Zabibu!

Mzee wewe mkali
Lakini sijakubali
Mbona meliweka mbali
Swali langu la awali?

Kupenda sio hisia
Bado hujaniambia
Vipi linajisikia
Kisu kinapoingia?

Kupenda sio kuhisi
Ni tendo lenye kiasi
Lizukalo kwa wepesi
Kati ya wenye nafasi

Doriani lapendeza
Machoni linaliwaza
Hebu puani sogeza
Harufuye taiweza?

Moyoni utalipenda
Na mti utaupanda
Mwenyewe utajipinda
Hisia zitakushinda

Mwenye kula hujilamba
Sasa jibu naliomba
Mwenye kuliwa ni rumba
Au ni ngoma ya Pemba?


Nimetafuta majibu
Kuhusu hizo zabibu
Naona napata tabu
Kujalipata jawabu!

Labda yanapata raha
Pale ninapotafuna
Hakika siyo karaha
Yanaiva tunaona
 
Zabibu langu li tamu,
Pekee lanipa hamu,
Ni tamu tunda adhimu,
La kale kama ya Shamu!


Linaendelea...
Mzee Mwanakijiji
Umeonesha kipaji
Unastahili taji
Kwa kweli twakuhitaji.

Tunda lako la zabibu
Kulila naona tabu
Halinipi maajabu
Ya kushangaza mababu

Saizi yake ni duni
Kulila uwe makini
Laweza dondoka chini
Au teleza kooni

Mimi halinipi hamu
Kwa vile ni la msimu
Ukila leo binamu
Kuja tena ni mwakani

Ukilikosa zabibu
Utakula nini babu?
Utakufika ububu
Uishie kwa tabibu

Utaitaja mizimu
Kisa zabibu adimu
Utaitamani ndimu
Ujiondolee hamu

Zabibu tunda hafifu
Rojo yake si nadhifu
Rangi haina wasifu
Ukila linakukifu

Zabibu kwao porini
Ukilileta mjini
Lajipeleka sokoni
Liishie mnadani

Nimejaribu Nanasi
Kula kwa kujinafasi
Nikaona ukakasi
Nimewachia papasi

Nikaonja embe dodo
Nikadhani ni uhondo
Sikujua ni uvundo
Alouacha Mwawado

Chungwa, ukwaju na ndizi
Sili hata kwa hirizi
Ni chakula cha machizi
Mimi Mola kanijazi

Malimao mafenesi
Nayo pia si mepesi
Ladhaye haihalisi
Sitaki kukosa nyusi

Mimi tunda langu dafu
Nalila bila kukifu
Polepole bila hofu
Tena si kwa uhalifu

Kwanza naanza kufua
Kumbi zisije chafua
Nisije pata mafua
Nishindwe tamba kifua

Kisha ninatabasamu
Dafu ninalisalimu
Hicho ni kibinadamu
Unapoingiwa hamu

Sasa nagonga kifuu
Tena si kama mafuu
Nakuta maji makuu
Baridi kama ya juu

Halafu kuna rojoye
Hainao mfanowe
Mimi yanipa kiwewe
Sitoitaja siriye

Sifa ya dafu mwenzangu
Halina msimu kwangu
Wakati wote ni langu
Nalila sina uchungu

Kiangazi nalipata
Anajua Mbalawata
Masika sikosi hata
Wakati wote nanata.

Jamani dafu ni tamu
Tena haliishi hamu
Ulaji wake timamu
Kwa mitindo kemkemu

Nasifia langu dafu
MwanaK nakuhofu
Usinichezee rafu
Kuninyang’anya waifu.

Nitakutemea mate
Uende ukanitete
Mcheza hawi kiwete
Ngoma yataka matao!
 
Mdomo umeachama, dafu unalisifiya!
Mbona sina la kusema, macho yananipwaiya,
Yote uwezayo chuma, dafu walikumbatia,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.

Mti wake ni mrefu, kukwea mimi siwezi,
Kimo kinanipa hofu, wa kijiji si mkwezi,
Bora ni yale matofu, kufua dafu siwezi,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.

Namkumbuka Salumu, ati ataka madafu,
Akajifanya mwalimu, madafu akiyasifu,
Kaukwea kitalaamu, mnazi wa Bwana Sefu,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.

Mwisho akafika juu, meno katukenulia,
Akakunjua miguu, huku akishangilia,
Mara chini huyo puu!, wenzake tukakimbia,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa!

Miguu imevunjika, imetokea begani,
Mbavu zikaparanyika, zimetokea kiunoni,
Damu imetapanyika, kamrudia Manani,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa!

Sasa yote ni ya nini, madafu kuyatafuta,
Zabibu mbona laini, adhabu hutoipata?
Ukishika vidoleni, mdomoni wazileta,
Kamwe dafu sitokula, sababu nakupa!
 
Mdomo umeachama, dafu unalisifiya!
Mbona sina la kusema, macho yananipwaiya,
Yote uwezayo chuma, dafu walikumbatia,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.

Mti wake ni mrefu, kukwea mimi siwezi,
Kimo kinanipa hofu, wa kijiji si mkwezi,
Bora ni yale matofu, kufua dafu siwezi,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.

Namkumbuka Salumu, ati ataka madafu,
Akajifanya mwalimu, madafu akiyasifu,
Kaukwea kitalaamu, mnazi wa Bwana Sefu,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.

Mwisho akafika juu, meno katukenulia,
Akakunjua miguu, huku akishangilia,
Mara chini huyo puu!, wenzake tukakimbia,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa!

Miguu imevunjika, imetokea begani,
Mbavu zikaparanyika, zimetokea kiunoni,
Damu imetapanyika, kamrudia Manani,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa!

Sasa yote ni ya nini, madafu kuyatafuta,
Zabibu mbona laini, adhabu hutoipata?
Ukishika vidoleni, mdomoni wazileta,
Kamwe dafu sitokula, sababu nakupa!
Kwanza nina sikitiko, kwa habari ya maziko,
Salumu huko aliko, Mola mpe pumziko,
Nasi tutafika huko, tutote huku tuliko,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Pili ninamlaumu, nafsi kuihujumu.
Si mjuzi maalumu, ukwezi haufahamu.
Yeye hakuwa mwalimu, kwa nini kujituhumu?
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Vipi kukwea minazi, na yeye sio mjuzi?
Alikuwa mwanafunzi, hadi kutokwa pumzi,
Hajaupata ujuzi, aparamia minazi,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Lo! Masikini Salumu, fani umeipa doa,
Watu wanakulaumu, kwa ulivyojiondoa,
Hujawa mtaalamu, wala hukupata ndoa,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Nikirudi kwenye dafu, nabaki muaminifu,
Kwa mapenzi yakinifu, sitoacha langu dafu,
Wala halitonikifu, sasa na hata halafu,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Hapa nimepata funzo, katika hili gumzo,
Kumbe tunda ni matunzo, kila siku tangu mwanzo,
Kwa raha na matatizo, imara weka mawazo,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Tunda zuri ni lolote, unalomezea mate,
Bara na pwani upite, kushoto kulia kote,
Kiona wameza mate, tia nanga usisite,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Mwingine apenda tende, we waweza usipende,
Neemah ala kwa mbinde, tena kwa shingo upande,
Bora milima apande, akashindie makande,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Nyani Ngabu kwa machenza! ala akichezacheza,
Kelly atampokeza, huku akimkonyeza,
Mengine atayasaza, aweke juu ya meza,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Mapera atayabeza, eti kula hatoweza,
Kisa yanamtatiza, harufuye yamkwaza,
Tena yanampa giza, ashindwa hata kuwaza,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Balantanda na embe, mwenyewe aita dodo,
Atakula na atambe, mbele yake hondohondo,
Ngoja sasa ajilambe, anatia madoido,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Suki mpatie ndizi, anageuka mchizi,
Utamu amemaizi, asahau hata kazi,
Usizitaje kunazi, za Kibunango mjuzi,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Wewe zako ni zabibu, hupendi kuziharibu,
Zina thamani ajabu, kama ilivyo dhahabu,
Kwa imani yako babu, magonjwa zinayatibu,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

Salamuni ndugu zangu, wala Sangara na Changu,
Tunda la mtu si langu, nalipa heshima chungu,
Msidharau wanangu, heshimuni walimwengu,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.

JF kuna raha, vipaji twakumbukia,
Twawaona wa madaha, na wale wa kurukia,
Wamakonde pia Waha, wote wote waingia,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
 
Maamuma ndugu yangu si kila tunda ni zuri
Walitwonya wakuu sichukue pima shubiri
Kumbuka Hawa na Adamu walivoleta shari
La kati tunda walimega maovu yakajiri
 
jamani tunda nanasi
kula uwe na nafasi
unapojaa ukwasi
hautajifaidia

kwa chakula cha mchana
mezani kimejazana
juisi yake mwanana
hakika utasifia

nanasi liwe shinani
wachuma kiulaini
hakuna purukushani
mkononi wachukua

Embe dodo kule juu
hadi lidondoke puu!
kweli kwa mtaji huu
hupaswi kulisifia

jamani hizo zabibu
hasa alolima babu
sana sana kwa ulabu
kama wataka kulewa

nakukaribisha kwangu
leo maulidi yangu
ule nanasi mwanangu
ni tamu tena murua


I like JF! Sio siasa tuuuuu kila wakati. I like these majibizano
 
Tunda zuri ni la kwako
Lile la peke yako
Ulalo kivyako vyako
Wakatamani wenzako!

La kwako la peke yako
Hata kama bokoboko
Utalila kwa viboko
Bila hata sokomoko
 
Tunda zuri ni la kwako
Lile la peke yako
Ulalo kivyako vyako
Wakatamani wenzako!

La kwako la peke yako
Hata kama bokoboko
Utalila kwa viboko
Bila hata sokomoko
Hapo nakukubalia
Tunda lako kujilia
wengine wabaki lia
Huku wakichungulia

Chako ni chako mwanangu
Cha mwingine si cha kwangu
Nipatacho ndicho changu
Alichonigea Mungu

Kila mwenye tunda lake
Kazipenda sifa zake
Ndipo kachukua kwake
Akalifyonze kivyake

Mwanakijiji kwaheri
Japo siendi safari
Kuagana ni vizuri
Ya Mungu yako dahari

Na apendapo Manani
Kesho 'taniona ndani
Sijui kwa mada gani
Ila si kwa ushindani

Ninawashukuru wote
Walosoma tungo zote
Na walochanga chochote
Ili mradi tu sote.
 
Wanawane mwanishangaza,hayo matunda kuyasifia
Ukweli daima hamtoweza,kunishawishi kuyatumia
Daima kwangu la kwanza,Embe dodo ninalitumia
Mimi wa Usukumani,embe dodo namba wani

Embe dodo lapatikana,kila mkoa wa Tanzania
Zabibu ni adimu sana,wachache ndo lawafikia
Dafu ni ngumu sana,mnazini kukwea kulifikia
Mimi wa Usukumani,embe dodo namba wani

Utamu wa ndizi jamani,kwa embe dodo cha mtoto
Nikiweka ndizi tumboni,navimbiwa kama Mpoto
Ewe Suki mwanawani,jaribu dodo si la msoto
Mimi wa Usukumani,embe dodo namba wani

Maamuma na Mwanakijiji,wa bure ushauri nawapa
Tunda zuri kama mwahitaji,Embe dodo ndio supa
Ukila shushia ya baridi maji,ya mtungini si ya chupa
Mimi wa Usukumani,embe dodo namba wani

Embe dodo Usukumani,baada ya chakula laliwa
Daima walikuta mezani,kwa vipande limekatwa
Vyakula vya Usukumani,mtindi,viazi-matovolwa
Mimi wa Usukumani,embe dodo namba wani

Embe dodo tunda letu,daima twalila tutakavyo
Twakata vipande vyetu,na kuvila itakiwavyo
Pia kulinyonya ndo zetu,kama mtoto anyonyavyo
Mimi wa Usukumani,embe dodo namba wani


Litaendelea….


Na; Balantanda Masalakulangwa(Sauti ya Gamboshi)
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom