Zaidi ya wafanyakazi 150 wapoteza kazi baada ya kusitishwa ujenzi wa hoteli

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,365
8,097
Wafanyakazi 150 wa Mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tano Blue Amber, wamepoteza kazi baada ya Wizara ya Ardhi kusitisha mkataba wa ukodishaji ardhi kwa Kampuni ya Pennyroyal Zanzibar licha ya kuwapo amri ya Mahakama ya kutaka ujenzi kuendelea.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wafanyakazi hao wamesema wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kusitisha ujenzi wa hoteli hiyo na nyumba za makazi baada ya mfumo wao wa maisha kuvurugika pamoja na familia zao.

“Tumepokea kwa mshtuko mkubwa sana kusitishwa kwa ujenzi wa mradi sasa hatuna kazi ya kufanya hali ya maisha imekuwa ngumu,” alilalamika dereva Ziada Haji Makame.

Fundi mashine, Haji Zaja Haji, alisema mradi wa ujenzi wa hoteli hiyo ya kimataifa ulikuwa umefikia hatua kubwa na tangu ulipoanza vijana wengi wamenufaika katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Tunaomba serikali kuangalia upya madhara ya kusitisha mkataba wa ukodishwaji wa ardhi kwa maendeleo ya sekta ya uwekezaji vitenga uchumi Zanzibar,” alisema Haji Ali Haji.

Kwa upande wake, John Haji Khamis, alisema kitendo cha kusitisha mkataba wa ukodishwaji wa ardhi kunaweza kurudisha nyuma wawekezaji ambao wameanza kujitokeza kuanzisha miradi katika sekta ya uwekezaji Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo habari na mmiliki Kampuni ya Pennyroyal, Brian Thomson, “usitishaji wa mkataba wa ukodishwaji wa ardhi umetolewa licha ya Kampuni ya Pennyroyal ilikuwa imepokea amri kutoka Mahakama Kuu ya kuendelea na ujenzi.”

Akifafanua katika taarifa hiyo alisema, mwaka 2014 kampuni yake ilipata hatimiliki hekta 411 baada ya kukamilisha usanifu wa mradi, ukawasilishwa na kuidhinishwa na Mamlaka ya Kukuza Uchumi Zanzibar (ZIPA) na kupewa hadhi ya mwekezaji wa kimkakati Zanzibar.

“Uidhinishaji mwingine wote wa kisheria ikiwamo cheti cha tathimini ya athari kwa mazingira ulitolewa na mamlaka zote husika.

Alisema Kampuni ya Pennyroyal imeanzishwa mwaka 2012 na kupewa hati miliki mwaka 2014 pamoja na kibali cha uwekezaji mwaka 2018 baada ya kukamilisha sifa na masharti ya uwekezaji vitenga uchumi Zanzibar.

Hata hivyo, Brian katika taarifa hiyo alisema Juni mwaka 2021, Kampuni ya Pennyroyal Limited iliarifiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwa serikali ilikusudia kutoa sehemu ya ardhi chini ya umiliki wake kwa mwekezaji kutoka nchini Dubai (UAE).

“Hii ilifuatiwa na barua kutoka kwa serikali kwamba ilikuwa ikitaka kutekeleza agizo la Mahakama Kuu ambapo kampuni ya wahusika wengine ilishinda kesi ilihusisha viwanja namba 1107 na 1113, viwanja hivyo vikiwa katika sehemu ya ardhi ya Pennyroyal.

“Tumejitahidi kuhakikisha mradi huu hauporomoki hata hivyo jitihada zetu zimeambulia patupu kwani serikali imekataa kubadili msimamo wake tumewajulisha wamiliki wote watarajiwa wa nyumba ambazo walikuwa wamewekeza katika aina tofauti kuhusu yaliyojitokeza,” alisema Brian katika taarifa hiyo.

“Viwanja vinavyodaiwa na serikali kuwa na mgogoro ni hekta 20 kati ya hekta 411 zilizokuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Pennyroyal Limited tangu kuwekeza mradi huo.

Hatua ya serikali kusitisha mkataba wa ukodishwaji wa ardhi kwa Kampuni ya Pennyroyal imeibua mjadala mkubwa kutokana na kujitokeza wakati serikali ikiendelea na utekelezaji wa mpango wa kukuza uchumi kupitia mpango wa uchumi wa buluu.

Kwa upande wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudriki Ramadhan Soraga, alisema serikali imesitisha mkataba wa ukodishaji wa ardhi lakini Kampuni ya Pennyroyal wanaendelea kumiliki kibali cha uwekezaji.

“Mkataba wa ukodishwaji wa ardhi kweli umesitishwa, lakini bado wanaendelea kumiliki kibali cha uwekezaji wakati kesi inaendelea mahakamani na kwa upande wa serikali suala hili lipo kwa mwanasheria mkuu wa serikali,” alisema Waziri Soraga.
 
Back
Top Bottom