Zama za hapa kazi tu, ziliwahitaji nani na nani kufanya kazi na Rais John Magufuli

Leslie Mbena

JF-Expert Member
Nov 24, 2019
207
677
Leo 12:15pm, 23/02/2020.

Pamoja na ukali wa Rais John Magufuli bado Waziri wake anadiriki kuhujumu uchumi,hapa ndipo unapoona suala la uadilifu lilivyo gumu.

Pamoja na ukali wa Mwalimu Julius Nyerere bado Waswahili walikuwa wanaiba na yapo mashirika mengi yalikufa.

Baada ya kupata Uhuru wapo watu walioanza kujipanga kuwa sasa Mwalimu Nyerere kama Rais atuteue kwenye nafasi mbalimbali ili Mambo yetu yakae vizuri.

Kama ambavyo Rais John Magufuli anavyopambana na rushwa ndivyo Mwalimu Julius Nyerere alivyopambana na rushwa hata kuanzisha Azimio la Arusha.

Kuhitaji Uongozi siyo tatizo hata kidogo,lakini ni Uongozi wa namna gani? Uongozi unahitaji ujivue gwanda la kujipendelea na kujivika gwanda la maslahi ya wengine.

Siyo rahisi kama wengi wetu tunavyofikiri,Miiko ya kimaadili ya kazi inasema hivi,Kiongozi ukipewa zawadi unayoona tafsiri yake ina utata unatakiwa uipeleke kwa katibu mkuu kiongozi,niulize ni lini umewahi kuona orodha ya waliopeleka zawadi kwa Katibu Mkuu Kiongozi?

Kitako Cha andiko hili ni kuonyesha tunu tuliyojaaliwa kuwa nayo katika Taifa la Tanzania hasa katika Awamu hii tano na namna tunu hiyo inavyostahili kupata watu sahihi wa kushirikiana nayo kuweza kulisaidia Taifa la Tanzania.

Kila mmoja angependa amuone Chief Mkwawa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga akifanya kazi na Rais John Magufuli. Tungependa kumuona Mwalimu Julius Nyerere akiishi katika zama hizi za "Hapa Kazi Tu"

Tungependa kumuona Edward Moringe Sokoine akiishi katika zama hizi za Hapa Kazi Tu.Tungependa kumuona Edward Sokoine bega kwa bega wakianzisha vijiji vya Ujamaa kama sehemu muhimu ya Maendeleo ya Taifa letu.

Ndugu John Magufuli na Edward Sokoine wanaamini katika usawa kwa kila mtu na wote wanapenda watu wathaminiane kwa kila hali.

-Kwa nini naanza moja kwa moja na Edward Sokoine kama mtu aliyefaa kuwepo katika Zama hizi za Hapa Kazi Tu?

Ni kwa sababu Edward Moringe Sokoine aliamini sana vijiji vya Ujamaa kama sehemu muhimu ya maendeleo ya Taifa la Tanzania, alipenda usawa kwa kila mtu na alipenda watu wathaminiane kwa kila hali,Hakuwa na mzaa kwenye utendaji wake na mpaka sasa ushupavu wake bado unakumbukwa na watu kama mfano wa kuigwa ili kulipeleka mbele gurudumu la Maendeleo.

Edward Sokoine,Kiongozi Shupavu,mtu mwenye historia kubwa kwa Taifa la Tanzania,ndiye Kiongozi aliyepata kuaminiwa sana na Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere akiwa na historia ya kipekee.

Dhana ya ubora wa utendaji na umahiri wa kufuatilia mambo,viliasisiwa na Edward Sokoine.Viongozi wengi walifundishwa kufanya kazi kwa mipango,udhibiti na ufuatiliaji makini.

Vita ya Uhujumu Uchumi inayoendeshwa na Rais John Magufuli ina wasifu wote wa kupokea kijiti cha kazi nzuri iliyoanzia ngazi ya Awamu ya kwanza iliyoongozwa na Mwalimu Julius Nyerere katika utendaji kazi wa Edward Moringe Sokoine.

Mambo yote ambayo leo hii yana ubatizo wa "Ufisadi uko nyuma yalibeba jina la asili la "Uhujumu Uchumi" katika hilo Edward Sokoine anakumbukwa sana alivyopambana katika nafasi ya utendaji Mkuu wa Serikali.

Bado kumbukumbu imebaki,kwamba mwanzoni mwa miaka 1980,anakumbukwa ukamanda wake kupitia kioo cha "Vita ya Uhujumu Uchumi"

Leo utendaji wa Hayati Edward Moringe Sokoine unabaki kuwa mfano wa kuigwa na kwa kiasi kikubwa kinachofanyika sasa kinashabihiana na maeneo ya Zama za Sokoine.

-Daktari Salim Ahmed Salim,Mwanadiplomasia aliyetukuka,Mjamaa wa kweli,Mpigania Uhuru wa Waafrika,Msemaji wa Waafrika,Committed Pan Africanist.

Akiwa na miaka 17,Daktari Salim Ahmed Salim aliongoza kikundi chenye mlengo wa kisiasa kichoitwa "All Zanzibar National Student Organisation" na baadae akawa mhimili katika vuguvugu la ukombozi wa Mzanzibari.

Mwalimu Julius Nyerere alimteua kuwa balozi wa Tanzania nchini Misri,na baadae kupelekwa New York,Marekani kama Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa kamati ya Kuondoa Ukoloni barani Afrika. Daktari Salim Ahmed Salim alipambana bila kuchoka kuondoa utawala wa kireno na utawala wa masetla kusini kwa Afrika.

Daktari Salim akiwa mtu mwenye mamlaka ya juu katika maamuzi mbalimbali yaliyohusu Afrika katika Umoja wa Mataifa,alipinga vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kwa Waafrika kusini walikuwa wanadai Uhuru wao.

Aliwaunganisha Waafrika kupinga Nelson Mandela kuwekwa katika Orodha ya watu hatari duniani, aliwaunganisha Waafrika kupinga Afrika ya Kusini kuondolewa katika Umoja wa Mataifa.Mambo haya yanabaki kama kipimo katika utendaji uliotukuka wa Daktari Salim Ahmed Salim.

-Philip Mang'ula,Kijana wa Mwalimu Nyerere,Mfuasi mtiifu katika itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea.

Katika siku za mwanzo za kutekeleza Itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea,Mwilimu Julius Nyerere aliwatuma watu kama Philip Mang'ula kupita katika kila kijiji kuhakikisha itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea inatekelezwa.

Azimio la Arusha ni tamko rasmi la kisiasa lilikosudiwa kuongoza Tanzania katika njia ya ujamaa kadiri ya maelekezo hasa ya Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kuleta usawa katika Jamii yote ya Watanzania na kuondoa unyonyaji wa Wachache kuwa na mali nyingi.

Philip Mang'ula aliongoza utekelezwaji wa tamko la Arusha lililokuwa na utekelezwaji wa Itikadi ya chama cha TANU,Siasa ya ujamaa, Siasa ya kujitegemea, Uanachama wa TANU na kulitekeleza Azimio la Arusha.

Kiini cha Azimio la Arusha kilikuwa kupeleka salamu kwa mabepari kuwa "Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi, mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena".

Philip Mang'ula ndiye ngazo ya nidhamu na uadilifu katika Chama Cha Mapinduzi CCM,Philip Mang'ula ndiye Katibu Mkuu wa CCM aliyechukia Ufisadi na Rushwa na katika Uongozi wake kama Katibu Mkuu wa CCM,tulishuhudia watu wakichaguliwa kwa uchapakazi na utendaji uliotukuka.

Mwaka 2010 Katika harakati za kukiokoa Chama Cha Mapinduzi kilichokuwa kimetawaliwa na kashfa za Ufisadi ilionekana kuwa Philip Mangula angeweza kufaa kuja kurudisha nidhamu na Uadilifu ndani ya CCM.

Japo alishastaafu Philip Mangula akaombwa kurudi kuhudumu katika nafasi ya Umakamu wa Mwenyekiti.

Kwa hakika tulimuona akiingia kwa kupiga mkwara mzito kuwa katika kipindi cha miezi 6 ya uongozi wake, kuwa atahakikisha kila aliyepata uongozi ndani ya CCM kwa rushwa anang'oka,na baadae tuliona dhana ya kujivua gamba ikija.

-Cleopa David Msuya si geni masikioni mwa wengi. Alikuwa Waziri Mkuu wa nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Edward Sokoine, aliwahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu mara mbili, kuanzia Novemba 7, 1980 hadi Februari 1983.

February 2015 kwenye kipindi cha Dakika 45 baada ya saa mbili usiku katika luninga ya ITV nilimsikiliza Cleopa Msuya akiongea mengi lakini nime kamata machache kama ifuatavyo,hii ilikuwa February 2015 na kwa hakika baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 Rais Mteule alifanyia kazi mambo haya yote na Leo February 2020 yote aliyozungumza Cleopa Msuya mnamo mwezi February 2015,yote yamefanyiwa kazi.

Tujikumbushe aliyoyasema Cleopa Msuya February 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.

-Uchumi uwanufaishe wote kama Azimio la Arusha lilivyowanufaosha Watanzania wote.

Bado Watanzania hawafanyi kazi kujipatia kipato, kwa mfano kilimo.
Huduma za jamii kama mashule, barabara na afya zimeongezeka sana,taasisi za kudhibiti sheria kama polisi au takukuru haziwajibiki ipasavyo na hazifanyi kazi kama wanavyotakiwa,

Rushwa imezidi katika taasisi za serikali haieleweki pembe za ndovu toka Tanzania zinakamatwa Singapore bila hatua mahsusi kuchukuliwa au watu kuwajibishwa.kesi zinazogusa hisia za umma zinachukua muda mrefu sana hadi wananchi wanakosa imani ya kutendeka kwa haki, mfano kesi za EPA kuchukua miaka 5.

Watu wanaficha fedha nje na aidha idara husika hazina weledi kuchunguza au hakuna nia ya kufanya,Nashauri Rais ajaye ana majukumu ya kukuza Real Economy kwa kuimarisha viwanda na ajira ,katiba mpya inabidi ifikie mwisho kimchakato na isiingizwe siasa katika mchakato huo,

Wapinzani hawakuwa na sababu kususia mchakato huo vyombo vya habari vimejikita katika vitu vya kisiasa kuliko kuelimisha wananchi juu ya mambo muhimu.

Cleopa Msuya alizungumza mengi sana lakini cha msingi ni kwamba kichwa chake bado kiko intact.
Na ushauri uliotolewa kwa mambo tuliyokuwa tunayaona ulikuwa ni ushauri wa kimsingi kabisa na kwa hakika alivyoingia Rais John Magufuli aliutekeleza ushauri huo kwa asilimia 100.

“Kabla ya uhuru idadi ya watu ilikuwa milioni nane na sasa tuko zaidi ya watu 53 milioni, kuna haja ya kuwa na uchumi unaokua badala ya kuzalisha bila mafanikio, Serikali iwe makini katika kuimarisha mambo muhimu kama nishati,” anasema na kuongeza:

“Serikali inatakiwa kufikiri juu ya kuimarisha masuala ya umeme nchini wakati wawekezaji wanapoingia ili kusaidia uchumi kukua haraka na kuepusha kutokea kwa mambo yaliyozikumba nchi za Kiarabu.” Cleopa Msuya,February 2015.

Ndugu zangu watu niliowataja hapo juu kama wangekuwepo katika Zama hizi za "Hapa Kazi Tu" basi tungeona Taifa likipiga hatua kubwa sana kiuchumi na kimaendeleo.

Kama Watanzania tutawaenzi Majabari hayo japo kwa asilimia 30% kwa uwajibikaji na kutenda kazi sio maneno maneno basi tungekuwa na Taifa lenye nguvu za kidola na kiuchumi.

Nimalizie kwa Mfano uliotukuka wa Edward Sokoine ambaye kinashabihiana sana na Ndugu John Magufuli.

Edward Sokoine aliiishi itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea kwa vitendo, aliwasakama walanguzi na wahujumu uchumi bila kuwaonea haya au aibu aliwaonyesha kidole.

Kuna kipindi kasi yake ilikuwa kubwa hadi muasisi mwenyewe wa Ujamaa na Kujitegemea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kupelekwa mchaka mchaka.

kwa kizazi kile ambao walimuamini na kutarajia taifa kupiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia utendaji wake uliotukuka bado hatuamini mazingira ya kifo chake kutokuwa na mkono wa mtu au watu "Wahujumu Uchumi.

Kifo cha Edward Sokoine ndicho kilichomtoa machozi hadharani Mwalimu Julius Nyerere huku akilia kwa sauti,Mungu aendelee kumuhifadhi Hayati Edward Moringe Sokoine hadi hapo tutapoungana naye katika makazi ya milele huko aliko amina.

Ahsante Mwenyezi Mungu kwa kutuletea Rais John Magufuli kwa mfano wa Edward Moringe Sokoine ili mapenzi yako yaweze kutimia katika Taifa la Tanzania.

Ahsante Mungu kwa kumbariki na kumlinda Rais John Magufuli,Ahsante Mwenyezi Mungu kwa kuibariki Tanzania.

Nikiishia hapa,Mimi ni,
Msemakweli Chakubanga,
Dar es Salaam.
0755078854.
 
Back
Top Bottom