Zijue dawa 10 za asili zinazotibu kikohozi

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,495
9,275
Kikohozi ni moja ya ugonjwa ambao huwapata watu karibu wote. Kunapotokea kuzibika au muwasho kwenye koo lako ubongo hutambua kuwa kuna wavamizi kutoka nje na hivyo huuamrisha mwili wako kukohoa ili kuondoa hao wavamizi.

Kukohoa pia kunaweza kuwa ni matokeo ya maambukizi ya virusi, homa, kuvuta sigara au matatizo ya kiafya kama pumu, kifua kikuu na kansa ya mapafu. Baadhi ya dalili za kikohozi ni muwasho kooni, maumivu ya kifua na msongamano mapafuni. Badala ya kutumia dawa za viwandani kutibu kikohozi unaweza kujaribu mojawapo ya hizi dawa za asili za kikohozi ambazo zinapatikana kirahisi jikoni kwako.

Dawa asili 10 zinazotibu kikohozi:

1. BINZARI (Turmeric) Dawa hii ya asili inao uwezo wa kutibu kikohozi hasa kikohozi kikavu. Ongeza kijiko kidogo kimoja cha unga wa binzari ndani ya kikombe kimoja (robo lita) cha maji ya moto, ongeza ndani yake tena kijiko kidogo cha pilipili manga ya unga, nusu kijiko cha chai cha unga wa mdalasini na kijiko kidogo kimoja cha asali mbichi, koroga vizuri na unywe mchanganyiko huu wote kutwa mara moja kila siku mpaka umepona.

2. TANGAWIZI
Tangawizi ni moja ya dawa maarufu kwa kutibu kikohozi. Tengeneza chai ukitumia tangawizi mbichi na ndani yake utumie asali na siyo sukari kwenye hii chai yako. Kunywa kikombe kimoja kutwa mara 3 kila siku mpaka umepona. Angalizo usitumie dawa hii kama una ujauzito mchanga chini ya miezi minne na hata ukiwa na ujauzito zaidi ya miezi minne basi tumia kikombe kimoja tu kwa siku. Unaweza pia kutengeneza juisi ya tangawizi freshi ukiongeza parachichi ndani yake na unywe kwa mtindo huo huo wa chai hapo juu.

3. LIMAU
Limau inaweza kutumika kwa namna nyingi katika kutibu kikohozi. Limau zina sifa za kuondoa maambukizi na pia limau lina vitamini mhimu ambayo hupigana na maambukizi na kukuongezea kinga ya mwili vitamini mhimu sana vitamini C. Changanya vijiko vikubwa viwili vya maji maji ya limau na kijiko kikubwa kimoja cha asali mbichi na unywe mchanganyiko huu mara 2 kwa siku kwa siku kadhaa.

4. KITUNGUU SWAUMU
Kitunguu swaumu kina sifa ya kuua bakteria na virusi mwilini sifa ambayo inakifanya kuwa dawa bora ya kutibu kikohozi. Menya punje 6 za kitunguu swaumu, kata vipande vidogo vidogo (chop) na uchanganye kwenye kikombe kimoja (robo lita) cha asali na uuache mchanganyiko huu kwa usiku mzima. Kuanzia kesho yake asubuhi chukua kijiko kidogo kimoja cha mchanganyiko huu na ulambe mara 2 kwa siku mpaka upone.

5. KITUNGUU MAJI
Moja ya dawa nyingine rahisi ya kutibu kikohozi ni kitunguu maji. Unaweza kunusa tu mara kadhaa harufu ya kitunguu na ukaona mabadiliko. Changanya kijiko kidogo kimoja cha juisi ya kitunguu maji na kijiko kidogo kimoja cha asali mbichi na unywe mara 2 kwa siku mchanganyiko huu kwa siku kadhaa.

6. MAZIWA YA MOTO NA ASALI
Maziwa ya moto na asali vinaweza kusaidia kutibu kikohozi kikavu na kupunguza maumivu ya kifua ambayo hutokeo kama matokeo ya kukohoa mfululizo kwa kipindi kirefu. Kwa matokeo mazuri kunywa dawa hii kabla ya kwenda kulala. Changanya kijiko kikubwa kimoja cha asali mbichi ndani ya nusu kikombe (ml 125) cha maziwa ya moto na unywe kabla ya kwenda kulala kila siku. Hii itasaidia kusafisha na kulainisha koo lako haraka.

7. PILIPILI KICHAA
(Cayenne) Pilipili kichaa (zile ndogo ndogo sana huwa kali kweli kweli) zinasaidia kupunguza maumivu ya kifua yatokanayo na kikohozi cha mfululizo kwa muda mrefu. Pia huuamsha na kuuchangamsha mwili. Changanya robo ya kijiko cha chai cha unga wa pilipili kichaa, robo kijiko kidogo nyingine ya tangawizi ya unga, kijiko kidogo kimoja cha siki ya tufaa, kijiko kikubwa kimoja cha asali na vijiko vikubwa viwili vya maji. Kunywa mchanganyiko huu mara 2 kwa siku kila siku mpaka umepona.

8. JUISI YA KAROTI
Karoti zina vitamini na viinilishe vingi mhimu ambavyo vinaweza kusaidia kutibu kikohozi. Tengeneza jusi freshi ya karoti, isiwe nzito sana wala nyepesi sana, tumia asali katika juisi hii na unywe kikombe kimoja kutwa mara 2 kila siku kwa siku kadhaa mpaka umepona.

9. ZABIBU
Zabibu zinazo kazi na sifa kuu ya kuondoa makohozi na uchafu mwingine kwenye mfumo wako wa upumuwaji wa mwili. Kadri unavyoondoa haya makohozi kwenye mfumo wako ndivyo unavyopona kwa haraka kikohozi. Unaweza kula tu zabibu kadhaa kila siku au tengeneza juisi freshi ya zabibu na unywe kikombe kimoja kutwa mara 2 kwa siku kadhaa mpaka umepona.

10. LOZI (Almonds)
Lozi zina viinilishe mhimu ambavyo husaidia kutuliza dalili za kikohozi. Loweka lozi 6 ndani ya maji kikombe kimoja (ml 250) kwa masaa 8 mpaka 10. Kisha zichuje na uzisage na urudishie ndani ya maji yake na uongeze kijiko kidogo kimoja cha siagi na ule mchanganyiko huu kijiko kidogo kimoja kutwa mara 3 kila siku mpaka dalili za kikohozi zimepotea.

Dawa asili hizi zinaweza kukutibu na kuondoa dalili za kikohozi bila kukuachia madhara kama ambavyo ungetumia vidonge au dawa za kizungu. Kama dalili na ugonjwa utaendelea zaidi ya wiki 2 hata baada ya kutumia dawa hizi tafadhari muone daktari kwa uchunguzi na msaada zaidi.
 
Asante sana mkuu miss zomboko ; ngoja nijaribu asali na limao huenda litanisaidia kutatua kikohozi cha mwanangu maana amemaliza dawa zote na bado anaendelea kukohoa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom