Zanzibar: Siku 100 za utawala wa Rais Mwinyi, mafanikio na changamoto

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,796
11,959
Wiki chache baada ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuingia madarakani, kulishuhudiwa sherehe kadhaa zisizo rasmi, watu wakipika na kula, wakifurahi na kucheza kwa dufu. Hawakuwa wanafurahia ushindi wake, bali uamuzi wa kutowarudisha wizarani baadhi ya mawaziri wenye historia zenye ukakasi katika macho ya Wazanzibari.

Wakati huu ambao baadhi ya Masheha wameondoshwa katika nafasi zao vilevile, sherehe zimezuka tena. Namna ni ile ile, kupika karamu na watu kula.

Ni wazi kwamba kuna watendaji wa serikali hawakuujenga vizuri uhusiano wao na wananchi. Kwa kutumia vibaya nyadhifa zao. Ndio maana kuondoka kwao ni vifijo na nderemo kwa jamii.

Rais Mwinyi amezisuuza roho za wengi kwa maamuzi yake. Zilisuuzika zaidi ilipobainika kaandika barua kwa Chama cha ACT Wazalendo, akikikaribisha katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Barua ile ilikuwa ni ishara ya wito wa maridhiano ya kisiasa, yatakayozalisha ahueni na mshikamano katika jamii ya Wazanzibari. Maridhiano yaliyoondoka tangu uchaguzi wa 2015.

Kusikiliza changamoto
Utawala wake umeingia madarakani na mbinu ya kusikiliza changamoto za sekta mbali mbali. Mikutano maalum ya ndani huandaliwa kuwasikiliza wadau na wafanyakazi wa sekta hizo.

Imefanyika katika sekta ya biashara, elimu, afya na bandari. Pia amekutana na viongozi wa kidini. Fauka ya hayo, amekutana na wadau na wanaharakati kuzungumzia tatizo sugu visiwani Zanzibar, udhalilishaji wa watoto.

Changamoto zinazoibuliwa katika mikutano zinadhihirisha uwajibikaji mdogo wa utawala uliopita. Kwa tafsri pana; hakukuwa na ufuatiliaji kuhusu kipi kinakwenda vipi. Na lipi limekwama wapi na kwa nini.

Kuisafisha SMZ
Ni mapema kusema kafanikiwa katika uongozi wake. Ingawa si mapema kusema kaanza vizuri siku zake mia moja za mwanzo kuiongoza nchi hiyo.

Ni kasi inayofanana na ile ya Rais John Pombe Magufuli. Ziara za kushtukiza. Amezifanya katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na Bandari kuu ya Malindi.

Kumeshuhudiwa kuenguliwa na kuteuliwa sura mpya katika serikali yake. Kusimamishwa kazi baadhi ya watumishi wa Umma ili kupisha uchunguzi.

Kauli yake mbiu husema, "sitofukua makaburi." Akiwa na maana hana mpango wa kuwaandama watumishi kwa matendo yao ya nyuma, ingawa kaahidi hatokuwa na muhali kwa yatakayotendwa ndani ya utawala wake.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Chande Omar, ni mtumishi wa karibuni zaidi kukumbana na panga la utawala wa Rais Mwinyi. Ameondolewa baada ya ripoti ya kamati ya uchunguzi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, kamati hiyo imebaini ukiukwaji wa sheria na taratibu za nchi ikiwemo kuajiri wafanyakazi wasio na sifa katika shirika hilo.

Pia ripoti iliyowasilishwa katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, imesababisha maafisa kadhaa wa vikosi vya SMZ kusimamishwa kazi kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za Umma.

Utumbuaji wa aina hii ni jambo jipya katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Wabadhirifu walipeta kwa sababu ya ile tabia ya Kizanzibari, "kuoneana muhali". Watawala walishindwa kuwawajibisha hata wale watumishi waliowateuwa wenyewe.

Rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya pesa za Umma, ubaguzi katika utoaji wa ajira ni kati ya machache yaliyotamalaki kwa awamu tofauti ndani ya SMZ.

Sio kwamba huko nyuma hayakujuulikana kwamba yapo. Tofauti ya utawala huu na zilizopita, utawala wa Dkt. Mwinyi umeamua kuyaibua madudu na kuyaweka hadharani.

Kupambana na mila na siasa za kihafidhina
Kairithi nchi ikiwa katika mila za ajabu sana. Zenye kila sura ya upendeleo, chuki na kuendesha mambo kwa kujuana.

Chukua mfano hai. Unaposikia ripoti ya uchunguzi imebaini ZBC inatoa ajira kwa watu wasio na sifa. Hili ni jambo lililozoeleka katika sekta nyingi za SMZ, watu hupewa ajira kwa sababu ya kadi zao za chama, ama kwakuwa familia zao ni wakereketwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Siasa zenye itikadi za kihafidhina kutoka kwa baadhi ya makada wa CCM visiwani, kwa miaka mingi zimechochea pakubwa chuki na ubaguzi.

Dkt. Mwinyi anaonekana kuzipa mgongo mila na siasa za aina hiyo, hilo huenda likamletea upinzani usio wa wazi kutoka kwa vigogo wa CCM waliokuwa wananufaika na uwepo wa mambo hayo kwa miaka mingi.

Jambo analoweza kujivunia hadi sasa, ni uungwaji mkono kutoka kwa wananchi wa Zanzibar. Kuna kila dalili raia wanazitazama juhudi zake kwa jicho la matumaini bila kujali mirengo yao ya kisiasa.

Changamoto zinazomkabili


Ukuaji wa uchumi na kupatikana kwa unafuu wa maisha ya raia, daima ni mizigo kwa kiongozi yeyote yule. Dkt. Mwinyi anakabiliwa na mizigo hiyo pia, kuhakikisha anayaboresha maisha ya Wazanzibari kwa miaka yake mitano.

Chini ya kauli mbiu ya utawala wake, "uchumi wa buluu," atakuwa na kazi ya kuleta matokeo chanya ya msemo huo. Vita vyake dhidi ya ufisadi na mambo yote yaliyokuwa yakiumiza nchi, haviwezi kuwa vita vitupu visivyo na mafanikio.

Kwa faida ya amani ya Zanzibar kwa siku za usoni, anakabiliwa na changamoto ya kuzisafisha taasisi muhimu kama Vikosi vya Usalama hasa vya SMZ na Tume ya Uchaguzi.

Taasisi hizo huchangia pakubwa kuingiza Zanzibar katika mitafaruku wakati wa uchaguzi, kwa sababu mara nyingi hushindwa kusimama katikati, huishia kukaa upande wa chama tawala.

Rais Mwinyi ana nafasi nzuri ya kuleta mageuzi katika sekta hizo sugu kwa sababu hana kambi, kwa maana ya makundi. Timu mpya ya viongozi wanaonekana kuwa na ari ya kuungana naye kuleta mabadiliko.

Safari ya uongozi wake sio fupi, haijafika hata mwanzo wa mwisho. Illa siku mia za mwanzo zimetoa mwanga wa matumaini kwa Wazanzibari wengi.
 
Apambane bei karafuu kuwapa nafuu pembejeo wakulima walime tena kwa wingi. Boresha sana biashara pia zbar iwe bandari huru na kodi nafuu.
 
Na aimarishe muungano sana kwa kushughulikia kero zilizopo. Miaka 50 au 100 ijayo kunaweza kusiwe na huto tuvisiwa na nyote mkaishia kuhamia bara. Msipuuzie Muungano

Screenshot_20210208-105628_US%20Newspapers.jpg
 
Ni lazima alishuhulikie suala la masheikh waliowekwa vizuizini bara kuonesha kuwa kweli yeye ni Rais wa Zanzibar! Awe jasiri kuthibiti mapato yanayotokana na watalii wanaokuja Zanzibar; Wengi wao hasa wa kutoka Italy wanalipia huduma zao huko kwao na kuja huku ambako wanatumia fedha kidogo sana hivyo Zanzibar haifaidiki na mapato kutokana na watalii hawa!!! Ni kazi ngumu kuthibiti ufisadi huu kwani unawashirikisha watu wazito wengi hapo visiwani.
 
Staili yake ya uongozi inaendana na JPM sema sasa yeye hawabani mafisadi ili watapike mabilioni kama alivyojinasibu JPM sasa sjui pesa za miradi mikubwa atatoa wapi kama hafukui makaburi!
 
Back
Top Bottom