Yaundwe Majukwaa ya Wabunge kila Mkoa

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,214
3,587
wpid-bunge-tanzania1.jpg

Taswira kwa hisani ya:

Katika jamii yoyote ile ya binadamu tangu enzi za ujima hata sasa, binadamu wamejiwekea mifumo inayowaongoza katika jamii zao. Ni bahati mbaya sana kwamba siku zote ambazo misuguano ya kimaslahi imetokea katika jamii hizi, huwa lawama zimeelekezwa kwa watu wenye dhamana na hatamu za kuongoza mifumo hiyo na siyo kwa watu wanaoongozwa.

Yawezekana kwamba ndiyo maana siku hizi katika michakato ya mabadiliko ya maboresho ya mifumo hii, mwelekeo wa upepo wa lawama kwa warasimu wa mifumo hii umebadilika na kuwaelekea wanaoongozwa kuwa na wao pia wana mchango katika ama mafanikio au kushindwa kwa mifumo hii na kwamba dhana ya uwajibikaji wa pamoja kwa mafanikio au matatizo ya mifumo hii ni jukumu la wote wanaoongoza na wanaoongozwa katika mifumo hii, yaani jamii nzima.

Lugha huwa inakuwa tamu sana na ya kueleweka kirahisi pale ambapo warasimu wanabebeshwa zigo la lawama za mfumo kushindwa na lugha inakuwa chungu sana na ngumu kueleweka pale ambapo wanaoongozwa katika mifumo hii wanapotupiwa lawama na warasimu kuwa na wao wana mchango katika mfumo kushindwa kutimiza malengo tarajali. Jamii hulazimika kupita katika vipindi vigumu vya mabadiliko ambayo nayo yasiporatibiwa kwa umakini wa ziada huweza kusababisha matatizo makubwa kuliko ilivyotarajiwa na kwamba jamii huweza kusambaratika na kuandika historia hasi kabisa.

Njia ambayo imetafitiwa mara nyingi na kuonekana inafaa katika kubuni maendeleo, kuyapangilia, kuyaelekeza kunakohusika, kuyaratibu na kuyadhibiti; ni jamii kujenga ushirikiano na mshikamano kwa hatua zote za maendeleo hadi kufikia kufaidi matunda yake, kinyume na hapa misuguano itabakia kuwa ni haki ya kuzaliwa ya jamii hizi ambapo hata mazuri yaliyokwishafikiwa yataporomoka na kusambaratika na kubaki historia tu. Dhana ya wagawe ili uwatawale haina nafasi katika kizazi hiki cha leo chenye uelewa, utashi, uwezo, na thubutu kubwa ya kuathiri mambo kwa mtazamo wao.

Ili kufanikisha kujenga ushirikiano na mshikamano wa jamii, hapa ndipo jukumu la msingi sana la warasimu linapodhihiri na kulazimika kwa namna yoyote iwayo ile ndani ya wigo wa sheria kuviishi viapo vyao vya kutumikia jamii iliyowakabidhi dhamana hizo nyeti sana. Katika kufanikisha hili, umakini mkubwa wa ziada unatakiwa kuelekezwa kuhakikisha kuwa jamii nzima isibakie tu kushirikishwa katika hatua zote za msingi na kwamba inapofika hatua ya kugawana matunda ya mchakato wa maendeleo yaliyopatikana basi kundi la wanyonge linabaguliwa kwa vigezo na sheria ambazo zinatafsiriwa na wanyonge hao kuwa ni kandamizi tu.

Bahati mbaya kuwa jamii haijapata kujuwa ni kwa nini makundi maslahi yenye sura ya kimatabaka yanaibuka tu wakati wa kugawana matunda ya mchakato wa maendeleo na kwamba wakati wa kutafuta maendeleo hayo kwa jasho la maji na damu huwa wanajamii wote wanaongea lugha moja inayofanikisha upatikanaji wa matunda hayo pasina kujali kuwa wengine wanashiriki kuyatafuta wakiwa ndani ya ofisi zenye viyoyozi huku wengine wakiwa kwenye jua kali sana.

Na hii imebaki kuwa changamoto kubwa sana kwa watawala kuwa ni vipi wataweza kusimamia na kuratibu kwa ufanisi mkubwa sana usio na manung’uniko; mgawanyo sawia wa keki ya jamii nzima. Ni katika hatua hii ambayo kama ikikosa majibu maridhawa ya udhibiti basi jamii huanza kutafakari hatua za mabadiliko ya mfumo kwenda mbadala wake wakiwa na matumaini makubwa ya kufikia malengo japo wakati mwingine matarajio yao hayo yamekuja kinyume.

Tafsiri nyepesi ya aya mbili hizo hapo juu ni kuwa maendeleo yatafsiriwe kuwa ni ya umma mzima na siyo ya vikundi maslahi ambavyo vinazuka hata nje ya wigo wa sheria huku vikiwa na ngome imara na nguvu kubwa ambavyo vinalenga kujenga matabaka katika jamii iliyokuwa na umoja na amani katika hatua ya mwanzo ya kubuni, kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo na kwamba inapofika hatua ya kufaidi matunda basi vikundi-matabaka hivi vinazaliwa vikiwa na mikakati ya kutishia amani na mshikamano wa jamii hizi.

Andiko hili linatoa changamoto kuwa muda umefika wa taasisi zote kubwa ambazo ni mihimili ya demokrasia katika jamii yetu ya Tanzania ziandike historia mpya ya kuanza kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano wenye lengo la pamoja la kuhudumia umma kwa ufanisi mkubwa unaotokana na bidii na dhamira ya kweli vinavyolenga umma mzima. Mipaka ya mihimili hii inastahili kubaki kama ilivyo kwa nia nzuri sana ya udhibiti miongoni mwao, ila mipaka hii isiwe vikwazo dhidi ya ujenzi wa mshikamano, ushirikiano na umoja kwa maslahi ya umma.

Ni katika mantiki na muktadha huo kwamba andiko pia linatoa changamoto kwa waheshimiwa wabunge wetu kuanzisha uundwaji wa majukwaa yao ya ki-mkoa yenye lengo la kusukuma mbele kwa kasi kubwa harakati za maendeleo ya mikoa yao. Hii isitafsiriwe kinyume kama ni muendelezo wa dhana ya ukanda ambayo haijapata kibali katika jamii yetu kutokana na upinzani mkali dhidi yake.

Majukwaa haya ya ki-mkoa ya waheshimiwa wabunge yaundwe pasina kujali vyama vya siasa, itikadi, mrengo, kabila, imani, rangi, jiografia wala daraja la ubunge yaani wa kuchaguliwa, viti maalum na wakuteuliwa.

Yawe majukwaa ya waheshimiwa wabunge wote na yashirikishe serikali kwa njia ya uwakilishi toka katika ngazi zote za serikali ndani ya mkoa na wadau wengine wa maendeleo.

Hii itasaidia pia watu wote katika mikoa hii wakiongozwa na serikali, wabunge na wawakilishi wa makundi mbalimbali ndani ya mkoa husika kuongea lugha moja ya maendeleo huku wakitekeleza kwa vitendo falsafa ya umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.

Hapa pia majukwaa haya yawe huru kuchota utajiri wa uzoefu, hekima, busara na uelewa wa dhana nzima ya maendeleo katika mikoa yao toka kwenye hazina za watangulizi wao [wabunge wastaafu] na viongozi wastaafu na wanaoendelea na ajira zao ambao wanatoka katika mikoa hiyo.

Uendeshaji wa majukwaa haya lazima uheshimu sheria, kanuni na taratibu za bunge ikiwemo bila kulazimika kuvunja katiba ya nchi wala kwenda kiyume na viapo vya waheshimiwa wabunge. Wananchi katika zama hizi wanahitaji maendeleo zaidi ya itikadi za kisiasa na makundi maslahi yasiyowakilisha umma mzima.

Kimsingi ndoto ya maendeleo kabla ya kutekelezwa; huanzia kwanza kwenye akili ya mtu na kuanza kukuwa na kufikia hatua ya kuwa fikra ambayo ikitafsiriwa hubadilika na kuwa dhana ambayo pia ikitekelezwa kupitia mipango madhubuti basi hutafsirika kama maendeleo kwa matokeo chanya ya utekelezaji wake ambayo kwa msamiati rahisi huitwa matunda ya maendeleo.

Hivyo hali hii huwapo kwa binadamu wote wenye akili timamu na ndiyo dira yao katika maisha yao ambayo wanaweza kuifikia tu pale ambapo watakuwa na mfumo mzuri wa jamii utakaoweza kuwapatia warasimu wenye fikra pevu wa kuweza kutafsiri ndoto ya maendeleo kwenda kwenye uhalisia wake kwa kuongoza jitihada na hatua zote muhimu zinazoweza kuifikisha jamii hiyo katika upatikanaji wa matunda hayo ya maendeleo.

Utekelezaji wa hatua hizi muhimu ndiyo hufanyika mzani wa kupima uwezo wa kiongozi katika kuongoza na kuratibu mchakato mzima kuelekea katika dira tarajali ya maendeleo ya watawaliwa wake ambapo kinyume chake hufanya tafsiri ya kiongozi na dhana nzima ya uongozi kuwa hasi kwa wanajamii wake ambapo kama hakuna misingi na mikakati imara ya kukabiliana na matatizo katika jamii hiyo basi fikra mpya za kudai mabadiliko huzaliwa mioyoni mwa wanajamii na kuwa na shauku kubwa ya kutekeleza mabadiliko hayo kwa gharama iwayo yote ile pasina kujali matokeo yake kama yatakuwa chanya au hasi na bila kujali matokeo hayo yatadumu kwa vizazi vingi au la.

Andiko linapenda kuipa jamii ya kitanzania changamoto kubwa kuwa uchaguzi unapoisha, hatuna budi kila mzalendo pasina kujali nafasi na dhamana yake katika jamii kuweka kando tofauti na misuguano ya kisiasa na kwamba sote tunatakiwa kuongea lugha moja ya kusaka maendeleo kwa udi, uvumba na manemane mpaka tuhakikishe kuwa tunatafsiri ndoto na dira ya maendeleo kwa kuchagiza kwa nguvu zote utekelezaji wa ilani ya uchaguzi inayoshika hatamu na kwa kuhakikisha kuwa tunaziba mianya yote ya uvujaji wa kila kilicho chetu ili kuiepusha jamii na migogoro isiyo lazima ya maslahi. Ni hapa ambapo wenye itikadi mbadala wanatakiwa kuwa walinzi wa kweli wa maslahi ya jamii nzima.

Kwa vile bunge ni chombo nyeti sana ambacho wananchi wanakipa dhamana ya kuisimamia serikali yao, muda ni muafaka sasa kwamba tujaribu kutekeleza dhana hii ya majukwaa ya wabunge katika ngazi ya mikoa ili tuone kama tunaweza kuwa na msimamo mmoja, dhamira moja, na dira moja ya kutufikisha tuendako bila kuiachia jukumu hili zito chama kinachoshinda uchaguzi tu huku wengine tukibaki kuwa watazamaji na wachambuzi tu pasina kujuwa kuwa maendeleo yoyote yanayopatikana huwa yanafaidisha wote walio na chama na wasio na chama, wenye dini na wasio na dini ikiwemo tofauti ya rangi zetu.

Wananchi wanahitaji dhana ya umoja wa waheshimiwa wabunge uzaliwe katika fikra za wabunge wenyewe kwanza ili waje wawaunganishe wananchi pia majimboni kuwa kitu kimoja.

Ushindani wa kiitikadi ufanyikie Bungeni tu kama ilivyo ada na desturi ya demokrasia ya kibunge popote duniani lakini wajapo majimboni hawana budi kuwa kitu kimoja kwa nia ya kuwaunganisha wapiga kura wao pia kuwa kitu kimoja ili kuharakisha maendeleo.

Wananchi wanahitaji kuona umoja wa wabunge wao bila kujali vyama vyao; ukiwaongoza katika kufikia maendeleo na siyo kwamba wanahitaji tofauti za kiitikadi za wabunge wao kwa kipindi chote wawapo madarakani. Tofauti za kiitikadi zina muda wake kama kipindi cha kampeni za uchaguzi na labda huko kwenye vikao vya bunge lakini muda mwingine uwao wote ule uliobaki ni wa kusaka maendeleo.


Dhana ya majukwaa ya wabunge ya mikoa kama ikitekelezwa itasaidia pia kudhibiti utoro wa wabunge majimboni maana wenye hulka ya utoro pasipo sababu za msingi watalazimika kuhitajika kwenye majukwaa haya ili kushiriki kuweka mikakati ya pamoja.

majwalaoriko@yahoo.co.uk
 
Back
Top Bottom