Yusuph Manji si mkombozi Yanga - Madega

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Mimi nimefurahi sana kusikia Yanga wamemtolea nje huyu Manji, hasa ukitilia maanani alitaka kuifanya iwe klabu yake.

Yusuph Manji si mkombozi Yanga - Madega
Mwandishi Wetu
HabariLeo; Thursday,October 11, 2007 @00:06


MWENYEKITI wa Yanga, Imani Madega amemshutumu aliyekuwa mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Manji kuwa ana lengo la kuiangamiza.

Madega aliyasema hayo alipozungumza na wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali jana kujibu shutuma alizozitoa Manji juzi alipokutana na baadhi ya wazee wa klabu hiyo katika makao makuu ya Yanga mitaa ya Jangwani na Twiga Kariakoo.

“Nimewaita ninyi watu wa mwisho katika utaalamu wa habari za michezo ili mnifikishie taarifa hizi kwa wanachama, wapenzi na Watanzania watakaoamua kuona kati ya uongozi ulio chini yangu na mfadhili nani ni pumba na nani ni mchele,” alisema mwenyekiti huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Katika kikao chake na baadhi ya wazee juzi, Manji alisema ameamua kutosaini mkataba mwingine na uongozi huo kutokana na viongozi kutotekeleza yaliyopo kwenye mwafaka na kutoa masharti kwamba endapo atatakiwa kurudi kwenye ufadhili, ni lazima viongozi watekeleze yaliyomo kwenye mwafaka huo.

Madega alisema: “Habari hizo alizosema Manji juu ya uongozi wangu ni uongo mtupu, ukweli ni kwamba ujio wa Manji ndani ya Yanga unaonekana kama ni ukombozi wa kifedha, lakini ukweli ni kuwa amekuja kwa lengo moja tu, la kuiangamiza klabu ya Yanga kabisa na hatimaye kuunda kampuni ambayo kinadharia yeye ndio atakayekuwa mmiliki mkuu.”

Madega alisema kitendo cha Manji kuwaambia wanachama kuwa viongozi ndio chanzo cha yeye kutoendelea na mkataba, si cha kweli kwani uongozi uliamua kutoyafanyia kazi matakwa yake kutokana na kugundua mapungufu kwenye rasimu ya katiba ya mwafaka.

“Uongozi wangu uliingia madarakani tarehe 30/5/2007, wiki moja baadaye niliitwa ofisini kwa mfadhili tukiwa na watu watano. Katika kikao kile ajenda kuu ilikuwa ni sisi viongozi wa juu baada ya kuchaguliwa tusaini mkataba uliokuwa unatayarishwa ili timu ya Yanga ihamie Kampuni na rais wake awe ndugu Francis Kifukwe…

“Binafsi nilihamaki sana kwa kuwa ninaamini mimi ni mtu mzima mwenye akili timamu, msomi na nina uwezo wa kawaida wa kuchanganua mambo, na zaidi kitaaluma mimi ni mwanasheria na kazi yangu ni wakili wa kujitegemea. Nalinda heshima yangu zaidi kuliko maslahi, hivyo kwa uwazi kabisa sikukubali kufanya vile kama kiongozi mkuu hadi hapo Katiba ya Yanga pamoja na mwafaka nitakapoupitia kikamilifu, bila ya shaka chanzo cha kutoelewana kwetu na mfadhili kulianzia baada ya kikao kile,” alisema Madega.

Alisema kwa kipindi kile hakukubaliana na matakwa ya Manji kwa kuwa kama kiongozi aliyechaguliwa na wanachama wa Yanga kwa kura nyingi ana jukumu la kusimamia Katiba kikamilifu.

“Kwa wakati ule hata uongozi ulikuwa haujakamilika kwa kutoteua wajumbe watano wa Kamati Kuu hivyo nisingeweza kutoa maamuzi makubwa kama yale bila kuwapo kwa uongozi wa Yanga kwa mujibu wa Katiba,” alisema.

Aidha, alisema alikutana na uongozi wake kujadili Katiba kwa kina na rasimu ya mwafaka na kugundua ikiwa na mapungufu mengi na mojawapo ni utata ulipo juu ya kuuzwa kwa hisa.

“Baada ya kugundua hati ya mwafaka kwa kina kamati iligundua kuwa Kampuni ya Yanga itakuwa na hisa shilingi milioni sita, hisa moja itauzwa shilingi elfu moja na kufanya mtaji kuwa shilingi bilioni sita endapo hisa zote zitauzwa…

“Kifungu cha 3.2.2 cha rasimu ya mwafaka kinaipa klabu hisa saba tu kati ya milioni sita, thamani ya hisa saba ni shilingi elfu saba, hii ndiyo thamani ya kampuni kwenye klabu…

“Hisa 3,059, 993 zenye thamani ya shilingi bilioni tatu zitatengwa pembeni na zitatakiwa klabu kuzinunua ndani ya miaka miwili na klabu ikishindwa basi zitauzwa kwa watu wengine…

“Hivi tujiulize klabu itapata wapi shilingi bilioni tatu ndani ya miaka miwili ili iweze kununua hisa, na asilimia 51 ya hisa zote za kampuni bali itakuwa na hisa saba tu zenye thamani ya shilingi elfu saba, rasimu ya mwafaka inasema kwamba mfadhili atamnunulia kila mwanachama hisa 10 zenye thamani ya shilingi elfu kumi,” alisema.

“Ina maana mwanachama mmoja ana thamani kubwa ndani ya kampuni kuliko klabu itakayokuwa na thamani ya shilingi elfu saba na ndio maana klabu haikutakiwa kuwa na mwakilishi kwenye Bodi ya Kampuni kwa kuwa haina hisa nyingi kwenye kampuni,” alisema.

Alisema Manji amefikia hatua ya kuudharau uongozi kwa kutangaza kutoendelea kudhamini kupitia vyombo vya habari na kesho yake akaenda klabu kuhutubia huku akijua wazi kuwa yeye si mwanachama, kiongozi wala mfadhili.

“Ni maadili gani anayoyazungumzia Manji zaidi ya kuwa chanzo cha vurugu ndani ya Yanga kwa wale wanaonufaika kutoka kwake…mwisho nasema kuwa sitokuwa tayari kuiona Yanga ikiuzwa na kutawaliwa na mtu mmoja kwa nguvu ya pesa, masikini na mwanawe, tajiri na mali zake, Manji baki na mali zako au heshimu Katiba. Vinginevyo baki na mali zako au fadhili timu nyingine,” alisema Madega.

“Wazee na wanachama wachache waroho wa Yanga kuweni macho na msiwasaliti wazee wenzenu ambao walifanya juhudi kuifanya Yanga iwe na jina kubwa, mkiendelea kufanya hivyo kwa hakika historia itawahukumu, uongozi uko imara kutetea maslahi ya Yanga,” alisema.

Hata hivyo, Madega alikiri kuomba Manji awalipe mishahara wachezaji hasa wale wa kigeni kwa vile alihusika katika kuwasajili na kuwaahidi mishahara.

“Yanga kwa sasa haina hela, na wachezaji wa kigeni ni kweli wana mikataba na wanalipwa fedha nyingi, kwa hiyo atulipie tu mpaka labda mwezi wa tano ligi ikiisha basi, sisi tutajikuna unapofikia mkono, wakishindwa basi tutaingia mitaani na kutafuta wachezaji tunaoweza kuwalipa,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Manji alisema hana haja ya malumbano na Madega.

“Ndio alivyosema hivyo, mimi sina haja ya kulumbana naye, yeye ni kiongozi najua anayoyafanya ni kwa niaba ya viongozi na wanachama wake, sina haja na wala sihitaji kabisa malumbano,” alisema mfanyabiashara huyo maarufu anayemiliki Kampuni ya Quality Group.

Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved
 
Yu wapi madega maana leo hii huyo manji analiliwa jangwani
 
Wanayanga wakiona hivi,watamshutumu alitumwa na simba kama mzee Akilimali
 
Chiz madega alikula pesa ya ukarabati uwanja Kaunda na jengo kupiga rangi akaendea kuzifanyia kampeni Lugoba agombee ubunge akaanguka hata kura ya maon hakupita kule CCM wajanja wakala kapotea ye nani yanga?
 
anafuta style ya kutoka Madega walimpiga hela ya kugombea ubunge akaharibu Yanga...Sitaki kabisa uongozi au mambo ya mpira naachana nayo leo anakuja kidogo kidogo...kauli hizi amezisahau..
 
Ni miaka 8 sasa tangu Oct 12, 2007.

Aliyoyafanya hayasemeki, bali yanaonekana kwa macho.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom