Zanzibar imepewa nguvu kubwa - Zitto; Ahofia mabavu ya dola kuteka mamlaka ya wananchi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Zanzibar imepewa nguvu kubwa - Zitto; Ahofia mabavu ya dola kuteka mamlaka ya wananchi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Nov 10, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Nov 10, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  [h=1][/h]
  Muswada wa Katiba mpya


  Mwandishi Wetu


  Ahofia mabavu ya dola kuteka mamlaka ya wananchi


  MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ametoa maoni yake kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Katiba mpya, unaotyarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano ulioanza mapema wiki hii bungeni mjini Dodoma. Ili kufahamu zaidi kuhusu maoni ya Zitto, endelea kusoma makala haya.
  KAMA kuna jambo moja ambalo huunganisha Taifa ni Katiba ya Taifa hilo. Katiba huweka misingi mikuu ya nchi na namna ya kujenga na kuendesha Taifa. Hivyo Katiba inapaswa kuwa ni matokeo ya mwafaka wa kitaifa kwenye masuala yote ya msingi ya nchi husika. Tanzania imekuwa ikiongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara. Kabla ya hapo kulikuwa na Katiba ya Uhuru ambayo ilitokana na mwafaka wa wapigania Uhuru wa nchi yetu, baadaye Katiba ya Jamhuri ya Tangayika na kisha Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kabla ya kubadili jina na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


  Ukiachana na Katiba ya Uhuru, Katiba nyingine zote hazikutokana na mwafaka wa kitaifa bali matakwa ya tabaka la watawala. Katiba ya kudumu ya mwaka 1977 ni zao dhahiri kabisa la utawala wa chama kimoja ambacho kilikuwa na dhamira ya kushika hatamu za uongozi. Kutokana na hali hii haikuchukua muda kwa wasomi mwaka 1983 kuanza harakati za kuifanyia mabadiliko makubwa. Kati ya matokeo ya mabadiliko hayo ni kuwamo kwa Haki za Msingi za Binaadamu katika Katiba katika mabadiliko ya mwaka 1984, miaka saba tu tangu kuandikwa kwa Katiba ya kudumu.

  Takribani mwaka mzima huu kumekuwa na madai ya kuandikwa kwa Katiba mpya. Madai haya si mapya kwani huibuka na kusinyaa kila baada ya Uchaguzi Mkuu. Itakumbukwa kwamba mwishoni mwa miaka ya 1990 kundi la vyama vya siasa liliunda Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (KAMAKA) ili kudai kuandikwa kwa Katiba mpya.


  Hata hivyo, safari hii sauti ya mabadiliko imekuwa ni kubwa sana kiasi cha Serikali kusikia na hivyo kupeleka bungeni muswada wa Marejeo ya Katiba kwa lengo la kuandika Katiba mpya ya nchi yetu. Muswada huu umeleta kelele nyingi na manung’uniko mengi sana kutoka kwa makundi mbalimbali ya jamii kuanzia vyama vya siasa, viongozi wa dini na Asasi za Kijamii. Baadhi ya Asasi za Kijamii zimeunda Jukwaa la Katiba ili kuweza kuratibu vizuri juhudi za kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


  Sababu kubwa ya kupingwa kwa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ni kwamba mchakato umewekwa kwenye Dola mno na hasa kwenye Urais. Rais anateua tume ya kukusanya maoni, Rais pia ndiye anateua Bunge la Katiba. Watu wengi tungependa kuona mchakato unakuwa kwa wananchi zaidi. Serikali imefanya marekebisho kadhaa na kupanua wigo wa mjadala wa Katiba na pia kumhusisha kikamilifu Rais wa Zanzibar katika mchakato.


  Baadhi yetu tunaona kama nafasi ya Zanzibar katika mchakato imepewa nguvu kubwa kupita kiasi. Nadhani Zanzibar inastahili kupata nafasi hii katika mchakato wa Katiba. Jambo ambalo ni vizuri tulitilie maanani ni kwamba Muungano wa Mwaka 1964 ulihusisha nchi mbili huru zenye hadhi sawa mbele ya sheria za kimataifa. Linapokuja suala la kuandika Katiba ya Muungano, pande mbili za Muungano zinakuwa na hadhi sawasawa. Kwamba Zanzibar ishiriki kwenye masuala ya Muungano tu ni hoja inayojadilika iwapo tu Katiba ya Muungano ingetofautisha kinagaubaga taasisi za kimuungano na zisizo. Kwa mfano Sura ya Bunge katika Katiba ni lazima ijadiliwe na pande zote mbili ingawa Bunge wakati mwingine hupitisha miswaada ambayo si masuala ya Muungano. Aina ya Muungano wetu inatulazimisha kufanya hivi tunavyofanya sasa. Mkataba wa Muungano ni lazima uheshimiwe kama ulivyo sasa.


  Katiba mpya yaweza kuweka makubaliano mapya lakini muswada wa sasa ni lazima utambue nafasi halali ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya sasa na Hati za Muugano. Suala hili ni la kisheria na sio suala la idadi ya watu au ukubwa wa eneo la nchi husika. Nchi ya Ushelisheli yenye watu 80,000 ina nafasi sawa na Tanzania yenye watu 42 milioni katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN). Zote zina kura moja tu. Huu ndio ukweli na hatuna budi kukubaliana nao.


  Muswada unampa mamlaka Rais wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar kuteua Tume ya Katiba. Tume hii ma-Rais hawatapata ushauri wa mtu mwingine yeyote kwa mujibu wa kifungu cha (6) na vifungu vidogo (1), (2) na (3). Wanasiasa wakiwamo wabunge, wawakilishi, viongozi wa vyama ngazi za taifa, mkoa au wilaya hawatakuwa na sifa za kuteuliwa.


  Inawezekana kabisa waandishi wa muswada walikuwa na mantiki ya kuuondoa mchakato kwenye mikono ya wanasiasa. Nia hii njema haikufikiriwa vizuri hata kidogo. Njia hii haijengi mwafaka. Tume hii sio ya wataalamu, ni tume inayopaswa kuwa na sura ya kitaifa. Nafasi ya wanasiasa katika mchakato wa kukusanya maoni ni muhimu sana katika kuhalalisha mchakato wenyewe. Tume lazima ionekane ni Tume ya Taifa na sio Tume ya ma-Rais. Hivyo kipengele hiki cha kuwanyima sifa wanasiasa kinapaswa kufutwa katika muswada. Wabunge na wawakilishi kwa kuwa ni sehemu ya Bunge la Katiba wasiwemo katika tume, lakini viongozi wengine wa kisiasa wawe na haki ya kuteuliwa kuwa wajumbe.


  Lakini pia Rais ateue Tume kutokana na maoni kutoka katika makundi yenye maslahi ya karibu na Katiba ya nchi na hivi ni vyama vya siasa.

  Ninapendekeza kwamba katika wajumbe 30 wa tume ya kukusanya maoni ya Katiba, 10 watokane na vyama vya siasa vyenye wabunge kwa uwiano wa CCM wawili, CHADEMA wawili, CUF wawili, NCCR wawili, TLP mmoja na UDP mmoja. Kila chama cha siasa chenye wabunge kupitia kiongozi wake bungeni kipeleke majina ya watu wanaowapendekeza kuwa katika Tume ya Katiba na kutokana na mapendekezo hayo, Rais atawateua kuwa wajumbe. Masharti mengine ya nusu kutoka kila upande wa Muungano yazingatiwe.


  Muswada unapendekeza kuwapo kwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume. Kifungu cha cha saba kifungu kidogo (1), (2) na (3) kinaweka utaratibu wa kupatikana kwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume. Muswada unasema uteuzi wa mwenyekiti na makamu utazingatia kwamba mmoja atoke upande mmoja wa Muungano na mwingine upande wa pili wa Muungano. Ingawa muswada hausemi waziwazi lakini ni dhahiri kwamba mwenyekiti wa tume atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar. Sitaki kujenga hoja kwamba mwenyekiti na makamu wachaguliwe na wajumbe wa tume kutoka miongoni mwao lakini ni dhahiri mwenyekiti wa tume anapaswa kuwa mtu mwenye heshima kubwa hapa nchini. Ningependekeza kwamba ma-Rais wateue wenyeviti wenza badala ya mwenyekiti na makamu wake ili kuweka nafasi sawa kwa pande mbili za Muungano. Hapa nchini tunao Watanzania ambao wamefanya kazi iliyotukuka katika nyadhifa mbalimbali na sasa ni wastaafu wasio na nia yoyote ya madaraka ya kisiasa wanaoweza kuongoza vizuri kabisa tume hii. Ni mapendekezo yangu kwamba Dk. Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Sinde Warioba wawe wenyeviti wenza wa Tume ya Katiba. Uzoefu wao katika uongozi na kuijua kwao nchi kutasaidia sana kuhakikisha kwamba mchakato wa kukusanya maoni na kisha kuandika Katiba unakuwa na mafanikio kwa kuzingatia misingi ya taifa letu.


  Muswada unapendekeza kwamba hadidu rejea za tume zitolewe na ma-Rais. Kifungu cha nane cha muswada kuhusu hadidu rejea nadhani hakina mantiki sana. Madhumuni ya muswada yanasema pamoja na mambo mengine muswada unaweka masharti kuhusu hadidu rejea za tume. Wakati huo huo muswada unasema hadidu rejea zitakuwa ni hati ya kisheria itakayozingatiwa na tume katika kazi zake.


  Mantiki ni kwamba hadidu rejea zinapaswa kuwa sehemu ya muswada kama ‘schedule’ ili kuzipa nguvu ya kisheria badala ya tangazo katika gazeti la Serikali. Hadidu rejea zikiwa ni sehemu ya muswada zitajadiliwa na Bunge na kupitishwa hivyo kuwa ni jambo ambalo limefikiwa kwa mwafaka wa wawakilishi wa wananchi.


  Muswada unataka uamuzi wa kura ya maoni kuhusu Katiba uwe ni kukubaliwa na nusu ya Watanzania katika kila upande wa Muungano. Nadhani hapa tunacheza na Katiba ya nchi. Katiba ya nchi inapaswa kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura wa pande zote za Muungano yaani kila upande theluthi mbili. Hii itaipa Katiba uhalali (legitimacy) na hivyo kuheshimiwa na wananchi na watawala. Kuna woga gani uliopo kutaka Katiba ikubalike na nusu ya wapiga kura? Mifano ya nchi nyingi duniani Katiba inapaswa kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura. Hata jirani zetu wa Kenya ilikuwa hivyo na hata kura ya maoni kuhusu mwafaka huko Zanzibar ilikuwa hivyo. Kwa kuwa Katiba ni chombo cha mwafaka wa kitaifa, muswada utamke kwamba Katiba mpya itakuwa imepita iwapo theluthi mbili ya wapiga kura watapiga kura ya ndio.

   
 2. k

  kazuramimba Senior Member

  #2
  Nov 10, 2011
  Joined: Jun 14, 2011
  Messages: 107
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Hivi mbona watu mnakua wajinga na vilaza kiasi hiki?hivi unatuletea maoni ya huyu mnafki hapa ili yatusaidie nini?Acheni ujinga wa kukariri huyu Zitto kasha filisika kisiasa hana jipya.Ndumi la kuwili tena ni pandikizi la CCM.Anajidai anatoa maoni wakati nyuma ya pazia ni mtu hatari kuliko Rostam.Ashukuriwe Mungu kwa kuwafunua watu wanafki kama hawa kabla hawaja pata madaraka makubwa.
   
 3. GHIBUU

  GHIBUU JF-Expert Member

  #3
  Nov 10, 2011
  Joined: Jan 13, 2011
  Messages: 3,188
  Likes Received: 705
  Trophy Points: 280
  si mbaya kwa mtazamo
   
Loading...