Yaliyojiri katika Mkutano Mkuu wa CHADEMA Desemba 18, 2019 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar

Molemo

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
14,534
13,225
WanaJF duniani kote,Wasalaam!

Ni asubuhi tulivu kabisa katika jiji la Dar es Salaam huku habari kubwa inayovuma ikiwa ni mkutano mkuu wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA chenye wanachama milioni 6 na nusu wenye kadi.

Kama ripota wa JF nipo hapa Mlimani City nimekesha kwa lengo moja tu la kuihabarisha dunia kupitia JF kila kitakachojiri.

Leo ni hitimisho la zoezi refu la uchaguzi ambapo Mkutano mkuu utamchagua Mwenyekiti mpya na Makamu wake wawili.

Hata hivyo kuna dosari kidogo ilmetokea kwenye mkesha wa mkutano mkuu ambapo Polisi wenye magari na silaha walivamia eneo la Mlimani City na kushusha bendera zote za CHADEMA zilizopambwa kuashiria Mkutano Mkuu huu.

Haijajulikana hasa sababu ni nini kwa sababu Chama Cha Mapinduzi kinapofanya Mkutano wake Mkuu jijini Dodoma Mji wote na viunga vyake hupambwa kwa bendera za CCM.

Kwa sasa asubuhi hii tayari maandalizi yote ya ukumbi utakakofanyika mkutano mkuu yamekamilika. Tunatarajia takribani wajumbe 1300 kuhudhuria mkutano mkuu huu.Pia wageni wengi wanatarajiwa kuhudhuria wakiwemo viongozi wa vyama vyote vya siasa,mashiriia ya kimataifa ya ndani na nje, viongozi wa dini nk.

Vyombo vyote vya habari vya ndani na nje vimealikwa vikiwemo CNN na BBC.

Tunatarajia kuwaletea Live updates hapa kwa kila kitakachotokea.

4E31FDCE-75C1-480C-841C-02E67FCC9EC4.jpeg


A2DE9165-58DE-4F36-BE2C-B63E98018E58.jpeg





Updates No 2
Muda huu kwa sasa tayari ukumbi umefurika wajumbe na vikundi mbalimbali vinatumbuiza kusubiri ujio wa Kiongozi Mkuu wa chama Freeman Mbowe kuingia ukumbini akiwa na msafara wake.

Naam, kwa sasa Mwenyekiti Freeman Mbowe anawasili huku ukumbi ukiwa umelipuka kwa shangwe hoihoi nderemo na vifijo.Wajumbe wote wamesimama kama heshima kwa shujaa huyu wa mageuzi nchini.

Mkutano Mkuu umeanza rasmi na viongozi wakuu wameshaingia wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na kukaa kwenye viti vyao.

Kwa sasa Meya wa DSM Issaya Mwita ameitwa kuwakaribizha wageni kwenye mkutano mkuu huu

Kwa sasa wankaribishwa na kutambuliwa wageni mbalimbali wa vyama vya siasa vikiwemo NCCR, NLD, CUF, CCK, TLP nk

Wageni wengine waliotambuliwa ni kutoka Taasisi mbalimbali kama Mtandao wa jinsia TZ,Repoa,Walemavu nk Pia wapo viongozi wakuu wa dini.Pia yupo Naibu Msajili wa vyama vya siasa Sixty Nyahoza.

Ubalozi wa Marekani umewakilishwa na wajumbe watatu ambao wamekwisha fika mpaka sasa.

Msomi Dr Azaveli Lwaitama ndiye anayetoa salaam katika mkutano mkuu.Anashutumu watu wasiopenda demokrasia.Na amesema yeye ni mwanachama wa Chadema."Hiki Chama kina maneno mawili muhimu sana, maneno hayo ni Maendeleo na Demokrasia, bila Demokrasia hakuna Maendeleo, Maendeleo yanaletwa na Demokrasia," Prof. Azavery Lwaitama amemalizia.

Sasa anatoa salaam mbunge kutoka Burundi wa chama cha FNL aliyekuja kuwakilisha Burundi.Anatoa salaam kwa Kiswahili na kuchanganya na kiingereza.Ujumbe wake mkubwa ameomba CDM wasikate tamaa

Viongozi wa dini sasa wanazungumza ambapo Sheikh Salum Kundecha Amir wa Shura ya Maimamu ameongea kwa niaba ya waislam.Kwa upandecwa Wakristo anayezungumza ni Askofu Mkuu wa Makanisa ya Moravian Tanzania Emmaus Mwamakula.Askofu Mkuu Mwamakula ameelezea kuhusu haki na ustawi katika kuimarisha demokrasia.

Viongozi wa kanda sasa ndiyo wamekaribishwa kutoa salaam kwa niaba ya kanda zao na ameanza Mwenyekiti wa Kanda ya Pemba akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini na baada ya hapo Kanda ya Magharibi

Kwa ujumla viongozi wengi waliozungumza hasa wa vyama vya upinzani na viongozi wa dini wamemwagia sifa Mwenyekiti Freeman Mbowe kwa hotuba yake aliyoitoa Mwanza na kunyoosha mkono wa maridhiano kwa serikali.

Baada ya viongozi wote wa Kanda kuzungumza ameitwa Msanii Mbunge aa Mikumi Prof Jay kutumbuiza na ameshangiliwa sana na wajumbe.

Baada ya burudani wameanza kuitwa viongozi wa Mabaraza na wameanza viongozi wa Bavicha.Mwenyekiti wa Bavicha John Pambalu amelaani kufukuzwa chuo kwa viongozi wa serikali ya wanafunzi na kusema Bavicha imeshaongea na wanasheria kuona namna ya kuwasaidia.

Salaam za pili za mabaraza zimetoka kwa Baraza la Wazee na katika salaam zake Mwenyekiti wa Wazee amelaani hujuma mbalimbali zinazofanywa dhidi ya kukandamiza demokrasia nchini.Ametoa wito kwa Rais Magufuli kuanza mazungumzo ya kuimarisha demokrasia nchini.

Mwisho limeitwa Baraza la Wanawake Bawacha na Mwenyekiti wake Halima Mdee ambaye ametoa wito wanawake waendelee kuheshimiwa ndani ya Chadema kwani wameonyesha uwezo mkubwa katika kuongoza Chadema na kusema chama kwa ujumla kimeamua kuwekeza kwa wanawake

Baada ya Salaam za mabaraza sasa inafuata burudani kutoka kwa Mbunge Joseph Mbilinyi ikiwa nu kuwaweka watu sawa kwa ajili ya kumkaribisha Mwenyekiti Freeman Mbowe kuhutubia.

Kabla Mwenyekiti kuhutubia Lazaro Nyalandu na Esther Bulaya wameitwa kwa dakika chache kuzungumza na wajumbe.Nyalandu amesema aliamua kuhamia Chadema baada ya kuona CCM ya sasa imeacha njia aliyoasisi baba wa Taifa Mwl Nyerere.Nyalandu amelaani dola kupokonya mamlaka ya Bunge na Mahakama na ndiyo sababu kubwa ya kuachana na chama hicho na kujiunga Chadema.Amesema anasimama katika mkutano mkuu kama Nabii Ezekiel wa Biblia kwa kuiambia CCM anguko lao limefika.Nyalandu amekula kiapo mbele ya mkutano mkuu atasimama na Chadema mpaka mwisho wa Uhai wake na atailinda Chadema mpaka mwusho wake.

Zinafuatia sasa Salaam kutoka Brussels Ubelgiji ambapo Katibu Mkuu amekuja kumkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tundu Antipas Lissu azungumze na wajumbe wote.Lissu ametoa salaam kwa njia ya skype na kupongeza mno kwa kazi kubwa iliyofanyika na Chadema kuzidi kuimarika.Lissu kasema tayari amepona na amekuomba chama kiandae mazingira salama ya yeye kurejea nyumbani.

Updates No 3:
Sasa ni Mwenyekiti Freeman Mbowe anahutubia rasmi wajumbe na Taifa kwa ujumla

Mwenyekiti Mbowe ameelezea mambo mengi na kubwa ni kuomba wajumbe wa Mkutano Mkuu waridhie mabadiliko ya Katiba ili kuongeza adavya mwaka ya uanachama kutoka shilingi 1,000 mpaka shilingi 2,500.Amesema kwa Ada hiyo chama kitakuwa na uwezo wa kukusanya shilingi bilioni 15 kwa mwaka kwa idadi ya wanachama milioni 6 na laki 5 wenye kadi

Pia Mbowe amezindua rasmi mfumo wa Chadema Digital ambapo wanachama eatatumia simu zao kulipa ada na kupata Taarifa zote muhimu

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Mbowe ametoa tamko rasmi la chama kwamba uchaguzi ule ni Haramu na Hautambuliki.Kutokana na sababu hiyo Mbowe ameagiza waliokuwa wagombea wote wa Chadema kote nchini kuunda serikali vivuli kwa ajili ya kuhudumia wananchi.

Mbowe amesifu kampeni ya Chadema ni Msingi ambapo amesema walizunguka kila kijiji nchi nzima na kuandikisha wanachama milioni 6 na nusu.Kiongozi huyo amesema dhihirisho la hicho kilichofanyika ni jinsi Mkutano Mkuu huu ulivyopendeza na kufurika wajumbe

Mbowe kwa kutumia nafasi yake kama Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini amesema ataongoza mazungumzo ya kuunda umoja wwnye nguvu yatakayowahusisha vyama vyote vya siasa,viongozi wa taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Mbowe amesikitishwa na hali iliyofikia sasa ya vyombo vya Habari kuogopa kutangaza habari za Chadema ambapo amesema waliwasiliana na vituo vyote vya Telesheni ili kutangaza mubashara mkutano mkuu Lakini wote waliogopa na kusema ni vigumu kwao kutangaza mkutano wa Chadema.

"Hakuna kitu chenye thamani kuliko uhuru, umoja na utu wetu kiongozi yeyote ambaye ajatambua ulazima wa uhuru wetu hata akifanya kitu gani siwezi kumpongeza" amesema Mbowe

Mbowe amesema , "Magufuli, atuko Chadema kwaajili tunataka kumng’oa madarakani kabla ya uchaguzi mkuu, lakini hatuko tayari kuona nchi hii inaendelea kuendeshwa katika misingi yakubaguana kwahiyo nilichagua kuto kumsifu"

“Vipaumbele vyetu haviko kwenye barabara wala kwenye ndege ni furaha katika familia, uhuru wa watu wetu ni uhuru wa wao wachaguwe wawe chama gani” amesema Mbowe.

"Tunataka Chadema tulete bashasha katika miyoyo ya Watanzania tunataka waone faraja kuwa katika nchi hii, asilimia 90 ya vijana katika nchi yetu ukiwapa fursa ya kwenda nje au kubaki Tanzania, watachagua kwenda nje"- Mbowe ameendelea kusema

"Tunawaambia vyama vingine hasa Chama Cha Mapinduzi tulipo amua kuchagua slogan ya ‘ No hate no fear’ tulikuwa tuna maana kwamba ukatili, visasi siyo sera yetu ameendelea kusema Mbowe.

"Baada ya hotuba yangu tutazindua rasmi mfumo wa chama wa kidigitali kwamba sasa chama chetu kimekuwa, kimejipanga kiteknolojia, tunajua jambo hili litawasumbua wenzetu"- kiongozi huyo ameendelea kusisitiza.

'Tamko la chama ni ‘Hatutambui uchaguzi wowote uliofanyika wa serikali za mitaa, nchi hii kama NEC inampongeza Rais na Rais anaipongeza NEC hivi ni kweli, halafu unaona watu wazima wanashangilia unajua ndiyo sababu nchi yetu imekwama"- Mbowe amesisitiza.

"Uwenyekiti wangu sio wakujitafutia ni wakupewa na wananchi. Tunakwenda kufanaya mambo ambayo hayajafanyika nchi hii au Afrika kwa chama chochote cha kisiasa, kuanzaia mwaka huu tutafanya kitu kinaitwa ‘Digital Campaign’"- Mbowe smemalizia.

Updates No 4
Sekretariati ya Chadema imeamua kutoa Tuzo kwa utumishi uliotukuka kwa wanachama wawili waliotoa muda wao kuhamasisha zoezi la Chadema ni msingi lililozaa mafanikio makubwa kwa chama.Wanachama waliopewa tuzo hizo ni Agnesta Lambert na Freeman Mbowe.Hata hivyo wakati wa kutoa shukrani kwa tuzo hiyo Mwenyekiti Freeman Mbowe aliikataa tuzo hiyo na kusema iwaendee wanachama na viongozi wote waliojitolea muda wao kufanikisha zoezi hilo.

Baada ya hapo limefuatia zoezi la kuzindua sera za chama na viongozi wote wa Kanda wamekabidhiwa nakala kwa niaba ya Kanda zao na hatimaye kupiga picha ya Pamoja na Msajili Msaidizi wa vyama vya siasa nchini kama ishara ya uzindizi.

Na hapa ndipo umefika Mwisho wa sehemu yetu ya kwanza ambapo Mkutano Mkuu umeahirishwa kwa muda kwa ajili ya chakula na baada ya hapo itafuata sehemu ya pili ya uchaguzi mkuu wa chama.

Tunawashukuru wote kwa kuwa nasi hapa tangu Alfajiri ya leo.Mungu Awabariki sana.

#NoHateNoFear

Wasalaam
Molemo wa JF

=======

UPDATES: 19 Dec 2019 (MATOKEO)

MWENYEKITI

Freeman Mbowe 886 (93.5)✔
Cecil Mwambe- 59 (6.2%)
Zilizoharibika: 3

MAKAMU MWENYEKITI BARA
Tundu Lissu-930 (98.8%)✔
Sophia H.Mwakagenda-11 (1..2%)
Zilizoharibika 9

MAKAMU MWENYEKITI ZANZIBARI
SAID ISSA MOHAMED
NDIYO 859 (88.7%)✔
HAPANA 95
Zilizoharibika12


 

Attachments

  • Screenshot_20191218-182644_Facebook.jpg
    Screenshot_20191218-182644_Facebook.jpg
    90.3 KB · Views: 1
  • Leo-nikiwakilisha-Jimbo-la-Bukene-katika-Lumola-Steven-Kahumbi-Facebook.mp4
    9.5 MB
Cecil Mwambe ni damu mbichi japo wahenga wanasema mpini mpya husababisha machacha na njia mpya haikosi visiki na miiba.

Freeman Mbowe ni damu ya mzee japo wahenga wanasema uzee si busara na ukiona nyani mzee ujue amekwepa mishale mingi.

Wakati tunasubiri matokeo rasmi, unadhani kwa siasa za awamu ya tano, nani anafaa kupeperusha bendera ya uenyekiti wa chama kikuu cha upinzani?
 
Hapo msajili wa vyama vya siasa hawezi kutia neno. Anasubiri wafuasi wakatae uonevu ili atoe barua ya onyo kwa chadema. Viongozi wa dini nao wanashihudia kinachoendelea lkn wako kimya. Ngoja tusubiri kuona dini na madhehebu yake watatuma wawakilishi wa aina gani maana siku hizi nao wameshaunga juhudi.
 
Hapo msajili wa vyama vya siasa hawezi kutia neno. Anasubiri wafuasi wakatae uonevu ili atoe barua ya onyo kwa chadema. Viongozi wa dini nao wanashihudia kinachoendelea lkn wako kimya. Ngoja tusubiri kuona dini na madhehebu yake watatuma wawakilishi wa aina gani maana siku hizi nao wameshaunga juhudi.

Usitarajie jipya kutoka kwa hawa Viongozi wa Imani ,wana weza kuyukemea na kutuasa sisi lakini sio kwa watawala Mkuu.
 
Hapo msajili wa vyama vya siasa hawezi kutia neno. Anasubiri wafuasi wakatae uonevu ili atoe barua ya onyo kwa chadema. Viongozi wa dini nao wanashihudia kinachoendelea lkn wako kimya. Ngoja tusubiri kuona dini na madhehebu yake watatuma wawakilishi wa aina gani maana siku hizi nao wameshaunga juhudi.
Nisamehe, yale ni matakataka tu!
 
Back
Top Bottom