kutoa maamuzi ya mambo yanayohusiana na milki au matumizi yao ya ardhi.

· Haki ya kila mwanamke kupata,kumiliki,kutumia na kuuza au kuigawa ardhi kuwa sawa na haki ya mwanaume yeyote kwa viwango na masharti sawa

SHERIA ZA ARDHI ZA MWAKA 1999 NA SHERIA ZINGINE ZENYE MGUSO KATIKA ARDHI.

Maana ya ardhi

Ardhi ni ile inayojumuisha vitu vyote vilivyo juu na chini ya uso wa nchi vikiwemo majengo, uoto wa asili na maendelezo yote yaliyofanywa isipokuwa madini na bidhaa za mafuta na gesi.

Makundi ya ardhi

Ardhi imegawanyika katika makundi matatu ambayo ni:-

1. Ardhi ya kawaida/jumla: ni ardhi yote ya umma ambayo siyo ardhi ya hifadhi wala ardhi ya kijiji. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya ardhi Na.4,1999 inajumuisha ardhi ya kijiji ambayo haikaliwi wala kutumiwa na wanavijiji. Kamishna wa ardhi ndiye msimamizi wa kundi hili la ardhi.

2. Ardhi Hifadhi: ni ardhi iliyotengwa kwa shughuli maalumu kama vile hifadhi za misitu, barabara, vyanzo vya maji nk. Kundi hili liko chini ya usimamizi wa mamlaka mbalimbali za aina ya ardhi husika.

3. Ardhi ya Kijiji: hii ni ardhi iliyo ndani ya kijiji kilichosajiliwa na kubainishwa mipaka. Kwa mujibu wa sheria ya serikali za mitaa (Mamlaka za Wilaya), ya mwaka 1982 na kuwa chini ya usimamizi wa Halmashari ya Kijiji. Pia ardhi ya kijiji ni ardhi iliyotengwa chini ya sheria ya uundwaji wa vijiji,1965.Vilevile, ardhi ya kijiji ni ardhi ambayo si hifadhi, na kwa muda wa miaka kumi na miwili kabla ya sheria ya ardhi ya vijiji,Na.5 kutungwa, wanakijiji wamekuwa wanaikalia na kuitumia kama ardhi ya kijiji na pasipo kuwepo na aina yoyote ya umiliki au matumizi kabla au wakati wa ya kipindi hicho

MFUMO YA UMILIKAJI WA ARDHI

Kuna aina kuu mbili za umilikaji wa ardhi nchini Tanzania


· Umilikaji ardhi kimila: Huu ni utaratibu wa umilikaji ardhi kwa kufuata taratibu za kimila na desturi za jamii husika. Aina hii ya umiliki hutumika katika ardhi ya kijiji kama ilivyobainishwa katika sheria ya ardhi ya vijiji Na.5,1999

· Umilikaji ardhi kwa Hati: huu ni utaratibu wa hati unaotumika na kutolewa katika kundi la ardhi ya kawaida/jumla. Katika utaratibu huu mtu anaweza kumiliki ardhi kwa hati ya miaka 33, 66 au 99 na anakuwa na hadhi ya upangaji.

Upatikanaji wa Ardhi

Ardhi inaweza kupatikana kwa njia zifuatazo:-

i. Kurithi

ii. Kusafisha pori/eneo lisilo na mmiliki

iii. Kununua

iv. Kupewa zawadi

v. Kugawiwa na serikali

Mamlaka za usimamizi wa ardhi

1.
Halmashauri ya Kijiji- Hii haimaanishi kuwa Halmashauri ya Kijiji ni mmiliki wa ardhi ya kijiji bali ni msimamizi tu na haina mamlaka ya kugawa ardhi au kutoa ruhusa ya kutumia ardhi kimila bila idhini ya mkutano mkuu wa kijiji.

2. Mkutano Mkuu wa Kijiji- ndicho chombo chenye madaraka ya juu kijijini juu ya masuala yote ya yakiwepo masuala ya ardhi kama vile kuthibitisha na kukubali au kukataa maombi ya ardhi ya kijiji.

3. Kamishna wa Ardhi- ndiye mtendaji na msimamizi mkuu wa makundi yote ya ardhi na amepewa majukumu ya kiushauri kwenye ardhi ya vijiji.

Dhana za msingi katika mfumo wa milki na matumizi ya ardhi

· Utwaaji: hii ni mamlaka aliyopewa Rais ya kuchukua sehemu yoyote ya ardhi ya Tanzania na kisha kuigawa au kubadili matumizi kwa manufaa ya umma. Mamlaka hya yamebainishwa katika sheria ya Utwaaji,ya mwaka 1947

Katika utwaaji wa ardhi kuna mambo muhimu ya kuzingatia kama ifuatavyo:-

o Kutoa ilani ya kusudio la kutwaa ardhi husika

o Kutoa muda wa siku 90 za kutoa pingamizi kama lipo

o Kufanya tathmini ya mali na rasilimali na kulipa fidia kamili ya haki na wakati

· Uhawilishaji: ni mamlaka aliyopewa Rais ya kubadilisha ardhi kutoka kundi moja kwenda kundi lingine mfano kutoka ardhi ya hifadhi au jumla kuwa ardhi ya kijiji.

Katika uhawilishaji wa ardhi kuna mambo muhimu ya kuzingatia kama ifuatavyo:-

· Kutoa ilani kuhusu uamuzi huo kwa mmiliki wa ardhi husika na nakala kwa mamlaka husika.

· Rais kuingia katika eneo alilohawilisha ndani ya siku 60 baada ya ilani.

· Kutoa muda wa pingamizi usizopungua siku 20 au usiozidi siku 40.

· Kulipa fidia kamili, ya wakati na ya haki.

SURA YA TATU

MFUMO WA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI TANZANIA


Moja ya kanuni za msingi za sera ya taifa ya ardhi ni pamoja na kuanzisha mfumo ulio huru, unaofanya kazi kwa haraka na wa haki kwa ajili ya kuamua migogoro ya ardhi, ambao utasikiliza na kuamua migogoro ya ardhi bila ya ucheleweshaji usioa wa lazima

Maana ya migogoro ya ardhi

Wengi wetu tutakubaliana na ukweli kwamba migogoro ni kitu kibaya hasa kutokana na madhara yake, yawe ya muda mfupi au mrefu. Kwa kifupi, migogoro inajumuisha mabishano, mahitilafiano, ugomvi, mapigano, vita n.k baina, na kati ya watu, vikundi au jamii tofauti. Kutokana na hilo, basi, ipo haja ya kuendelea kubadilishana maarifa, uelewa, na uzoefu kuhusu namna migogoro inavyotokea sehemu mbalimbali na njia zinazotumika kuitatua ili yatusaidie kuepuka na kudhibiti utokeaji wa migogoro ya aina hiyo katika maeneo yetu.

Aina za migogoro ya ardhi

i. Wakulima na Wafugaji

ii. Wakulima kwa Wakulima

iii. Kijiji na kijiji

iv. Wafugaji kwa wafugaji

v. Wanakijiji na wawekezaji

vi. Mamlaka za hifadhi na wanaviji

Vyanzo vya migogoro ardhi

Vipo vyanzo vingi vya migogoro ya ardhi kama vile mgawanyo usio wasia wa mamlaka juu ya ardhi na utoaji wa haki kwa watumiaji,wananchi kutofahamu haki na wajibu wao juu ya masuala ya ardhi ,kipanuka kwa miji na kumeza maeneo ya vijiji,ukiukwaji wa sheria za ardhi miongoni mwa watendaji na uhaba wa rasilimali

Utatuzi wa migogoro ya ardhi

Migogoro ya ardhi hutatuliwa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na misingi iliyoainishwa katika Sheria ya Mabaraza na Mahakama za utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Na. 2 ya Mwaka 2002. Hata hivyo, ikumbukwe kwamba kabla ya kutungwa kwa Sheria hii ya 2002, migogoro ya ardhi ilikuwepo na ilikuwa ikitatuliwa kwa njia mbalimbali kama vile kwa njia ya kiutawala na katika ngazi za kifamilia na mila.

Vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi

a)
Baraza la Ardhi la Kijiji

Baraza la ardhi la kijiji linaundwa na Halmashauri ya Kijiji na kuthibitishwa na mkutano mkuu. Baraza linaundwa na wajumbe 7 ambao 3 kati yao lazima wawe wanawake na kila mjumbe atatumikia kwa kipindi cha miaka 3 na anaweza kuteuliwa tena.

Sifa za Wajumbe

· Awe na ufahamu juu ya sheria za kimila za eneo husika

· Awe mkazi wa kijiji husika

· Asiwe mbunge

· Asiwe hakimu

· Asiwe mtu mwenye umri chini ya miaka 18

· Asiwe mtu aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la kukosa uamifu au kukosa maadili

· Awe raia wa Tanzania na mwenye akili timamu

Kazi za Baraza

· Kupokea malalamiko ya ardhi kutoka kwa wanakijiji wa kijiji husika

· Kuitisha vikao vya kusikiliza madai ya migogoro kutoka kwa walalamikaji

· Kusuluhisha migogoro ya ardhi iliyoletwa mbele yake kwa lengo la kufikia mapatano baina ya wahusika.

·

Baraza la Ardhi la Kijiji linapaswa kutatua migogoro kwa njia za kimila au misingi ya haki asilia endapo taratibu za kimila hazitoi mwanya huo au njia na taratibu nyingine zozote ambazo wajumbe hao watakuwa wamepata katika mafunzo. Pia mjumbe wa Baraza la ardhi la kijiji hataruhusiwa kuwa msuluhishi katika shauri lolote ambalo yeye au mmoja wa jamaa zake wa karibu anayo maslahi. Kikao halali cha mkutano wa Baraza la Ardhi la Kijiji kitakuwa na wajumbe wasiopungua 4 ambao kati yao 2 lazma wawe wanawake.

Upande usioridhika na usuluhishi wa Baraza la Ardhi la Kijiji unaweza kupeleka shauri lake katika Baraza la Kata

b) Baraza la Kata

Mabaraza haya si mapya bali ni yale ambayo wakati mwingine husuluhisha migogoro ya masuala ya madai na jinai pamoja na migogoro inayohusiana na masuala ya ardhi.

Wajumbe wa Baraza watateuliwa na kamati ya maendeleo ya kata ambapo mtu yeyote mkazi wa vijiji vinavyounda kata husika anaweza kuwa mjumbe. Baraza litaundwa na wajumbe wasiopungua 4 na wasiozidi 8 ambao kati yao 3 watakuwa wanawake. Wajumbe wa Baraza watatumikia kwa kipindi kisichozidi miaka 3 na wanauwezo wa kuchaguliwa tena. Sifa za Wajumbe

· Asiwe mbunge

· Asiwe mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji au Kamati ya Maendeleo ya Kata

· Asiwe mwenye umri chini ya miaka 18

· Asiwe mwanasheria au mtu yeyote aliyeajiriwa katika idara ya Mahakama

· Asiwe mtu aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la kukosa uamifu au kukosa maadili

· Awe raia wa Tanzania na mwenye akili timamu

Kazi za Baraza

· Kuagiza urejeshwaji wa ardhi iliyonyang’anywa na kumtaka mtu atomize wajibu wake ndani ya mkataba

· Kutoa amri au maagizo ya kisheria na kuagiza ulipaji wa gharama zitakazo kuwa zimetumiwa na atakayeshinda kesi au mashahidi wake

· Kutoa agizo lolote ambalo litakuwa Ia haki kwa hukumu itakayotolewa

Baraza lina mamlaka ya kushughulika na mgogoro wa mali au ardhi iliyopo ndani ya kata husika na kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya mali au ardhi inayogombaniwa yenye thamani isiyozidi shilingi milioni tatu.

Baraza la Kata linapaswa kutatua migogoro kwa njia za kimila au misingi ya haki asilia endapo taratibu za kimila hazitoi mwanya huo au njia na taratibu nyingine zozote ambazo wajumbe hao watakuwa wamepata katika mafunzo.

Pia mjumbe wa Baraza la Kata hataruhusiwa kuwa msuluhishi katika shauri lolote ambalo yeye au mmoja wa jamaa zake wa karibu anayo maslahi.

Kikao halali cha mkutano wa Baraza la Kata kitakuwa na wajumbe zaidi ya 3 na 1 au zaidi awe mwanamke.

Rufaa

Upande usioridhika na maamuzi ya Baraza la Kata kuhusiana na masuala ya ardhi unaweza kukata rufaa katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya husika ndani ya siku 45.

c) Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya

Baraza hili linaudwa na Waziri katika ngazi ya Wilaya, Mkoa au Kanda na linajukumu la kusikiliza mashauri yote ndani ya eneo lake liliko anzishwa. Waziri pia atamteua mwenyekiti wa Baraza la Ardhi ambaye ataapishwa na Jaji wa Mahakama Kuu na atalitumikia kwa muda wa miaka 3 na anaweza kuteuliwa tena.

Waziri baada ya kushauriana na Mkuu wa Mkoa atateua wajumbe wasiozidi 7 ambao kati yao 3 watakuwa wanawake. Wajumbe wote watatumikia baraza katika kipindi cha miaka 3 na wanaweza kuteuliwa tena.

Sifa za Wajumbe

· Awe na umri usiopungua miaka 21 na mkazi wa kudumu wa Wilaya husika

· Asiwe mbunge, diwani, mjumbe wa Halmashauri, mjumbe wa Baraza la Ardhi la Kijiji au Kata

· Asiwe mtu aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la kukosa uamifu au kukosa maadili

· Awe raia wa Tanzania na mwenye akili timamu

Kazi za Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya

· Kuangalia kumbukumbu za maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Kata

· Kupokea ushahidi wa ziada kama utakuwa umeletwa

· Kufanya uchunguzi itakapoonekana ni lazima

· Kuthibitisha uamuzi uliotolewa na Baraza la Kata

· Kutengua/kukataa au kurekebisha uamuzi.

· Kufuta shauri lililo amriwa na Baraza la Kata

· Kuita na kuchunguza kumbukumbu za mashauri ya Baraza la Kata kwa madhumuni ya kujiridhisha na maamuzi yaliyotolewa

· Kuagiza baraza la kata kupitia upya au kurekebisha uamuzi uliofanyika.

Baraza litasikiliza kesi zote kwa kutumia sheria za ardhi za mwaka 1999 au mashauri yanayotajwa katika sheria zote ambazo zinaipa mamlaka Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya. Lugha inayotumika ni Kiswahili au Kiingereza isipokuwa kumbukumbu na hukumu zitaandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

Baraza lina mamlaka ya kusikiliza mgogoro wa ardhi iliyopo katika Wilaya, Mkoa au Kanda husika. Kadhalika, Baraza lina mamlaka ya kusikiliza na kutoa maamuzi ya migogoro ya ardhi ambayo thamani ya mali isiyo hamishika haizidi shilingi milioni hamsini na mali inayoweza kukadiriwa kwa thamani ya shilingi zisizozidi milioni arobaini. Katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya upande wowote unaweza kuwakilishwa

Rufaa

Upande usioridhika na maamuzi ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya unaweza kukata rufaa katika Mhakama Kuu ndani ya siku 45 iwapo shauri lilianzia Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya na siku 60 iwapo shauri lilianzia Baraza la Kata.

d) Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi

Mahakama hii inaundwa na Majaji wanaoteuliwa na Rais na inasikiliza rufaa kutoka Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya na pia inaweza kusikiliza mashauri kwa mara ya kwanza kwa vigezo vifuatavyo:-

· Shauri la madai ya mali isiyohamishika yenye kiwango cha thamani inayozidi shilingi milioni hamsini

· Mashauri mengineyo ambayo mali husika inakadiriwa kuwa na thamani ya fedha inayozidi shilingi milioni arobaini.

· Mashauri yote ambayo yanaihusisha Serikali chini ya Sheria ya Uwekezaji ya 1997, Sheria ya Ardhi ya 1999 na Sheria ya Utwaaji wa Ardhi ya mwaka 1967.

· Mashauri yote yanayohusika na mashirika ya umma

· Mashauri yoyote ya ardhi chini ya sheria yoyote iliyoandikwa ambapo mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hayakupewa mahakama au Baraza lingine.

Uwezo wa Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi

· Inaweza ikaamuru Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kutafuta ushahidi zaidi au kukubaliana na mashauri ya Baraza hilo.

· Kubadili au kubatilisha maamuzi ya awali

· Kushauri Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya na kukagua kumbukumbu zake wakati wowote na kutoa mwongozo kwa baraza hilo

· Kuangalia upya madai ya awali ya walalamikaji pamoja na ushahidi usio wa halali.

· Mtu yeyote anaweza kuwasilisha madai yake kwa kumtumia mtu mwingine

Muhimu: Kutokana na mrundikano wa kesi za migogoro ya ardhi katika Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi, mwaka 2009 Jaji Mkuu alitoa waraka ambao uliruhusu Mahakama zote Kuu kusikiliza migogoro ya ardhi nchini.

Mahakama ya Rufaa

Mahamaka ya Rufaa inaundwa na Jaji Mkuu ambaye huteuliwa na Rais. Katika ngazi hii Rais akishauriana na Jaji Mkuu atateua Majaji wa Mahakama ya Rufaa. Mahakama ya Rufaa itakuwa na uwezo wa kusikiliza rufaa toka kwa mtu yeyote ambaye hataridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu.

SURA YA NNE

MFUMO WA UTAWALA, USIMAMIZI RASILIMALI NA HAKI ZA RAIA KATIKA MUUNDO WA SERIKALI ZA MITAA

MUUNDO WA UTAWALA KIJIJINI.

Mkutano Mkuu wa Kijiji
.

a. Mkutano Mkuu wa Kijiji ni chombo kikuu cha utawala kijijini na ndicho chenye madaraka ya kujadili na kufanya maamuzi ya mwisho kijijini. Mkutano mkuu wa kijiji unaundwa na wanakijiji wote wenye umri usiopungua miaka 18 na wenye akili timamu. Maamuzi halali ya mkutano mkuu wa kijiji ni sharti yapitishwe na angalau asilimia 30 ya wananchi wote wanaounda mkutano mkuu wa kijiji.

b. Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Kijiji ni mwenyekiti wa kijiji. Yeye ndiye huongoza mijadala katika mkutano mkuu wa kijiji akisaidiana na Afisa Mtendaji Kijiji.

c. Mwenyekiti wa Kijiji anapaswa kutoa taarifa ya mkutano ikiambatana na agenda za mkutano angalau siku 7 kabla ya kufanyika mkutano.

Vikao vya Mkutano Mkuu wa Kijiji

a. Mkutano mkuu wa kawaida: Mkutano mkuu wa kijiji unatakiwa kuwa na kikao kimoja kila baada ya miezi mitatu yaani vikao 4 kwa mwaka.

b. Mkutano Mkuu wa dharura: Mkutano huu unaweza kuitishwa kama ikionekana kuna sababu maalum za kuitisha kikao cha dharura. Ingawa sheria haisemi nani anaweza kuitisha mkutano wa dharura, ni busara wanakijiji kupitia mkutano mkuu wa kijiji kujiwekea utaratibu nani mwingine na katika hali gani anaweza kuitisha kikao cha dharura.

c. Mkutano Mkuu wa Uchaguzi: huu ni mkutano maalum ambao hufanyika kila baada ya miaka 5 kwa madhumuni ya kuchagua mwenyekiti wa kijiji pamoja na wajumbe wa halmashauri ya kijiji.

Kila mjumbe wa mkutano mkuu wa kijiji bila kujali jinsia au hadhi yake katika jamii ana haki sawa ya kushiriki kikamilifu kutoa mchango wake, kupiga na kupigiwa kura bila ubaguzi au kipingamizi chochote

Majukumu ya Mkutano Mkuu wa Kijiji

a. Kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijiji itakayotolewa na serikali ya kijiji

b. Kupokea, kujadili na kupitisha taarifa ya mapato na matumizi ya fedha ya kijiji pamoja na mapendekezo ya kodi, ushuru na vyanzo vingine vya kuongeza mapato ya kijiji.

c. Kupokea na kujadili mapendekezo ya serikali ya kijiji kutunga sheria ndogo

d. Kupokea, kujadili na kuyafanyia uamuzi masuala yahusuyo ugawaji wa ardhi na matumizi ya rasilimali nyingine kijijini.

Maamuzi ya mkutano mkuu wa kijiji yanaweza kuwa:-

a) Uamuzi wa kutekelezwa

b) Agizo

c) Pendekezo

d) Azimio

Halmashauri ya Kijiji

· Halmashauri ya Kijiji ni chombo kikuu cha utendaji katika utawala wa kijiji. Hata hivyo halmashauri huwajibika kwa Mkutano Mkuu wa Kijiji.

· Halmashauri ya kijiji inaundwa na Mwenyekiti wa Kijiji, wenyeviti wa vitongoji ambao huchaguliwa na wakazi wa vitongoji husika na wajumbe wengine watakao chaguliwa na mkutano mkuu.

· Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji huchaguliwa na Mkutano Mkuu wa uchaguzi kila baada ya miaka 5. Kila mwanakijiji mwenye umri usiopungua miaka 21 ana haki ya kugombea na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri

· Wajumbe katika Halmashauri ya Kijiji wanatakiwa wasizidi 25 na wasipungue 15 ambao kati yao wanawake wasiwe chini ya robo ya wajumbe wote.

Vikao vya Halmashauri ya Kijiji

· Halmashauri ya Kijiji itakuwa inakutana mara moja kila mwezi, yaani mara 12 kwa mwaka. Hata hivyo mikutano ya dharura inaweza kuitishwa wakati wowote litakapotokea jambo la dharura

· Kikao halali cha Halmashauri ya Kijiji ni mahudhurio ya nusu ya wajumbe wa halmashauri hiyo.

Majumkumu ya Halmashauri ya Kijiji

· Kutafakari maamuzi, maazimio na mapendekezo ya mkutano mkuu wa kijiji na kubuni mbinu na njia za kutekeleza.

· Kupokea na kufanyia kazi taarifa za mikutano ya vitongoji na kamati zake na kuainisha mambo yanayohitaji kuamriwa na mkutano mkuu wa kijiji.

· Kupokea, kutafakari na kuyafanyia kazi maagizo na mapendekezo kutoka ngazi nyingine za utawala na utendaji hususan Kamati ya Maendeleo ya Kata na Halmashauri ya Wilaya

· Kubuni sera na mwelekeo wa kijiji na kuyapendekeza katika mkutano mkuu wa kijiji

· Kuandaa mipango ya muda mrefu ya maendeleo ya kijiji.

· Kutunga sheria ndogo kwa mashauriano na mkutano mkuu wa kijiji

· Kupokea, kutafakari na kuamua au kupendekeza maombi ya ugawaji ardhi na rasilimali nyingine za kijiji katika mkutano mkuu wa kijiji.

Katika utekelezaji wa shughuli zake, Halmashauri ya Kijiji inatakiwa kuzingatia maslahi na ushiriki wa wanakijiji katika kutoa maamuzi.

Kamati za Halmashauri ya Kijiji

Muundo na uendeshaji

· Sheria inaipa uwezo halmashauri ya kijiji kuunda kamati zake 3 ili kusaidia utekelezaji wa majukumu yake. Kama hizo ni:-

o Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango

o Kamati ya Huduma za Jamii na Shughuli za kujitegemea

o Kamati ya Ulinzi na Usalama

· Licha ya kamati hizo halmashauri ya kijiji au mkutano mkuu wa kijiji unaweza kuunda au kuiagiza halmashauri ya kijiji kuunda kamati zingine za kudumu au za muda kushughulikia jambo maalum.

· Ingawa kamati hizi ni kamati za halmashauri ya kijiji na wajumbe wake huwa wajumbe wa halmashauri ya kijiji, sheria haizuii mwanakijiji yeyote kuwa mjumbe wa kamati

Uongozi wa Vitongoji na nafasi yake katika serikali za mitaa/kijiji

Mambo ya muhimu kuzingatia

o Kitongoji ni sehemu ya kijiji na si ngazi ya utawala inayojitegemea

o Mikutano ya vitongoji ni mahala pa kuendeleza mijadala na siyo pa kufanya maamuzi

o Mwenyekiti wa kitongoji pia ni mjumbe wa halmashauri ya kijjiji na jukumu lake kubwa ni kuwa kiungo kati ya wakazi wa kitongoji na halmashauri ya kijiji

o Mawasiliano yote kati ya mwenyekiti wa kitongoji na viongozi na watendaji wa ngazi ya juu hayana budi yapitie katika serikali ya kijiji na yasiwe moja kwa moja

Miradi yote hata ikiwa katika kitongoji ni ya kijiji chini ya usimamizi wa halmashauri ya kijiji

SURA YA TANO

MPANGO MATUMIZI BORA YA ARDHI

Sheria ya Mipango Matumizi ya Ardhi Na.6 ya mwaka 2007
imeweka misingi na malengo ya kupanga matumizi ya ardhi kuwa ni:

· Kuwezesha ufanisi na usimamizi muafaka wa matumizi ya ardhi

· Kuwezesha wamiliki na watumiaji wa ardhi kuwa na matumizi na uzalishaji bora wa ardhi

· Kuwezesha matumizi endelevu ya ardhi

· Kuwezesha na kuasisi mfumo wa kuzuia migogoro ya matumizi ya ardhi

· Kuweka mfumo wa kuratibu ujumuishaji wa kisekta katika ngazi mbalimbali

ikiwemo miundo ya kisiasa na kiutawala

· Kuweka mfumo wa kuhuisha misingi ya maendeleo ya taifa iliyoainishwa katika sera za Serikali

Misingi hii ni muhimu ili kuhuisha upanukaji wa makazi, maeneo ya kilimo, maeneo ya malisho, ukataji miti kwa matumizi mbalimbali, mahitaji ya maji n.k. ambavyo vinazidi kuongeza mzigo/kani kwenye ardhi kwa matumizi mbalimbali na kusababisha kuongezeka kwa idadi ya migogoro miongoni mwa watumiaji wa ardhi,kutokuwa na uhakika wa miliki na matumizi ya ardhi, maendeleo duni ya soko la ardhi lisilo rasmi, uharibifu wa udongo na vyanzo vya maji,Ufyekaji misitu,ongezeko la kuhamahama kwa watu na mifugo,kupanuka kwa ukame na tishio la jangwa.

Ngazi za Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi huandaliwa na kutekelezwa katika ngazi mbalimbali ikiwemo:-

· Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi

· Mipango ya Kanda

· Mpango wa Wilaya wa Matumizi Bora ya Ardhi

· Mpango wa Kijiji wa Matumizi Bora ya Ardhi.

Mpango wa Kijiji wa Matumizi Bora ya Ardhi:- ni utaratibu wa kutathmini na kupendekeza namna mbalimbali za matumizi ya maliasili/rasilimali, (mf- ardhi na misitu) ili kuinua hali ya maisha ya wanakijiji na kuondoa umaskini. Utaratibu wa kupanga, kutekeleza na kuhuisha matumizi ya ardhi unafaa zaidi iwapo utafanyika kwa njia ya ushirikishwaji, ikiwa na maana kuwa watumiaji wakubwa wa ardhi ambao ni wanakijiji wanashirikishwa kikamilifu.Ili kuhakikisha kuwa wanakijiji wanashiriki kikamilifu, ni muhimu kuzingatia makundi mbalimbali yaliyopo katika kijiji (mf- wakulima, wafugaji, pamoja na jinsia na rika), ambayo yanaweza kuwa na utashi na malengo yanayotofautiana.

Timu ya PLUM (Wilaya) huwezesha Halmashauri ya Kijiji kuunda Kamati ya Usimamizi wa Ardhi ya Kijiji ambao kwa pamoja hufanya tathmini shirikishi ya kijiji ,kuweka Mpango kazi wa jamii, na hatimaye kuandaa rasimu ya mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji, ambayo huwasilishwa kwenye Mkutano wa Kijiji kujadiliwa ili kupelekea kwenye mpango kamili wa matumizi bora ya ardhi.

Sheria Ndogo za Usimamizi wa Matumizi Bora ya Ardhi Vijijini

Sheria ndogo zinaweza kutungwa kwa ngazi ya halmashauri za miji, wilaya na kijiji; na lazima zisipingane na Sheria za Kitaifa. Sheria ndogo za vijiji zinatungwakulingana na Sheria ya Serikali za Mitaa Na.7 (1982) Fungu la 163–167.

Kwa usimamizi wa ardhi (PLUM), sheria ndogo zinaweka msingi wa usimamizi kisheria, na zinaangaliwa kama nyenzo za kutia nguvu utekelezaji wa makubaliano maalumu ya wanakijiji yanayohusu usimamizi wa maliasili na mipango ya matumizi ya ardhi.

Hatua za upangaji na utekelezaji

Mwongozo wa Ushirikishwaji Katika Mipango na Usimamizi wa Matumizi Bora ya Ardhi Vijiji ni unabainisha hatua kuu 6:-

(i) Maandalizi Wilayani: Uhamasishaji, kuunda timu ya PLUM ya wilaya, na kuweka Mpango wa Utekelezaji wa PLUM wa wilaya.

(ii) Tathmini ya Matumizi ya Ardhi Vijijini: Uhamashishaji taasisi za kijiji; Elimu ya Sera na Sheria za Ardhi; Tathmini ya matumizi ya ardhi na raslimali; kubaini matatizo fursa na vikwazo; na kuweka Mpango Kazi wa Jamii.

(iii)Kubaini, kuweka na kupima mipaka ya ardhi ya kijiji; utatuzi wa mogogoro ya mipaka; Masjala ya Ardhi ya Wilaya; utoaji Cheti cha Ardhi ya Kijiji. Kuandaa ramani ya msingi ya matumizi ya ardhi ya kijiji

(iv) Upangaji Matumizi Bora ya Ardhi ya Kijiji: Ushirikishwaji katika mipango na usimamizi; kuainisha hatua stahili za usimamizi; na Sheria Ndogo za Usimamizi wa

Matumizi Bora ya Ardhi.

(v) Utawala wa Ardhi ya Kijiji: Masjala ya Ardhi ya Kijiji; Utoaji, usajili na usimamizi wa Hatimiliki za Kimila; na Utatuzi wa migogoro ya miliki.

(vi) Hatua Stahili za Usimamizi: Utekelezaji wa Hatua Stahili za Usimamiaji wa Ardhi na Uimarishaji (Mafundi sanifu wa kijiji; Uimarishaji; Tathmini;Ufuatiliaji na Urejeaji Mipango).

Tathmini Shirikishi ya Kijiji

Timu ya PLUM huwezesha Halmashauri ya Kijiji ikijumuika na Kamati ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Kijiji kufanya Tathmini Shirikishi ya Kijiji inayolenga matumizi ya ardhi. Hii hufanyika kwa kukusanya, kuchambua na kuwekea kumbukumbu takwimu muhimu za kijiji kwa kila kitongoji kama vile idadi ya watu, mifugo, vyanzo vya maji, misitu, huduma za kiuchumi, kijamii n.k. Pia Timu ya PLUM huwezesha. Halmashauri ya Kijiji ikijumuika na Kamati ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Kijiji kuchambua na kutathmini matatizo, vikwazo na fursa za utatuzi katika matumizi ya ardhi.

Kuweka Mipaka ya Vijiji

Baada ya kukamilisha Hatua ya 2 ya ‘PLUM’, itajitokeza bayana kama mipaka ya kijiji

inatambulika na au iliishapimwa.Timu ya ‘PLUM’ ya Wilaya inaweza kurahisisha kazi hii kwa kuhakiki kupitia Ofisi ya Ardhi ya Wilaya na kuweka orodha ya vijiji katika makundi yafuatayo:-

(i) Vijiji ambavyo vimepimwa (vina ramani ya mipaka) na havina migogoro ya mipaka. Vijiji hivi moja kwa moja viandaliwe Cheti cha Ardhi ya Kijiji.

(ii) Vijiji ambavyo mipaka yake inatambulika (lakini havijapimwa) na havina migogoro ya mipaka. Vijiji hivi vinaweza kuandaliwa ramani ya mipaka kwa njia rahisi ya chombo cha upimaji (GPS), na kuandaliwa Cheti cha Ardhi ya Kijiji.

(iii) Vijiji ambavyo mipaka yake iliishapimwa, lakini kwa sasa vina migogoro ya mipaka kama vile vimegawanyika. Migogoro ya mipaka itatuliwe kwanza, na kubaini mipaka inayokubalika kwa pande husika.

(iv) Vijiji ambavyo havijapimwa na vina migogoro ya mipaka. Migogoro ya mipaka itatuliwe kwanza, na kubaini mipaka inayokubalika kwa pande husika.

Jukumu la awali na la msingi ili Halmashauri ya Kijiji isimamie ardhi ya kijiji kwa mujibu wa sheria, ni kutambua mipaka ya kijiji na kupata Cheti cha Ardhi ya Kijiji. Katika kufanya hili, Halmashauri ya Kijiji husika haina budi kuwasiliana na mamlaka za ardhi inayopakana na kijiji; kama vile Mamlaka za Hifadhi, na Halmashauri za Vijiji jirani; ili wakubaliane mpaka wa ardhi yao. Halmashauri ya Kijiji, aghalabu itakasimu shughuli hii kwa kamati; kama vile Kamati ya kusimamia Matumizi ya Ardhi au Mazingira.

Masjala ya Ardhi ya Kijiji

Kifungu cha 21 cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji (1999), kinaelezea jinsi ya kuanzisha na kusimamia Masjala ya Ardhi ya Kijiji na Wilaya. Ili Halmashauri ya kijiji itoe na kusajili Hatimiliki ya Kimila, ni lazima ianzishe Masjala ya Ardhi ya Kijiji inayosimamiwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO). Ofisi ya VEO inaweza kupanuliwa au kukarabatiwa ili kuwa na chumba cha Masjala chenye hadhi na sifa ya kudumu. Kwa hiyo pamoja na kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi, ratiba ya utekelezaji wa mpango huo ihusishe na ujenzi wa masjala ya ardhi ya kijiji na wilaya kamasehemu ya mchakato wa utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi, ili kuwezesha usajili wa hatimiliki za ardhi kwa wamiliki. Masjala ya ardhi ya kijiji na wilaya yasitumike kusajili hati miliki za kimila kwa ajili ya watu binafsi pekee, bali pia kusajili maeneo ya matumizi ya pamoja na ya jumuia k.v. maeneo ya huduma za jamii, maeneo ya malisho, misitu ya aina mbalaimbali, vyanzo vya maji, hifadhi ya wanyama pori (WMAs), kilimo cha umwagiliaji n.k. kwa vikundi husika ili kulinda maeneo hayo yasivamiwe.

Cheti cha Ardhi ya Kijiji

Mara mipaka ya kijiji ikiishawekwa na kupimwa, mamlaka husika (Kamishna wa Ardhi) atatoa Cheti cha Ardhi ya Kijiji kwa Halmashauri ya Kijiji kwa mujibu wa Fungu la 7 (6–12) la Sheria ya Ardhi Vijiji ya 1999. Hii ni hati muhimu inayopaswa kutunzwa na Halmashauri ya Kijiji, inayotumika kumaanisha mamlaka ya Halmashauri ya Kijiji kusimamia ardhi ya kijiji.

Utoaji wa Cheti cha Ardhi ya Kijiji

Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinatolewa kwa jina la Rais, akikasimu mamlaka yake kwa Halmashauri ya Kijiji kusimamia Ardhi ya Kijiji. Cheti hiki kinahakikisha kukaliwa na kutumia kwa ardhi ya kijiji na wanakijiji kwa kuzingatia taratibu na kanuni za kimila zinazotumika katika ardhi, ambako kijiji kipo.

· Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinaandaliwa na Ofisa Ardhi wa Wilaya kwa kutumia Fomu ya Ardhi ya Vijiji Na. 16,

· Kuwekewa mchoro wa mipaka ya kijiji na eneo lake

· Kusainiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji na Afisa Mtendaji wa Kijiji,

· Kusajiliwa wilayani na kupewa namba ya usajili.

· Cheti hutumwa kwa Kamishna wa Ardhi kusainiwa na kuwekwa lakiri.

· Ofisi ya Kamishna hubaki na nakala moja kwa kumbukumbu,

· Nakala mbili hutumwa kwa wilaya husika, ili nakala moja ibaki katika Masjala ya Ardhi ya Wilaya, nakala moja ipelekwe kwenye Masjala ya Ardhi ya Kijiji husika.

Inapotokea mipaka ya ardhi ya kijiji ikabadilishwa vyovyote vile, ni wajibu wa Halmashauri ya Kijiji kumjulisha mapema Kamishna wa Ardhi mabadiliko hayo. Vilevile Halmashauri ya Kijiji inapaswa imtumie Kamishna wa Ardhi Cheti cha Ardhi ya Kijiji, ili Kamishna afanye mabadiliko yaliyotokea katika cheti husika. Kwa mintarafu hii; Kamishna wa Ardhi atatunza Daftari ya Ardhi za Vijiji.

Usajili wa Vijiji

Utoaji wa Cheti cha Ardhi ya Kijiji usichanganywe na Usajili wa Vijiji unaofanywa na Msajili wa Vijiji kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 7 ya mwaka 1982.

Usajili wa kijiji ni uthibitisho wa kuanzishwa kwa kijiji, ambacho mipaka yake inapaswa kutambuliwa na kuandaliwa Cheti cha Ardhi ya Kijiji. Sheria ya Ardhi Vijiji ya 1999 inatambua na kujumuisha mamlaka haya, katika Fungu la 7 (12).

Hatimiliki ya Kimila

Hii ni hati inayotolewa na Halmashauri ya Kijiji ili kuthibitisha umiliki wa Ardhi wa mwombaji kwa taratibu za Kimila.

· Itatolewa katika fomu maalumu

· Kitatiwa saini na mwenyekiti pamoja na afisa mtendaji wa Kijiji

· Kitatiwa saini au alama na mtu ambaye atapewa Hatimiliki ya Kimila inayohusika katika ukurasa wa cheti hicho

· Kitatiwa saini, kuwekwa lakiri na kusajiliwa na afisa ardhi wa wilaya husika

· Kinaweza kutolewa kwa kipindi kisicho na kikomo au kwa kipindi chochote ambacho ni pungufu

· Kitalipiwa kodi ya pango na wageni au wasio wenyeji wa kawaida pamoja na taasisi isiyo ya kijiji

Cheti hiki kitatumika ipasavyo kulingana na mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji husika.

Aina za Matumizi ya Ardhi kwenye ngazi ya Kijiji

Aina ya matumizi ya ardhi katika vijiji vingi hapa nchini ni :-

(a) Maeneo ya Makazi (maeneo ya majengo)

Hili ni eneo linalotumiwa au lililotengwa kwa ujenzi wa nyumba za kuishi na huduma mbalimbali.

(b) Maeneo ya Kilimo

Maeneo yanayotumika au yaliyotengwa kwa kulima mazao.

· Mazao ya kudumu (muda mrefu):

· Mazao ya msimu:

· Mazao ya umwagiliaji:

· Kilimo msitu (mseto):

© Maeneo ya Kuchungia

Maeneo yanayotumika au yaliyotengwa kwa uchungaji huria k.m. nyanda, malisho, nyika.

(d) Maeneo ya Misitu

Maeneo yaliyo na mimea asilia yenye miti mingi.

(e) Maeneo ya maji/vyanzo vya maji

Maeneo ya mito, maziwa, makinga maji, mabwawa, ardhi owevu (majimaji), chemichemi n.k.

(f) Maeneo ya Wanyama pori

Maeneo yaliyotengwa hasa kwa matumizi ya wanyamapori na mimea asilia.

(g) Matumizi mengine ya ardhi

Matumizi mengine maalumu katika baadhi ya vijiji k.m. uvuvi, uchimbaji madini, nishati, njia za mawasiliano, maeneo maalumu kimila k.v. tambiko n.k.

Sheria Ndogo za Matumizi ya Ardhi Vijijini

Sheria ndogo za vijiji zinahusu taratibu ambazo huwekwa na mamlaka za wenyeji, ambazo hapana budi kufuatwa katika eneo fulani. Sheria ndogo zinaweza kutungwa kwa ngazi ya halmashauri za miji, wilaya na kijiji; na lazima zisipingane na Sheria za Kitaifa.

Sheria ndogo zinaweka msingi wa usimamizi na matumizi ya ardhi na zinaangaliwa kama nyenzo za kutia nguvu utekelezaji wa makubaliano maalumu ya wenyeji.

Kutunga Sheria Ndogo za Kijiji

Kulingana na Sheria ya Serikali za Mitaa Na.7 (1982) Fungu la 163–167 ufuatao ni

muhtasari wa taratibu za kutunga Sheria Ndogo za Kijiji:-

· Halmashauri ya Kijiji inaweza kuanzisha utaratibu huu wakati inapoona kuna haja, na kujadili malengo na maudhui ya Sheria. Kwa upande wa Sheria Ndogo zinazohusu matumizi ya ardhi ni vyema kuhusisha Kamati ya Usimamizi wa Ardhi, na Timu ya ‘PLUM’ ya Wilaya kupata ushauri wa kiufundi.

· Halmashauri ya Kijiji huwaagiza viongozi wa vitongoji na wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Ardhi, kuandaa mikutano ya vitongoji au aina nyingine ya sehemu ya kijiji kwa majadiliano na wanakijiji, juu ya malengo na maudhui ya Sheria Ndogo.

· Viongozi wa vitongoji na au Kamati ya Usimamizi wa Ardhi, hutoa ripoti ya matokeo ya mikutano midogo kwenye Halmashauri ya Kijiji. Halmashauri ya Kijiji pamoja na Kamati ya Usimamizi wa Ardhi, hutumia matokeo haya kutayarisha Rasimu ya Sheria Ndogo kwa msaada wa timu ya PLUM ya wilaya.

· Timu ya Wilaya (PLUM) huwasilisha rasimu kwa Hakimu wa Wilaya au Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ili kuhakikisha kuwa maudhui hayakiuki au kugongana na sheria ndogo za wilaya na pia Sheria na Sera za Kitaifa.

· Hatimaye, Halmashauri ya Kijiji huwasilisha rasimu ya Sheria Ndogo kwenye Mkutano wa Kijiji kwa majadiliano na kuidhinishwa. Ni vyema kumkaribisha Afisa Mtendaji Kata na Diwani kwenye mkutano huu.

· Sheria Ndogo pamoja na muhtasari wa Mkutano wa Kijiji hupelekwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata ambayo huhakikisha kuwa matakwa na maslahi ya vijiji vingine jirani yanalindwa.

· Afisa Mtendaji wa Kata au Diwani wa Kata huipeleka Sheria Ndogo katika Halmashauri ya Wilaya kuidhinishwa na inapohitajika kusaidia utekelezaji wake. Wilaya hupeleka nakala ya Sheria Ndogo iliyotiwa sahihi na Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya kwenye Halmashauri ya Kijiji, ikionyesha tarehe ya kuanza kutumika kwake.

· Ni wajibu wa Halmashauri ya Kijiji kutangaza kwa wanakijiji uamuzi wa Halmashauri ya Wilaya. Hii inaweza kufanyika katika Mikutano ya Kijiji, au vitongoji, ikisaidiwa na kuitangaza kwenye makutano ya umma na hadhara nyinginezo.

MWISHO.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom