Ya wapi maisha bora? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ya wapi maisha bora?

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Ngambo Ngali, May 27, 2010.

 1. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #1
  May 27, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Ya wapi maisha bora, Yale tuloahidiwa,
  Visiwani nako bara, hakika tuliambiwa,
  Mambo kuwa barabara, chama tukikichagua
  Wanaoona waseme, ya wapi Maisha Bora?

  Kauli mbiu ilikuwa, ikawekwa kwenye Chama,
  Hili na lile ikawa, na vinywani wakasema
  Watanzania tutakuwa, na maisha bora na mema
  Waliosikia waseme, ya wapi maisha bora?

  Siku zazidi kimbia, kama vile langalanga,
  Ulingoni kufikia, tunakiona kilanga,
  Maisha yamefifia, kwa wajanja na wajinga
  Waliosema waseme, ya wapi maisha bora?

  Mfano mmoja natoa, usidhani ni utani,
  Mjasiriamali Tanzania, anapita mitaani,
  Plastiki kugombea, mkono uende kinywani
  Hivi hayo utasema, kweli maisha bora?

  Umeme hapa nyumbani, bei juu si utani
  Imeshapita angani, inakaribia juani
  Mlalahoi kabaini, umeme hauwezekani,
  Ni yepi Maisha bora, Yale waliyoyasema?

  Misosi acha kusema, haiingii kinywani
  Tanzania sio pema, kusema utatamani,
  Sukari kitu lazima, buku mbili karibuni,
  Maisha bora ni ndoto, walizoziota wenzetu.

  Nishati usijaribu, kuingia kituoni,
  Mkweche wako jaribu, dizeli waitamani,
  Hapo watakapojibu, haitakaa akilini,
  Lita elfu mia saba, je haya maisha bora?


  Ni mengi ningeyataja, nawaachia wenzangu,
  Anyisile hebu chuja, bila kujali undugu,
  Kama wengine mwaja, kujibu tatizo langu,
  Maisha yaliyo bora, Ni kweli tumeyapata?

  Ningeweza endelea, vidole vyatetemeka,
  Huruma namuonea, wale waliojikweka
  Kuni, jembe na shoka, mpaka jua latoweka
  Hawajui walani, kujaza matumbo yao.
  [FONT=&quot]Lakini bado waambiwa, maisha bora yaaja[/FONT]
   
 2. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #2
  May 27, 2010
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,666
  Likes Received: 164
  Trophy Points: 160
  Bahati mbaya mimi sio fundi wa mashairi ningeongeza beti kadhaa. Ubarikiwe mkuu kwa shairi safi
   
 3. The Son of Man

  The Son of Man JF-Expert Member

  #3
  May 27, 2010
  Joined: Feb 9, 2010
  Messages: 12,126
  Likes Received: 1,705
  Trophy Points: 280
  Maisha bora kwa watz na uongozi huu hayawezekani!
   
 4. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #4
  May 27, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,304
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 135

  Walitufanya majuha,
  Kutukosesha furaha,
  Na za uongo nasaha,
  Tena huku wakihaha,

  Asante Ngambo Ngali,
  Kwa lako zuri swali,
  Tabidi kuwa wakali,
  Na wayajibu maswali,

  Kweli mbuzi yake kamba,
  Ipo siku twawabamba,
  Kama mvuvi na kamba,
  Baharini akitamba.

  Wametulisha upepo,
  Bila hiari kuwepo,
  Na wamejifanya popo,
  Na bila miti kuwapo.

  Maisha bora ya wapi,
  Hatutaki jibu fupi,
  Ukweli wao u wapi,
  Tusidanganywe kwa pipi.

  Watanzania tungane,
  Pamoja tushikamane,
  Tena tusikunje nne,
  Sote tushirikiane.
   
 5. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #5
  May 28, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Jamaa tumeg'amua, shere walotuchezea
  Na sasa wameamua, kutuletea hadaa
  Kwani wameelewa, maisha bora yapaa
  Jamaa wameshituka, uongo tumebaini.

  Baada ya muda kupita, ahadi haijawa kweli
  Mikakati kutafuta, kuwapata wafadhili
  Na jibu wakalipata, wakatangaza na dili
  Ni afadhali kununua, kulikoni kudanganya

  Mojawapo kasimama, bajeti kakatua
  Na jibu akanguruma, ili kiti kuchukua
  Mafedha ya wakulima,lazima kuyachukua
  Ili waweze shinda, lazima kuwe na pesa

  Keti chini usikie, ni hamsini bilioni
  Hizi ndio wapatiwe, kuwaingiza kitini,
  Usukani wachukue, kuturudisha shidani
  Fedha zote ni za nini, wakati maisha ni bora

  Wahenga waliyasema, pale palipo udhia
  Na wewe umekwama, kweli penyeza rupia
  Ili uweze simama, ndicho wachokusudia
  Hawa watu wenye chama, na sasa wameamua
  Kura sasa ni bidhaa, wa wala si ridhaa.

  Anyisile nakubali, Watanzania tuungane,
  Pamoja tushikamane, tena tusikunje nne,
  Sote tushirikiane, kuyakataa mapene

  Bilioni hizo zao, tuzione kama sumu
   
 6. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #6
  May 31, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,304
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 135
  Ngambo Ngali umenena, tena kwa hisia kali,
  Ukweli siyo fitina, yapasa kuwa wakali,
  Tuwaumbue firuna, kwa kutumia akili,
  Yabidi kuwa makini, na yao fedha haramu.

  Nyingi ahadi kupewa, tena pasi na aibu,
  Tumekuwa waonewa, tena tumekuwa bubu,
  Hawataki kosolewa, eti na tusijaribu,
  Yabidi kuwa makini, na yao fedha haramu.

  Tusiogope vichaka, kuanzisha njia mpya,
  Wenye panga na mashoka, hata wale na pataya,
  Tusimame bila choka, sisikilize riwaya,
  Yabidi kuwa makini, na yao fedha haramu.

  Hawafai tena hawa, tena wote wameoza,
  Wafanana na haluwa, isofanana na chaza,
  Na wamelegea hawa, na hawawezi jikaza,
  Yabidi kuwa makini na yao fedha haramu.

  Yabidi kuwa makini na yao fedha haramu,
  Watufanya masikini, wa akili na fahamu,
  Tena hazimo kichwani, sote ni wenda wazimu,
  Yabidi kuwa makini, na yao fedha haramu.

  Sote tena kwa umoja, twelimishane pamoja,
  Ni sisi wenye haja, kuutengeneza umoja,
  Kabla ya mwingine kuja, kutuletea viroja,
  Yabidi kuwa makini na yao fedha haramu
   
 7. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #7
  Jun 1, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Sote tena kwa pamoja, twelimishane pamoja,
  Ni sisi wenye haja, kuutengeneza umoja
  Kabla ya wengine kuja, kutuletea viroja
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora.

  Kudai kilicho bora, kazi rahisi hakika
  Siku ya kupiga kura, alfajiri waamka
  Haitakuwa hasara, kwani haki waitaka
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

  Kama fedha wamekupa, tuliza zako akili
  Wala usilete pupa, icheze vizuri dili
  Chagua aliye supa, muache wa pilipili
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

  Miaka mitano sasa, hakuna walichofanya
  Mwanajipiga misasa, vihela kutudanganya
  Kwa kutumia mapesa, haki zetu kunyang'anya
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

  Njia mpya nabaini, kwa mbali yajongelea
  Tusafiri vijijini, mambo haya kueleza
  Hela chafu si utani, demokrasi inaua
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

  Tuhubiri kila kona, sokoni na mashuleni
  Kwa marefu na mapana, sebuleni na vyumbani
  Uwezo hawana tena, sasa hatuwatamani
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

  Twataka kilicho bora,kuliko hiki cha enzi
  Mwanza Mbeya na Tabora, uacheni usingizi
  Tuwe makini na kura, tusije leta ajizi
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

  Hela zao tuzitupe, kama vile ni uchafu
  Kwenye giza na kweupe, panapo anga na sakafu
  Lazima tuwe mapepe, pasi kuwepo na hofu
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

  Anyisile namaliza, Bujibuji muambie
  Tunaweza kutimiza, vijana tuwaimbie
  Wazee kuwahimiza, wamama wasaidie
  Waungwana amkeni, kudai kilicho bora

   
 8. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #8
  Jun 2, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,304
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 135

  Kudai kilicho bora, ni kweli si kazi ngumu,
  Tusitumie bakora, kusababisha ugumu,
  Tusiruke kama chura, na mbeleni kutodumu
  Hekima yahitajika, kulijenga taifa bora.

  Kweli haki twaitaka, waungwana amkeni,
  Kuziondoa hizi taka, zisishike usukani,
  Hatuyaki mashaka, kupoteza umakini,
  Hekima yahitajika, kujenga taifa bora.

  Miaka mitano sasa, hakuna walichofanya,
  Wamezidi kwa anasa, na zao tabia mbaya,
  Wamezidisha mikasa, tena hawana haya,
  Hekima yahitajika, kujenga taifa bora.

  Njia moja ilobaki, hata mimi naiona,
  Tung'oe vyote visiki, maendeleo kuona,
  Tuache zetu hamaki, jema tukishaliona,
  Hekima yahitajika, kujenga taifa bora.

  Kalamu siraha kubwa, Bujibuji tamweleza,
  Naye Mundu bwna mkubwa, tazidi kumhimiza,
  Tusiogope wakubwa, mabaya kuyachomoza,
  Hekima yahitajika, kujenga taifa bora.

  Wakikupa we pokea, akili mwako kichwani,
  Tena sije wafokea, upoteze tumaini,
  Malengo kujiwekea, ili uwe wa thamani,
  Hekima yahitajika, kujenga taifa bora.

  Ili kuweza fikia, kwenye yale yalo bora,
  Lazima kuwafukia, woote wasiyo bora,
  Vijijini kuwafikia, kuwapa elimu bora,
  Hekima yahitajika, kujenga taifa bora.
   
 9. Zed

  Zed JF-Expert Member

  #9
  Jun 4, 2010
  Joined: Mar 28, 2009
  Messages: 359
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Maisha bora kwa kila mtanzania yapo katika kijitabu cha ilani ya uchaguzi CCM 2005... ukiyataka jipatie nakala.
   
 10. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #10
  Jun 5, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,304
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 135
  hee!! ama kweli kuna kazi ya ziada
   
 11. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #11
  Jun 6, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Walisimama jukwaani, kauli walizitoa
  Ofisini mikutanoni, bayana kuelezea
  Maisha bora nyumbani, wao wangetupatia
  Hakika hawakusema, kitu juu ya kitabu.

  Ilani ya uchaguzi, haiongezi ugali
  Kuupata ufumbuzi, tunalisemea hili
  Sisi si wanafunzi, kuvipekua vitabu
  Tukitaka maisha bora, tuwaondoe wakongwe

  Ilani hiyo kitabu, lakima kutekeleza
  Kama inaleta taabu, shurti kutelekeza
  Hii ndio sababu, nataka kuwaeleza
  Hatuna maisha bora, wakongwe wapumzike

  Sasa miongo mitano, hakuna tulichonacho
  Inatuuma mikono, tunaitoa mimacho
  Sana sana ni kibano, hakuna tulichonacho
  Chama kikongwe bai, pumzikeni salama

  Wakati umewadia, ni Oktoba hakika
  Sehemu ya historia, oktoba ikilazimika,
  Lazima kusaidia, kura kuziandika,
  Ukipewa karatasi, usichague wakongwe.
  Wameshindwa siku zote, kamwe sasa hawawezi
   
 12. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #12
  Jun 6, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Kazi ipo yaani ukiwa na nakala ya ilani ya uchaguzi utapata maisha bora? Tunataka utekelezaji bwana sio maandishi, ona waziri mkuu wa Japani kashindwa ahadi moja tuu kaachia ngazi
   
 13. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #13
  Jun 6, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Hekima yahitajika, kujenga taifa bora
  Kilicho bora twataka, tutakipata kwa kura
  Akili zahitajika, mambo yawe barabara
  Jamani tuhimizane, Oktoba i karibu

  Uchaguzi ndio njia, kuondoa wasofaa
  Madaraka washikilia, haki kweli wamechoka
  Na sasa wasubiria, Oktoba itapofika
  Jamani tuangalie, tena tusidanganyike

  Tuwape elimu bora, ndugu zetu vijijini
  Siku ya kupiga kura, wasiingizwe mjini
  Wasizifanye papara, waongo kuwabaini
  Kama hicho watafanya, maisha bora si haba
   
 14. Zed

  Zed JF-Expert Member

  #14
  Jun 9, 2010
  Joined: Mar 28, 2009
  Messages: 359
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Lazima Oktoba tujiulize ya wapi maisha bora waliyotuahidi? Hivi sasa tunayo bora maisha... kesho na kesho kutwa hatujui... langu wazo ni kejeli kwao... Je maisha bora yatakuwapo kwenye ilani ya 2010 tena?
   
Loading...