Ze-comedy Tz Wavunja Mkataba

Mkombozi

JF-Expert Member
Feb 19, 2008
794
402
SOURCE GLOBAL PUBLISHER

Uchunguzi wa Ijumaa Wikienda, wikiendi iliyopita kwa kuhusisha vyanzo mbalimbali, wakiwemo wasanii wa Ze Comedy, umebaini vipengele kadhaa ambavyo kiuhalisia na kimazingira ndivyo vimesababisha mtafaruku huo.

Ripoti ya uchunguzi huo, inapingana na tamko la Kiongozi wa kikundi hicho, Isaya Mwakilasa ‘Wakuvwanga’ alilolitoa kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Ijumaa iliyopita kwamba wanaacha Channel 5 ili kupumzika.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, ‘hali ya hewa’ ya Ze Comedy ndani ya luninga hiyo, ilichafuliwa kwa kiasi kikubwa na mtangazaji mmoja wa kike wa televisheni hiyo.

Ilielezwa kwamba ‘bifu’ la wazi kati ya mtangazaji huyo (jina tunalihifadhi) na Ze Comedy, lililokua na kufikia kiwango cha kuichanganya menejimenti ya Channel 5, liliibua manung’uniko kwa wachekeshaji hao wakidai kuwa hasimu wao anapendelewa.

“Akina Masanja (Ze Comedy) waliwalaumu viongozi kwamba wanampendelea ... (linatajwa jina la mtangazaji) na kushindwa kumchukulia hatua kwasababu aliwaponda hadharani tena kwenye kipindi chake,” kilisema chanzo chetu.

Bifu hilo, lilidhihirika miezi michache iliyopita pale mtangazaji huyo alipowaponda hewani Ze Comedy kwa kukiita kipindi chao ni upuuzi. (Habari ya bifu hilo, iliandikwa na gazeti hili kwa mara ya kwanza).

Akiliuma sikio gazeti hili wikiendi iliyopita, mmoja kati ya wasanii wa Ze Comedy alikiri kuwa mtangazaji huyo ni sehemu ya mambo yaliyochangia wao kusaini ‘out’. Alisema: “Ni vitu vingi vimesababisha tuondoke, lakini naye ni mmojawapo.”

Akiendelea, Msanii huyo alisema, sababu nyingine ya wao kupeana ‘talaka’ na Channel 5 ni mkataba ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa unawalalia wao, huku ukiinufaisha zaidi televisheni hiyo.

“Mkataba ulikuwa unatubana sana, tukitaka kufanya ‘shoo’ inakuwa ngumu, tukikipata ‘tenda’ za u-MC tunakatazwa, lakini sasa hivi tupo huru, mwenye shida na sisi aje,” alisema.

Habari zaidi zinasema kuwa kabla ya Ze Comedy kuvunja ‘ndoa’ na Chanel 5 wiki iliyopita, wasanii hao waliugomea uongozi wa kituo hicho, wakidai hawatarekodi igizo jipya mpaka walipwe ‘vijisenti’ vyao walivyofanyia shoo mbalimbali za jukwaani ambavyo Wikienda haikupata idadi yake.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu ndani ya televisheni hiyo, mgomo huo ndiyo uliosababisha kikundi hicho kushindwa kurusha mchezo mpya Alhamisi iliyopita, badala yake vikaoneshwa vipande vya zamani.

Alipotupiwa swali hilo na mwandishi wetu, Wakuvwanga alijibu: “Nimesema ni sababu nyingi zimesababisha tuondoke, lakini sidhani kama ni busara tuweke kila kitu hadharani ndani ya muda mfupi.”

Mmoja wa wasanii wa Ze Comedy (jina tunalo), alisema kuwa baada ya kupeana ‘talaka’ na Channel 5, uongozi wa televisheni hiyo uliwapa notisi ya kuhama kwenye nyumba ambayo uliwanunulia, iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Alisema: “Hatujahama, tulionesha nyaraka zinazoonesha kuwa ile nyumba ni yetu, uongozi ulitununulia kama sehemu ya mkataba wetu wa kazi.”

Aidha, siku moja tu baada ya kuwepo taarifa kuwa Ze Comedy wameng’atuka Channel 5, zilizuka habari kuwa kikundi hicho cha vichekesho tayari kimeshaingia makubaliano na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), kitengo cha televisheni kwa ajili ya kurusha hewani vipindi vyao.

Mbele ya taarifa hiyo, ilidaiwa kwamba tayari kikundi hicho kimeshaanza kurekodi michezo ambayo itaanza kurushwa hivi karibuni na luninga hiyo, baada ya makubaliano ya mwisho kuafikiwa na kila upande.

Akilijibu hilo, Wakuvwanga hakukanusha, isipokuwa alisema: “Ni mapema mno kuliongelea hilo, halafu hatuwezi kusema tupo kwenye mazungumzo na nani au makubaliano yapi mpaka tutakaposaini mkataba.”

Naye Mtangazaji wa Channel 5, Sekioni David ‘Seki’ ambaye pia ni Meneja wa Ze Comedy, amekumbwa na dhoruba zito baada ya kupigwa chini kazini kutokana na kile kinachosemwa kuwa yeye ndiye anayewavimbisha kichwa wasanii hao.

Hata hivyo, Seki alisema kuwa aliulizwa na uongozi wa televisheni hiyo achague kazi ama Ze Comedy, hivyo akaamua kuambatana na wasanii hao.

Gazeti hili lilimtafuta Meneja wa Channel 5, Denis Busulwa ‘Sebo’ ambaye alisema hana ubavu wa kulizungumzia hilo na akaomba atafutwe mwenyekiti wa kituo hicho, Regina Mengi.
Mwenyekiti huyo alipotafutwa kwa simu, msaidizi wake alisema kuwa hawezi kupatikana kwasababu yupo mkutanoni.

Aidha, uongozi wa TBC haukuweza kupatikana ili uthibitishe uvumi huo wa kuwanyakua Ze Comedy, ingawa vyanzo vyetu kituoni hapo vilisema kuwa wasanii wa kikundi hicho wamekuwa wakienda mara kwa mara na kuzungumza na mkurugenzi tu.
 
Upepooo Niouonaoo....madam Ritha Ana Hali Mbaya Sana Maana Amekosa Deal Hilo Ze Comedy...na Atakosa Tena Mwakani...bbs..sababu..hatapewa Favor Tena Kama Alivyoozeaa..na Airtime Za Bure Au Za Kukopaa..kwa Eatv,itv..sababu Kila Mtu Anajua...tuone Na Tusubiri Ni Muda Tuu
 
tatizo letu wabongo ndio hilo kupenda kunenepea kwenye migongo ya watu wengine?? Hivi kazi wanayoifanya hao akina Mpoki, Joti na wenzake bado mtu mzima anataka kuwalalia?? Bora wameachana nao...Mbegu za kuwanyonya watu bado ipo tu Tz.. Na huyo mtangazaji lazima atakuwa Salama tu maana ndio mwenye kiherehere..Poleni vijana ndio maisha kazeni buti..
 
tatizo letu wabongo ndio hilo kupenda kunenepea kwenye migongo ya watu wengine?? Hivi kazi wanayoifanya hao akina Mpoki, Joti na wenzake bado mtu mzima anataka kuwalalia?? Bora wameachana nao...Mbegu za kuwanyonya watu bado ipo tu Tz.. Na huyo mtangazaji lazima atakuwa Salama tu maana ndio mwenye kiherehere..Poleni vijana ndio maisha kazeni buti..
Hivi sekioni david 'seki' yuko wap?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom