ZANTEL yaona cha moto mahakamani..................

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,172
Hukumu yaitikisa Zantel

Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 15th December 2010 @ 07:45

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zanzibar Telecom Limited (Zantel), imetikiswa na pigo la kisheria baada ya kukumbana na hukumu ya kutakiwa kumlipa mfanyabiashara wa Dar es Salaam mamilioni ya shilingi.

Katika kesi Namba ya 305 ya mwaka 2007, Zantel ilishitakiwa na mfanyabiashara Haidari Y. Rashidi wa Kampuni ya Nararisa Enterprises ikitakiwa kulipa fidia ya Sh milioni 53.4 kutokana na kusitisha mkataba wake wa kuiuzia viyoyozi kampuni hiyo ya simu.

Hata hivyo, baada ya mvutano wa kisheria katika mahakama nchini, iliamriwa kuwa Zantel inapaswa kumlipa Haidari zaidi ya Sh milioni 800, badala ya maombi ya mshitaki ya Sh milioni 53.

Gazeti hili limefanikiwa kupata nyaraka za mwenendo wa kesi hiyo ambayo hukumu yake inaelezwa kuwa imeuchanganya uongozi wa Zantel na mawakili wake kutokana na kile kinachoonekana ‘kupaishwa’ kwa malipo hayo kwa zaidi ya mara 15 ya fidia iliyokuwa imeombwa na mdai.

Hukumu iliyompa ushindi Haidari ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema.

Uamuzi huo unaelezwa kuunyima usingizi uongozi wa Zantel ambayo hata hivyo iliamua kulipa deni kwa kile kinachotajwa kuwa ni kuheshimu uamuzi wa mahakama, ingawa kuanzia hapo uongozi wa kampuni hiyo ya simu umeelezwa kuwa unahaha kutaka kutenguliwa kwa hukumu husika.

Baadhi ya watendaji wakuu wa Zantel na mawakili, wanailalamikia hukumu hiyo wakidai kuwa kiasi cha fedha ilichoamriwa kulipa ni kikubwa mno pengine kushinda uwezo halisi wa mahakama iliyotoa hukumu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zantel, Norman Moyo alielezea kutoridhishwa na hukumu hiyo, akidai ni kubwa na yenye maumivu kama mwekezaji.

“Imetushangaza hata sisi, tunatafakari cha kufanya, lakini kimsingi tunadhani ni hukumu yenye utata. Tumelipa fidia hiyo kubwa kwa sababu ya kuiheshimu mahakama, lakini hatujatendewa haki na hatudhani kama hali hii inaleta picha nzuri kwa mazingira ya uwekezaji…tunatafuta jinsi ya kupata haki yetu,” alisema Moyo.

Historia ya kesi hiyo inaonesha kuwa Juni 27, 2007, Haidari kupitia kampuni yake ya Nararisa aliingia mkataba na Zantel wa kuiuzia viyoyozi 36 vya thamani ya Sh 73,296,000, lakini hadi kufikia Agosti 3, mwaka huo, siku ya mwisho ya mkataba, nusu ya viyoyozi hivyo vilikuwa havijapelekwa Zantel.

Kutokana na kushindwa kulipwa fedha kama yalivyokuwa makubaliano ya mkataba, Haidari alilazimika kukimbilia mahakamani kutaka alipwe Sh milioni 53.4 zilizokuwa zimebaki, huku akidai kwamba ili kuipatia Zantel viyoyozi, alilazimika kuomba mkopo wa Sh milioni 48 kutoka Benki ya Eurafrican Bank ambao ulikuwa unaendelea kukua kutokana na kucheleweshewa malipo na hata kufikia deni la Sh milioni 252.

Lakini madai hayo yalipingwa na Zantel iliyosisitiza kutohusika na suala hilo kwa kuwa mdai alishakiuka masharti ya zabuni, kwa kushindwa kukamilisha ndani ya wakati idadi ya viyoyozi vilivyohitajika.

Zantel kupitia kwa wakili wake, Juvenalis Ngowi wa Kampuni ya East African Law Chambers, ilipinga madai hayo kwa maelezo kwamba, hayakuwa na msingi na yaliyojaa utata kutokana na mlalamikaji mwenyewe kushindwa masharti ya mkataba.

Msingi mkuu wa kilio cha Zantel ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni miongoni mwa wanahisa, ni hisia za uonevu wa kutakiwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha tofauti na kile kilichokuwa kimeombwa na mdai.
 
Msingi mkuu wa kilio cha Zantel ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni miongoni mwa wanahisa, ni hisia za uonevu wa kutakiwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha tofauti na kile kilichokuwa kimeombwa na mdai.

Inatakiwa mwandishi ambaye alidai wana nyaraka zote za shauri hili kutueleza riba na gharama nyingine za kesi zilikuwa ni shilingi ngapi?

Vinginevyo habari hii kama ilivyo bado haina mashiko....................
 
Back
Top Bottom