Zbar Kwa Tanzania ni kama Eritrea kwa Ethiopia? Je Zanzibar watajitenga?

Mdondoaji

JF-Expert Member
Mar 17, 2009
5,108
1,136
Serikali ya umoja wa kitaifa itaumbua wengi

Wahafidhina wa siasa za chuki waanza kuhaha

HATIMAYE kaburi la historia ya siasa za chuki na uhasama wa kulipiza kisasi Zanzibar, limeanza kuchimbwa.

Ni Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad, walioandaa silaha za mapambano kuiangamiza historia hiyo na kufanya mambo kuwa mapya; licha ya upinzani wa hapa na pale.

Akiwahutubia wanachama wa CCM Zanzibar, Novemba 6, mwaka jana, Rais Karume aliweka wazi nia hiyo aliposema: “Ndugu zangu, mimi na Maalim Seif tuliulizana; hivi mpaka lini tutaendelea na siasa hizi za chuki, uhasama na ugomvi? Hivi tunataka turithishe watoto wetu haya tuliyorithi sisi?”

Kisha akabainisha kwa kusema: “Mimi naamini hakuna anayependa hali hii, sote tunapenda tuishi katika hali ya amani, utulivu umoja na mshikamano”.

Ni kipi hicho mabwana hawa wawili wa vita walichokubaliana? Taarifa za ndani zinasema kwamba, walipokutana Ikulu ya Zanzibar, Novemba 5, 2009, viongozi hao walithubutu kukanyaga salama na kishujaa mahali ambapo tume lelemama za CCM za kutafuta “mwafaka” kwa mpasuko wa kisiasa Visiwani ziliposhindwa, kwa kukubaliana mambo makuu mawili:

Kwanza, ni kutambua kusahau na kusameheana yote yaliyopita na kufanyakazi kwa pamoja kwa lengo la kuleta mabadiliko makubwa kwa maisha ya wananchi wa Zanzibar”.

Swali ambalo wengi tunajiuliza ni je; Karume atathubutu kwa moyo mmoja kulitupilia mbali tambiko la chuki, uhasama na kulipiza kisasi lililoasisiwa na baba yake, Abeid Amani Karume tangu mwaka 1957, na ambalo ndilo lililosababisha kifo chake Aprili 7, 1972?

Je, ana ubavu wa kulidhibiti kundi la wahafidhina wa chuki, uhasama na ulipizaji kisasi linalojiita “Wakombozi” na “Warithi” halali wa sera za hayati Abeid Amani Karume? Na hao “Wakombozi” ndio kina nani?

Je, ni yapi hayo yaliyopita aliyoyazungumzia Rais Karume? Na kwa nini yameachwa kuendelea kuathiri mustakabali wa siasa za Zanzibar hadi leo?

Hapana ubishi kwamba hatua inayochukuliwa na Karume na Sharrif ni ya kishujaa na yenye mwelekeo sahihi; na tayari imepongezwa na mataifa makubwa ya Marekani, Norway, Umoja wa nchi za Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa (UN) na wote wanayoitakia mema Zanzibar.

Ni hatua sahihi pia kwa manufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu mpasuko wa kisiasa Visiwani una athari mbaya kwa Muungano; kwa maana “kidole kinapoumia mwili mzima husisimka kwa maumivu”.

Lakini pamoja na hayo, tayari maridhiano haya ya kuunda “Serikali ya Umoja wa Kitaifa” (SUK) Visiwani, yameanza kutia hofu, mfadhaiko na kuzua upinzani kutoka kambi za kihafidhina Visiwani na Bara.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Kongamano la Vijana wa CCM wa Vyuo Vikuu nchini, Mei 2, 2010, Rais Karume alionyesha kukerwa na pia kukasirishwa na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wanaopitapita kushawishi wananchi kupinga SUK, na kuwaona watu hao kuwa wamepitwa na wakati, na kwamba hawajui kusoma alama za nyakati.

Aliwataja wengine kuwa ni viongozi wa ngazi za juu wa Chama na Serikali, na kuwaelezea kama watu hatari wanaotakiwa kuogopwa; na pia kwamba hawawatakii mema wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

“Nawaomba waache; sitaki kuendelea zaidi katika suala hili kwa sababu naweza kuwaumbua viongozi wote wanaopinga suala hili”, alionya.

Hofu juu ya kuundwa kwa SUK imejikita katika makundi na sura mbili. Sura ya kwanza ni ya kundi miongoni mwa Wazanzibari wenye msimamo mkali waliojipa ukuu na haki ya kumiliki siasa za Zanzibar kama warithi halali wa Mapinduzi ya 1964 na sera zake.

Hawa na nasaba zao, wanajiona kama ndio pekee wenye haki ya kutawala, na wengine wote wasio na historia ya Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), ni watu wa kutawaliwa milele. Tutaona baadaye chimbuko la dhana hii ya kibaguzi na kidikteta.

Wanaona kuwa, kama uhasama wa sasa wa kisiasa na wa vyama utamalizika, na uongozi wa nchi kuwa wazi kwa Wazanzibari wote, “ufalme/usultani” wao na koo zao utafikia kikomo pale Zanzibar itakapoanza kuzingatia utawala bora.

Kundi hili linalojiita “Wakombozi” (Liberators), na linalodai kuwa lina makubaliano ya siri tangu enzi za Rais Amani Abeid Karume, kwamba Wazanzibari waliokuwa wanachama wa vyama vya zamani vya siasa mbali na ASP, wasipewe nafasi za uongozi katika Chama, Serikali ya Zanzibar wala Serikali ya Muungano.

Katika miaka ya karibuni kambi hii ilikuwa na Wazanzibari wakongwe wafuatao: Brigedia Abdullah Said Natepe (kinara), Ali Mzee, Hassan Nasoro Moyo, Muhamed Seif Khatibu, Dakta Salmin Amour.

Wengine ni Seif Bakari, Hafidh Suleiman, Brigedia Ramadhan Haji, Brigedia Khamis Hemed, Aboud Twalib na wafuasi wao.

Kundi hili lisilotaka mabadiliko ya sera za zamani za Baraza la Mapinduzi na madhumuni ya Chama cha ASP (kilichofutwa), ni kinzani kwa kundi lingine linalojiita la “Wanamstari wa mbele” (Frontliners) lenye kutaka mabadiliko likiwa na watu kama Salim Ahmed Salim, Seif Sharrif Hamad, Hamad Rashid, Khatib Hassan na Adam Mwakanjuki, Isaac Sepetu, Shaaban Mloo, Ali Salim Ali, Haji Pandu na wanaharakati wengine.

Kuanzishwa kwa SUK ni ushindi hatua ya kwanza kwa kundi la Frontliners ambao hauwezi kupokelewa vizuri na kundi la Liberators ambalo baadhi yao au wafuasi wao ndio hao Rais Karume amewaonya waache kupinga maridhiano, vinginevyo atawaumbua.

Mapatano ya Karume na Seif Sharrif Hamad wa kundi la Frontliners, kwa vyovyote vile, yatakuwa yamewaduwaza Liberators wasiweze kuamini kinachotokea, kwani siku zote waliamini kwamba Rais Amani Karume asingeweza kuziasi sera na programu za uhasama za toka enzi za marehemu baba yake zinazoendelezwa na kundi hili ambalo linajiita pia kuwa ni “Walinzi Watetezi na Wafia Mapinduzi”.

Kwa sababu hii, hatua ya Rais Amani Karume ni ya kijasiri na kishujaa; yenye kuonyesha ukomavu wa kisiasa na uzalendo wa hali ya juu. Hekima na busara aliyoionyesha kiongozi huyu ni ya kihistoria katika uongozi Visiwani.

Sura ya pili ya hofu juu ya SUK inatoka Tanzania Bara; hususan hofu kuhusu hatima ya Muungano. Itakumbukwa kwamba, moja ya sababu zilizomfanya hayati Abeid Karume aunganishe nchi yake na Tanganyika ilitokana na hofu ya kupinduliwa na wahasimu wake wa siasa za mrengo wa Kikomunisti ndani ya serikali yake kama kina Abdulrahman Babu, Abdullah Kassim Hanga, Othman Sharrif na wengine.

Kwa sababu hii, Rais Nyerere aliombwa na kukubali kupeleka Zanzibar, kikosi cha askari 300 kumlinda Karume na serikali yake. Na pale alipoombwa mara ya kwanza kuunganisha nchi yake na Tanganyika, naye akaonyesha kusita, Nyerere alitishia kuwaondoa askari hao ili wahasimu wake wamkaange; Karume akanusa hatari na kukubali kuungana hima!

Kwa kipindi chote cha utawala wa nguvu wa Karume, tangu Mapinduzi ya 1964 hadi alipouawa Aprili 7, 1972 “uasi” ndani na nje ya serikali yake, na katika chama tawala cha ASP lilikuwa jambo la kawaida na kufuatiwa kila mara na hatua za kikatili kama vile watuhumiwa kutiwa kizuizini na hata kuuawa kikatili.

Tuhuma nyingi zilielekezwa zaidi kwa wanachama wa zamani wa vyama mfu vya miaka ya 1950 vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), Umma Party (UP), ndugu zao na wanaharakati wengine wa siasa za mrengo wa ki-Karl Marx/ki-Lenin.

Na pale Karume alipotangaza kwamba pasingekuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 50, na kwamba milango ya uongozi ilikuwa imefungwa kwa waliokuwa wanachama wa ZNP, ZPPP, UP, ndugu zao na “wakorofi” wengine; hapo siasa za chuki, uhasama na kulipiza kisasi vikaota mizizi na kushamiri hadi leo.

Kwa muda mrefu, chuki na uhasama miongoni mwa Wazanzibari imetumiwa na Serikali ya Muungano kushinikiza mambo mengi kwa jamii ya Kizanzibari (hata yale ambayo hayamo katika mkataba wa Muungano) bila kukataliwa kwa imani kwamba, kwa Wazanzibari, Muungano haukwepeki; kwa maana bila kuwapo Serikali ya Muungano watamalizana wao kwa wao.

Kumalizika kwa uhasama huo wa kisiasa wa enzi na enzi miongoni mwa Wazanzibar (kama tutakavyoelezea baadaye) na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kunaweza kuzua na kueneza hofu kwamba pengine Zanzibar inaweza kuthubutu safari hii kujitoa kwenye Muungano au kushinikiza mambo ambayo hayakutarajiwa yatekelezwe ili kuwe na amani ndani ya Muungano.

Kwa mfano, nani aliyetarajia kwamba Zanzibar, kwa jeuri na bila ya hofu, siku moja ingeamua kuwa na bendera yake ya taifa, wimbo wa taifa, ngao ya taifa, jeshi la taifa, kuwa mwanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuzuia mafuta yake yasiwe ya Muungano; kama ilivyofanya, na sasa inataka kujiunga na Shirikisho/Jumuiya ya Afrika Mashariki kama nchi?

Hofu hii ya Watanzania Bara juu ya SUK inaweza kufananishwa na hofu kama hiyo ya zamani kwa Serikali ya Ethiopia juu ya kujitoa kwa Eritrea kwenye muungano unaofanana na huu wa kwetu na kuwa nchi huru mwaka 1993. Nitaelezea kwa kifupi kabla ya kuangalia chimbuko la uhasama Visiwani, na juu ya yale yanayotakiwa kuvunjwa ili kudumisha amani na utulivu.

Eritrea ilitawaliwa na Wataliano kwa miaka 50 hadi 1941 waliposhindwa vita na Waingereza. Kufuatia ushindi huo, Uingereza iliruhusu nchi hiyo kujitawala kama nchi huru chini ya usimamizi wake. Hapo vyama vya siasa na vya wafanyakazi vikaanzishwa pamoja na vyombo vya habari huru kwa ajili ya elimu kwa umma.

Mwaka 1952, wakati hatima ya Eritrea ilipojadiliwa na Umoja wa Mataifa, Ethiopia ilitaka ipewe nchi hiyo kwa madai kwamba kihistoria ilikuwa ni sehemu ya ufalme wa Ethiopia. Hapo kukatokea mzozo.

Wakati nchi jirani za Kiarabu zilitaka Eritrea iwe taifa huru, Waeritrea wenyewe, ambao idadi yao wakati huo ilifikia 3,000,000, waligawanyika; nusu yao ambao ni wa madhehebu ya Kikristo, na wa kabila la Tigraya waishio maeneo ya milimani karibu na Mji Mkuu, Asmara, waliunga mkono Muungano na Ethiopia.

Kwa upande wa pili, nusu ya Waeritrea ambao ni Waislamu, wanaoishi sehemu za jangwa karibu na Bahari ya Sham na bonde la Magharibi, walitaka Eritrea ipewe uhuru.

Mwafaka ukafikiwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa wa kuunda Shirikisho la Ethiopia na Eritrea ambapo Serikali ya Ethiopia ilipewa kusimamia mambo ya Nje, Ulinzi, Fedha, Biashara, Bandari na Forodha.

Chini ya Muungano huu ambao muundo wake unafanana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Eritrea, kama ilivyo kwa Zanzibar, iliruhusiwa kuwa na serikali yake na bunge huru kusimamia mambo yake.

Tena, kama ilivyo Zanzibar ndani ya Muungano, iliruhusiwa kuwa na bendera yake, lugha zake za taifa, ambazo ni Kitigrinya na Kiarabu.

Toka mwanzo, mtawala wa Ethiopia, Mfalme Haile Selasie aliuona Muungano huo kama ambavyo Rais Nyerere alivyouona Muungano wa Tanzania kuwa ni hatua ya mwanzo tu kuelekea muungano kamili kwa kuunda nchi moja.

Kero na kelele juu ya muungano zilianza kusikika pale watawala wa Ki-ethiopia, kwa ubaguzi na kujuana, wakisaidiwa na wanasiasa Wakristo wa Kitigraya, walipoanza kuvuka mipaka ya mambo yaliyokubaliwa chini ya Mkataba wa Muungano kwa kuongeza mambo kwa njia ya shinikizo, vitisho na uthibiti kwa Waeritrea.

Kwa njia hii, uhuru ambao Waeritrea walifurahia kwa muda baada ya ukoloni wa Kitaliano (na kabla ya muungano), kama vile haki za kisiasa, vyama vya wafanyakazi na uhuru wa vyombo vya habari, vilidhibitiwa. Hapo tena dhana na kelele juu ya Ethiopia kutaka kuimeza Eritrea, kama ambavyo Wazanzibari wanalalamikia kutaka kumezwa na Tanganyika, ikazua moja ya kero za Muungano.

Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa Aprili 26, 1964, ulibainisha mambo kumi na moja tu ya Muungano, baadhi yakiwa ni yale yale yaliyokuwa chini ya Muungano wa Ethiopia na Eritrea tuliyoyaeleza hapo mwanzo.

Na kama ilivyokuwa kwa Ethiopia/Eritrea, Serikali ya Zanzibar iliachwa kusimamia mambo yote yasiyo ya Muungano, na vivyo hivyo kwa Serikali ya Tanganyika.

Lakini kama ilivyokuwa kwa Ethiopia/Eritrea, kadri Muungano wa Tanzania ulivyopiga hatua mbele, mambo ya Muungano yalizidi kuongezwa kwa njia ya Amri za Rais (Decrees) kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano na kufikia 23.

Katiba ya muda ya 1965 (ibara ya 12) ilimpa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya utendaji kwa mambo yote (11) ya Muungano na kwa Tanganyika; kwa maana kwamba Rais wa Muungano alikuwa sasa ndiye Rais wa Muungano na hapo hapo Rais wa Tanganyika.

Vivyo hivyo, ibara ya 49 ya Katiba hiyo, ilitoa mamlaka ya kutunga sheria kuhusu mambo ya Muungano na kwa ajili ya Tanganyiika, kwa Bunge la Muungano. Ndiyo kusema kwamba, Bunge hilo la Muungano sasa lilikuwa ndilo Bunge la Tanganyika pia.

Mwaka 1967 Bunge lilitunga Sheria Na. 24 ya 1967 iliyompa Rais wa Muungano na Rais wa Tanganyika uwezo wa kupachika jina “Tanzania” katika sheria zote pale jina “Tanganyika” liliposomeka.

Hii ilimaanisha kwamba “Tanganyika” sasa ndiyo iliyogeuka kuwa “Tanzania”, na “Tanzania” ndiyo Tanganyika, lakini Zanzibar ikabakia kama Zanzibar.

Ni kwa misingi hii kwamba, Sheria ya Tafsiri za Vifungu vya Sheria (Interpretation of Laws and General Cluses Act) Na. 30 ya 1972 (kifungu cha 3) iliweza kutafsiri neno “Jamhuri” kumaanisha “Jamhuri ya Tanganyika inayojumuisha Jamhuri ya Muungano”

Kama ambavyo uhuru na uwapo wa vyama vya siasa na vya wafanyakazi ulipigwa marufuku kwa amri ya mtawala wa Ethiopia nchini Eritrea (1959) na bendera ya nchi hiyo kufutwa (1958); vivyo hivyo mwaka 1977 hapa kwetu, Chama cha ASP kiliunganishwa na TANU kuunda CCM kama moja ya mikakati ya kuimarisha Muungano.

Lakini ukweli ni kwamba mambo ya vyama vya siasa si moja au sehemu ya mambo chini ya Mkataba wa Muungano wala sehemu ya Sheria za Muungano (Acts of Union) kwa utekelezaji.

Ni kwamba kelele za Eritrea, kama zilivyo kelele za Zanzibar juu ya kero za Muungano, hazikuwa za uongo; kwani ubabe wa Ethiopia (kaka mkuu ndani ya Muungano, kama ilivyo Tanganyika) ulianza kujionyesha dhahiri kwa kushinikiza mambo yasiyo ya Muungano.

Kwa mfano, mwaka 1958 bendera ya Eritrea ilifutwa ambapo mwaka 1959 Sheria za Ethiopia zilishinikizwa pia kutumika Eritrea, vyama vya siasa na vya wafanyakazi navyo vikapigwa marufuku.

Ubabe huu ulikwenda mbali zaidi kwa kudhibiti habari na vyombo vya habari, lugha za taifa za Kitigranya na Kiarabu zikapigwa marufuku, na nafasi yake kuchukuliwa na lugha ya Kiethiopia ya Amhari kama lugha ya taifa.

Kana kwamba hayo yalikuwa hayatoshi, mwaka 1962 Bunge la Eritrea lilishinikizwa kukubali kufutwa kwa Shirikisho na Bunge hilo kulazimishwa kujifuta lenyewe ili Eritrea imezwe na Ethiopia. Kuanzia hapo, Eritrea ilihesabiwa na kupewa hadhi duni kama moja tu ya majimbo 13 ya Ethiopia. Na mapambano ya Waeritrea yakaanzia hapo.

Vikundi vya wapiganaji wa msituni vya Eritrea vikaanzisha vita ya ukombozi ambapo Serikali ya Selasie ilitumia silaha nzito na ukatili mkubwa kujaribu kuizima. Ukatili huu ulidhalilisha utaifa wa Waeritrea, wakaapa kutorudi nyuma hadi uhuru upatikane.

Hatimaye, Mei 1991, Kanali Mengistu Haile Mariam alizidiwa nguvu na muungano wa majeshi ya waasi wa Eritrea na Tigray na kukimbilia uhamishoni.

Matokeo ya kura ya maoni iliyoitishwa Julai 1991, chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kujadili hatima ya Eritrea yaliwezesha Eritrea kurejeshewa uhuru kamili mwaka 1993, na hivyo kufunga ukurasa wa miaka 30 ya vita kwa nchi hiyo.

Kwa kuzingatia mfano huo wa Eritrea, hatuwezi kuyapuuza malalamiko ya Wazanzibari juu ya uendeshaji wa Muungano wetu wenye kuzua kero. Kama ambavyo Serikali ya Ethiopia ilivyoutumia utengano wa Waeritrea milioni tatu kushinikiza mambo yake yasiyo ya Muungano, na hatimaye Eritrea kumezwa ndani ya Ethiopia; ndivyo nasi tulivyo na kila sababu ya kuhofu juu ya SUK iwapo Wazanzibari wataungana na baadaye kutaka tafsiri sahihi ya muundo wa Muungano wetu ambao, kwa muda mrefu, kero zake zimekosa utashi wa kuzitafutia ufumbuzi.

Na ingawa SUK haiwezi kuzua mtafaruku kwa Muungano wetu kama ilivyokuwa kwa Ethiopia na Eritrea, lakini lazima tujiandae kwa mazingira mapya Visiwani chini ya SUK ambayo, kwa vyovyote vile, yatagusa mstakabali wa Muungano.

Na wale wanaoshiba na kujinenepesha kwa uhasama na chuki za kisiasa Visiwani na ndani ya Muungano, wana kila sababu ya kuhofia nafasi zao kwa mambo yajayo. Ni kina nani hao, na kwa yapi?

….Itaendelea wiki ijayo.

Source: Raia Mwema

Nice piece of an article!!!
 
Nakubaliana na hoja za Ndugu Mdondoaji kwa sehemu kubwa. Nionavyo mimi makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) imekuwa faclitated kwa kiasi kikubwa na Karume. Karume anaonyesha msimamo wa kati ku- balance kati ya matakwa ya wale msimamo mkali wa kimapinduzi na wenye msimamo wa wastani kwa upande mmoja. Kwa upande mwingine, ni kujaribu kupunguza jazba kwa wapinga mapinduzi ambao kimsingi wanona kuwa walidhulumiwa na mapinduzi ya Jan 1964. ukitafakari kwa undani unaweza kugundua kuwa wapinzani hao wanaona kuwa wanelekea kwenye ushindi kwa maana kuwa itakuja siku moja ZAnzibaritaweza kuondokana na muungano na hivyo kuweza kutimiza ndoto zao. Lengo la Karume ni zuri sana kwa siasa za Zanzibar na Muungano. Ni lazima wapinzanzani wa mapinduzi na muungano wajifunze yanayojiri kwa sasa na waachane na mtazamo wa kale. Muungano katika dunia ya leo si jambo la kupiga kura ya ndio au hapana. Vile vile walio katika madaraka ni lazima waone, waangalie, watazame, watafakari na wachukue hatua za thati na za kweli kutatua kero za muungano bila kuegemea fikra za kichama. wasipofanya hivyo wapinzani wa mapinduzi na muungano wataendelea na vitmbi vyao na kuyumbisha taifa na hata kuweza kfikia hali ya Erithrea Na Ethiopia SI AJABU!
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom