Ya Achebe, Ngugi na Siasa Za Tanzania

Idimi

JF-Expert Member
Mar 18, 2007
14,963
10,457
Kwa kweli siasa zina mambo sana. Kwa wengi waliosoma elimu ya sekondari Tanzania miaka ya themanini na tisini (na pengine hata sasa) nadhani sio rahisi sana kuwasahau waandishi wawili muhimu sana wa fasihi wa Afrika. Waandishi hawa ni Chinua Achebe wa Nigeria na Ngugi wa Thiong’o kutoka Kenya. Watu hawa wamekuwa ni sehemu kubwa ya mabadiliko ya kisiasa mwa nchi nyingi za Kiafrika. Hata mabadiliko ya kisiasa yanayotokea sasa nchini mwetu yaliwahi kuandikwa na waandishi hawa kwa nyakati tofauti, kuhusu siasa za Afrika. Wameandika sana kuhusu historia ya Afrika, kwa mtindo wa fasihi, kiasi kwamba wanawavisha uhusika watu katika vitabu vyao kiasi kwamba mtu unapata picha kamili ya nini kilitokea zama hizo.
Nimeamua kuwakumbuka hawa waandishi adhimu kutokana na vuguvugu la siasa nchini mwetu na kuona jinsi siasa za Afrika kwa ujumla wake zinavyoshabihiana. Tanzania ni kama zilivyo nchi nyingine za Kiafrika, kwa hiyo kinachotokea kwa wenzetu huenda kilitokea ama kikatokea na kwetu pia.
Ukisoma kitabu cha Chinua Achebe cha ’A Man of the People’ ambapo wahusika wakuu ni waziri wa utamaduni Chifu Nanga na mwalimu Odili Samalu, utabaini nilichodondoa hapo juu. Chifu Nanga na kundi la mawaziri wenzake maharamia walikuwa wamehodhi madaraka ya nchi kiasi kwamba wenzao wote wasio wa kundi lao walikuwa hawana suala la kusema iwapo mmojawapo wa vigogo wa kundi hili atafanya maamuzi. Kulipotokea kuporomoka kwa uchumi nchini mwao, waziri wa kilimo alipendekeza kuongeza uzalishaji wa kahawa, ambapo kwa kipindi hicho ndio lilikuwa zao kuu la biashara la liliiletea nchi pesa nyingi za kigeni. Mawaziri wenzie mafisadi wakamnyamazisha waziri huyu. Badala yake wakaishauri serikali ichapishe pesa nyingi zaidi ili ziwekwe katika mzunguko! (Nadhani wachumi watanisaidia hapa, kama hatua hii ni mwafaka). Matokeo yake uchumi wa nchi ukawa unaporomoka kwa kasi.
Mwalimu Odili yeye alikuwa na mawazo tofauti na serikali (iliyokuwa chini ya akina Chifu Nanga) juu ya namna bora ya kukuza uchumi. Mwalimu huyu akaamua kugombea ubunge katika jimbo analoongoza hasimu wake wa kisiasa Chifu Nanga. Kama haitoshi, Chifu Nanga anamshawishi mpenzi wa Odili na kumtorosha. Kwa hiyo Odili aligombea kwa malengo mawili ikiwa ni pamoja na kumyang’anya jimbo Chifu Nanga kama kulipiza kisasi kwa kuporwa mpenziwe.
Kwa kufupisha hadithi hii ni kwamba wakati wa kampeni za Odili kulitokea vurugu sana zilizosababishwa na wafuasi wa chifu Nanga kiasi kwamba serikali iliingilia kati na kufanya mapinduzi ya kuwaondoa mafisadi katika madaraka. Baada ya mapinduzi, kigogo Chifu Nanga alikuwa anataka kutoroka kwa kutumia mtumbwi (alivaa kama mvuvi), bahati haikuwa yake kwani alikamatwa na kufunguliwa mashataka kwa kuhujumu uchumi.
Hali kadhalika, kitabu cha Ngungi wa Thiong’o kiitwacho ’Petals of Blood’ kina maudhui yanayofanana na hayo hapo juu. Wahusika wakuu katika kitabu hiki ni vigogo wenye pesa chafu akina Chui, Kimeria na Mzigo. Wahusika wengine ni mwalimu Karega, mjasiriamali Abdulla na dada aliyekuwa anajiuza aliyeitwa Wanja. Kwa ujumla kitabu kinasimulia jinsi nchi aliyoitaja mwandishi ilivyokuwa imetopea kwa ufisadi, michango isiyoisha na kutowajibika kwa viongozi kwa wapiga kura wao. Mwandishi anasimulia jinsi wananchi walivyokuwa wamekabiliwa na njaa baada ya ukame na kumwendea mbunge wao kwa msaada, na jinsi mbunge alivyowatolea nje. Ujumbe wa kwenda kwa mwakilishi wao huyu kupata utatuzi wa shida zao uliongozwa na Wanja na Abdulla. Wanja aligeuka kahaba baada ya serikali kuchukua mashamba yaliyokuwa yanampa riziki aliyorithi kutoka kwa wazazi wake bila fidia. Mashamba hayo ya Wanja na wananchi wengine yalichukuliwa ili kupisha ujenzi wa barabara ya kuunganisha nchi yao na sehemu nyingine za Afrika (Trans Africa Highway) na upanuzi wa mji. Kijiji alichokuwa anaishi pia kikachukuliwa na kubadilishwa kuwa jiji kubwa na wamiliki wa vitegauchumi wa jiji hili miongoni wakawa akina Chui, Kimeria na Mzigo. Ikumbukwe kuwa ni hawa waliokuwa wameshiriki kunyang’anya mashamba ya wananchi. Kwa ujumla mwandishi anasimulia jinsi wananchi walivyokuwa wameichoka serikali yao, kwani ilikuwa haitendi kile walichoiagiza wala kile walichoahidi katika kampeni zao. Matokeo yake, kuna siku mbunge litupiwa maganda ya machungwa usoni baada ya kutoa majibu yasiyowaridhisha wapiga kura wake (hata Tanzania hii inatokea, kwa kuzomea wabunge). Hatima ya yote ikawa ni baadhi ya wananchi kuchukua hatua mikononi kwa kuwachoma moto watu waliokuwa wanatuhumiwa kwa uharamia wa uchumi, ambao ni Chui, Kimeria na Mzigo. *Nilisoma vitabu hivi kitambo kidogo, hivyo kama nitakuwa nimekosea majina ya wahusika mnisahihishe*
Simulizi hizo mbili kutoka kwa wanafasihi mahiri wa Afrika zinatufundisha mambo mengi sana ambayo sisi wapiga kura na watawala wetu tunapaswa kujifunza. Kwamba cheo ni dhamana na hufi nacho, leo unacho na kesho wapiga kura wakiamua kuchukua basi ujue hunacho. Viongozi wetu hawataki kuwajibika kwa wapiga kura wao. Kwamba, wananchi wanapoamua kukaa kimya wakati baadhi ya mambo yanapotendeka sio kwamba wanakuwa mbumbumbu, ila wanatafakari nini cha kufanya, na wakiamua hakuna wa kuwazuia, wanafanya! Viongozi wetu wasitake wapiga kura wao wakafikia hatua ya kuanza kuwarushia mawe na maganda ya machungwa (hii imetokea Dar es Salaam tayari), kwani hii dalili ya hatua za mwisho kabisa ambazo wananchi wanaamua kuchukua baada ya kuona kuwa mambo yanaenda vile wasivyotaka. Nisingependa tufike mbali zaidi ya hapa.
Mungu Ibariki Tanzania.
 
Salvation shall come from the hills,from the blood which flow in my veins , i say a son shall rise ,his duty will be to serve and lead the people. ...Ngugi Wa Thiong'o in (WEEP NOT CHILD)

Have this prophecy been fullfiled to the Tanzanian society?
 
yes we need jesus for our life, I become jesus, you become jesus, we all become jesus for each other, I die for you, you die for me we die for each other, to save our land.

and he who will lose his life for my sake will gain it, and he who will gain it will lose it......dont you see that cain was wrong. i am my brothers keeper ( Kihika in grain of wheat by Ngugi)
 
Mkuu Mtupori heshima mbele,
kweli umenikumbusha mbali sana miaka ile nilipokuwa A-level.Kweli hao kina Ngugi na Achebe utafikiri wanaiongelea Tanzania yetu ya leo hii,pia ningependa kukukumbusha ile play ya "AN ENEMY OF THE PEOPLE" inayomhusu Dr. Peter Stockmann na juhudi zake za kupambana na viongozi mafisadi ambao mpaka wanazuia na kulinunua gazeti (nadhani ni "Herald" kama bado sijasahau)ili tu lisiongelee mambo ya msingi ya Dr. Stockmann ambaye mpaka mwisho anasema "The greatest man in the world is who stands alone..."Wakuu linganisheni maudhui ya kitabu hicho na mambo ya Bunge letu,vyombo vyetu vya habari mf. Habari Corp,Zitto,Dr. Slaa na Upinzani kwa ujumla...
 
Mkuu Mtupori heshima mbele,
kweli umenikumbusha mbali sana miaka ile nilipokuwa A-level.Kweli hao kina Ngugi na Achebe utafikiri wanaiongelea Tanzania yetu ya leo hii,pia ningependa kukukumbusha ile play ya "AN ENEMY OF THE PEOPLE" inayomhusu Dr. Peter Stockmann na juhudi zake za kupambana na viongozi mafisadi ambao mpaka wanazuia na kulinunua gazeti (nadhani ni "Herald" kama bado sijasahau)ili tu lisiongelee mambo ya msingi ya Dr. Stockmann ambaye mpaka mwisho anasema "The greatest man in the world is who stands alone..."Wakuu linganisheni maudhui ya kitabu hicho na mambo ya Bunge letu,vyombo vyetu vya habari mf. Habari Corp,Zitto,Dr. Slaa na Upinzani kwa ujumla...

Kwa kweli nilikuwa nimesahau kukitaja kitabu hicho cha Bw Henrik Ibsen, nashukuru kama umekipitia pia. Kwa kweli maudhui ya vitabu hivi na kile kinachotokea Tanzania kwa sasa vinarandana mno, na mpaka hapo najipa moyo kuwa wakombozi wa Tanzania yenye neema ni sisi wote wenye uchungu na nchi yetu. Haiwezekani kundi dogo la watu wanafaidi matunda ya uhuru wakati sie wote tunastahili matunda hayo.
Hakika mpaka kieleweke mwaka huu.
Mungu Ibariki Tanzania.
 
Back
Top Bottom