Yona agombana na Wamarekani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Yona agombana na Wamarekani

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mdondoaji, Mar 29, 2010.

 1. M

  Mdondoaji JF-Expert Member

  #1
  Mar 29, 2010
  Joined: Mar 17, 2009
  Messages: 5,106
  Likes Received: 45
  Trophy Points: 145
  FAMILIA ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Daniel Yona, iko katika mvutano unaomhusisha aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini, Mchungaji Charles Stith. Katika mvutano huo, Serikali ya Tanzania imeshtuka dakika za mwisho, ikishangaa na kuahidi kuchukua hatua stahili, Raia Mwema imebaini.

  Mvutano huo unahusisha moja kwa moja kundi la wawekezaji wa Marekani waliokuwa tayari kuwekeza mamilioni ya dola nchini katika mradi wa ujenzi wa nyumba nafuu, kwa makubaliano mahsusi na kampuni ya Yona.

  Yona, ambaye kwa sasa anashitakiwa katika Mahakama ya Kisutu kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka alipokuwa Waziri, amejikuta katika mvutano baada ya kutaka kujitoa katika makubaliano ya uuzaji wa eneo kwa kampuni ya Kimarekani ya Enterprises Homes Tanzania Ltd (EHTL).

  Kampuni ya Yona inayoitwa Devconsult International Ltd iliingia mkataba na Enterprises Homes Tanzania Ltd kuuza ardhi yenye hati namba (Plot No). 384, Block ‘A’ Kunduchi kwa bei ya Dola za Marekani 650,000 (zaidi ya Sh milioni 650).

  Lengo la EHTL kwa kushirikisha wadau wengine ni kufanikisha ujenzi wa awali wa nyumba 45 za gharama nafuu, ambazo ni sehemu ya ujenzi wa nyumba nafuu mpya 5,000 utakaokamilika mwaka 2012.

  Mradi huo wa aina yake unalenga kusaidia ndoto ya Serikali kuwapatia wananchi makazi bora ya gharama nafuu, lakini habari zinasema kampuni iliyokusudia kununua ardhi hiyo kwa familia ya Yona, ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba wa awali ikiwa ni pamoja na kulipa fedha kabla ya kukabidhiwa eneo husika.

  Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mfadhili wa mradi huo kupitia EHTL ni kampuni binafsi ya Marekani, Overseas Private Investment Corporation (OPIC), pamoja na taasisi nyingine za fedha zikiwamo Benki ya Eurafrican Bank na taasisi ya mikopo Ghana.

  Kila nyumba ilipangwa kugharimu dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh milioni 100) au pungufu ya kiwango hicho. Mkataba wa mkopo wa kuuziwa nyumba hiyo kwa mlalahoi wa Tanzania utadumu kwa miaka 15.

  Hata hivyo, hivi karibuni Devconsult iliamua kujitoa katika mpango huo na hivyo kuhatarisha malengo yaliyokusudiwa, baada ya kampuni hiyo ya kina Yona kushindwa kuwashawishi wawekezaji hao kulipa fedha husika kwa mujibu wa mkataba.

  Lakini pamoja na kitisho hicho, Wawekezaji wa Marekani wenye malengo hayo bado hawajakata tamaa isipokuwa wamekuwa wakifanya kampeni wakidai kwamba ni vigumu kuendesha shughuli za kiuwekezaji nchini Tanzania bila kueleza ukweli kwamba walishindwa kulipa fedha kwa wakati kama walivyokubaliana katika mkataba.

  Taarifa kutoka kwa wawekezaji hao zinabainisha kuwa wana matumaini familia ya Yona itarejea katika mpango huo ili hatimaye kuufanikisha, huku kukiwa na taarifa za suala hilo sasa huenda likaingia katika mkondo wa kimahakama.

  Habari zaidi zinasema kwamba mbali ya kuwa familia ya Yona kutaka kuuza eneo hilo, mmoja wa wanafamilia naye aliingizwa katika kampuni hiyo ya Wamarekani kama mwana hisa kwa nia ya kufanikisha malengo ya ujenzi wa nyumba hizo huku kukiwa na watu wengine maarufu nyuma yao.

  Wakati mvutano huo ukiendelea, takwimu nchini hasa za Benki Kuu zinabainisha kuwa mahitaji ya nyumba bora Tanzania yemefikia nyumba milioni 2.

  Dar es Salaam pekee, wastani wa mahitaji ya viwanja kwa ajili ya ujenzi ni 20,000 lakini uwezo wa utoaji kwa mwaka ni 700, na hivyo takriban asilimia 97 ya mahitaji hayatekelezwi.

  Kuhusika kwa Balozi Charles Stith

  [Balozi Charles Stith]

  Balozi Charles Stith

  Balozi Stith, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti na Kumbukumbu za marais wa Afrika (APARC), kilichoko katika Chuo Kikuu cha Boston, Marekani ndiye Mwenyekiti wa Enterprises Homes Tanzania Ltd.

  Balozi huyo wa zamani wa Marekani nchini, wakati wa utawala wa Rais Bill Clinton, amewahi kuuelezea mradi huo kuwa ni ukombozi kwa Watanzania wenye uwezo mdogo kiuchumi kumiliki makazi.

  “Suala hili la mkopo nafuu wa nyumba utawanufaisha Watanzania wengi na kujiona ni wadau wa kweli katika maendeleo ya nchi yao.

  “Hiki tunachofanya ni mapinduzi makubwa katika umiliki wa makazi katika hii nchi (Tanzania),” anasema Balozi Stith akizungumzia mradi huo.

  Shirika la Overseas Private Investment la Marekani (OPPIC) ambalo ndilo mfadhili wa mradi huo ni wakala wa Serikali ya Marekani ulioanzishwa kwa lengo la kukusanya na kuwezesha mitaji na maarifa kutoka nchini Marekani kuwekezwa kwa kushirikisha wadau wengine katika nchi mbalimbali duniani.

  Msimamo wa kigogo wa EHTL

  Akizungumzia sakata hili, mmoja wa viongozi wa kampuni ya Enterprises Homes Tanzania Ltd (EHTL), Kyle McKinney anasema hakuna sababu za kujitoa au kusitisha mpango huo kwa kuwa umefikia hatua za mwisho na tayari wafadhili kadhaa wameridhia kusaidia.

  Kwa mujibu wa McKinney, wakati Benjamin Mkapa (akiwa Rais) alifika Marekani Septemba 1999 na kuipigia debe Tanzania kama moja ya nchi nzuri za kuwekeza katika Afrika, akitaka wawekezaji wa kigeni wakiwamo Wamarekani kuwekeza Tanzania.

  “Pamoja na kikwazo hiki bado tuna nia ya kuendelea na mradi lakini kama Bw. Yona (Daniel) na kampuni yake watatii masharti ya mkataba na kukubali kubadilisha hati ya umiliki katika Wizara ya Ardhi,” anasema McKinney.

  Mkono wa Daniel Yona

  Waziri huyu wa zamani wa Nishati na Madini, Yona anahusika moja kwa moja na barua yake ya Desemba 8, mwaka 2009 inathibitisha.

  Katika barua hiyo Daniel Yona, anamweleza Sadock Maggai wa kampuni ya uwakili ya IMMMA (IMMMA advocates) ambaye kwa wakati huo alikuwa mwakilishi wa EHTL, kwamba; makubaliano (uuzaji ploti ya Oktoba 23, 2006) kati ya kampuni mbili (Devconsult International Ltd na Enterprises Homes Tanzania Ltd) yamesitishwa na kampuni ya Devconsult.

  Yona katika barua hiyo anasema; “makubaliano yamesitishwa na kwa hivyo anaomba kurejeshewa nyaraka zote kutoka Enterprises Homes Tanzania Ltd-EHTL.

  Lakini katika majibu yake kwa barua hiyo ya Yona, Maggai ambaye ni wakili alifafanua kuwa EHTL haiko tayari kurejesha nyaraka yoyote ambazo ndiyo msingi wa makubaliano kati ya kampuni hizo na kwa maana hiyo, kuna mkataba wa kisheria kati ya kampuni hizo mbili.

  Taarifa zaidi zinabainisha kuwa baadaye Wakili Maggai alijitoa katika jukumu la kumwakilisha mteja wake (EHTL) kwa madai ya kuwapo kwa mgongano wa maslahi kati yake na Yona (familia).

  [Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Daniel Yona]

  Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Daniel Yona

  Alipoulizwa kuhusu mvutano huo, Daniel Yona alikataa kuzungumza kwa kina akiishia kuweka bayana kuwa uamuzi wa kusitisha makubaliano kati ya kampuni hizo mbili umefanywa na watoto wake na si yeye.

  Hata hivyo, mawasiliano mbalimbali yanabainisha kuwapo kwa utata ikidhihirika kuwa Yona ndiye amekuwa akitoa baraka zote katika kusitisha mkataba huo kupitia wanawe.

  Kiini cha mvutano chaanzia BoT

  Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha kuaminika nchini, uamuzi wa kusitisha makubaliano yaliyofikiwa umetokana na sababu kuu mbili.

  Kwanza, ni mtihani wa kisheria (kesi yake mahakamani) ambao Yona kwa sasa anapambana nao na pili, mapendekezo mapya mradi wa ujenzi wa nyumba wa Benki Kuu, ambao utahusisha takriban dola za Marekani milioni 40 (zaidi ya Sh bilioni 40).

  Kampuni na taasisi binafsi za Tanzania zinatarajiwa kunufaika na fungu hilo la fedha na hasa zinazojihusisha na masuala ujenzi.

  Chanzo cha kuaminika cha habari, kinafichua siri kubwa ya maandalizi ya ulaji inayohusisha maofisa kadhaa wa Benki Kuu.

  Maofisa hao wamejipanga kuandaa washirika wao kibiashara kuanzisha au kutafuta kampuni za masuala ya ujenzi na ardhi, kwa ajili ya kujichotea mabilioni hayo. Mradi huo unaohusisha BoT ulitangazwa rasmi Novemba 14, mwaka 2009.

  EHTL yatoa notisi

  Tayari EHTL imetoa notisi kwa kushirikiana na OPIC katika kukabili kile kilichoelezwa kuwa “kitisho kutoka kwa Serikali ya Tanzania-Wizara ya Ardhi kuzuia mchakato wa utoaji hati kwa jina la Enterprise Homes Tanzania Limited kwa mujibu wa nyaraka haraka halali zenye sahihi husika.”


  Waziri Chiligati ashangaa

  Katika maelezo yake kuhusu sakata hili, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati alisema hakuwa na taarifa zozote kuhusu kuwapo kwa mradi huo lakini akiahidi kuwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete itahakikisha mradi huo unakwamuliwa.

  Source: Raia Mwema

  Niliwahi kusema kuwa huu mradi wa nyumba ni dili na hizo pesa ziko hatarini kuliwa benki kuu. BOT wanatengeneza EPA nyengine. Unganisheni habari hii na habari nyengine za nyuma mh Tanzania sijui lini tutafika!!!
   
Loading...