Ziara za wanasiasa majimboni kujisafisha zinatia shaka

Fidel80

JF-Expert Member
May 3, 2008
21,947
4,452
Mwananchi-leo
WANASIASA wa Tanzania siku hizi, wanashangaza kutokana na tabia yao ya kutaka kuonekana safi, hata wanapotuhumiwa na mambo mazito yanayohusiana na matumizi mabaya ya nafasi na madaraka waliyokabidhiwa na wananchi kusimamia rasilimali za taifa.


Tangu tupate uhuru na hasa baada ya kutangazwa Azimio la Arusha, kumekuwa na utamaduni wa wananchi kupanga au kupangiwa kufanya maandamano ya kuunga mkono mambo muhimu yanayofanywa na viongozi wao wa kitaifa, kama njia mojawapo ya kuhamasisha utekelezaji wake.


Kwa mfano baada ya Azimio la Arusha kutangazwa, nchi nzima kulikuwa na maandamano ya kuunga mkono juhudi za Baba wa Taifa kuifanya nchi hii kuwa ya Ujamaa na Kujitegemea. Si hilo tu, hata yalipotolewa maazimio mengine kama ya Siasa ni Kilimo, Elimu ya Upe na mengineyo, Idara ya Propaganda ya chama tawala (TANU na CCM) iliandaa maandamano yaliyoambatana na matembezi ya mshikamano nchi nzima kuunga mkono maazimio hayo.


Hata Rais Jakaya Kikwete alipolivalia njuga suala la filamu ya mapanki (Dar Nightmare), wananchi wa Mwanza na hasa wanachama wa CCM waliandaa maandamano makubwa ya kuunga mkono hatua hiyo ya rais kwa sababu, kwa asilimia kubwa ililihusisha jiji hilo katika mambo yaliyohadithiwa kwenye filamu.


Hata hivyo, kadiri siku zinavyozidi kwenda maandamano ya mshikamano yamekuwa yakibadilisha maana, kwani sasa baadhi ya wanasiasa wameanza kuyateka nyara, kwa ajili ya kutetea maslahi yao binafsi badala ya kuinufaisha jamii.


Baada ya kashfa za ufisadi kuibuka nchini, baadhi ya wanasiasa wanaotuhumiwa kuhusika kwenye majanga hayo, wamekuwa wakitumia fedha zao kuwakusanya watu ambao huandamana na wao kupata jukwaa la kujitetea kuhusiana na mambo yaliyowakuta.


Kwa mfano, baada ya kashfa ya Richmond kuibuka hadharani kupitia bungeni, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu wadhifa wake. Lakini muda mfupi yaliandaliwa maandamano makubwa ya jimboni kwake, ambako alipata mapokezi makubwa na yeye (Lowassa) kupewa jukwaa la kuwaeleza sababu za kujiuzulu kwake.


Na sasa, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge aliyejiuzulu mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya kubainika kuwa ameficha Sh1.2 bilioni katika Kisiwa cha Jersey, ambazo zinachunguzwa kama zilipatikana kwa njia ya rushwa kupitia mkataba wa ununuzi wa rada, amesafiri kwenda jimboni kwake ambapo amepata mapokezi makubwa na yeye kupata nafasi ya kueleza sababu za kujiuzulu uwaziri.


Kinachotushangaza ni hatua ya wanasiasa ambao wanatuhumiwa kushiriki kwenye kashfa mbalimbali wanavyojihusisha kuandaa maandamano ya kuwapokea, kana kwamba wamefanya jambo kubwa na la maana kwa jamii ya watanzania.


Kitendo cha wao kwenda majimboni kwao na kupokelewa kwa mbwembwe, kisha kuwaeleza wananchi sababu za kujiuzulu kwao, kinatafsiriwa kuwa wanajisafisha kutokana na kashfa wanazotuhumiwa, jambo ambalo si sahihi kufanyika wakati madai hayo yako kwenye hatua ya uchunguzi. Labda wangefanya hivyo baada ya kusafishwa na mamlaka husika kuwa hawahusiki, hapo ingekuwa bora zaidi.


Inashangaza kuona ndugu zetu hao, wanatumia fedha nyingi kwenye mambo hayo, ambazo kama wangezitoa kwa maendeleo ya majimbo yao, zingesaidia kuwapunguzia wananchi kero za kijamii zinazowakabili, kama vile ukosefu wa dawa hospitalini, vifaa vya kujifunzia shuleni na mengineyo.


Tunawaomba wanasiasa kutotumia njia hiyo kuwapumbaza na kuwahamasisha wananchi kuandamana ili kuwaunga mkono katika mambo ambayo dhamira yao haiwatumi na wala haikubaliani nayo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom