Zanzibar 2020 Zanzibar: Maalim Seif akamilisha Awamu ya Kwanza ya kampeni Pemba

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
674
1,000
Na MWANDISHI WETU, PEMBA
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amekamilisha awamu ya kwanza ya ziara yake ya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Visiwa vya Pemba na sasa anaelekeza nguvu zake Unguja.

Awamu hiyo ya kwanza iliisha jana (Ijumaa) Septemba 18, 2020, ambapo alifanya mikutano mitano ukiwamo ule wa ufunguzi wa kampeni.

Taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Abeid Khamis Bakar Leo Septemba 19,2020 ilisema Maalim Seif licha ya kufanya kampeni za majukwani, aliweza kufika katika maeneo ya wananchi na kujionea shughuli zao za kimaisha.

Ilisema mgombea huyo wa ACT-Wazalendo alitembelea maeneo ya kilimo cha mboga mboga, Mwani, wavuvi, wafugaji wa kuku pamoja na wafanyabiashara wa maduka mbalimbali.

“Wananchi wengi walionekana kuvutiwa sana na kitendo hicho na kueleza kuwa ni moja ya njia ya kuelewa matatizo ya wananchi pamoja na nini kinahitajika katika kuendeleza kazi zao hizo.

“Akiwa katika vikundi hivyo, Maalim Seif aliwaomba wananchi wampigie kura Oktoba 28, 2020 na yeye atahakikisha changamoto ambazo zinawakabili anazitatua zote ndani ya miezi sita ya mwanzo ya utawala wake.”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Abeid alisema Maalim Seif akiwa katika kikundi cha uzalishaji nyanya kilichopo katika Kijiji cha Ziwani Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba aliahidi kuwapatia meshine za umwagiliaji maji ili iwe rahisi katika kuendeleza kilimo hicho na wakulima nao kupata faida yenye tija.

Pia alisema wakulima wengi wa mboga mboga Pemba hali zao si nzuri kiafya kutokana kukosekana kwa vifaa vya umwagiliaji na kueleza kuwa wakulima wanatumia nguvu kubwa kubeba ndoo za maji vichwani ili kuhami kilimo chao.

Kuhusu zao maarufu la Mwani, mgombea huyo wa Urais aliwaambia wakulima hao ambao hutumia bahari kufanya kilimo hicho kuwa atahakikisha wanapata boti (vihori) vya kulima Mwani mnene ambao hulimwa katika maji mengi na huuzwa kwa bei ya Sh 15000 kwa kilo katika soko la dunia.

“Wazalishaji wengi wa mwani Zanzibar hulima mwani mwembamba kutokana na ukosefu wa vitendea kazi, mwani ambao bei yake haizidi Sh 1000,”alisema.
Aidha akiwa katika Mifugo ya kuku huko, Mtambile Wilaya ya Mkoani Pemba Maalim Seif alipokea changamoto nyingi zinawakabili wafugaji ikiwemo bei za vyakula vya kuku pamoja na upatikanaji wa madawa jambo ambalo husababisha kuku kupoteza maisha au kuchelewa kutoa tija kwa mifugo hiyo.

Wafanyabiashara ya maduka eneo la Kiungoni Mkoa wa kaskazini Pemba walimueleza Maalim Seif kuwa kitu pekee ambacho Serikali inafanya kwao ni kuchukua kodi tu.

“Hapa tunalipa kodi za majengo, tunalipa leseni ya biashara, tunalipa kodi ZRB pamoja na pesa ya usafi kwa baraza la mji, kilio chetu kikubwa ni kwamba hali ya maisha ni ngumu, wateja hakuna, bidhaa zinaharibika madukani".

Akizungumzia hali hiyo, Maalim Seif alieleza kushangazwa kwakwe na hatua ya serikali ya SMZ kujali zaidi mapato kutoka kwa wafanyabiashara, lakini hawawatengenezei mazingira mazuri ya ufanyajibiashara hizo.

“Ninaahidi katika Serikali yetu itakayoongozwa na ACT-Wazalendo tutawapa kipaumbele wafanyabiashara wa hali zote".

Katika mikutano yake yote kisiwani Pemba, Maalim Seif alirudia kauli yake ya mara kwa mara kuhusu umuhimu wa vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Bara (NEC) kutenda haki sawa kwa vyama vyote kwani ikikosekana haki amani nayo itakuwa shakani.

Alisema wananchi wengi wamenyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambacho ndio kinampa ruhusa ya kupata shahada ya kupigia kura Zanzibar.
“Tunatuma salamu kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuhusu upigaji wa kura ya mapema ya tarehe 27 Oktoba.

"Tunajua suala la upigaji kura ya mapema si chochote bali una ni nia ovu ya Tume ya Uchaguzi kutaka kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake wa urais, lakini tunasema wazi kama ni kura ya mapema tutakwenda kupiga wote". alisisitiza Maalim Seif.

Leo Septemba 19, 2020 Maalim Seif atakuwa katika majimbo ya Unguja kuanzia saa 8:00 mchana mpaka saa 12 jioni akiwakutanisha wananchi wa majimbo ya Kikwajuni na Jang'ombe katika Uwanja wa Alabama.
.
 

Automata

JF-Expert Member
Mar 3, 2015
2,511
2,000
Bila huruma ya ZEC Sultan Seif kampeni angelikuwa anaziona kwenye TV - zikifanywa na wenzie
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom