Ya Usafiri Kigamboni ba Wimbo wa Gezaulole zama hizo! (Makala, Mwananchi)

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246







Sunday, 08 January 2012 11:43

Na Maggid Mjengwa


Gezaulole baba, Gezaulole mama ee,Twendeni Kibugumo na Mwanadilato
kwenye makao mapya,Gezaulole baba, Geza ulole mama eee!
Ndugu zangu,
Hapa nanukuu gazeti la Mwananchi Jumatano juma la jana; Majuzi, Dk Magufuli alifanya ziara ya ghafla katika eneo la vivuko hivyo na kuwaambia wananchi waliomzomea kwamba kama wakishindwa kulipa nauli hiyo ya Sh200 ni vyema wakapiga mbizi baharini au kuzunguka Kongowe kuingia katikati ya jiji au warudi vijijini wakalime.- Mwisho wa kunukuu. (Mwananchi, Jumatano, Januari 4, 2012)

Utotoni katika jiji la Dar es Salaam, nilishuhudia kwa macho yangu msako wa wazururaji. Niliona jinsi mgambo wa jiji walivyokuwa wakiwadhalilisha vijana na watu wazima kwa kuwakamata, kuwafunga mashati na kuwapandisha kwenye malori tayari kwa safari za kwenda Gezaulole. Kosa lao? Walikuwa wakizurura mijini bila kazi. Hivi, anayetafuta kazi atabaki nyumbani kuisubiri, si ni lazima apige mguu kuitafuta? Sijui leo ungefanyika msako wa wazururaji Dar yangehitajika malori mangapi?

Na miaka ile ya sabini tulipokuwa watoto tulisikia hata nyimbo za redioni kuhimiza wazururaji waende kwenye vijiji vipya vilivyoandaliwa na Serikali kama makazi ya Wazururaji. Watoto wa enzi hizo huenda tunakumbuka wimbo huu;

Gezaulole baba, Gezaulole mama ee,Twendeni Kibugumo na Mwanadilato kwenye makao mapya,
Gezaulole baba, Geza ulole mama eee!

Na Kigamboni ya enzi hizo ilikuwa shamba kweli. Wengi wa waliofikishwa huko Gezaulole na vijiji vingine kule Kigamboni wakayaanza maisha mapya ya vijijini.

Kuna waliokimbia Gezaulole wakarudi tena mjini au kwenye vijiji vyao vya asili. Kuna waliobaki huko Gezaulole, wakafyeka mapori yao. Wakaanza kilimo. Wakaizoea hali mpya. Wakajenga familia zao huko.

Ajabu, leo wenye fedha ndio wanaokwenda kuyanunua kwa bei ya hadaa, maeneo ya watoto na wajukuu wa wazururaji wa enzi za Mwalimu. Kuna watoto na wajukuu wa wazururaji waliobaki na vieneo vidogo. Miongoni mwao ndio hao wanaofanya shughuli za kusukuma mikokoteni na kuendesha maguta.

Ndio hao, waliokisikia kilio cha kutaka uwepo wa pantoni ya uhakika kwa miaka nenda , miaka rudi. Wamesikia kilio cha kujengewa daraja pia na ahadi zake. Na sasa wanaongezewa nauli ya kivuko kwenda na kurudi mjini.
Ni hivi; mkazi wa Magomeni hata kama hana nauli anaweza kutembea kwa miguu kukatisha Jangwani na akamwona mgonjwa wake Muhimbili, au kwenda kuhangaikia kibarua Kariakoo. Na jioni ikifika, hata kama hana nauli ya daladala, atakatisha Jangwani na kufika Magomeni kwenye chumba chake cha kupanga.

Lakini, mkazi wa Kigamboni kama hana nauli ya mia mbili ya pantoni na kama anataka kuvuka kwenda kumwona mgonjwa wake Muhimbili au kuhangaikia kibarua Kariakoo ana mawili, kwa mujibu wa Magufuli; ama apige mbizi au azungukie Kongowe, kwa miguu, mwendo wa nusu siku kama si siku nzima. Na hapa ndipo ilipo hoja ya msingi ya kumfikiria mtu wa kawaida wa Kigamboni, Gezaulole na kwingineko ngambo ya pili ya bahari.

Na hali ya uchumi wetu kwa sasa si nzuri. Kule Kigamboni na vijiji vyake bado kuna wengi wanaojishughulisha na kilimo. Tunafanya makosa kuweka viwango vya juu vya ushuru huku kiuchumi jambo hilo liko wazi; kuwa litayafanya maisha ya mtu wa kawaida kiuchumi yawe magumu zaidi.

Kupanda kwa ushuru kusikoenda sambamba na kuongezeka kwa kipato cha wakazi wa Kigamboni kuna maana moja tu; kuwa gharama za bidhaa na huduma zitapanda kwa watu wa Kigamboni. Lakini si kwa Mtanzania wa Kigamboni tu. Hata wakazi wa jiji walio nje ya Kigamboni nao wataathirika kwa kupanda kwa kiwango cha juu cha ushuru wa kuvusha bidhaa na abiria kwenye kivuko cha Kigamboni.

Maana tunajua, kuwa kuna tani nyingi za mazao ya nafaka na matunda yanayovushwa kutoka Kigamboni na kuletwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuongezeka ushuru kwa zaidi ya asilimia mia moja kiuchumi kuna maana ya kuongezeka kwa gharama ya bidhaa zinazovushwa na hivyo basi kuongezeka kwa bei. Hilo halitachangia kuongezeka kwa uzalishaji, litadumaza. Halitasaidia kuchangia kukua kwa uchumi.

Nauli na ushuru mpya ulioongezeka haviwatakii Wanakigamboni Safari Njema ya kiuchumi bali ni kuwatakia ' Wazame Salama!' Kiuchumi kama hawawezi kupiga mbizi!

Kwa hakika, ukisoma na kutafakari viwango vipya vya ushuru wa kuvuka na pantoni ndipo utakapoelewa kuwa waliofanya maamuzi ya kupandisha viwango hivyo walikurupuka. Viwango hivyo ni sawa na ' Kuwachoma walalahoi ganzi ya kiuchumi'. Ni hao ndio watakaohumia zaidi.

Vinginevyo, kwa kusema kuwa asiye na nauli arudi kijijini akalime ina maana pia, kuwa kuishi Jangwani, Mburahati na Mabibo kunaweza kuwa na nafuu zaidi kwa mtu wa Kigamboni mwenye hali ngumu kiuchumi. Kwamba hatimaye tunawaambia watoto na wajukuu wa wazururaji wa enzi za Mwalimu; Rudini mjini. Na wimbo ule leo labda ungeimbwa hivi;

Mburahati mama, Mburahati baba ee,

Rudini Jangwani, na Mwananyamala kwenye maisha bora!
Haki ya Mungu!

Ni tafsiri yangu tu.
Maggid Mjengwa,
Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo



 
Back
Top Bottom