Zilikuwa nyakati za Chico, Nat King Cole, Dean Martin, Sammy Davis Jr, Sidney Poitier..Ukipenda Sal

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,792
31,804
20170202_212905.jpg



Baada ya kusoma taazia ya Abdallah Tambaza sina nguvu ya kuandika chochote kuhusu rafiki yangu Mohamed Awadh maarufu kwa jina la Chico. Taazia ya Abdallah mimi imenitia simanzi kiasi ya machozi kunilengalenga kila ninapopita sentensi moja kwenda nyingine sababu ni kuwa Abdallah alikuwa ananitajia mambo na watu niliokuwa nawafahamu na wengine tayari wameshatangulia mbele ya haki. Nikawa kama vile watu hawa nawaona tena. Miezi kama miwili hivi nilikutana na Chico Masaki akiwa amekaa na wajukuu zake ndani ya gari. Tulisalimiana kwa bashasha sana na wala haukunipikitikia kuwa ile ndiyo itakuwa mara yetu ya mwisho kuonana. Mazikoni Kisutu nimekutana na Abdallah kisha nikamuona na ndugu yake Mwinyikhamisi yeye ni mkubwa kwangu kwa umri na aliponiona tu Mwinyikhamisi anahangaika kusimama maana alikuwa kakaa chini miguu inampa tabu. Kila nikimzuia kunisimamia yeye ndiyo anashikilia kushika mkono wangu asimame tusalimiane. Namwambia, ‘’Ka Mwinyi starehe, starehe…’’ Wapi hanisikii anailazimisha miguu yake isimame anisalimie mimi mdogo wake. Mapenzi na heshima iliyoje mkubwa kumsimamia mdogo. Hivi ndivyo wazee wetu walivyotufunza. Allah awarehemu.

8aobHTr34I-5Dcd0FRj6259scyuS8-r4Ev7p5lHr0PKU2WeNcEsbU4zrmsu44PgSJ6tlViMWa85m_Ikdc7lT7DTZ8cBbXBAxQhj09hTYV54JwuW-7LoGQre1I16OWtbxDISeF47Xo0sK1B8Bt8tm0_tpyvvrg3AXqNgShhzMkyTWII1NpXlIq1racegG2nH5qz2XkGNfHZ_ztNyY2wJt2hivI8bG2r4Qa9wZ6AZIK7matSK23WB4rWEiGILRV1HGrfLVZVMQlwHFzz2JyRWndPZF555l9adxjGqf2z9Sg5fPr0rgKTrW6mz71wS7Iqa7IzOa_7afhv3S9EQceXvNBY4kFjEvH1Vef9LpZIW16ls1XQmvUC0w0qdmwf7a1dn_DcAxXn68dt246pXE6Uorm4or73d_3C8kdsS1p61rsGyDiAiMCs5LkazhkC4dPRBPjLvS3iX_E8KhQuhLXNyPcwoeCfVUKCHWDnbVBsm47mvj1tkmeCI8PwHub8lyeMZ03UzPtxa35RfufdCj6-wzuGrG3OlZDA3vRVwDE1GAPJT8U8Nz5n0YjwtblTYMFw5MGqMIq4vFLE-TSy_r0mWN1IOgmLE3uLGFq03UyGZX7WJYh6vPYg=w923-h692-no

Kulia ni Mwinyikhamis, Abdallah Tanbaza na Ibrahim wote hawa ni ndugu
wakiwa katika khitma ya Dar es Salaam Saigon Club


Niko katika, ''keyboard,'' sasa naandika. Msiba wa Chico umetugusa wengi khawa vijana wa Dar es Salaam. Mwinyikhamis alikuwa mchezaji mpira wa sifa katika New Port Club wakati wa ujana wake. Leo Mwinyi hawezi kusimama. Inanijia mechi moja ambayo naamini iko katika kumbukumbu ya wenzangu wengi wa wakti ule. New Port imepangiwa kucheza na Brazil, timu ya wababe watu wakorofi wa sifa mji mzima unawafahamu kwa shari yao ingawa walikuwa na mpira mzuri wa wachezaji wa kusifika. New Port, club ya vijana waungwana, wastaarabu wanaocheza soka la kupendeza. Mashabiki wanajiuliza itakuwaje mpira huu leo na wahuni wale?

Saa kumi jangwani pamefurika. Hii ni mechi ya kikombe mfano wa ''league,'' kwa sasa. Wakati ule vilabu vya mtaani villikuwa na nguvu na uongozi thabiti wa kuweza kuchezesha mechi nzuri zilizojaza watazamaji na kuibua gumzo mji mzima. Brazili kuna Kitwana (Victor Mature) mbabe wa sifa, Mrisho (Wanted) mbabe wa sifa, Abdallah Mkwanda (Inger Johannsson), mbabe pia, Suleiman Jongo (Rory Calhoun) mchezaji mpole na muungwana sana lakini anacheza timu ya wababe, Mohamed Ndava. Shamte Kobe (Bingwa wa Mieleka na ngumi), Hamisi (Marlon Brando), Sadiki Ngwira (Kitonsa), Salum Hussein (Livingstone Madegwa) mtoto wa Sheikh Hussein Juma ana boli safi sana. Wengi katika hawa wametangulia mbele ya haki Allah awarehemu. New Port wanajua kuwa leo wanacheza meshi muhimu na watu washari na wababe wa mji.

New Port, akina Mwinyikhamis na wenzake wametandaza boli staili ya TPC mpira unatembea kwenye majani na wanakwepa hila zote za ubabe hakuna kukunjana mashati. Brazil imefedheheka kwa sababu mechi imeishia sare na wababe hawakuweza kutamba. Hata hivyo New Port wametoka kwenye mechi ile hoi kama wamepigana round 15 na Muhammad Ali. Brazil usiku ule ule wamewafata New Port club kwao kudai wapewe siku ya mechi ya marudiano. Wamefika New Port wamepanda baiskeli zao na kuziegesha kwa vishindo. Wanatafuta shari ile waliyoikosa uwanjani.

Uongozi wa New Port walifanya kikao cha haraka na uamuzi ukawa hawataki kurudiana na Brazil, wahuni wale na wapewe ushindi. Asubuhi taarifa zimeenea Kariakoo nzima na pembezoni kuwa ile mechi ya marudiano haitakuwapo New Port wamekataa kucheza na wametoa ushindi. Brazil wakautangazia mji kuwa New Port wamejisalimisha. Hii ilikuwa 1965 au 1966 maana nakumbuka mimi nilikuwa niko shule ya msingi.

Msomaji nimekuletea kisa hiki kirefu upate kujua Dar es Salaam aliyokulia Chico na sisi sote wa uzao ule ilikuwaje.

Chico alikuwa mmoja wa wacheazaji wa Everton Club iliyokuwa Mtaa wa Narung’ombe si mbali sana na nyumbani kwao Mtaa wa Tandamti mtaa aliokuwa akiishi Mzee Mshume Kiyate rafiki mkubwa wa Mwalimu Nyerere na mmoja katika wazee wa Baraza la Wazee wa TANU lililoongoza harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mtaa huu umebadilishwa jina na kuitwa Mshume Kiyate lakini sasa takriban mwaka wa ishirini kibao cha jina la Mshume Kiyate hakijawekwa kwa sababu ambazi si tabu kuzifahamu. Sasa hii Everton baada ya mtafaruku ndiyo ilikuja kuundwa Saigon na baada ya muda na uhasama wa muda mfupi Everton ilikufa na wote wakajiunga na Dar es Salaam Saigon hii tuijuayo hivi sasa. Turudi kwa Chico.

Chico alikuwa akicheza kama mlinzi na namkumbuka Chico kwa uchezaji wake wa ukakamavu, staili ikiitwa ''kikiri,'' Chico akicheza, ''halfback,'' na alikuwa, ‘’hard tackler’’ mchezaji aliyekuwa akiingia kufata, ''loose ball,'' anakumba mpira na mguu wako. Navikumbuka viatu vyake vya mpira alivyokuwa akivaa – ''Adidas Admire.'' Kulikuwa siku zile na aina mbili za viatu vya Adidas, ''Adidas Admire,'' na ''Adidas La Plata.'' Maarufu ambavyo wengi tukivaa ilikuwa ni ''La Plata.'' Hivi vilikuwa na njumu yaani, ‘’studs,’’ unyayo mzima wakati, ''Admire,'' njumu zilikuwa chache na zilikuwa za kufunga na ‘’spanner.’’ Chico alikuwa kijana, ‘’special.’’ Simkumbuki kijana yoyote katika timu zetu za mitaani aliyekuwa akivaa, ''Admire.''

Ndani ya uwanja Chico alikuwa nahodha mzuri. Yuko nyuma na mbele marehemu Jumanne Masimenti, Jalala, Oshaka (Mazola), Mashaka (Alfredo Di Stefano), Juma Abeid, Ali Kodo, Maufi wanashambulia sauti ya Chico itasikika akihamasisha kwa Kiingereza kisafi kilichonyooka mpira upelekwe goli la adui. Utasikia akipiga kelele, ‘’Push the ball forward,’’ ‘’Score,’’ au ‘’On him,’’ yaani asiachiwe mpira adui. Inawezekana hapo anamuhimiza Ahmada Digila (Danny Blachflour) au Khalid Fadhil (George Young) wapeleke mpira mbele. Chico uongozi na ukamanda alianza toka utoto hakuanzia katika Jeshi la Polisi. Kwa kweli tulikuwa tukisikia sauti hii mori ulikuwa unapanda na hakika tukiongeza juhudi katika kushambulia au kulinda goli. Huyu Ahmada alikuwa umri wangu. Yeye ni mtoto wa Sheikh Digila wa Mtaa wa Nyamwezi nyumba yake ilikuwa karibu na msikiti wa Makonde. Ahmada alipata elimu kubwa sana ya dini. Ahmada alikuwa na kasi ya ajabu katika kusoma Qur’an. Kwenye khitma yeye anawea kukumalizia juzuu hata tatu wewe moja hujakamilisha. Alikuwa ''midfielder,'' hodari katika vijana wa Saigon pamoja na Hassan (Gilbert Mahinya). Hassan Gilbert baadae alikuwa kuwa mtaalamu wa, ''Systems,'' katika moja ya mashirika ya umma na siku tulipokutana Mlimani City akiwa na mabinti zake wakubwa waliojipamba kwa hijab alinifahamisha kuwa amestaafu kazi baada ya kufikisha miaka 60. Nilpomfahamisha kuwa nami nami pia nishapumzika akanambia taarifa zangu anazo kwani alikuwa akinifuatilia huko Tanga nilipokuwa nafanyakazi. Nilifarajika kusikia hayo kuwa hata baada ya miaka ya kutengana wana Saigon walikuwa wakitaka kujua nani yuko wapi na anafanya nini.

Hivi ninavyoandika ni kama vile najiona niko Mnazi Mmoja tunafanya mazoezi na wakati mwingine tukijifunza kuachiana pasi za haraka za kuwazuga maadui. Namuona Ghalib Hamza, maarufu kwa jina la Guy. Chico juu ya ushujaa wake wa kuwakumba washambuliaji hathubutu kumfata Guy akiwa na mpira. Guy alikuwa hana kimo, mfupi lakini ana maungo kiasi. Kilichokuwa kikitutisha kwa Guy ni ile, ‘’ball control,’’ yake na ‘’dribbling skills,’’ angeweza kumzunguka Chico na hata kumtia harusi, yaani kupitisha mpira katikati ya miguu yake. Kulikuwa na Mohamed Ramadhani Kondo (Garincha), Rashid Vava mchezaji rafu club nzima tukimuogopa. Wote wenzetu hawa wametangulia mbele ya haki. Naamini wasomaji vijana watapata tabu sana kuelewa haya majina niliyoyataja, hizi ''nicknames za akina Mazola, Di Stefano, Blanchflour. Hawa walikuwa katika wakati wetu wa miaka ya 1960 ndiyo wachezaji mpira maarufu wa vilabu tofauti vya Ulaya.

Chico alikuwa na baiskeli yake, ‘’sports’’ nyuma aliiandika, ‘’Thunderbird’’ na mwenyewe akiita baiskeli yake kwa jina hilo. Alikuwa anaipanda kwenda shule kavaa vizuri sana na kichwani kavaa, ‘’baseball cap.’’ Amechomekea shati lake jeupe alilolivalia T Shirt nyeupe ndani ndani na kiunoni amevaa, ‘’army belt.’’ Hii ilikuwa mikanda myeupe ya ‘’canvass,’’ yenye, ''buckle,'' ya fedha au ''gold,'' inayong’aa. Mmarekani amekwishakazi. Vijana wote tuliokuwa tukijiona, ‘’fashionable,’’ tukivaa hivyo lakini Chico mwenzetu alitushinda kwa kuwa ilikuwa kama vile mambo yale yako katika damu yake.

Nakikumbuka vyema chumba chake pale kwao. Kilikuwa nadhifu na alikuwa na ‘’record player,’’ yake na sahani za santuri nyingi za nyimbo mbalimbali za wanamuziki wa zama zile. Sasa hapo ndipo utakapotambua kuwa Chico alikuwa, ‘’special.’’ Mimi nilikuwa na ‘’record player,’’ yangu, ‘’Dansette,’’ imetengenezwa Uingereza, Sussex, nakumbuka ile label. Chico santuri zake zilikuwa ni Nat King Cole, Ray Charles, Dean Martin na wanamuziki mfano wa hao kama Sammy Davis na wengine. Muziki mgeni kwa wengi kwa wakati ule. Nyimbo alizokuwa akizipenda na akaniambukiza na mimi kuzipenda ni, ‘’Ramblin Rose,’’ na ‘’The Good Times,’’ zote za Nat King Cole. Hadi leo kila nikizisikia nyimbo hizi huwa nakumbuka utoto wetu katika mitaa ya Kariakoo.

sHTFOQNsLM1ftNy7aNpDDY6CfSN-YVm-7S_0d663cmLzyYRRfwHQJNbHx8Fl6FhNScbc_caBd9OBQH2hY9c56cwvQtr98JnH0TUV3wXiObetweotHpTUE3obU9Jpy2R5QR3ivzfc957Lnr56HmF7njG85Z_HAeARULLbUkWYabUS9lb1JzqEalMzpzPCWKnn70pShix4KosC6KOznIOPGMDTzzT7TkEAJZxqLrQO6QQIT1-SbqyJzqe1ofKqdYD7sUwC18-0QDOjmmTTKBov5ImT_Ivr5h7W4aoqruKRGTm4Yl_T1__PJQ854BwC3veLOrjMCgCd6Vsu-Mxym4lyoYx8R3V0AIR0lQJbr_Nwgrze6Tk9WIScs54zStx3oD3PSSvwHS7dWkHrHt9uOF3bqtSlEYIMSFd2ls0PggUR4jh95-5zLxQX7p0X92m6fZHaw1Z8NsWBHSUmyixdCbWTcPC8NAan6vTM0Dwye8dJsMLGbVj8pufVYseDmAvNdRFzDUupBJsMFPjWoC__r2BExB56f37y8dko1HqCfBiqFgeFPZLvEmWgbu__lP7gbym9W0L_oyApXpwXlQGASddeNDuLiQz2tTqDoCR9Bvg1oRSqmaKTJA=w480-h317-no


Kushoto mstari wa mbele Hussein Shebe, Henin Seif, kulia wa pili ni Raymond Chihota, Hussein,
(pass) Mbaraka ''Bata'' picha ilipigwa mapema 1960


Miaka ya 1960 ilikuwa miaka ya patashika si Dar es Salaam tu bali dunia nzima na ndiyo maana Waingereza wakaipa jina miaka hiyo kuwa ni, ‘’Roaring 60s.’’ Dar es Salaam ilikuwa na mastaa wake wakivuma kama Hussein Shebe, Raymond Chihota na Henin Seif kuwataja wachache katika Chipukizi Club, timu ya waimbaji vijana wakipigiwa muziki na The Blue Diamonds, ''band,'' ya vikana wa Kigoa. Kulikuwa na Sammy Davis Jr Salim Hirizi akiimba nyimbo maarufu, ''Summer Time,'' kwa umahiri mkubwa. Katika hawa waimbaji kubwa lao alikuwa Sal Davis. Siku Sal Davis alipokuja na Hussein Shebe Mtaa wa Tandamti kuwaamkia wazee wake Hussein nyumbani kwa kina Mohamed Jaggan ilikuwa gumzo la mtaa mzima na sisi ambao hatukuwapo kumuona Sal Davis tulisikitika sana. Uhuru wa Tanganyika uliingiza katika nchi mambo mengi kutoka Ulaya yaliyotuvutia sisi vijana. Huu ulikuwa wakati wa wazimu wa mambo mengi sana kutoka Marekani na Ulaya. Sote tukisukumwa na ujana tulikumbwa na wimbi hili. Haya ndiyo yalikuwa maisha ya sisi vijana katika Dar es Salaam ya miaka ile ya 1960 na Chico hakuweza kuliepuka wimbi hili kama vijana wengi walivyoshindwa.


5sZPOFll4GRIAJQlc13eyK4L3RzXOTxon-N42VImzBxus4z1BtUDthAzl_28uaWEKH-IgYe8k3F7ru4QddNyFQXEhtVWQ8f-lMJNAxFfbmzUPXW_3q3h-t7vmE2Z6B5G-bExO4PgXgtQhFoXhFGxZd5ExOgPt6frZbPnXG3Pypmk4mf7AQFDa6iiyga2tSbtT4_BMZT8c0GrwSx7GeuUDCf6NEK_zbyszX8Kq5Ebj4JMSJ4dHiVVUyHCzDNL8Dmb22GnkTiiXBPTD2KLGNj_Y2-NeIF6zlANJ8aW2QcwkQnbqc0ljwZb8C5j67MNqcYX8Rsk44yOJqxSVy6eEs8pR2VQML1PV_X_H1J_b0dhhpwzTDdClZLV1uwkciUlqCrsLHua26VXcX-mKe3aUY4Ujc6r9o2kpryTFXXczqaCK3P8I34-Xj7aoKyH1TudQyliHusZcElIW3_WjujZVNPLKqkVy3jjDYK0k_IQuL9ObRxXpiGAACefLuRvSw870p5oNRD1voq0rJwK-gUfk5trhp6OkkIy5G4XCH9Qp36o2utQdMQuB-t3XX2mRZOx005Z-WHEXGOJHieoHIbD3TuzTOiOq_LsVTUb5GsJ6F1Sj0Bgl558UMb5cw=w480-h360-no

Salum ''Sammy Davis Jr'' Hirizi kama alivyo hivi sasa

xQfAqWcEVCtCleTuI7SVqXH07ms6T7HCleDITMMrHvLZnq35gBYz2Sz-KoDn_GlyxQfn9KFkNZJlu_BpI8S5DQ5_yhdh4ksOX5oEIiHIPH_JwhoAHfoYhRzxfxSuLCVZ4z4EgPSVKP38_d8gemEP6ygJo5kPhXTturzHP8TLMjMGMIugjPd_39fN5yLSCZEeIXYHMVxdiioMpISkIx9Db9YQseuEoe-JoztznYTYQVncpuOy0zGat6Uf1NJY8gwdwb-6-l1ZishMyTXEoFAmG1OJvhQl4C0CCubzFWnNPkMLXpdor_SVQaZhLrWLevCvOxZms9IFV74LC-l4rl2C1cXDDPH95PhYkvNmEdjGnRjNr-LOPfr3Ub4ypkVhk8_h0ebW7gpTDXuWkpbXfRY9_x9aZfPR75qMzPBraTu6EFrNqeX3LLU5c7Xv-qSpeDuIS2GwxHa0pknDWLTW0genQsaSsqp3lKlrY2HWPHtkUBQ9SqyyiVhpkHVGh3ZmsPUrSyTmSVcZb5S5bHeESz0LrApryupHDJMuqbbGjeTSh5V46e-XFpXixEnVOOI4iKBGMRKSZLHtJVcqGYjv_t8vEpcl-Xiwrc_1O35317vD5YLBkS2a2Jyb=w392-h692-no

Sal Davis Katika Onyesho Ujerumani 1960s

Ilikuwa Chico ndiyo, ‘’alinijulisha,’’ mimi kwa Sidney Poitier na nikaanza kuingia kila senema yake ilipokuja mjini. Sidney Poitier katika miaka ile hakuwa maarufu kwa vijana wengi wa Dar es Salaam. Wengi wetu tulikuwa na John Wayne, Richard Widmark, Alan Ladd, Victor Mature, Marlon Brando na mfano wa hao na wala haikutupitikia kuwa tunaweza kwenda senema Empire, Avalon, Empress au Chox kuangalia senema, ‘’actor,’’ Mnegro kama Sidney Poitier au Jim Brown. Chico alikuwa, ‘’special,’’ yeye akimjua Sidney Poitier, Eartha Kitt na wengineo siku nyingi sana. Kuanzia hapo na mimi nikabadilika. Nakumbuka senema za Sidney Poitier alizokuwa akipenda kunihadithia kama ni kama ''Lilies of the Fied,’’ ‘’A Patch of Blue,’’ na nyingine nyingi.

p3173_p_v8_ac.jpg


Ujana haukawii kukimbia. Haukupita muda tukakua na ikawa lazima tukubali kuwa wakati wa mchezo umepita tunaingia ukubwani. Chico alitushangaza wengi alipojiunga na Jeshi la Polisi kwani si katika kazi ambazo, ‘’watoto wa mjini,’’ tulizipenda na kubwa ni kuwa kazi ya jeshi ilikuwa inahitaji kufanyakazi nje ya Dar es Salaam na wengi wakiona dhiki kuondoka mjini. Sasa hapa ndipo ninapotaka kuhitimisha kuwa Chico alikuwa, kwa kweli na kwa hakika kabisa alikuwa ‘’special.’’

Chico alijiunga na Jeshi la Polisi na aliitumikia nchi yake kwa uadilifu mkubwa. Alifanyakazi takriban kila mahali na kuacha jina lililotukuka. MIaka mingi baada ya sisi kutoweka hapa duniani, itakapokujaandikwa historia ya watoto wa Dar es Salaam na nini wamefanya katika taifa hili nina hakika Kamanda Chico jina lake litakuwa juu.

Allah amlaze pema ndugu yetu Mohamed Awadh Saiwaad maarufu kwa jina la Chico aliloishi nalo utotoni hadi ukubwani.

1SoH8DK4E3Rp_beqWUyYroAl-85hb9m-PN4bznGLJnUNTJ1wOrOPPizdFyw0WRQb4WwsF_y_c05aJ0Gpzw9FLkPTKYnmFxuDV2FCPT-IzVcux6cmW_FAK61H5TaBLc8UHpyhvAnAaMWONyVsBqcl9M8LNNUbsW6pb7ccfcpLpXJ49Yeuxmh7qHWC0JVJGuvvoJYOgaBPKQwvb_1HTQsz_1OAC6iNohPCGbWvUVMaKGhPe8J0r46TP6PUU9jxtRbYCwHZg2KAP9b2JTvqT2vygbWBBV1JylEp0X2kOLdhMP7kYM0CWmhiOgNg4-9vbhkWy7VloajuTqcvVPZ7KL5Rh7A5IETn6OXibuj86BEKZD6qct17MCwkzStB4eGGvtpKTiy80E0cH4ScWnCBwds6C05ft0A32XnFBhC-P2AqWaB6JbetvAN5WUc65LvAoY341l8tGAolg5XO70LVK2q221VfYr7WZ6C6VGKgLJOrYHp4SXP549dmX9dIYZw-lZ9JM_tCGziJx2au8B56vfz5RQRe38MNG3l9dkoXsxpftcUQc1RvAeMOs1qVeDM2Ul2ycDCsJwRY9s98Wz5XdSYTUElvdTvfWYjdq8WkmNZfSosaSte2AtCb_Q=w670-h526-no

Mwandishi akiwa Viwanja Vya Mnazi Mmoja ambako Everton na kisha Saigon
walikokuwa wakicheza mpira. Nyuma ni barabara iliykuja kupewa jina la Bi. Titi
Mohamed na ukivuka barabara hiyo ni Soko la Kisutu maarufu kwa jina la Soko
Mjinga. Picha ilipigwa 1966
 
Shukurani sana mzee wetu kwa historia nzuri ya maisha yenu ambayo ni funzo kwetu ss vijana wadogo. Kweli mliutumia ujana wenu na uzee wenu vzr na kuishi katika maelewano na ushirika mzuri na ni furaha pia kuishi na kuona uzee wenu baadhi yenu na inakuwa inawakumbusha mbali kila mkifikiria mambo makubwa mliyo wahi kuyafanya, Mara nyingine nikisoma historia kama hizi inanikumbusha jinsi muhhamed Ali alivyo enda hospital kumuona the smoking Joe baada ya maongezi ya hapa na pale Ali alimuaga Joe wakati anaondoka Joe akamuita , hey champ Ali akamjibu yes Joe , Joe akarusha ngumi hewani akisema this one for you champ, Ali akatabasamu na kusema bye Joe . nikisoma stori kama hizi nami nawaza kama ss nasi tutafika uzeeni kama hivi na kuyakumbuka mengi tuliyoyafanya ujanani na marafiki zetu wa ujana wetu, be blessed mzee.
 
Nikisoma hii historia ilotukuka ya watu waliofanya maisha yako yawe ni ya furaha sio tu kipindi hicho hata sasa unapokumbuka unajiona haujawah na hautaweza kuwa peke yako
Nimependa aina yako ya uandishi inayohamasisha kusoma yaliyomo nna hakika kupitia hii stori ndefu uliyoiandika kiufupi ungeweza hats kutunga kitabu have a nice time
 
Wapi chet baker miles Davis John Coltrane Sydney bichet sonny rollings max roach Charlie Parker na wengine?
 
Shukurani sana mzee wetu kwa historia nzuri ya maisha yenu ambayo ni funzo kwetu ss vijana wadogo. Kweli mliutumia ujana wenu na uzee wenu vzr na kuishi katika maelewano na ushirika mzuri na ni furaha pia kuishi na kuona uzee wenu baadhi yenu na inakuwa inawakumbusha mbali kila mkifikiria mambo makubwa mliyo wahi kuyafanya, Mara nyingine nikisoma historia kama hizi inanikumbusha jinsi muhhamed Ali alivyo enda hospital kumuona the smoking Joe baada ya maongezi ya hapa na pale Ali alimuaga Joe wakati anaondoka Joe akamuita , hey champ Ali akamjibu yes Joe , Joe akarusha ngumi hewani akisema this one for you champ, Ali akatabasamu na kusema bye Joe . nikisoma stori kama hizi nami nawaza kama ss nasi tutafika uzeeni kama hivi na kuyakumbuka mengi tuliyoyafanya ujanani na marafiki zetu wa ujana wetu, be blessed mzee.

Putinelimusu,
Muhimu ni kuishi kwa wema na mapenzi na wenzako na kuheshimiana.
Ntakupa kisa.

Katika club yetu kulikuwa na kijana mmoja katoka Usambaa kaja Dar
kwakazi za ndani lakini alikuwa umri sawa na mimi kiasi miaka 15 hivi.

Tajiri yake labda kwa kuona ule umri mdogo ilikuwa ikifika saa kumi jioni
anamruhusu anakuja pale Mnazi Mmoja kujumika na sisi kucheza mpira na
sisi watoto wenzake.

Huyu kijana tukaingiliananae kwa mapenzi makubwa na akawa mwenzetu
Nyumba aliyokuwa akifanyakazi ilikuwa mitaa ile ya Lumumba.

Huyu kijana akipenda mpira na akiumudu kwa kiasi chake.
Miaka mingi sana ikapita mimi sasa mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Nakaa Masaki na ili nifike chuoni inabidi nitembee kwa miguu kupitia Mikoroshoni
hadi Ali Hassan Mwinyi na Kawawa kuwahi basi la chuo.

Ilikuwa nikishaswali tu alfajiri natoka kuwahi basi.

Njiani sehemu za hapo Mikoroshini kulikuwa na hoteli maarufu jamaa wengi
wanakunywa chai hapo au kununua vitafunio kabla hawajakwenda makazini kwao.

Siku moja nakunywa chai naona mtu kanisamamia mezani kwangu.
Nanyanyua kichwa namuona yule kijana lakini sasa sote si watoto tena.

Tukasalimiana kwa bashasha na nikamuuliza yuko wapi siku zote hizo.
Akanambia yuko Dar es Salaam na hiyo ni hoteli yake.

Nilimshukuru Allah.
Rafiki yangu katoka kuosha sufuria na leo ana hoteli yake anaendesha.

Leo tunatazamana ''as equals,'' si tena Mohamed Said mtoto wa afisa na yeye
mfanyakazi wa ndani.

''Eusobio hii hoteli yako siku yoyote kuna tatizo niulize kwa vijana hapa.''
Eusobio ndilo lilikuwa jina langu la mpira.

Nikajua nishapata mahali pa kukopa chai siku hali ikiwa tete.

Nimekileta kisa hiki ili kikufikirisheni vijana mtafakari kuwa kuna kesho ambayo
hatuijui.
 
Nikisoma hii historia ilotukuka ya watu waliofanya maisha yako yawe ni ya furaha sio tu kipindi hicho hata sasa unapokumbuka unajiona haujawah na hautaweza kuwa peke yako
Nimependa aina yako ya uandishi inayohamasisha kusoma yaliyomo nna hakika kupitia hii stori ndefu uliyoiandika kiufupi ungeweza hats kutunga kitabu have a nice time
Sajumo,
Ule ulikuwa wakati mwingine kabisa.

Miezi miwili hii nimeondokewa na marafiki zangu vipenzi huyu Chico
na mwingine binti kafariki Ulaya.

Angelikuwa mwanamme ningaliandika taazia yake.

Niliandika maneno haya kwa baadhi ya marafiki zetu ambao mie na
yeye wakituhusu:

''Siku moja tuko Ulaya alinichukua retaurant moja akiwa na binti yake.

Akanambia angependa mimi nimueleza mwanae yeye alikuwaje wakati
tuko shule na tulipokuwa tunakua Dar es Salaam ya 1960.

Nilijua kuna kitu anataka mwanae ajifunze kutoka kwake.

Basi mimi nilimweleza jinsi nilivyomjua mama yake na vipi tulivyokuwa
shule.

Nilimwambia kuwa katika wasichana wazuri pale shule mama yake
alikuwa mmojawao.

Nikamwambia pia alikuwa na kipaji kikubwa cha kucheza dansi vizuri
sana na cha michezo na timu yao ya Mkoa wa Dar es Salaam Basket Ball
ilichukua kikombe 1968 (picha ya timu hii ninayo yuko na wasichana watatu
katika timu ile waliondoka Tanzania kwenda kutafuta maisha Ulaya).

Nilimweleza mengi na nikamwambia kuwa mama yake ndiye aliyenifanya mimi
niache mpira nimfuate yeye nende kucheza Basket Ball...''

Those where the days which we thought would never end.
Sasa tumekuwa watu wazima na uzee umeingia tunasubiri...
 
Kuna zile habari za Chiko za upande wa pili mbona hazipo kwenye huu wasifu wake
 
Zote nishaziona ya Miles ahead ilitoka mwaka jana

Katafute documentary ya jazz iliyotengenezwa na Ken Burns utanjoy

Too bad hapa Dar hakuna Jazz clubs
Saul...
Ahsante sana.

Nilikuwa Paris miaka michache iliyopita na karibu na hoteli yangu
palikuwa na jazz club.

Sikuweza kwenda.
Nyakati zimepita na kila mwenyeji wangu akinishawishi nimemkatalia.
 
Yamagashi,
Imekuwaje ndugu yangu mbona unakuja na maneno yasiyopendeza?
Huwezi hata kuweka heshima kuwa sisi tumefiliwa na mpendwa wetu?
Heee aisee mzee wangu sijui huwa unaishi vipi ni wapi mimi nilipokukosea heshima ? Yaani kukuambia uende pale Moshi utapata taarifa zake za upande wa pili ili ujazie wasifu wako imekuwa nongwa ?
 
Heee aisee mzee wangu sijui huwa unaishi vipi ni wapi mimi nilipokukosea heshima ? Yaani kukuambia uende pale Moshi utapata taarifa zake za upande wa pili ili ujazie wasifu wako imekuwa nongwa ?
Yamagashi,
Basi kaka niwie radhi.

Ila mimi najua mtu akishaandika taazia ndiyo inakuwa hivyo ilivyoandikwa.
Inakuwa hivyo kwa kuwa kwa kawaida khasa taazia ina akisi mtu alivyomjua
marehemu.

Haambiwi arejee kuandika habari ambazo yeye hazijui.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom