Zanzibar: Watumishi 11 mbaroni kwa kujipatia fedha wakitoa vyeti feki vya Chanjo ya Corona kwa Wasafiri

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,499
9,279
MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) inawashikilia watu 11 wakiwemo wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa kutengeneza vyeti bandia vya chanjo ya Covid-19 kwa watu mbalimbali wanaosafiri kwenda nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Zaeca, Ahmed Khamis Makarani akizungumza na waandishi wa habari jana alisema jumla ya vyeti bandia 548 wimetolewa kwa wasafiri wa nje ya nchi.

Makarani alifahamisha watumishi waliokamatwa ni kutoka katika Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto makao makuu Mnazimmoja pamoja na watumishi wa kitengo cha chanjo ya Covid-19 mjini Unguja.

Wafanyakazi wengine waliokamatwa kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ni kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Kitengo cha Ukaguzi wa Wageni wanaoingia nchini pamoja na sekta ya utalii.

Makarani alisema watumishi hao walikuwa wakitengeneza vyeti bandia vya chanjo ya Covid-19 na kuwapatia wageni na watu wengine wanaosafiri kwenda nje ya nchi na kujipatia fedha.

Alisema matukio kama hayo yaliwahi kujitokeza katika siku za nyuma kwa baadhi ya watu kusafiri nje ya nchi baada ya kupatiwa vyeti feki vya chanjo ya Covid-19 na kusababisha kuibuka kwa malalamiko.

“Tunawashikilia watu 11 ambao ni watumishi wa serikali katika Wizara ya Afya pamoja na vitengo vyake vinavyotoa chanjo ya Covid-19 kwa uchunguzi ambapo watumishi hao walikuwa wakitengeneza vyeti bandia kwa watu wanaosafiri nje ya nchi na kujipatia fedha kinyume cha sheria,” alisema mkurugenzi huyo.

Akifafanua zaidi alisema watendaji hao walichokuwa wakikifanya ni kuingilia mtandao wa mfumo wa kutengeneza vyeti vya Covid-19 uliokuwa halali na kuuvunja baada ya kupata alama za siri za utengenezaji wa vyeti hivyo.

Baadhi ya wafanyakazi wanaoshikiliwa ni Hassan Vuai Hassan mkazi wa Kwarara mfanyakazi sehemu ya Maabara, Yassir Said Ali mfanyakazi wa taasisi binafsi ya ZACP Kitengo cha Covid-19, Jamali Abbasi Abdallah mfanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume pamoja na Mohamed Juma mfanyakazi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar.

Wengine ni Asya Gharib Haji mfanyakazi sehemu ya Maabara na Arafa Abdi-Hakim mfanyakazi wa Kitengo cha Covid-19.

Mapema Makarani alisema Zaeca inaendelea kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi la kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili wafanyakazi wa Shirika la Umeme (ZECO) la kuchukua fedha za kuwaunganishia wananchi umeme bila ya kupata huduma hiyo.

Chanzo: Habari Leo
 
Back
Top Bottom