WOMESA Tanzania waadhimisha siku ya bahari kwa kufanya usafi wa mazingira fukwe ya Coco beach

pantheraleo

JF-Expert Member
Jan 5, 2013
691
878

1566983825184.png

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Bahari, Meneja Huduma za Bahari,Mafunzo na Vyeti kutoka Wakala wa Meli Tanzania(Tasac) Iroga Nashon Iroga(katikati)akishiriki kufanya usafi eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam ikiwa ni Siku ya kuadhimisha Siku ya Bahari Afrika.Kwa hapa Tanzania siku hiyo imeadhimishwa na Umoja wa Wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya bahari(WOMESA).
UMOJA wa Wanawake Wanaofanya kazi katika sekta ya bahari(WOMESA) nchini Tanzania wamefanya usafi kwa kusafisha ufukwe wa Bahari ya Hindi katika eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam Salaam.

WOMESA barani Afrika wameadhimisha Siku ya Bahari ambayo huadhimishwa kila ifikapo Julai 25 na leo umoja huo kwa upande wa Tanzania wameiadhimisha kwa kufanya usafi eneo hilo huku wakitumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa jamii kutunza fukwe zetu kwa kuzifanya kuwa safi wakati wote na kuchukia vitendo viovu vinavyofanywa na watu wasio wema baharini.

Akizungumza baada ya kufanya usafi eneo hilo kwa kuondoa taka na hasa za plastiki, Katibu wa WOMESA Tanzania na Mjumbe wa Kamati Tendaji wa umoja huo Dk.Devotha Edward Mandanda amesema wameadhimisha hiyo kwa kufanya usafi ikiwa ni sehemu ya kuiunga mkono juhudi za Serikali ambayo imeamua kwa vitendo kukataa matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.

"WOMESA katika Mkutano Mkuu wa mwaka moja ya makubaliano yalikuwa ni kupiga vita uchafu unaotokana na plastiki na hasa katika maeneo ya baharini kwani ni hatari kwa usalama wa viumbe vya majini.Kwa kweli ni bahati kwa Tanzania kwani baada ya uamuzi ule hapa kwetu nako Serikali ikatangaza kupiga marufuku mifuko ya plastiki.

"Hivyo kwa WOMESA Tanzania tunasema tumepata bahati maana hili limetekelezwa kwa vitendo na ndani ya muda mfupi. Hivyo tumeona katika kuadhimisha Siku ya Bahari kwetu hapa nchini tufanye usafi katika eneo la Coco Beach kwa kuondoa taka za plastiki.Pia tunaomba jamii nayo ione umuhimu wa kutunza fukwe zetu nzuri,"amesema Dk.Mandanda.

Akifafanua zaidi kuhusu uamuzi wao wa kufanya usafi eneo hilo Dk.Mandanda amesema mbali ya usafi huo wamekutana na vijana waliopo kwenye fukwe hiyo ambao wamekuwa wakijihusisha na kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo ya kufundisha kuogelea na kutoa elimu kuhusu bahari kwa kubadilishana nao mawazo na kupeana misingi yenye maadili mema ya kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.

Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Bahari, Meneja Huduma za Bahari,Mafunzo na Vyeti kutoka Wakala wa Meli Tanzania(Tasac) Iroga Nashon Iroga amesema wanaupongeza umoja huo kwa kutambua na kuona umuhimu wa kusafisha maeneo ya fukwe na kusisitiza fukwe za Tanzania ziko salama.

"Tumeshiriki kuadhimisha Siku ya Bahari kwa kufanya usafi,wenzetu wa WOMESA Wametambua kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Serikali ya kuweka mazingira safi yakiwemo ya fukwe,"amesema Iroga na kuongeza umefika wakati kwa jamii ikawa inapata elimu ya matumizi ya fukwe za bahari ili kuondoa changamoto ambazo zinajitokeza.

Wakati huo huo wakiwa katika fukwe hiyo WOMESA pamoja na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi maalum kwa ajili ya usalama wa baharini wamepokea malalamiko kuhusu uwepo wa vitendo vya ubakaji wanavyofanyiwa baadhi ya wanawake wanaokwenda kuogolea.Hata hivyo Polisi wamesema walishaweka mikakati na mbinu mbalimbali za kukomesha tabia hizo zinazofanywa na baadhi ya vijana.

Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Beach Boy katika eneo hilo la Coco Beach Bakari Salum amesema ni kweli siku za nyuma kulikuwa na malalamiko ya watu kudai wanabakwa lakini waliamua kuweka mkakati wa kukomesha tabia hizo na sasa hazipo.

Amesema baada ya malalamiko kuzidi waliamua kuandikisha majina wanachama wao,hivyo akitokea mtu anataka kwenda kuogelea au anataka huduma yoyote ya baharini basi kuna utaratibu wa kuandika majina ili likitokea tatizo pawepo na mahali pa kuanzia na tangu utaratibu huo uanze vitendo vya hivyo vimekoma.


Chanzo: Michuzi blog
 
Back
Top Bottom