Zanzibar: CUF yamtengua Ali Makame kwa kosa la kuwania Uspika wa Baraza la Wawakilishi

CUF Habari

JF-Expert Member
Dec 12, 2019
239
234
Screenshot_20201108-133911.png


TAARIFA KWA UMMA:

Ndugu wanahabari!

Karibuni tena kwenye Ukumbi huu wa Shaaban Khamis Mloo ambapo Leo tena tunapenda kuongea na Umma wa Watanzania kupitia kwenu.

Wiki moja iliyopita tulikutana hapa kwa ajili ya kuuhabarisha Umma juu ya Msimamo wa CUF- Chama Cha Wananchi kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar uliofanyika Oktoba 27 na 28 na ule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, tuliweka wazi Msimamo wa Chama wa kutoyatambua Matokeo ya Chaguzi zote hizo kwa ngazi zote ikiwa ni pamoja na Udiwani, Uwakilishi, Ubunge, Urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha tuliweka bayana Msimamo wetu kama Chama kwamba hatutoshiriki Uchaguzi Mkuu wowote mpaka pale itakapoundwa Tume huru ya Uchaguzi; kwamba tutaomba Msaada wa Jumuiya za Kimataifa katika kuipigania Demokrasia ya kweli hapa nchini; na kwamba tutaanzisha vuguvugu la kudai Katiba mpya itakayosimamia Demokrasia ya Kweli na Utawala Bora. Tamko letu pia liliwaomba wapenda haki na Demokrasia kote nchini kufunga siku ya Alhamisi Novemba 5 na kufanya Dua/Maombi Maalum kwa ajili ya kumshitakia Mwenyezi Mungu udhalimu uliofanywa kwenye Uchaguzi Mkuu na kumuomba apitishe Hukumu yake kwa haki na Watanzania waishuhudie Hukumu ya Mola wetu, ambaye ndiye Mungu wa Mussa aliyemshinda Firauni ( Pharaoh) bila ya kujali Nguvu alizopewa na Mungu zikampa Kiburi na Jeuri, na hatimaye kuwanusuru Wana wa Israeli, licha ya unyonge waliokuwa nao.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba Funga na Dua/Maombi vilienda vizuri na kwa sasa ni jukumu letu Kusubiri tukiwa na Yakini kwamba Mungu Mwenye Nguvu ametusikia na atatujibu. Tusiwe na haraka.

Jana Novemba 7, 2020 jioni kulikuwa na Mchakato wa Kuwachagua Spika na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, katika kukamilisha Mchakato wa Uchaguzi ambao sisi CUF- Chama Cha Wananchi tumeupinga na kuyakataa Matokeo yake.

Kinyume na matarajio ya Viongozi na wanachama wa CUF- Chama Cha Wananchi, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mheshimiwa Ali Makame Issa alikuwa ni miongoni mwa waliojitokeza kugombea nafasi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, nje ya Ridhaa ya Chama.

Mheshimiwa Ali Makame ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati Tendaji na pia ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi aliyeshiriki Vikao vilivyopitisha Maamuzi ya Msimamo wa Chama kuhusu Uchaguzi Mkuu ulioharibiwa.

Isitoshe, Mheshimiwa Ali Makame ni miongoni mwa Viongozi Waandamizi waliokuwa pamoja na Msemaji Mkuu wa Chama ( Mwenyekiti) wakati anafikisha kwenu Tamko la Chama la kutoutambua Uchaguzi Mkuu.

CUF ni Chama Cha Wananchi.

Vyovyote iwavyo, Maslahi mapana ya Taifa yanatangulizwa mbele dhidi ya Maslahi ya mtu binafsi au kikundi cha watu.

Kutokana na yaliyojitokeza Oktoba 27 na 28 kule Zanzibar, kuna wananchi kadhaa waliouawa na wapo waliosababishiwa Ulemavu wa kudumu. Wapo pia waliodhalilishwa kwa namna mbalimbali katika kufanikisha Udhalimu uliopangwa na kutendeka.

Ni dhambi kubwa sana kushiriki kwa namna yoyote na kwa kisingizio chochote katika kuhalalisha Unyama uliofanyika.

CUF- Chama Cha Wananchi kisingependa kuona yeyote katika Viongozi wake akiiga Viongozi wa vyama vingine vinavyowasaliti Wananchi kwa kuunga mkono au kushirikiana na Serikali zitokanazo na Ubakaji wa Demokrasia ili kulinda Maslahi binafsi ya Vyama hivyo au Viongozi wao.

Dhambi hii ya kusaliti maisha na damu ya Wananchi, haiwezi kuvumiliwa na CUF- Chama Cha Wananchi.


Katiba ya CUF-Chama Cha Wananchi ya 1992, Toleo la 2019 inampa Mwenyekiti wa Chama Mamlaka ya Kuteua Viongozi kadhaa ikiwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu. Mamlaka hii ya Mwenyekiti Kuteua inaenda pamoja na Mamlaka ya Kutengua Uteuzi.

Kwa kuzingatia maelezo haya, CUF- Chama Cha Wananchi kinapenda kufikisha kwa Umma wa Watanzania Ujumbe ufuatao:-

1. Chama kinawaomba radhi Watanzania kutokana na ukakasi uliosababishwa na Mheshimiwa Ali Makame Issa kwa kujitokeza kwake hadharani kugombea nafasi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar bila ya ruhusa ya Chama;

2. Mheshimiwa Ali Makame Issa amekiuka Maamuzi ya Chama na pia amejichukulia Maamuzi binafsi katika Jambo ambalo lilihitaji Baraka ya Vikao vya Chama.

Ikumbukwe kwamba hata kama Chama kingeyakubali Matokeo ya Uchaguzi Mkuu, suala la mwanachama yupi agombee nafasi ya Spika lingepitia Maamuzi ya Vikao vya Chama;

3. Kwa kuzingatia (1) na (2) hapo juu, Mamlaka ya Uteuzi ( kama ilivyofafanuliwa na Katiba) imetengua Uteuzi wa Mheshimiwa Ali Makame Issa. Hivyo Mheshimiwa Ali Makame Issa si Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zanzibar kuanzia leo Novemba 8, 2020 kupitia Barua yenye Kumb. Na. CUF/AK/DSM/MKT/06/2020 ya Novemba 8, 2020; na

4. CUF-Chama Cha Wananchi kinapenda kutoa wito kwa Viongozi na wanachama wake nchi nzima kuzidisha Nidhamu katika muda huu wa Kuipambania Demokrasia ya Kweli na Utawala wa Sheria. Nidhamu ni silaha muhimu na ya lazima ili kushinda vita hii.

Ndugu wanahabari!
Nawashukuru nyote kwa kazi nzuri ambayo siku zote mmekuwa mkiifanya kwa Maslahi mapana ya Tanzania yetu.



HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Imetolewa leo Novemba 8, 2020 na:

Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na UMMA
CUF- Chama Cha Wananchi
 
Inashangaza sana Prof Lipumba nae anaamini eti Maalim Seif alimshinda Dr Hussein Mwinyi.

Anaonekana kama hataki kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Znz kwa sababu zisizo za msingi.
 
Shetani hana rafiki, Lipumba kanyimwa wale Wabunge kumi alioahidiwa pale IKULU na Magufuli.
Siasa za kipumbavu sana hizi.
 
Lipumba tamaa zako za fisi zimesababisha yote haya! Uliamua kujiunga na shetani ukidhani ana rafiki! Yale alokuahidi Magufuli siku ile ikulu ndo mbunge mmoja? Pole sana.
 
Kwa hiyo, walicho tengua ni cheo chake ndani ya chama (Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zanzibar) na siyo uwana chama na kuchaguliwa kwake kwenye Baraza la Uwakilishi Zanzibar?

Nilitarajia au atleast nilidhani kwa kupinga matokeo ya uchaguzi wange mfukuza uwanachama na hivyo kukosa sifa ya kuwa kwenye baraza la uwakilishi Zanzibar.
 
Back
Top Bottom