Ya Ekelege Wa TBS Na Akina Filikunjombe- Tafsiri Yangu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ya Ekelege Wa TBS Na Akina Filikunjombe- Tafsiri Yangu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Jan 29, 2012.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Jan 29, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180


  ”Ex Africa simper aliquid novi". Maana yake: "Kila kukicha kitazuka kioja kingine Afrika."- PTOLEMY, mwanafalsafa wa Kiyunani alipata kuandika:

  Ndugu zangu,


  Wakati mwingine unapotazama kinachowasilishwa kwenye runinga ni kama vile unaangalia mchezo wa kuigiza. Juzi usiku niliangalia taarifa ya habari ya TBC 1. Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma ilikuwa ikimkaanga Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la viwango Tanzania, TBS. Ni kioja kingine katika vingi tunavyovishuhudia kila kunapokucha. Yale yale- Ex Africa simper aliquid nava!


  Naam, kwa kuangalia kilichokuwa kikionyeshwa na TBC1, basi, unapata hofu, kuwa katika nchi hii hatuna Tanzania Bureau of Standards bali Tanzania Bureau of Sanaaz! Na hakika, taarifa ile inaonyesha, kuwa, tumekubali wenyewe, kuwa katika nchi hii, idara nyeti kama ile ya kudhibiti viwango vya bidhaa iongozwe kitapeli-tapeli. Kwa kweli iInatisha.


  Maana tumeambiwa, kuwa TBS hawana ofisi Singapore na Hong-Kong. Wana ofisi hewa. Hivyo basi, na makusanyo ya dola mia tatu za gharama za kuangalia viwango kwa gari moja yanaishia kwenye mifuko ya wajanja.

  Tumeambiwa kuwa hata Wabunge hao walipokuwa huko waliweza kununua stika feki za TBS kwenye mitaa ya huko Singapore! Hiyo yaweza kumaanisha pia, kuwa hata baadhi ya bidhaa tunazonunua hapa nchini zimewekwa stika feki za TBS.

  Ndugu zangu,


  Huu ni uhalifu mkubwa. Na kioja katika hili, mtuhumiwa wa kwanza kwenye uhalifu huu anaruhusiwa kubaki na funguo ya ofisi. Kwamba na kesho Jumatatu atatinga ofisini. “Rushwa hii ni kama kansa ya damu”- Alipata kutamka Mwalimu Nyerere. Na hakika rushwa inatutafuna. Taifa linaangamia.


  Tuliona, kuwa Wabunge wale waliishia kumwomba Katibu Mkuu Joyce Mapunjo alinde heshima yake kwa kutoendelea kumbeba Ekelege. Na hapa ndipo lilipo tatizo la Msingi. Ni kasoro za kimfumo. Wabunge wanasema wana mengi ya kusema kuhusu Ekelege. Mengine watayasema bungeni. Hili nalo ni tatizo. Kwanini wasiyaseme yote?


  Tunarudi kule kule, Wabunge wetu wana kwenda ku-deal na Ekelege na si mfumo. Tunasahau, kuwa mfumo tulio nao ndio unaozalisha akina Ekelege kwa maelfu. Na huyo Ekelege wa TBS anaweza kuwa ni samaki wa ukubwa wa kati. Katika nchi kuna kina ‘ Mi-Kelege’ kwa maana ya samaki wakubwa na ‘ Vi-Ekelege’. Hao wa mwisho ni kama dagaa kwenye kundi la akina Ekelege.


  Ndio, tatizo ni mfumo. Katiba yetu ya sasa inaifanya ofisi ya CAG isiwe na meno ya kuuma, iishie kubweka tu, na wakati mwingine isibweke sana. Katiba yetu ya sasa inamfanya CAG awajibike kwa aliyemteua, na hapa ni Rais anayetokana na chama. Hivyo basi, kuna chama cha siasa pia , ambacho CAG anawajibika nacho na anachopaswa kukiogopa katika utekelezaji wa majukumu yake.

  Si tuliona kigugumizi cha CAG kwenye suala la Jairo na Luhanjo.


  Na tuna Kamati za Bunge mfano wa hii ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma. Nayo pia, kwa Katiba yetu ya sasa haina meno. Inaishia kubweka na wakati mwingine haitakiwi kubweka sana kama kubweka huko kutahatarisha ’ maslahi’ ya Chama tawala chenye wajumbe wengi kwenye Kamati za Bunge.


  Ni juzi hapa Kamati ya akina Filikunjombe imebweka sana. Lakini, inasikitisha, kuwa Katiba ya sasa imeinyima Kamati hiyo meno ya kuuma. Si ndio maana tukasikia, kuwa hata Mbunge yule wa Mwibara , Kangi Lugora akitamba kuwa , wakiwa Singapore alishakunja shati na ngumi pia. Akamrushia konde la hasira Ekelege, na amesema mwenyewe, kuwa kama si Filikunjombe kulidaka konde lake, basi, mambo yangekuwa mengine.


  Hapa Mbunge Kangi Lugora anadhihirisha tatizo hili la kimsingi la Kamati kukosa meno. Labda aliona kubweka peke yake hakutoshi, na kwa vile meno hana, basi, akaamua kukunja ngumi ili watwangwane makonde na Ekelege. Kitendo cha Mbunge Lugora ni kosa la jinai na pia ni utovu wa nidhamu. Ni kitendo cha aibu kufanywa na mtu mzima yeyote, iwe nyumbani au ugenini.


  Ndio, inaturudisha kwenye kuangalia upya mfumo wetu na hasa Katiba yetu ili walau tupunguze hatari ya wabunge wetu kupewa majina ya Tysons na Matumlaz! Kwenye masuala ya kisiasa na kijamii hakuna kupambana kwa ngumi, bali nguvu za hoja. Na yenye kukiuka sheria, kanuni na taratibu huamuliwa kwa kufuata matatu hayo na ikibidi kwa kutumia mamlaka za kisheria, basi.


  Tufanye nini?


  Mabadiliko ya Katiba yanayokuja yaipe meno ofisi ya CAG na hasa kwa kuifanya taasisi hiyo muhimu kuwa inayojitegemea. Ofisi ya CAG kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali iwe na mamlaka ya kuwafungulia mashtaka watuhumiwa uhalifu kwenye Mahakama Huru . Na tunaposema mahakama huru ina maana Majaji wa Mahakama wasitokane na uteuzi wa Rais.

  Na Kamati za akina Filikunjombe?


  Katiba mpya ihakikishe inapunguza uwezekano wa wajumbe wa Kamati za Bunge kufanya safari nyingi nje ya nchi kwa ziara za kazi ambazo zingefanywa na ujumbe wa watu wawili au hata kutumia maafisa wa balozi zetu walio katika nchi husika. Kwa kweli, ziara ya Kamati ya Bunge yenye wajumbe wasiopungua wanane kwenda Singapore na Hongkong kutafuta ukweli wa kama TBS ina ofisi huko ni ufujaji wa fedha za wananchi. Tunaamini, kuwa Balozi wetu aliyeko China angepewa jukumu hilo angeweza kuja na majibu kama hayo ya akina Filikunjombe. Hii ni tafsiri yangu.


  Maggid Mjengwa,

  Iringa,
  Jumapili, Januari 29, 2012
  Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
   
 2. Japhari Shabani (RIP)

  Japhari Shabani (RIP) R I P

  #2
  Jan 29, 2012
  Joined: Jan 16, 2007
  Messages: 721
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 0
  Kwa nchi yetu kila idara au taasisi ni mradi madudu haya yaopo kila sehemu hata Ikulu yenyewe kila mtu anakula au anafanya ufisadi kwa nafasi yake hakuna wa kumuwajibisha mwingine,kila kiongozi ana madudu yake.Wanagawana rasilimali zetu hii ndiyo sera ya siri ya chama tawala CCM.Inauma lakini huu ndio ukweli,kama Mh.Rais JK alesema hajui kwanini Tanzania masikini jibu alitafute hapa.MUNGU IBARIKI TANZANIA.
   
Loading...