JamiiForums
JF Official Account
- Nov 9, 2006
- 6,227
- 5,267
Leo (Dec 14, 2016) mida ya mchana, polisi kutoka kituo cha Kati, Dar es salaam wakiambatana na Mkurugenzi mtendaji wa Jamii Media, Ndugu Maxence Melo, walifika katika ofisi za Jamii Media kwa ajili ya ukaguzi.
Zoezi hilo limekwenda sambamba na kuwahoji wafanyakazi (Social Media Engagers na Content Quality Controllers) juu ya utendaji wa shughuli zao za kila siku. Baada ya ukaguzi na mahojiano, polisi wameondoka na nyaraka za usajili wa Jamii Media ikiwemo cheti cha mlipa kodi, cheti cha BRELA, leseni ya biashara, n.k.
Pia polisi imewachukua wafanyakazi wawili kwa mahojiano zaidi.
Polisi wameelekea nyumbani kwa Maxence Melo ambako nako wamefanya ukaguzi ndani ya nyumba. Katika zoezi zima la ukaguzi, sehemu zote mbili, Jeshi la Polisi halikuhitaji wala kuchukua kifaa cha mawasiliano ya kimtandao kama router, flash, hard disc, au kompyuta.
Msafara umeelekea Polisi kituo cha kati kukamilisha mahojiano kati ya Mkurugenzi na wafanyakazi wawili waliochukuliwa.
Tunaomba umma utambue kwamba Jamii Media haina servers wala min-server ofisini kwake, nchini Tanzania wala Afrika. Pili, tunaomba watumiaji wa JamiiForums.com wasitiwe wasiwasi juu ya usalama wa taarifa zao. Teknolojia tunayoitumia (encryption) kumsajili mtumiaji wa JamiiForums.com haituwezeshi kumfahamu mtumiaji yeyote labda yeye akubali kwa hiari yake kujiweka wazi mtandaoni.
Imetolewa na Uongozi,
Jamii Media.