Simulizi: Zawadi - Sehemu ya 1-7

Dr Lizzy

Platinum Member
May 25, 2009
30,771
59,120
Na Lizzy

(Kisa hiki ni cha kutunga, mfanano wowote na watu au matukio halisi ni bahati tu na siyo kusudio langu. Haki zote za kunakili, kuchapa, au kutoa kwa namna yoyote ile iwe ya uchapishaji, digital au vinginevyo zimehifadhiwa. Kisa kizima au sehemu yake hairuhusiwi kutolewa mahali pengine bila ruhusa yangu na ya Mtandao wetu wa JF)


Alfajiri na mapema nilimsikia mama akiniita kwa sauti niamke. Taratibu nikajigeuza kutoka upande niliokua nimejilaza na kutazama juu kwenye paa letu lililokosa silingi bodi. Bati lililoezeka nyumba yetu ya kupanga lilikua limechakaa kiasi chake ila bado lilikua linatuhifadhi bila kero za kuvujiwa wakati wa mvua japo wakati wa joto dawa yake tuliipata!

"Hivi we Zawadi hunisikii?" nilishtushwa na sauti ya mama aliyekua ametoka uani kote kuja kunipigia kelele niachane na kitanda. "Mama nawe bwana...nimekusikia sana sema nilikua nasali kwanza ndo niamke .Kwani saivi saa ngapi?"

"We achana na mambo ya saa. Leo zamu yetu kufanya usafi embu wahi chooni huko kabla watu hawajaanza kupishana upate kisingizio cha kuchelewa shule.Alafu baadae jioni nikumbushe nna maongezi na wewe."

Wakati ananiagiza yote hayo alikua anaokota nguo nilizotupa chini jana yake na kuniwekea usoni kusudi niziweke sandukuni au kwenye box. Japo hua nakereka sana akifanya hivyo leo sikua hata na pumzi ya kuanza kulalamika, kwanza nlikua nafikiria hicho choo cha jamii kitakua kwenye hali gani asubuhi yote ile na nlivyo na kinyaa. arrrrrg sijui kwanini tusingekua kila nyumba na choo chao!

Mijitu mingine michafu...unakuta biashara zao zimesambaa pembeni sijui hua hawaoni au inakuwaje.Alafu bila hata aibu inaacha hivyo hivyo bila hata kumwaga maji juu juu.

Kabla ya kuinuka kitandani nikakumbuka kauli ya mama, eti ana maongezi na mie. Tangu lini tukataarifiana habari ya maongezi kama kunigombeza, si angenigombeza tu mara moja yaishe? Sikuwahi kusikia hiyo kauli toka kwake kabla kwahiyo nilibaki nikijiuliza hayo maongezi maongezi gani!Kheee usikute kanishtukia!!

Brrr brrrrr mngurumo wa nokia yangu uliotokea chini ya godoro ndio uliyonitoa kwenye mawazo yaliyokua yanataka kunikamata asubuhi asubuhi! Nikainama kidogo pembeni ya kitanda na kuingiza mkono chini ya godoro ili niwahi kujua nani huyo anaetaka kuniletea balaa asubuhi yote hii.

Utadhani watu wote sijawaambia wasiwe wananipigia hovyo! Ile naangalia namba nayo ikakata..wala sikutaka kujishukulisha nayo nikainuka kitandani kanga kifuani nikatoka mpaka uani. Baadhi ya majirani tayari walikua wameshateka maji mapema kuepuka foleni na wengine hata vyombo walishaosha.

Nikawasalimia kila mmoja kwa namna yake huku nikifuata ndoo ya maji ya chooni ili nikafanye usafi. Baada ya kuchukua maji nikatumia dakika zaidi ya mbili nikitafuta sabuni ya Omo kabla ya kumuuliza mama, "Mama!MAMAA!!! Eti sabuni iko wapi?" niliita na kuuliza kwa sauti kubwa japo sikuhitaji kufanya hivyo. "Kama sabuni ya unga babako alimalizia jana.

Nenda hapo kibandani kachukue paketi moja ila pesa mpaka baadae, mwambie Swedi ntampitishia jioni." Mama alijibu kwa sauti ya uchovu, yani wakati wowote ule ukitaka kumwona akinyongonyea kuomba pesa ya chochote kile.

Wakati mwingine nilikua natamani nimsaidie ila ningeanzia wapi, maana ingebidi nijieleze pesa yenyewe nimepata wapi! Kuchezea fimbo na ukubwa wote huu kwakweli ingekua soo, eti mtaa mzima ushuhudie dada mzima nalambwa za ******! Akhaaa!!Hata hivyo nlikua siombi pesa ya nauli au lunch kwahiyo mzigo kidogo niliwapunguzia.

Nilikatisha mawazo yangu hayo na kutoa tabasamu langu wakati napiga hatua nne za mwisho kuelekea kibandani. Swedi aliponiona tu alianza kunikenyulia mimeno yake. "Mambo Zawa mtoto laini kama nyama ya ulimi?" alinisalimia kwa mbwembwe. Bila hiyana nami nikamjibu huku nikipepesa macho kuona kama maandazi yalishaletwa, "Hehehe poa tu. Leo nimekua mlaini ehh?!" "

Sasa we unajiona mgumu?!" Alinijibu kwa swali huku akinyoosha mkono wake kwa nia ya kunishika bega.Nikakumbuka kwamba nilikua nimevaa kanga moja tu na kurudi nyuma kidogo! "Embu acha zako wewe...nipe omo niwahi zangu mie. Alafu pesa baadae...mama kasema ataleta mwenyewe."

Akanipatia pakiti moja ya omo na kipande cha andazi bila hata ya kumuomba.Nikamuaga na kuondoka...niligeuka nyuma mara mbili baada ya kuhisi ananiangalia na kukuta kweli macho yote kaelekeza kwangu.Hata mteja mpya aliyekua pale ni kama alikua hamuoni.

Baada ya kusafisha choo na bafu nilijimwagia maji mara moja na kujiandaa kwenda shule. Mama nae alikua anajiandaa kwenda kwenye biashara zake wakati baba alishadamka na kuondoka mapema sana kuwahi samaki wakubwa feri.

Mimi ndio kwanza nilikua nimeingia kidato cha nne Vijibweni Sec na baada ya miaka mitatu ya kukutana na watoto pamoja na walimu wale wale kila siku nilikua naona kama hamu ya kwenda shule inapungua.
Sijui kwasababu nilikua natamani kutokua mwanafunzi tena niishi nipendavyo?

Hivyo ndivyo nilivyokua nimeaminishwa na mwalimu wangu wa hesabu Mr Samea au Supa kama alivyojulikana kwa wengi. Siku moja tulipokutana nyumbani kwake baada ya shule aliniambia kwamba ni vile tu mimi ni mwanafunzi, ningekua sisomi angeshanioa ili tuwe pamoja kwa uhuru.

Huwezi amini nilifurahishwa na maneno hayo kwa kiasi gani. Niliamini kwamba hatua hiyo ingebadili maisha yangu nisingekua mtoto tena bali mtu mzima mwenye maamuzi yake. Juma nne hiyo hakukua na jipya lolote shuleni zaidi ya masomo tu na umbea.Hata kuongea na Mr Samea nje ya darasa sikuthubutu maana mawazo yangu yote yalikua kwenye maongezi yaliyokua yakinisubiria.

Hata mashosti zangu Ester na Mwajei sikuongea nao sana kama kawaida yetu mpaka wakaanza kunikaba na maswali. "Enhe mwenzetu una nini leo sura imekunjika kama mzee?!" yalikua maneno ya Mwajei hayo. Japo alikua rafiki yangu bado nisingeweza kukataa kwamba alikua binti mmbea sana, na kwakusuta watu ndio usiseme.

Yani siku zote nilikua nashukuru kwamba niko nae upande mmoja. Kabla sijamjibu Ester alidakia kiushabiki, "labda ana mimba." na wote wakaangua kicheko kabla ya kusogea karibu yangu ili niwape habari motomoto.

"Yani nyie..ndo urafiki gani huo wa kutakiana mambo ya ajabu ajabu hivyo?!Mnataka mzee Fadhili aninyonge ehhh?!" niliwatupia maswali bila kuwapa walichokitaka.Wakati wote wakijiandaa kusema kitu tulisikia kengele ya kurudi madarasani baada ya mapumziko ya mchana kwahiyo na sie tukainuka na kuelekea darasani haraka maana mwalimu wa zamu alikua amesimama karibu kabisa na tulipokaa na fimbo yake mkononi.


SEHEMU YA PILI
Masomo yaliyokua yanafuata baada ya mapumziko yalikua hesabu na fizikia na yote aliyafundisha mwalimu Samea! Nikautumia ukaribu wetu kupata ruhusa ya kuondoka na kuenda nyumbani bila maswali kabla hata somo halijaanza maana nilishaanza kujisikia vibaya.

Siku zote nimekua nikiwa na kiwewe au shauku ya kitu fulani napatwa na hali ya ajabu! Kama ni kitu kibaya basi wakati mwingine hua hata tumbo linaanza kuvuruga mpaka kufikia kuniuma,napatwa na hofu mpaka mwili unanitetemeka.

Hiyo ndio hali niliyokua nayo na nilijua fika kubaki pale shuleni kusingenisaidia hivyo nikaona bora niwahi nyumbani nijaribu hata kulala kidogo. Na hivi mama alikua hana kawaida ya kurudi nyumbani kabla ya saa kumi na moja sikua na wasiwasi wa maswali ya kwanini nimerudi mapema.

Nilitembea mwendo wa taratibu kuelekea kituo cha daladala cha pale Vijibweni, muda wote huo nilijaribu kujizuia nisiwaze chochote kile hivyo nikaokota kijiti na kuchora mstari mchangani kadiri nilivyokua natembea.

Bzzz bzzzz nilihisi mgurumo ukitokea ndani ya mfuko wa sketi ya kijani niliyokua nimevaa. Niliingiza mkono kivivu mfukoni na kutoa simu niliyonunuliwa na mwalimu Samea miezi nane au tisa iliyopita. "We vipi bwana unaondoka hata huagi? Usije ukakuta una mimba kweli alafu husemi.

Shaurilo!!" Ulikua ni ujumbe wa simu toka kwa Ester.Bila shaka aliyeandika alikua Mwajei maana yeye ndiye aliyekua mtaalamu wa madongo. Nilifikiria kujibu ila sikua na uhakika jibu gani niwape. Nikaamua niwapotezee mpaka ntakapojua kwa hakika mama alitaka kuongea nini nami ili niwape habari kamili.

Kabla sijarudisha simu mfukoni nikakumbuka simu iliyoingia asubuhi.Nikabonyeza vitufe kuangalia simu zilizoingia na kutoka ili kujua aliyenipigia alikua nani maana asubuhi sikuhangaika nayo. Nilikutana na namba ambayo sikua nimeihifadhi mle kwahiyo haikua na jina. "Oya...angalia basi unapoenda." ilikua ni sauti ya gadhabu kidogo kutoka kwa mwendesha mkokoteni wa maji ambae kidogo tu nilikua niuvae mkokoteni wake kwa kutoangalia mbele.Nikamwangalia na kumwambia "samahani " ya kizushi maana sikujali.

Nikachangamsha miguu kumalizia hatua chache zilizobaki kufika kituoni.Bahati nzuri sikua na haja ya kusubiria maana nilikuta tayari kuna daladala mbili zilizokuwa zinasubiria abiria ili waelekee Ferry. Nilichagua ile ambayo ilikua bado sana kujaa sababu sikua na haraka na nilikua natamani kukaa kwa utulivu.

"Denti bila sh. 50 haupandi" yalikua maneno ya konda aliyechafuka vumbi na kunuka jasho! Nikatoa noti ya sh.500 na kumkabidhi "kata ya mtu mzima, nakaa." "Alafu nyie madenti siwamaind kabisa .Wote mngetakiwa muwe mnalipa nauli kama watu wazima badala ya kujaza gari bure, au kama vipi serikali iwanunulie za kwenu." Alisema huku akinirudishia chenji yangu.

Ingekua siku nyingine ningeanza kubishana nae kuhusiana na swala la wao kunyanyasa wanafunzi mpaka kupata mashabiki kati ya abiria wengine ila kwa muda ule sikua na hamu ya kufanya vile. Nikaingia kwenye gari na kukaa siti ya pili kutoka mwisho upande wa dirishani.

MIEZI KADHAA BAADAE!
"Wiki ijayo ndio mitihani inaanza. Maandalizi mliyopata pamoja na juhudi zenu ndivyo vitakavyoamua kama mtatoa maua au miiba.Naomba tusiabishane tafadhali. Mkiniangusha ntawafuata huko huko majumbani kwenu niwalambe bakora, kwahiyo msidhani kwamba ndio tumemalizana. Nawatakia kila la kheri, mjitahidi, mjitume kuonyesha kwamba miaka minne mliyokua hapa mlikua mnasoma na sio kucheza. Kupumzika weekend hii ni muhimu kwa hiyo mambo ya disco subirini mpaka mrudi mtaani. Tutaonana jumatatu." maneno haya yalitolewa mwalimu mkuu wa shule, Mrs Matole.

Baada ya kumaliza kututisha alianza kuchezea fimbo yake kwa mikono yote miwili huku akitoka nje ya darasa tulilokuwamo. Watu walianza kuongea japo bado kuliwapo na mwalimu aliyebaki pale. Hakufurahishwa na kitendo kile hivyo alichukua rula iliyokuwepo kwenye dawati kwa kwanza kulia na kuligonga dawati hilo hilo mara tatu.Wote tulitulia na kujiweka sawa.

Hakua na mengi ya kusema hivyo alifanya kurudia machache tuliyosikia toka kwa mwalimu mkuu akaongezea na kwamba kila mmoja aje akiwa amejiandaa kikamilifu hiyo jumatatu. Kwamba tusije na kalamu zilizoisha wino tukitegemea kupuliziana kwenye chumba cha mtihani. Tuliitikia wote kwa pamoja kuashiria tumemuelewa nae alinyanyua rula aliyokua ameshika na kutupa ishara ya kuondoka.

Watu walianza kutoka kwa fujo kama wafungwa walioachiliwa huru huku wakipiga kelele za shangwe. Nilihisi kuboreka na hali ile maana walikua wananiongezea maumivu niliyokua nayo kichwani tayari. Siku ya nne hiyo tangu nianze kupata maumivu ya kichwa na uchovu usio na mpangilio bila kujua tatizo langu ni nini.

Mama alihisi nina malaria ila hakua na pesa ya kwenda kupima hivyo aliniomba nivumilie mpaka jumamosi atakapokusanya baadhi ya madeni anayowadai wateja wake. "Zawa uko poa?!" aliniuliza Ester huku akichuchumaa ili aweze kuona uso wangu niliokua nimeuinamisha chini. "Yeahh, kichwa tu kinagonga kwa mbali.Tangulieni nakuja." nilijibu bila kutazama juu.Mwajei alimvuta mkono akamnongoneza kitu kilichowafanya waangue kicheko huku wakitoka nje ya darasa.

Baada ya sekunde kadhaa niliinua kichwa na kugundua kwamba mwalimu Samea hakua ametoka mle darasani na wala hakua amesimama tena...alikua amekaa juu ya dawati macho ameyaelekeza mlangoni.Alipoona hamna mtu mwingine karibu alizungumza kwa sauti ndogo yenye chembechembe za hasira, "Jana ilikuaje hukuja?"

Nilivuta pumzi ndefu na kuishusha taratibu kabla ya kumjibu kwamba mama alinihitaji nyumbani mapema. "Kwahiyo na simu yano ukazima kwasababu?" aliuliza bila kunitazama. "Chaji iliniishia." nilijibu kwa ufupi.Nilikua nadanganya nae alijua.

"Tangulia ntakukuta." alisema huku akinitupia funguo za nyumbani kwake kisha akatoka na kuelekea ofisini. Sikutamani kwenda ila sio kama alikua ameniomba ama ameuliza kama ntapenda bali aliniagiza hivyo nilipaswa kutii na kufuata maagizo.

Kagiza nilikokakuta ndani kaliyafurahisha macho yangu hivyo niliyaacha mapazia yake nilivyoyakuta na kuelekea moja kwa moja kwenye sofa la watu wawili lililokuwamo mle ndani. Nilijiegesha kwenye sofa huku nikiwaza ntamkimbia vipi mwl pindi atakapofika pale. Nilikua nimeanza kumchukia na ndio sababu haswa ya mimi kumkwepa kila alipotaka kukutana nami faragha. Nilitamani nisingekua na ulazima wa kuonana nae kila siku ila sikua na ujanja, hata hivyo nilipiga moyo konde maana muda sio mrefu nisingekua mwanafunzi tena pale.

Kila nilipokumbuka kile kilichotokea wiki karibu tano zilizopita nilitamani kulia, wakati mwingine kumpiga hata kibao au kumuaibisha mbele ya wanafunzi na walimu wengine. Kama kawaida nilipita kwake baada ya shule na kufanya yale niliyozea huku yeye akiwa bize anatazama TV na mara chache kunitazama mimi niliyekua napika upande wa pili wa sebule.

Hakuacha kunitupia sifa za hapa na pale kuhusiana na mke wa aina gani ntakua kwake hapo baadae, siku zote maneno yake yalikua yakinipa tabasamu toka moyoni. Nilikua na matumaini na nilijua nimependwa. Pamoja na kufuatiliwa na vijana wengi wa umri wangu bado niliamini kwamba mwalimu ndio saizi yangu. Simu yangu ilipoita aliitoa kwenye mkoba uliokua pembeni ya sofa alilokalia na kunijulisha kwamba kuna mtu ananipigia.

Alikua Jerry, nilipokea na kumsalimu ''Mambo?'' ''Sio shwari wala nini. Ulivyofanya juzi sio fresh kabisak, yani mi niliacha mishe zangu nikakusubiria home pale alafu hukutokea.'' alijibu akionyesha kukereka. '' Tulikua tuko bize tunasoma bwana, muulize hata Ester anajua.'' Nilimjibu kabla ya kumuomba nimtafute baadae maana nlikua na kazi.

''Nani huyo?'' aliniuliza mwalimu. ''Kaka yake Ester.'' ''Alikua anataka nini?'' aliniongezea swali. ''Umm basi tu ananisumbua sumbua.'' nilijibu huku nikipiga hatua kuelekea lilipokuwepo jiko. Bila kutarajia aliomba nimpe simu yangu nami bila wasiwasi nilimpatia.

Kwa zaidi ya dakika kumi hakusema neno wala hakuelekeza macho yake ilipo TV, alikua akihangaika na simu yangu. Mpaka namaliza kupika na kutenga chakula hakuwa anaongea nami, nadhani hata kuniona hakuniona wakati naweka chakula mezani maana nilipomwita alishtuka. ''Chakula tayari hivyo.'' nilimwambia kwa kujiamini.

''Unaweza kuniambia huyu Jerry mmeanzana lini?Maana naona mnatumiana tu maujumbe.'' alisema huku akielekea mlangoni. Kabla sijamjibu nilishangaa kuona anafunga mlango kwa ndani mchana wote ule, kisha akaja nilipokua nimesimama na bilauri la maji mkononi. Akalichukua na kuliweka mezani kisha akasogea karibu sana na nilipokua kiasi kwamba hewa yote niliyovuta ilikua na harufu yake. ''We hunijui ehh?'' ndio maneno niliyoyasikia sambamba na kibao kikali cha shavu. Akili yangu haikuweza kufanya kazi kwa haraka sababu nilishtushwa sana na kile kitendo, nikabaki nimezubaa nisijue cha kufanya.


SEHEMU YA TATU
Alinishika mkono wa kulia kwa nguvu na kunivuta ulipokua mlango wa chumbani. Bila kunitazama usoni aliuachia mkono wangu na kunisukuma kitandani , hapo ndipo akili yangu iliporudi. Nilijua nini alichokusudia kufanya na nilihitaji namna ya kuzuia kitendo kile.

Kwa haraka niliinuka toka kitandani ili nitoke mbio ila sikupata mwanya huo maana mara hii baada ya kunisukumu alinikandamiza chini kwa mikono yote miwili. Mpaka wakati huo bado sikuelewa mabadiliko yale yalitokana na nini haswa. Macho yake yaliyokua yakinivutia mwanzoni yalinitazama kwa ukali, na kwa mara ya kwanza niliogopa kuangaliwa nayo.

" Unaniumizaaa" nililia kwa sauti ya chini. Hakuonekana kujali kwani ndio kwanza alinitazama kwa ukatili. "Malaya mkubwa wewe." alisema kwa gadhabu, "Huna shukurani kabisa. Unakula pesa yangu kumbe unaliwa na wengine huko?! Ngoja nikufundishe heshima kidogo" alisema huku akiwa ameshika shati langu tayari kulirarua.

Machozi yalinitiritika sambamba na sauti ya vifungo vilivyoanguka sakafuni, vilivyogonga ukutani na pia sehemu ya kitanda. Alisogeza uso wake kifuani kwangu kama mtu anaechunguza kitu kisha akaupandisha taratibu.Midomo yake ilipokaribia yakwangu nikafikiria namna ya kumuondoa juu yangu, alipoikutanisha tu yangu na yake nilimngata japo sio kiasi cha kumtoa damu!!

"Mamaaa" alilia huku akiruka kwa maumivu na kujilaza chali pembeni yangu huku akichunguza midomo yake kwa ulimi na mkono wake.Nikatumia mwanya ule kukimbia mpaka sebuleni na moja kwa moja nilielekea mlangoni. Mkono wangu ukiwa umeshika kitasa cha mlango tayari kuufungua nilihisi maumivu makali shingoni.

Alinigeuza akanitazama kwa hasira kisha akanikokota tena mpaka lilipokuwapo sofa bila kusema neno. Alinisukuma kisha akanyanyua miguu yangu na kuiweka juu. "Sasa urudie tena ushenzi uliofanya uone ntakachokufanya. Hivi wewe unanijua au unanifahamu? Si nakuuliza wewe?!" alinizodoa kwa kidole. Sikuweza kujibu maana kilio na kwikwi vilinitawala.

Kwa haraka nilifikiria kwamba hamna nnachoweza kufanya kujinasua toka mikononi mwake, na nilishajua kwamba nikileta ukorofi anaweza akanifanya chochote kile hivyo nilitulia na kuacha kilio changu kionyeshe hali niliyokua nayo. Alivua suruali yake huku akihema kwa nguvu baada ya kupandisha sketi niliyokua nimevaa mpaka kiunoni.

Akashika nguo yangu ya ndani na kuivuta juu na kuiachia mara mbili alafu akaanza kuishusha chini.Niliinua miguu yangu juu usawa wa kifua chake na kuibana kwa nguvu zangu zote. "Umeshazoea huko alafu hapa ndio unataka kujifanya mgeni?

Embu usinifanye mpumbavu." kauli yake hiyo iliniingia. Sikujua amepata wapi mawazo hayo wakati alijua fika sikuwahi kuhusiana na mtu kimwili. Mwenyewe aliniambia na kunisihi nisikubali kufanya hivyo hovyo kwasababu nastahili zaidi ya kufanywa chombo cha matumizi na mwanaume yeyote yule. Hata yeye alikua tayari kunisubiria nimalize shule ili aweze kunifanya mkewe kabla ya kunijua kimwili. Iweje leo ......!Mawazo haya yalikatishwa mikono yake miwili kufanikiwa kuachanisha miguu yangu.

Sikuona sababu ya kumzuia tena, machozi nayo yalishaanza kukauka japo bado kwikwi zilikuwa nami. Nilifikiria kupiga kelele ila nani angekuja? Sikujua kama majirani walikuwepo au hawakuwepo. Na hata kama walikuwepo, ingekuaje kama wasingehangaika kutaka kujua nini kinaendelea na kunisaidia? Si ningemkasirisha zaidi?

Japo kwa kutulia kungedhihirisha udhaifu wangu mbele yake sikua na ujanja. Kilichofuata pale yalikua maumivu makali ambayo nisingependa kuyakumbuka daima.Nilihisi kama mtu aliyekatwa na kisu sehemu laini.Niliweza kuachia yowe moja tu kabla hajaniziba mdomo na kuongeza nguvu na kasi kwenye kile alichokua akifanya. Nililia nikalia alafu nikalia tena.

Mishale ya saa kumi na mbili jioni niliondoka pale kwake nikiwa nimevalia shati ambalo halikua saizi yangu. Nilielekea moja kwa moja alipokua anaishi Ester. Kabla ya kufika kwao nilimtumia ujumbe kwa njia ya simu kumuomba tukutane Mwembeni .

Giza lilishaanza kuingia hivyo sikua na wasiwasi wa watu kunishangaa nilivyokua nimevimba uso au nilivyokua natembea. Hata Ester hakugundua tofauti yoyote mpaka nilifika alipokuwepo sababu kulikua na mwanga wa taa ya chemli iliyowekwa juu ya kibanda cha mboga mboga. "WEWE!!! Mbona hivyo umefanyaje?!" aliuliza kwa mshangao huku macho yamemtoka.

Alisogea karibu na kuugusa uso wangu kuona kama nilikua nimeumia, nilitazama chini nisijue cha kumjibu. "Niambie basi, home wamekumaind?" aliuliza tena, mara hii nilitikisa kichwa upande kuashiria hapana. "Naweza umm, kulala kwenu leo?"

Sikua nimetoa neno tangu kilichotokea kilipotokea hivyo nilishangaa sauti yangu ilivyokua imebadilika. "Hamna noma! Ntamwambia mama umekuja tumalizie kujiandaa kwa mtihani." maneno yake yalinipa ahueni, akanishika mkono na kuniongoza ilipokuwepo nyumba yao.

Tulizunguka uani na kuingia ndani bila kuzungumza, tulipofika kwenye korido aliita kwa sauti kumjulisha mama yake aliyekuwepo sebuleni kwamba nimefika kujiandaa kwa mtihani. Nashukuru Mungu umeme ulikua hamna hivyo sehemu kubwa ya nyumba ilikua imetanda giza isipokua sebuleni. "Hujambo Zawadi?!" mama yake alinisalimu kwa sauti ya upole.

Nilikohoa kwanza ili kulainisha sauti yangu kabla ya kumsalimu na kumjulia naye hali. "Alafu nyie sio mliseme leo mtapumzika kusoma? Au ndo usomi wenyewe huo?" mama Ester aliuliza huku akicheka nasi tukamuunga mkono. Ghafla nilitamani yule ndio angekua mama yangu. Mpole, mrembo na siku zote alikua kama hacheki basi anatabasamu.

Sikuwahi kumsikia akigomba au kumuona akiwa amekasirika. "Anyway, fanyeni mambo yenu chakula kikiwa tayari ntamwambia dada awaletee." alisema nasi tukaitikia asante kwa pamoja.Haikua mara ya kwanza mimi kulala kwa kina Ester hivyo sikua na wasiwasi ntakavyojieleza nyumbani.

Urafiki wetu watatu uliendelea hata nje ya shule na wote tulijulikana kwa kila familia ya mmoja wetu, na kipindi cha maandalizi ya mitihani tulipokezana kulala kwa kila mmoja ili tuwe tunasoma pamoja. Nilimpigia mmoja wa majirani zetu na kumuomba niongee na mama baada ya salam.

"Halo." mama alisikika.
"Mama, ni mimi.Pole na kazi."
"Enhe muda wote huu uko wapi?!" aliuliza bila kupokea pole yangu.
"Umm nilipita kwa kina Ester tukaanza kusoma mpaka sasa hivi ndo nashtuka.Nlikua nataka kukuomba kama naweza kulala ili tuendelee kusoma mpaka usiku."
"Yani wewe mtoto wewe.Kwahiyo hizo ratiba zako huwezi kuweka wazi mapema?!Haya utajuana mwenyewe na babaako hiyo kesho ukirudi."
"Asante mama, kesho basi." nilimalizia na kukata simu!

Kule chumbani kulikua na tochi kubwa iliyofanya kuwe na mwanga sana tofauti na ilivyokua sebuleni, hivyo nilimwomba Ester kama hatojali aizime au awashe mshumaa pekee. Tulikaa kitandani bila kuzungumza kwa muda kidogo ndipo apotaka kujua kilichonisibu. Nilimweleza mwanzo mpaka mwisho, alichofanya yeye ni kuitikia tu na kutoa macho mpaka nilipomaliza.

"Weeee! Kwahiyo akananiii?" "Mhuuu" nilijibu bila kutoa neno.
"Pole mwaya!Umemwambia mtu?!" aliuliza kwa tahadhari. "We ndo mtu wa kwanza kukwambia.We unadhani kwanini sikutaka kwenda nyumbani?! Nilivyovaa na huu uso sijui ningejieleza vipi. Mwenyewe nimejiona hapo kwenye kioo nikajiogopa!"

"Sasa utafanyaje?!" alinitupia swali jingine. "Sijui." jibu langu lilikua fupi maana ni kweli sikujua nifanye nini. Kuwaeleza nyumbani sijui ningeanzia wapi. "Umm labda tukimwambia mama yangu anaweza kujua nini cha kufanya." alitoa wazo ambalo halikua baya sana kwa vile nilivyomjua mama yake ila sikua tayari kuelezea tena kilichotokea. " Uhh uhh!!Labda kesho, ntafikiria."

"Ok! Kwahiyo sasa hakusema kitu wakati unaondoka?!"
"Aliniomba samahani ila sikumjibu nikavaa zangu na kuondoka.Kanipigia sijapokea alafu akanitumia meseji kwamba atanitafuta kesho na anaomba nisimwambie mtu." nilimjibu kwa sauti ambayo ilianza kufanana na ile niliyoizoea.Hata hasira niliyokua nayo ilikua imepungua.

"Kheeee!!Mshenzi kweli, yani kakufanyia hivyo alafu anakuomba samahani?!Kisa?!Ningekua wewe haki ya nani ningeshtaki awekwe ndani." maneno yake yalishapita mawazoni mwangu ila nilipotezea baada ya kugundua kwamba hata mimi ntakua matatizoni maana baba hatoelewa kabisa nilichokua nakifanya kwa mwalimu Samea mpaka yote hayo yakayokea.

"Nimefikiria ila nyumbani wakijua baba sijui atafanyaje. Ohhh alafu unajua kwanini aliniomba msamaha?!Kwasababu alivyomaliza alikuta damu kwahiyo akajua sikua nimefanya mapenzi na mtu kabla.Kumbe alivyoona meseji za Jerry akadhani nimetembea nae."

Muda huo huo Ashura alituletea chakula hivyo hatukuweza kuendelea na mazungumzo yetu. Nilishangaa kwamba niliweza kula karibu nusu ya chakula nilichotengewa, kwa muda nilihisi niko katika hali ya kawaida.


SEHEMU YA NNE
Siku iliyofuata tulichelewa kuamka kutokana na uchovu wa hadithi za usiku mzima. Aliyetuamsha alikua Jerry aliyetumwa na mama yake kutukaribisha kifungua kinywa. Aligonga mara mbili kabla ya kufungua mlango na kuingia ndani kwa kunyata, pamoja na kwamba tulimsikia wote tulifumba macho kama vile bado tumelala.

Alienda moja kwa moja dirishani na kusogeza pembeni mapazia yaliyokua yakizuia jua lililokua linawaka asubuhi ile lisiingie chumbani . Mwanga wa jua ulimmulika Ester aliyekua amelala karibu na dirisha na kumfanya amfokee Jerry kumwomba arudishe mapazia kama alivyoyakuta.

"Amka huko acha uvivu. Alafu we ni muongo kweli, jana siuliniambia Zawadi haji wewe?!" aliuliza Jerry. "Embu ondoka bwana!Au nimwambie mama unatusumbua...!MAMAA!!" yalikua majibu ya Ester ambae kwa wakati ule hakua tayari kuamka. "Mama mwenyewe ndio kanituma niwaamshe kwahiyo sitoki wala nini." nilishawazoea kwa vile ambavyo walikua wakichokozana mara kwa mara, haikua ajabu sababu umri wao haukuzidiana sana hivyo kila mmoja alitaka kumwonyesha mwenzake kwamba hawezi kumtawala.

Kwakua nilikua nimegeukia ukutani sikua na wasiwasi wa Jerry kuuona uso wangu, ila nilijua iwapo ataendelea kuwepo pale mpaka tuamke atauona tu. Nikavuta shuka tulilokua tumejifunika mpaka kichwani kisha nikatumia mkono wangu kujipapasa usoni ili nione kama bado ulikua umevimba. Nilihisi ulikua umerudi katika hali ya kawaida japo siku na uhakika.

Nikageuka na kulala chali kisha nikashusha shuka lile usawa wa ilipoanzia pua yangu kabla ya kumsalimia Jerry, "Mambo msumbufu?!" "Fresh tu mrembo, umeamkaje?!" alinijibu kwa uchangamfu. " Mmmh nimeamka kwa ubavu. Unaweza kutoka kidogo tuvae?" sijui kipi kati ya jibu na swali langu vilimfanya atabasamu ila alitabasamu kisha akatoka nje.

Mwanzoni mimi na Jerry hatukuwahi kuzoeana sana, tulionana kila nilipokuja kumuona Ester ila hatukuwahi kukaa chini na kuongea, japo alipenda kunitania mara kwa mara, mara nyingi tuliishia kujuliana hali tu basi. Nakumbuka tulianza kuzoeana alipoanza kunitafuta kwenye simu. Mwanzoni sikufahamu ni nani aliyenipigia hivyo kwa karibu wiki nzima sikujibu simu zake mpaka siku nilipowauliza Mwajei na Ester kama walikua wamempa mtu namba yangu.

Wote walikataa ila walipenda kuijua namba yenyewe, "Mbona namba yenyewe kama naijua?!" alidakia Ester baada kuiona. "Nakuja" alikimbia ofisini na kutoka na mikoba yetu tuliyokua tumeihifadhi tulipotumwa na mwalimu.Akatoa simu kabla ya kuomba kuona tena zile namba!! "Hahahaha." Aliangua kicheko huku akituonyesha alichokua akiona, jina la kaka yake.

"Wee!!Hahaha, kumbe mwizi mwenyewe tunamjua.Sasa we alipataje namba yako?!" aliuliza Mwajei. "Mi ntajuaje, muulize mdogo wake huyo hapo." ndilo jibu nililotoa wote tukabaki tunamkodolea Ester macho maana yeye ndie aliyekua mtuhumiwa mkuu kwa wakati ule. Baada ya kufahamu ilikua Jerry tulianza kumtumia meseji wakati ule ule kumchezea. Baadae tulijenga mazoea yaliyosababishwa na kuzungumza sana kwa simu pia ana kwa ana.

"Ahhhhh nimechoka!Mi natamani kuendelea kulala." alisema Ester huku akijikunyata na kuvuta shuka kivivu. " We endelea tu, mi naamka nikaoge nianze kujiandaa kwenda nyumbani." nilijibu nikiwa tayari nimetoka kitandani na kuchukua kioo kidogo kilichokuwepo kule chumbani. Uso wangu ulionekana kawaida, sikua na sababu ya kua na wasiwasi ila nilipopiga hatua nilikumbuka yaliyonikuta jana yake.

Nusu saa baadae nilishtushwa na kelele za mlango kutoka kwenye kausingizi kalikokatisha kumbukumbu yangu. Kichwa bado kilikua kikiniuma na uchovu niliohisi mwanzo ulikua umezidi maradufu. Mwalimu aliinua pazia moja na kuruhusu jua la jioni ile lipendezeshe muonekano wa kule ndani. Alienda mpaka kabatini na lilipokuwapo bilauri la maji ya kunywa na kumimina katika glass, akanywa kisha akaijaza tena na kuja nayo nilipokua nimekaa akayaweka upande wangu wa meza.

"Tunaweza kuongea kidogo Zawadi?" aliuliza kwa sauti ya upole nami nikamjibu kwa ufupi "Nakusikiliza."
"Alright! Zawadi kusema ukweli nimegundua kwamba umebadilika sana wiki hiz za karibunii, umenyongonyea mwenyewe hata kutabasamu hutabasamu kama nilivyozoea. Najua mimi ndiye niliyesababisha ila nilitegemea utakua umenielewa mpaka sasa maana nilishakueleza nini kilichonipata siku ile na samahani nimekuomba si chini ya mara ishirini .Naomba unisamehe tafadhali.

"Nilimtazama juu mpaka chini, alivyokua amekaa kinyonge, uso na macho yake yalivyokua yamekaa kipole nilitamani kumwambia nimekusamehe na kumaanisha ila nilipokumbuka alichonifanyia wiki kadhaa zilizopita nilimwona mtu mwingine tofauti kabisa na aliyekaa pale. Hivi anadhani yeye ni nani hata aweze kuniumiza kiasi kile alafu ategemee ntamsamehe tu sababu ameomba?

Eti alitarajia ningekua nimemwelewa, kwanini yeye asijaribu kunielewa mimi ili aache kunisukuma nimsamehe wakati anapotaka yeye mpaka pale ntakapokua tayari? Nilihisi damu ikinichemka kwa hasira, hakua na shukurani hata chembe. Hivi ni kwamba amesahau ni kwa kiasi gani ningeweza kumtia matatizoni kama ningewaeleza nyumbani?

Nilitamani kuyasema yote hayo kwa sauti ila sikua katika hali ya kujibizana. "Nataka kwenda nyumbani tutaongea siku nyingine." ndio jibu pekee alilopata toka kwangu. "Zawadi please.Yani hujui tu ni kiasi gani naumia kukuona ukiwa hivi, kama ningeweza kurudi nyuma haki ya Mungu nakwambia ungekua unacheka kwa furaha sasa hivi." nilihisi kwamba alimaanisha alichokua akikisema. Ghafla nilihisi kizunguzungu ila kabla sijapata nafasi ya kumwambia najiskia vibaya nilipoteza fahamu.

Nilishtuka baadae kwa kuhisi mwanga mkali machoni, nilipojaribu kuinua mkono wangu wa kushoto ili niutumie kukinga mwanga ule nipata maumivu kidogo nyuma kiganja. "Aaaaahhh!!" niliguna kwa sauti.
"Unajisikiaje?!" iliniuliza sauti ya kike. "Nimechoka alafu kichwa kinaniuma.

Niko wapi?!" niliuliza huku nikifungua macho taratibu ili kujua nilipo. " Usijali uko hospitali, embu naomba uniambie unaona nini?!" nakuona wewe, nilitaka kujibu ila sikufanya hivyo! "Vidole!Viwili!" nilisema na kuanza kupepesa macho kule ndani. Aliyekua akiniangalia alikua dada mrembo kweli.

Alikua amevalia kagauni keusi kalikofika chini tu kidogo ya magoti yake na koti jeupu lililokaribia urefu wa kagauni kake kalikoushika mwili wake wa saizi ya kati vizuri. Alikua mrefu kiasi hivyo viatu vya chini alivyokua amevalia vilimkaa vyema pamoja na gauni lake. Mkononi alishika kalamu na file alilokua akiandika alichojua yeye. Nywele zake zilikua zimenyolewa karibu kuisha, kama asingekua mzuri wa asili ingekua rahisi kumfananisha na mwanaume.

Macho yake yalikua ya mviringo na makubwa kiasi huku yakisindikizwa na pua pana kidogo iliyoendana na uso wake.Kama asingekua daktari hakika kujishughulisha na maswala ya urembo kungemfaa mno.

Hakukua na mtu mwingine mle ndani zaidi yangu na yeye, hata kitanda kilichokuwepo upande wa pili kilikua kitupu. Katikati kulikua na meza iliyotenganisha vitanda vile viwili na juu ya meza kulikua na maua mchanganyiko. Pembeni ya kitanda changu ilisimama chuma kubwa maalumu kwa kuwekea dripu.Juu yake uliningininzwa mfuko uliokua una maji, au sijui ilikia dawa iliyokua ikidondoka matone madogo madogo kila sekunde kuelekea mwilini mwangu.

Sikuhitaji kuuliza nilifikaje pale ila nilipenda kujua aliyenileta yuko wapi hivyo nikamuuliza yule daktari." Yuko nje hapo alikua anasubiria nikuangalie kwanza.Natoka niongee nae kidogo alafu atakuja kukuona, sawa ehh?!...Alafu, kwani ni nani wako?!" aliuniuliza huku akinitazama kiupande.

Nilijibu haraka bila kufikiria "Ndugu." "Ok!Ntarudi tena baadae kidogo" aliaga na kutoka huku akirudishia mlango nyuma yake.Kutokana na koti kubwa alilokua amevaa sikuweza kuona umbo lake lilivyokua kwa nyuma ila bado ilibaki mawazoni mwangu kwamba alikua dada mrembo kama sio mzuri.

Nilikumbuka mazingira yaliyonifanya nipoteze fahamu ila sikuwa najua ni kwa muda gani nilibaki vile. Nilipapasa macho kwenye kuta zote za chumba kile kuona kama kunasaa ila niliambulia patupu. Sikua na ujanja bali kusubiri huku nikihesabu matone ya dripu yalivyokua yakidondoka.

Muda sio mrefu aliingia mwalimu huku akifunga mlango kwa tahadhari . "Zawadi, unajisikiaje?!" aliniuliza kwa sauti ya chini. "Hovyo!" nilimjibu.

"Pole, Ila daktari amesema utakua fresh tu, ndo wanaangalia angalia vipimo wajue tatizo nini." sikua na haja ya kujua hayo yote ila haikua mbaya kusikia sauti yake. Nilijisikia vibaya kidogo maana nilijua atakua alishtuka sana nilipopoteza fahamu, ndipo nikakumbuka kwamba nyumbani walikua hawajui nilipo. "Saa ngapi sasa hivi?!" nilitaka kujua. "Ummm saa kumi na mb...ahhh moja kasoro."

"Nataka kumjulisha mama niko wapi asije akapata presha .Naweza kuazima simu yako?!" nilimuuliza huku tayari nikiwa nimekinga mkono tayari kuipokea. Bila kusema chochote aliitoa mfukoni na kunikabidhi. "Halo!"
"Shkamoo mama Asha!Zawadi hapa!" nilimsalimu jirani yetu.
"Mara haba mwaya, hujambo?!"
"Mi mzima!Naomba kuongea na mama kama upo karibu na nyumbani ehh?!"
"Tena niko nae hapa!!Haya huyu hapa...!" alisema na kumkabidhi mama simu.
"Mama!"

"Zawadi naona sasa umefanya mazoe kuzurura utakavyo na kupiga simu utadhani ulipoondoka nyumbani ulishindwa kuaga na kusema kama utapita kwa wenzako. Alafu wewe si juzi tu ulikua huko?!Au ndo umehama nyumbani?!" alinipokea kwa maswali kede wa kede.

"Mama! Sikiliza bwana, nipo hospitali.Nilianguka shuleni mwalimu akanileta hospitali sasa hivi ndio daktari kaniruhusu kuongea na simu!!" sijui kwanini nilidanganya ila nadhani ilikua sahihi kwa wakati ule. "Kheeee!We mtoto, sasa unaendeleaje? Embu nikamtafute baba yako tuje kukuona.Kwani uko hospitali gani?!" nilihisi mabadiliko kwenye sauti yake hivyo nikajaribu kumtuliza kidogo!!

"Sasa hivi najisikia nafuu.Nadhani ni kile kichwa tu na jua vilichangia!" nilimjibu kisha nikamuuliza mwalimu kwa kunong'oneza jina la hospitali tuliyokuwapo! "We unaongea na nani hapo?" kumbe mama alinisikia nikinong'ona. "Mwalimu aliyenileta, nlikua namuuliza tulipo." nilimjibu.

"Embu nipe niongee nae!" bila swali wala ishara nilinyoosha mkono wangu wenye simu kuuelekeza alipokua amesimama mwalimu akiniangalia! "Mama anataka kuongea na wewe." nilisema huku nikijiuma midomo yangu ya chini. Alipokea simu toka mikononi mwangu na kutoka nayo nje ya chumba tulichokuwemo.


SEHEMU YA TANO
Dakika chache baadae mwalimu alirudichumbani huku akitabasamu. Uso wake ulionekana kuchangamka hivyokupelekea uchovu na hofu vilivyoonekana kumtawala mapema vijifiche. Macho yake ya rangi ya kahawia yalionekana kutabasamu na midomo yakeiliyochongeka vyema ilionekana kuyaunga macho yake mkono.

Kwakumtizama tu ungeweza kutambua kwamba alipenda kufanya mazoezi. Japohakua mwalimu wetu wa michezo karibu kila mara tulipokua na kipindicha michezo alijitahidi kujiunga nasi, na alipendelea zaidi kuchezampira wa miguu kwasababu ulimpa mazoezi ya kutosha. Kwa wakati ulealikua amevalia suruali nyeusi ya kitambaa na shati jeupe la mikonomirefu iliyokunjwa usawa wa viwiko vya mikono yake.

Vyote vilimkaasawa sawa kuendana na mwili wake uliojengeka vyema. Urefu wakeuliokaribia sentimita 180 ,ngozi yake ya maji ya kunde, mwili ambaohaukuzidi kiasi, macho , pua, midomo na masikio vilivyoutosheleza usowake vizuri vilimfanya awe mwanaume anaevutia kimuonekano.

'' Kimekufurahisha nini?'' nilimuulizapindi alipoingia huku akitabasamu. ''Ahh nimefurahi tu.'' alijibuhuku akitembea kuelekea nilipokua nimelala mimi. Nilipoona vilenilisogea nyuma kidogo kuweka nafasi ili aweze kukaa iwapo angependakufanya hivyo. Nae kama aliyeyasoma mawazo yangu alikuja na kuketipembeni huku mgongo wake akiuelekeza mlangoni hivyo tukawatumetazamana.

''Dah! Mama yako anaonekana mpole kweli, japoulishaniambia leo ndio nimejihakikishia mwenyewe.'' alisema hukuakinyoosha mkono wake wa kushoto upande wa pili ili aweze kugusamkono wangu uliowekewa dripu.

''Vipi kwani?'' niliuliza nikiwa nashauku ya kujua walichoongea na mama. ''Basi tu anavyoongea. Mtaratibu sana, sauti yake tu inajieleza. Anyway alikua nawasiwasi kweli ila nimejitahidi kumuondoa hofu. Alikua anataka kujahospitali sasa hivi nikamwambia kwamba asubiri mpaka asubuhi ilimadaktari nao wawe wamepata majibu ya vipimo.

Kaniuliza kama mara nnehivi iwapo naamini utakua sawa , baada ya kumjibu ndio akatuliakidogo.Kwahiyo kesho asubuhi watakuja pamoja na mzee, dah sijui yeyeatakua vipi.'' alipomaliza nilitamani kutabasamu ila nilipomfikiriababa nikaghairi. ''Atakua kawaida tu.'' nilijaribu kumhakikishiahuku nikiomba kimoyo moyo iwe hivyo. '

'Kwani we utakuja kesho?''nilimrushia swali bila kua na jibu maalumu nililotaka ama tamanikupata toka kwake. '' I'm not going anywhere, watanikutahapa hiyo kesho.'' jibu lake lilinishangaza kidogo maana sikutegemeakwamba angelala pale, achilia mbali kuwa tayari kuonana na mzee Fadhili asubuhi iliyofuata. Pamoja na kwamba alikua anajua kwambababa na mama walikua hawajui chochote kuhusu kile kilichotokea katiyetu nilitegemea kwamba bado angeogopa kuonana nao uso kwa uso.

Nilifikirianini ambacho kingeweza kutokea iwapo mzee Fadhili angekua anajua,sijui angeanza kumwadhibu yupi kati yetu. Mama sikua na wasiwasi naemaana siku zote alikua mtaratibu na hakuwahi hata kunichapa. Alichoweza ni kunigombeza tena pale tu alipoona ulazima wa kufanyahivyo. Mzee Fadhili nae japo aliwahi kunichapa mara moja tu baada yakupita kwa wenzangu kucheza na kudanganya nilitumwa na mwalimu. Hakuamtu wa kuchezea hata majirani walilifahamu hilo hivyo aliheshimika aulabda aliogopeka kwa wengi.

Kwajinsi nilivyomfahamu baba nilifikiria kwamba labda angeanza na mimikwasababu ndie mwanae, au labda mwalimu kwasababu yeye ndie aliyekuamtu mzima hivyo alipaswa kujua kwamba halikua wazo zuri kua namahusiano na binti mdogo tena ambae bado anasoma. Binafsi nilijilaumumwenyewe kwa kiasi kikubwa kwasababu hakunilazimisha kua nae. Alinivutia na kunipendeza machoni pia moyoni hivyo nikamkubalia, kamakilichotokea siku ile kisingetokea nadhani bado ningeendelea kumuonakama malaika aliyetumwa kunilinda na kunipa furaha maana ndichoalichokua akifanya mwanzo.

''Vipi mbona unaonekana uko mbali sana kimawazo?'' mwalimu aliniuliza.''Basi tu, nafikiria mitihani.Sijui itakuwaje.'' nilimjibu japo sichonilichokua nikifikiria kweli. ''Wala usifikirie sana. Youwill do just fine. Binafsi sinawasiwasi na wewe kabisa, najua utafanya vizuri kama kawaida yako piamarafiki zako wale. Watu wa kuwaonea huruma ni kina Shaban , Zulpha ,Shukuru na washika mikia wenzao.'' kama ada yake alinipa moyo natukaishia kucheka kidogo kwa pamoja baada ya kukumbuka vitukowalivyokua wanafanya shuleni hawa washika mikia.

Ni kama vilehawakuja shuleni kujifunza au labda wenyewe walijua kwamba hawawezikujifunza chochote hivyo hawakuhangaika . Badala yake mara nyingiwalikua wakiishia matatizoni kwa yale waliyokua wakiyafanya. Binafsisikuwa na wasiwasi na mitihani hata chembe, nilikua nimejiandaa vyakutosha hivyo niliamini nitafanya vizuri. Nilichoogopa tu ni kuumwawakati wa mitihani, hivyo nilifumba macho na kumwomba Mungu kimyakimya aniepushie mbali hicho kilichokua kinaninyemelea.

Baadae tulisikia mlango ukigongwa na daktari akaingia baada ya mwalimukuitikia. ''Dr. karibu.'' mwalimu alimkaribisha huku akiinuka kutokapale alipokua amekaa na kusimama wima.''Anaendeleaje bibie?''aliuliza huku macho na mikono yake vikiwa bize na dripu niliyokuanimetundikiwa. '' Kichwa kimepungua kidogo ila najihisi mzitokweli.''

''Hiyo kawaida kabisa. Muhimu sasa upate maji ya kutosha nakitu cha kula alafu upumzike.Sawa? Kesho tutajua kwa uhakika ninikinaendelea kwenye hako kamwili kako.'' wakati anasema hayo hukuakitabasamu mkono wake ulikua tayari ukigusa paji langu la uso.

Kusema ukweli sikuwa nimekula kitu tokea mchana ila sikuhisi njaawala hamu ya kula. ''Yeahh unatakiwa ule.Ngoja nikakuangalizie kituhapo nje.'' alidakia mwalimu. ''Mi sisikii njaa bwana.'' nilijibukwa kudeka. ''We siumesikia Dr. alichosema lakini?Unatakiwa ulekitu ili mwili uwe na nguvu.'' kwa jibu lake hilo nilijua sinaujanja.

''Ahhh basi niletee halfcake na maziwamtindi.'' nilisema nilichoona kingefaa mimi kula kwa wakati ulebaada ya kufikiria kidogo. ''Poa nakuja sasa hivi.'' Waliongozana nadaktari kwasababu nae alikua amemaliza kufanya kilekichomleta.Aliahidi kwamba atamtuma nesi aje kuniangalia tena baadae,na iwapo litatokea tatizo au mabadiliko yoyote yale mwalimuamjulishe.


Mwalimu alirudi akiwa na mfuko mdogo mkononi.Alitoa halfcake mbili alizonunua, maziwa ya mtindi na soda mbili aina ya fanta. Japo sikuagizakitendo cha kuiona pale kilinifanya niitamani hivyo nikamuuliza kamaningeweza kuinywa kwa wakati ule. ''Sure! Nilijua tu utataka maana wewe na fanta utadhani umelogewa .'' alisema hukuakifungua kwa kutumia meno yake kisha akaiweka mezani.

Nilitabasamukwasababu ilionyesha ni kwa kiasi gani alikua akinifahamu. '' Sasainabidi uinuke kidogo maana huwezi kunywa ukiwa umelala hivyo.''Alichukua mto mwingine kutoka kwenye kile kitanda cha pili na kurudinao nilipokua mimi.

Akaweka mkono wake wa kulia shingoni na kuniuunuajuu kidogo kisha akatumia wa kushoto kuniweke mto mwingine wa ziadauliofanya kichwa changu kiinuke juu bila mimi kuamka. Kwasababusikuweza kutumia mikono yangu yote miwili alinipa soda nikashikamwenyewe kisha akanilisha halfcake moja. Nilipomaliza aliniuliza kamaningependa kuongeza ila nikakataa, akachukua moja iliyobaki naeakala.

Baada ya kula tuliongea kidogo, kuhusu nini sikumbuki maanausingizi ulianza kuninyemelea kwa mbali. Kabla sijapotelea kabisaniligundua kwamba mkojo uliokua umenibana muda wote ungenizidia usikuhivyo nilimwambia kwamba nilihitaji kwenda kujisaidia.

Akatoka nakurudi na nesi mama mtu mzima aliyefunga ile dripu kwa muda kishaakachomoa ule mrija toka mkononi na mwangu kabla ya kunisindikizauani. Niliporudi akarudisha kila kitu kama kilivyokua kisha akaondoka.
Mwalimu akanibusu kwenye paji la uso kisha nikalala.


SEHEMU YA SITA
''Zawadi, Zawadiiii'' ndio maneno yaliyoniamsha asubuhi ya pili.Nilifumbua macho yangu taratibu na kivivu ili kujua aliyekua ananiamsha ni nani. Mama alikua ameinama akinitazama usoni huku mkono wake mmoja ukiwa umenishika begani.

''Mama, shkamoo.'' nilimsalimu kwa sauti ya chini huku nikifumba macho yangu tena. ''Marahaba mwanangu, unaendeleaje?'' aliuliza bila kuondoa mkono wake begani mwangu. ''Nafuu mama! Umekuja na baba?'' swali hilo lilinitoka kabla sijayafumbua macho yangu na kuyaangaza mle chumbani kuona kama baba alikuwapo.

''Nimekuja nae ila yupo hapo nje anaongea na sijui ndo mwalimu wako yule.Alafu ilikuaje yeye ndo aliyekuleta hospitali , mashoga zako nao wako wapi?'' japo aliuliza kwa sauti ya utaratibu kama kawaida yake nilihisi shauku ya udadisi ndani yake.

Nilifikiria kwa sekunde kadhaa nimjibu nini kisha nikamjulisha kwamba niliwaomba watangulie tulipotoka shule na ningeungana nao baada ya kuongea na mwalimu kuhusu mitihani tuliyokua tukitarajia kuanza jumatatu, na nilipokua naongea na mwalimu ndipo nilipoanguka. ''Ahhhh ndo matatizo ya kutokua na pesa haya. Ungeshatibiwa tangu unaanza kujisikia vibaya haya yote yasingetokea.''

Jibu lake lilionyesha kuridhishwa na langu, ila lilinifanya nijihisi kama mkosaji kwa kumfanya mama ajione kama mzazi asiyeweza kutosheleza mahitaji ya mwanawe, hata pale anapokua mgonjwa. Nilitamani kutoa maneno ya kumfariji ila kabla sijafanya hivyo mlango uligongwa na kufunguliwa mara hiyo hiyo.

Wa kwanza kuingia alikua baba aliyekua amevalia kama ambavyo hua anavaa siku zote akielekea kwenye shughuli zake , kaptula, shati na ndala chakavu kiasi. Bila kusahau kofia yake chakavu aliyotumia kujikinga na jua. Japo kua ilikua imetoboka sehemu kadhaa juu na pembeni bado aliivaa kila siku. Rangi yake ya kijani ilikua imefifia kana kwamba ilikua imedumbukizwa kwenye jiki kwa nia ya kupoteza rangi yake ya awali.

Nyuma yake alifuatiwa na mwalimu kisha daktari yule mrembo aliyenihudumia jana yake.''Hujambo mama?" alinisalimu baba kabla sijatoa shikamoo niliyokua najiandaa kumpa. "Salama tu shikamoo baba!" nilimjibu huku nikimtazama ili niweze kumsoma alikua katika hali gani. Uso wake ulionyesha kuchoka kama ulivyokua wa mama ila alijitahidi kutabasamu hivyo nikajua alikua sawa.

Mwalimu yeye alisimama karibu kabisa na mlango huku akimtazama daktari ambae kwa wakati ule alikua akinipima. "Mrembo naomba uvute hewa ndani kwa sekunde chache kabla ya kuiachia kisha usubiri tena kwa sekunde chache kabla ya kuvuta tena ndani." maagizo hayo ya daktari yaliambatana na mkono wake mmoja ukisogeza kifaa chake kila kona ya kifua changu upande wa kushoto huku mwingine ukiwa umekishikilia kilipoishia sikioni mwake.

"Mapigo ya moyo yako normal, sasa ngoja niongee na wazee kidogo .Nikirudi nikute bado unapumua ehhhh!!!." aliniambia mimi uso wake ukiwa umejaa tabasamu lililoonyesha meno yake meupe yaliyojipanga vyema kabla ya kugeuka walipokua wamesimama baba na mama na kuwaomba wamfuate. "Kama hamtojali naomba twendeni ofisini tukaongee kidogo."


SEHEMU YA SABA
Kwa dakika nilitamani ningekua na uwezo wa kusoma mawazo ya baba nikajua nini kilikua kinaendelea kichwani kwake. Maana aliyofanya pale wodini yalikua nje ya matarajio yangu kabisa na hata nilipojaribu kufikiria nini kilichosabisha kile nilichoshuhudia sikufanikiwa. Nilidhani labda amechanganyikiwa, lakini hakuonekana kama mtu aliyechanganyikiwa bali mtu mwenye hasira zisizodhibitika.

Pamoja na kwamba baba hakusema neno baada ya zile purukushani hasira zake haziokuonekana kupungua. Wale waliomshika walimuomba watoke nje kidogo nae hakukataa. Akanitazama kwa jicho kali kisha akaongozana nao na kutoka nje ya wodi tuliyokuwamo.

Kitendo cha kubaki pale chumbani mwenyewe hakikunipa unafuu bali kilinifanya niogope kile kilichokua kikiendelea. Nilitamani mtu mwingine aje mle ndani ili nijuzwe kilichokua kinaendelea ila haikua hivyo. Mawazo ya kuchomoa dripu niliyokua nimechomekewa mkononi mwenyewe ili nitoke nje yalinijia ila sikuthubutu.

Sehemu ya 7 inaendelea hapa
Zawadi sehemu ya 7


Itaendelea.....
 
ahsante saaana lizzy,mimi ni mpenzi mkubwa sana wa hadithi.za shigongo,huwa hazinipiti.naisubiri kwa hamu
 
Kisukari bana hii sio ya Shigongo, ni ya Lizzy mwenyewe.

JB usione uvivu maana huo ndo kwanza mwanzo!!Subiri subiri nifike katikati.

Jestina vitu vinakuja mwaya.

FB najaribu jaribu dear. Ngojea mwisho kabla ya kutoa hongera usije ukaninyanganya bure!
 
Hakuna kulala hii ndio mida ya wezi, kwangu wameshanizowea wanajuwa nalala macho, kila wakipita wanaona taa ndani inawaka na sauti ya keyboard, kwahiyo swala wizi nimelizibiti kwa njia hii.
Mhh matola, hulali tena. au kwa ajili kesho ni jpili?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom